MAJINA YA WANAWAKE KATIKA BIBLIA ‘A’ HADI ‘Z’



            Kuanzia sura hii ya tatu na sura kadhaa zitakazofuata zitahusu wanawake baadhi waliotajwa majina yao katika Biblia. Hivyo, wanawake waliotajwa majina yao katika Biblia, nimejaribu kuwagawa kwa kufuata mpangilio wa herufi ya kwanza katika majina yao hadi ya mwisho. Kwa hiyo, unapopitia kila jina la mwanamke kunamambo mengi ya kujifunza katika maisha ya kiroho na ya kawaida, aidha, maana ya jina, tabia, matendo na imani.

Abia
            Jina hili linamanisha “matakwa ya Mungu”. Wakati mwingine jina hili humanisha Baba yangu ni Yehova. Mwanamke huyu alikuwa mke wa Hesroni, aliyemzalia mumewe mtoto wa kiume aitwaye Ashuri, babaye Tekoa. “Tena, baada ya kufa kwake Hesroni huko Kalebu-Efrata, ndipo Abia, mkewe Hesroni, alipomzalia Ashuri, babaye Tekoa” (1Nyakati 2:24).

Abiya
            Mwanamke huyu alikuwa mama wa Hezekia, aliyekuja kuwa mfalme na alitawala kwa miaka ishirini na tano (2Wafalme 18:2; 2Nyakati 29:1). Maana ya jina Abiya humanisha “Mungu wangu ni Baba”. Mwanamke huyu alikuwa ni binti wa Zekaria. Mumewe na Abiya aitwaye Ahazi, hakuwa mwema lakini mtoto wake alikuwa mwema. Hivyo, yawezakuwa Abiya alikuwa mama mwenye malezi mazuri kwa mtoto wake.
            Mtoto Wa mama huyu (itwaye Hezekia) alipotawazwa kuwa mfalme wa Yuda, alijitwisha kazi ya kuimarisha hali ya nchi kuhusu uchumi, kupindua utawala wa Waashuri, na kufanya uamsho na matengenezo ya kiroho. Mafanikio katika uamsho na matengenezo ya kiroho, ni miongoni mwa mambo makuu yaliyompatia sifa Hezekia ya kuwa mfalme mkuu na bora wa wakati wake (2Wafalme 18:1-8).
         
(a) Abigaili
             Mwanamke mwenye uzuri wa sura na akili njema. Alikuwa mke wa Nabali ambaye hakuwa na huruma, hekima wala wema ndani yake (1Samweli 25:3). Nabali maana yake ni “mjinga” ama “mpumbavu” (1Samweli 25:25). Nabali nusura angelileta msiba juu ya nyumba yake kwa sababu ya kuwatukana na kuwadhihaki Daudi na watu wake na kukataa kuwapa chakula kama asante kwa kazi yao ya kulinda mashamba yake dhidi ya Wafilisti waliotaka kuiba mavuno. Ilikuwa ni kwa sababu ya busara na maneno ya hekima na baraka ya Abigaili yaliyosababisha matatizo makubwa yasitokee kwa familia na mumewe (1Samweli 25:2-35).
            Inaonesha mama huyu alikuwa mwenye hekima na mwelevu wa akili. Waweza ona alivyokuwa mjuzi na stadi wa kupanga maneno yake kwa hekima, busara na adili: “Nakuomba, ulisamehe kosa lake mjakazi wako, kwa kuwa hakika BWANA; atamfanyia bwana wangu nyumba iliyo imara, kwa sababu bwana wangu anavipiga vita vya BWANA; tena uovu hautoonekana ndani yako siku zako zote” (1Samweli 25:28). Kwa baraka na maelezo ya hekima na busara ya Abigaili, Daudi aligaili kwenda kulipiza kisasi kwa Nabali (soma 1Samweli 25:33).
            Hivyo, kwa busara na hekima za Abigaili, Daudi aliweza kutii agizo lililo katika Kumbukumbu la Torati 32:35; Mambo ya Walawi 19:18; Mathayo 5:39 na Warumi 12:19 ya kuwa “Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu Mimi; Mimi nitalipa, anena Bwana” (Warumi 12:19). Hivyo basi, kama ambavyo mafungu yafuatayo yanavyothibitisha, Nabali alipokufa ghafla, Daudi alimtwaa Abigaili na kuwa mkewe (1Samweli 25:39-42; 1Samweli 27:3; 1Samweli 30:5, 18).

                                                            (b) Abigaili
             Abigaili huyu alikuwa ni dada yake na Daudi, ambaye Biblia haijaeleza habari zake kwa kina ya kwamba alitoka tumbo moja na Daudi (1Nyakati 2:11-17). Wachambuzi wengine wa maandiko ya Biblia, hudaui kwamba, Abigaili huyu na Daudi walitofautiana baba, ila mama ni mmoja. Wanazuoni hawa, huzidi kudai kuwa, baba wa Abigaili huyu aliitwa Nashaha, na hoja yao huwa imejengwa katika 2Samweli 17:25.
(a) Abihaili
            Katika Biblia, jina hili linatumika kwa mwanamke na mwanamume pia. Maana ya jina hili ni “Baba ni chanzo” au “Baba husababisha nguvu/mvuto”. Abihaili alikuwa mtoto wa kike  kutoka kwa mtoto wa kiume wa Merari wa kabila ya Lawi na mama yake alikuwa ni Surieli ambaye alikuwa mkuu wa nyumba za baba za jamaa za Merari (Hesabu 3:35).

(b) Abihaili
            Abihaili huyu alikuwa mke wa Abishuri wa kabila ya Yuda katika uzao wa Hesroni na Yerameeli,  na alimzalia mumewe watoto wawili waitwao Abani na Molidi  (angalia kitabu cha 1Nyakati 2:29).
(c)    Abihaili
           Abihaili huyu alikuwa binti wa Eliabu, mwana wa Yese (2Nyakati 11:18). Ikumbukwe kuwa, kulikuwa na uoleanaji mwingi sana katika familia ya Daudi. Baadhi ya matoleo mengine ya Biblia katika lugha ya Kingereza, yanaonesha kuwa, Abihaili huyu ni mke wa pili wa Rehoboamu.  Abihaili lilikuwa pia jina la mama yake Esta (Esta 2:15).

Abishangi
            Maana ya jina hili ni  “Baba yangu  huzurura au baba yangu husababisha kuzurura”. Mwanamke au binti huyu wa Kishunami, kwa sababu ya uzuri wake, alipewa jukumu la kumtunza na kumtumikia mfalme Daudi, alipokuwa hajiwezi kutokana na uzee. (1Wafalme 1:1-4). Kazi mojawapo ya Abishangi, ilikuwa kulala katika kitanda cha Daudi na kumpasha joto. Ingawa Abishangi hakuwa suria wa Daudi, lakini wachambuzi wengine wa Biblia walifikiri hivyo. Baada ya kufa kwake Daudi, mwanawe, aitwaye Adonia mwana wa Hagithi alionesha nia isiyokuwa na mafanikio ya kumuoa Abishangi (1Wafalme 2:13-25).
           Adonia alimwomba mfalme mpya wa Israeli (Sulemani), apewe ruhusa ya kumuoa Abishangi. Kwa desturi ya wakati ule, mfalme mpya alirithi masuria wa mfalme wa zamani (tazama 2Samweli 3:7-10; 12:7-8; 16:22), na hivyo Sulemani alitafsiri ombi la ndugu yake Adonia kama ilikuwa mbinu ya hila ili ajipatie kiti cha ufalme kilichoachwa na Daudi, baba yake. Kwa hiyo, Adonia alihukumiwa kifo kwa hatia ya maasi (1Wafalme 2:13-25).

Abitali
            Jina la mwanake huyu linamanisha “Baba ambaye ni kama umande”. Abitali alikuwa miongoni mwa wake zake Daudi.  1Nyakati 3:1-3 inamwelezea kuwa: “Basi hawa ndio wana wa Daudi, aliozaliwa huko Hebroni; Amnoni, mzaliwa wa kwanza, mwana wa Ahinoamu, Myezreeli; wa pili, Danieli, wa Abigaili Mkarmeli; wa tatu, Absalomu, mwana wa Maaka, binti Talmai, mfalme wa Geshuri; wa nne, Adoniya, mwana wa Hagithi; wa tano, Shefatia, wa Abitali; wa sita, Ithreamu, kwa Egla, mkewe”.  Angalia pia katika kitabu cha 2Samweli 3:2-4).

(a) Ada
            Ada huyu ni mwanamke wa kwanza kutajwa kwa jina bada ya Hawa. Ikumbukwe kuwa, watoto wote wa kike wa Adamu na Hawa hawakutajwa majina yao. Jina hili lilikuwa ni la mke wa Lameki (mtoto wa Kaini).  Hivyo, mwanamke huyu alikuwa ni mmoja wa wake wawili wa Lameki.  Ada alikuwa ni mama wa watoto wawili wa kiume waitwao Yabali na Yubali (Mwanzo 4:19)
(b)   Ada
             Mwanamke huyu alikuwa binti wa Eloni na alikuwa Mkanaani kutoka kabila la Wahiti. Ada huyu alikuwa miongoni mwa wakeze Esau (Mwanzo 36:2); na alimzalia Esau mtoto wa kiume aitwaye Elifazi. Moja wapo ya sababu ambayo ilimfanya Esau kuwa nje ya agano la Mungu na baraka zake, kwanza ni kwa kuoa wanawake wawili wa kabila la kipagani la Kaanani la Wahiti na baadae binti wa kabila ya Ishimaeli  (Mwanzo 26:34-35; Mwanzo 28:8-9).

 (a) Ahinoamu
            Ahinoamu huyu alikuwa binti wa Ahimaasi na mke wa Sauli, aliyekuwa mfalme wa kwanza wa taifa la Israeli. 1Samweli 14:50 inamripoti kuwa, “na jina lake mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu, binti Ahimaasi”.

(b)   Ahinoamu
             Mwanamke huyu alikuwa ni miongoni mwa wake nane wa Daudi, aliyekuja kuwa mfalme wa pili wa taifa la Israeli. Ahinoamu huyu, alikuwa mama wa mtoto wa kwanza wa kiume kwa Daudi, aitwaye Amnoni. (1Nyakati 3:1; 2Samweli 2:2).

 Alai
            Alai alikuwa ni mtoto wa kike wa Sheshani ambaye alikuwa na binti kadhaa. Alai aliozeshwa na baba yake kwa mtumishi wake aliyekuwa Mmisiri aitwaye Yarha. Kupitia kwa mumewe, Alai alimzaa Atai (1Nyakati 2:31, 34).
            Mwanamke mwingine aliyetumia jina hili, ni Alai ambaye alikuwa mama yake na Zabadi, mmoja wa mashujaa wa jeshi la Daudi (1Nyakati 11:41).

 (a) Ana
            Mwanamke huyu alikuwa mmojawa wa wakeze Esau (Mwanzo 36:2, 18, 25).  Ana huyu alikuwa ni binti wa Sibeoni na alikuwa mama wa Dishoni. Ana ni mama pekee aliyetajwa pamoja na watoto wake miongoni mwa wake wa Esau (Mwanzo 36:24, 29; 1Nyakati 1:38, 41). Jina la Ana linamaana sawa na Hana, linalomaanisha ‘upendeleo’ au ‘neema’. 

(b)   Ana
             Mwanamke huyu alikua nabii mwanamke kama alivyoelezewa katika Luka 2:36-38 (pamoja na taarifa zake zingine) kuwa, “Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri ......”. Jina hili la Fanueli humanisha ‘sura’, ‘njozi’ ama ‘muonekano wa Mungu’. Hakuna uhakika kwamba Fanueli lilikuwa ni jina la baba yake au mama yake Ana.  Jina hili linafana na Penueli, jina ambalo Yakobo alilipa lile eneo alishindana mieleka na Malaika.
            Jina la mumewe aliyefariki katika umri wa ujana halikutajwa. Ana aliolewa kwa miaka saba tu na kubaki mjane (baada ya mumewe kufariki) kwa miaka themanini na nne, hivyo, yaweza kuwa aliishi zaidi ya miaka mia moja. Ana alimcha Mungu, kwa kuomba usiku na mchana pamoja na kufunga.  Alikuwa ameshaoneshwa namna atakavyo zaliwa Masihi na Mkombozi wa ulimwengu wote. Maisha yake yote katika ujane wake, aliishi hekaluni (yawezakuwa alikuwa akihudumu kazi ya Mungu).

 Afia
            Waraka wa Paulo kwa Filemoni hasa katika utangulizi, Paulo anamtaja Afia katika orodha ya majina katika salamu yake (Filemoni 1:2, 3). Waraka huu ni kati ya barua ambazo Paulo aliziandika kutoka katika kifungo chake mjini Rumi (tazama Matendo 28:16, 30), na alimuandikia Filemoni, ambaye kanisa la Kolosai lilikuwa nyumbani kwake.  Afia ametajwa kwa sababu ya ukaribu wake na Filemoni, tofauti na hapo, yaweza kuwa asingetajwa katika waraka huo (Wafilipi 1:2).
            Afia, Arkipo na Onesimo waliuawa kwa kupondwa mawe kipindi cha utawala wa Kaisari Nero. Ikumbukwe kuwa, Onesimo ndiye aliyeenda Kolosai kupeleka ujumbe (waraka) kwa familia ya Filemoni.  Kwa baadhi ya wanazuoni wa teolojia, wanaamini ya kuwa, Afia alikuwa mkewe Filemoni na labda mama au dada wa Arkipo. Jina hili la Afia humanisha ‘malimbuko’, au ‘matokeo mazuri’. 
Aksa
             Mwanamke huyu alikuwa binti wa Kalebu, mkuu wa kabila ya Yuda Alikuwa binti pekee katika familia na alikuwa na kaka zake watatu (1Nyakati 4:15).  Aksa aliolewa na Othnieli, mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa baba yake (Waamuzi 1:12-13; Yoshua 15:16-17). Huyu pia, alikuwa ni mwanamke aliyehitaji vingi zaidi kutoka kwa mumewe (Yoshua 15:17-19). Jina hili linamaana ya ‘aliyepambwa’, ‘urembo’ au ‘kupendeza’.
            Aksa alikuwa maarufu sana kuliko kaka zake. Yaweza kuwa ni kwa sababu ya uzuri na urembo wake. Ikumbukwe kuwa, kwa mashariti ya baba yake, Aksa ilimpasa kuozeshwa kwa mtu ambaye angeupiga Kiriath-seferi na kuutwaa. Othnieli mwana wa Kenazi alifanikisha kuutwa Kiriath-sefari (Yoshua 15:16-17).   

 Asenathi
            Ni mwanamke aliyetolewa na mfalme ili aolewe na waziri mkuu wake (Mwanzo 41: 45-59; Mwanzo 46:20).  Alikuwa ni Mmisiri na mtoto wa Potifera, kuhani wa Oni, wa hekalu kuu la Jua huko Helipolis karibia na mji wa Kairo kwa sasa. 
            Asenathi aliolewa na Yusufu na alimzalia watoto wawili, waitwao Manase (maana yake, ‘Mungu ameniondolea matatizo yote hata kutoka nyumba ya baba yangu’) na Efraimu (maana yake, ‘Mungu amenifanya kuwa matunda katika nchi ya kushirikishwa’).

 Atara
            Huyu mwanamke alikuwa mke pili wa Yerameeli na alikuwa mama wa Onamu (1Nyakati 2:26). Jina la mwanamke huyu, linamanisha ‘taji’. Mke wa kwanza wa Yerameeli ambaye alimzalia watoto watano, Biblia haikulitaja jina lake (1Nyakati 2:26, 28).

 Athalia
            Maana ya Athalia ni ‘aliyetwaliwa nje ya Bwana’ au ‘Yehovah ameniumiza’. Athalia ni jina pia lililotumiwa na wanaume wawili katika Biblia (1Nyakati 8:26, 27; Ezira 8:7). Athalia alikuwa binti wa Ahabu na Yezebeli, aliolewa na Yehoramu wa Yuda, mtoto wa Yehoshafati (2Nyakati 22:1-3). Athalia alikuwa na ushawishi mkali juu ya mumewe na pia juu ya mwanaye aitwaye Ahazia, aliyekuwa mfalme wa Yuda baada ya baba yake. Athalia alikuwa ni mwanamke msumbufu na muuaji (2Nyakati 21:4-6; 2Nyakati 22:1-10; 2Wafalme 11:1-20).
           Ahazia alipouawa katika vita vya mapinduzi ya Yehu wa Israeli aliyetaka kuondoa Ubaali (2Nyakati 22:5-9), Athalia alipanda kiti cha enzi cha Yuda akaua wajukuu wake wote  (ispokuwa mmoja tu aliyetoroshwa) akaimarisha Ubaali wa mama yake katika Yuda (2Nyakati 22:10-12); 2Nyakati 24:7). Kutokana na mauaji aliyoyafanya Athalia, na yeye baada ya miaka sita aliuwawa katika mapinduzi mapya dhidi ya Ubaali, ambayo wakati ule yaliendeshwa mjini Yerusalemu, lakini bila ya kumwaga damu nyingi (2Nyakati 22:12-23:13-21).
           Wakati ule watu walipobomoa hekalu lake la Baali, madhabahu ya Baali na sanamu zake, walitengeneza upya ufalme wa  mbari ya Daudi walipomweka mjukuu wa pekee aliyesalia juu ya kiti cha enzi cha Yuda (2Nyakati 23:16-21). Kwa kuwa mwanamke huyu alikuwa muabudu miungu, hata mwanaye aliyekuwa mfalme wa Yuda alipotoka na kuwa mtenda maovu (2Nyakati 2:2-3; 2Nyakati 24:7).

 (a) Azuba (Azubu)
          Mwanamke huyu alikuwa mke wa Kalebu, mwana wa Hesroni. Baada ya Azubu kufariki, Kalebu alimuoa Efrathi (1Nyakati 2:18, 19). Maana ya jina hili ni ‘taabu’ au ‘huzuni/majonzi’. Ahadi ya Mungu huwa haiwaachi watu wake, kama ilivyooneshwa katika ishara ya jina kwenye Isaya 62:4. Kalebu ambaye ametajwa kama mume wa mwanamke huyu, sio yule aliyetajwa katika wapelelezi kumi na mbili katika Hesabu 13, bali ni miongoni mwa uzao wake. Azuba alimzalia Kalebu watoto watatu waitwao Yesheri, Shobabu na Ardoni,

(b) Azuba
            Azuba huyu alikuwa mama wa mfalme Yehoshafati wa Yuda ambaye alikataa kufanya ushirika na mfalme Ahabu wa Israeli aliyekuwa muabudu miungu (1Wafalme 22:42; 2Nyakati 20:31). Azuba alikuwa binti wa Shilhi na jina lake lilielezea ‘Jeshi la Bwana’, likimwongelea mwanamke anayemjua Mungu kama mlinzi wake.
            Alikuwa mke wa Mfalme Asa, mfalme wa tatu wa Yuda, ambaye alikuwa mtawala mzuri miongoni mwa wafalme wa Yuda. Kunaushahidi kuwa, Asa alikuwa mmoja wa wenye hofu na Mungu kwa wakati wake na alikuwa imara katika imani hivyo hata mwanae, Yehoshafati alifuata mkondo wake.

 Baara
            Baara alikuwa Mmoabu aliyeolewa na Shaharaimu wa kabila ya Benyamini alipoenda katika nchi ya Moabu. Kabla hajaachika, Baara alikuwa mke wa pili kwa Shaharaimu na alimzalia mumewe watoto wakati wakiishi wote kule Bara-Moabu (1Nyaka 8:8). Maana ya jina hili ni “iunguzayo” au “kiunguzacho”. Jina Baara limetokana na neno “beera”  lenye maana ya ‘unguza’, ‘ungua’ au ‘toa mwanga’.

 (a) Basemathi
            Mwanamke huyu alikuwa mmoja wa wake wa Esau, ambaye pia aliitwa binti wa Eloni Mhiti (Mwanzo 26:34). Esau alimuoa Basemathi kwa sababu baba yake (aitwaye Isaka) hakufurahishwa na wale wake wake wengine waliokuwa binti za Kanaani. Jina hili linamanisha ‘manukato’ au ‘harufu nzuri’. Kwa tabia, mwanamke huyu hakuwa mtu wa mashaka ama wasiwasi.

(b) Basemathi
            Basemathi huyu ametajwa na Biblia kama binti wa Ishmaeli, na mke wa Esau (Mwanzo 36:3-4). Alikuwa na mtoto wa kiume aitwaye Reueli (Mwanzo 36:10). Reueli alikuwa na wana wanne wa kiume, waitwao Nahathi, Zera, Shama na Miza (Mwanzo 36:13). Wachunguzi wengi wa Biblia, huamini kuwa Basemathi huyu ni tofauti na yule wa Mwanzo 26:34 (tuliyemtazama katika kipengele (a)). Miongoni mwa sababu zao ni kuwa, wa kwanza alikuwa binti Eloni, na huyu ni binti Ishimaeli. Kwa hoja hiyo, basi itakuwa miongoni mwa wake wa Esau, wawili walikuwa wanafanana majina yao.

(c) Basemathi
            Mwanamke huyu aitwaye Basemathi, alikuwa binti wa Sulemani na mke wa Ahimaasi aliyekuwa mmoja wa wakusanya ushuru wa mfalme katika Naftali. “Ahmaasi, katika Naftali; naye ndiye aliyemwoa Basemathi binti Sulemani” (1Wafalme 4:15).

 Bath-sheba
            Maana ya jina hili ni ‘binti wa saba’ au ‘binti wa shayiri’. Neno ‘bath’ linamanisha binti. Bath-sheba ni mwanamke ambaye uzuri wake ulisababisha uzinzi na mauaji. “Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho” (2Samweli 11:2-3) . Tamaa ya Daudi ilisababishwa na kubakia Ikulu kama mfalme bila cho chote cha kufanya, wakati taifa lake lipo vitani (2Samweli 11:1).
            Mwanamke huyu alitokea katika familia inayomcha Mungu. Bath-sheba alikuwa binti Eliamu na mke wa Uria Mhiti, aliyekuwa mtiifu na miongoni mwa  mashujaa wa mfalme Daudi. Daudi alizini naye, na akapata mimba  (2Samweli 11:2-5). Kisaha Daudi alifanya mbinu za uuaji ili Uria afe vitani, na baada ya hayo alimchukua Bath-sheba  awe mkewe katika nyumba yake ya ufalme (2Samweli 11:6-27).
            Baada ya hilo tukio, nabii Nathani alimuona Daudi ili kumpasha habari juu ya hatia yake ya uuaji na zinaa, akimtabiria kwamba familia yake mwenyewe ingeharibiwa kwa njia ya uuaji na zinaa (2Samweli 12:1-12; 2Samweli 13:1-29). Daudi alitubu dhambi zake (2Samweli 12:13; Zaburi 51), lakini msamaha wa Mungu haukuondoa kielelezo kibaya ambacho Daudi alikwisha kuwa kwa familia yake.
            Mtoto wa Daudi aliyezaliwa na Bat-sheba alikufa (2Samweli 14-23). Kufa kwake mtoto huyu ilikuwa mbadala wa Daudi kufa (2Samweli 11:13-14). Lakini baadaye walimpata mtoto mwingine wa kiume, Sulemani (2Smweli 12:24). Mtoto yule alikuwa mteule wa Mungu kwa kurithi kiti cha enzi cha ufalme wa Isreali (1Nyakati 22:9-10). Bath-sheba alimzalia Daudi watoto watano wa kiume (wa kwanza alikufa) waitwao Shamua, Shobabu, Nathani na Sulemani (1Nyakatin 3:5). Wakati wa uzee wa Daudi, mwana mwingine  wa Dauidi, aitwaye Adonia, alijaribu kumwondoa Sulemani katika madai ya kupata kiti cha enzi, lakini ushawishi wa Bath-sheba ulimhakikishia Sulemani ufalme (1Wafalme 1:11-31).
            Miongoni mwa wanawake watano pekee, wanaotajwa katika kitabu cha ukoo wa Yesu,  Beth-sheba  naye katajwa, ila si kwa jina bali kama aliyekuwa mke wa Uria (Mathayo 1:6). Kutajwa kwake ni kwa sababu mumewe wa pili aitwaye Daudi alitenda mema machoni pa Mungu, isipokuwa katika habari ya Uria, Mhiti (1Wafalme 15:5). Lakini kwa kosa la uzinzi na kumuua Uria, Daudi aliomba msamaha kwa Mungu (Zaburi 51; 2Samweli 11:13).

 Bernike
            Jina hili limetokana na neno la lugha ya Kiyunani (Kigriki) “bernicke” au “berenice” lenye maana ya ‘mshindi’ au ‘aliyebeba ushindi’. Hivyo, jina hili huelezea furaha ya ushindi au ushindi mwema. Bernike alikuwa binti mkubwa wa Herode Agripa wa kwanza ambaye alitawala kuanzia 38-45 BK na huelezewa kama mmoja wa aliyelitesa kanisa na kuua na kuwafunga Mitume wa Yesu (Matendo 12:1-4), na aliuliwa na Malaika wa Mungu, kwa sababu ya kutompa utukufu Mungu (Matendo 12:20-23).
            Biblia inamtaja Bernike mara kadhaa, akiwa ameambatana na Herode Agripa wakati Paulo akiwa amekamatwa, akiwa gerezani kabla ya kupelekwa Rumi (Matendo 25:13, 23). Herode Agripa na miongoni mwa wasikilizaji wengine wa hoja, ushuhuda na uetezi wa Paulo Mtume akiwemo na Bernike, waliona kuwa Paulo hana makosa na angeweza kuachiliwa huru (Matendo 26:30). Herode Agripa wa pili alikuwa kaka yake na Bernike.
            Ikumbukwe pia, Bernike alikuwa na ndugu yake wa kike, aitwaye  Drusila wote wakiwa dada zake Herode Agripa wa kwanza (Matendo 24:24; Matendo 25:13).

 Bilha
            Binti huyu kijakazi, alikuwa chini ya Raheli, mke kipenzi wa Yakobo kutoka kwa Labani (Mwanzo 29:29).  Baada ya Raheli kuona kuwa hawezi akamzalia Yakobo watoto, alimshawishi mumewe wajipatie uzao kupitia kwa Bilha kijakazi wao (Mwanzo 30:3-5). Bilha alimzalia Yakobo na Raheli watoto wawili wa kiume waitwao Dani na Naftali (Mwanzo 30:5-8; Mwanzo 46:25; 1Nyakati 7:13). 
            Kama alivyofanya mke wa Manoa katika kumtegemea Mungu (Waamuzi 13:2), Raheli hakupaswa kumshawishi mumewe kumjua Bilha aliyekuwa kijakazi, na wala haikumpasa kufanya mashindano na Lea mke mwenza. Yeye angezidi kumlilia Mungu kama Hana mkewe Elikana alivyofanya. Kosa hili la Raheli alilifanya na Sara kwa mumewe Ibrahimu (Mwanzo 16:2).
            Ikumbukwe pia, Bilha alilala na Reubeni, mtoto wa kwanza wa Yakobo (Mwanzo 35:22), na kosa hili, lilimgharimu Reubeni na uzao wake, kutokuwa sehemu ya Taifa au kabila za Israeli (1Nyakati 5:1). Tofauti na Reubeni, Yuda ambaye pia ni mtoto wa Yakobo kwa Lea mkewe, yeye naye alilala na mke wa mwana wake (Mwanzo38:14).

 Bithia
            Bithia alikuwa binti Farao na mumewe aliitwa Meredi (1Nyakati 4:18). Maana ya jina hili Bithia ni ‘Binti wa Yehova’. Kiushahidi, Bithia anatajwa kama binti wa Farao, japo jina  lake linaweza kuwa la Kiisraeli kutoka katika lugha ya Kiebrania “pernoth” au “paroth”  kutoka katika neno “para” lenye maana ya ‘kutangulia’ au ‘kuongoza’. Na kama baba yake alikuwa mfalme (Farao) wa Misri, wanazuoni wa Biblia hudhani ya kuwa, Bithia aliongolewa au labda alikuwa miongoni mwa Wamisri ambao  waliongolewa baada ya janga la bahari ya Shamu, katika mwujiza wa maji kuchia njia ili Waisreli wapite wakati wakifuatiwa na majeshi ya Farao.

 Damari
            Mwanamke huyu aliongolewa katika harakati za injili ya Paulo huko Athene (Matendo 17:34). Jina lake linamaanisha ‘kijana wa kike’. Wachambuzi wengine wa maandiko hudai kuwa, yaweza kuwa  Damari alikuwa mke wa Dionisio.

 (a) Debora
            Jina  hili la Debora humanisha ‘nyuki’. Huyu ni mwanamke aliyetumia maisha yake kama mlezi au mjakazi, na alimlea Rebeka. Debora aliambatana na Rebeka hata alipoolewa na Isaka, kutoka Padan-aramu. Aliishi na Rebeka mpaka alipokufa katika umri mkubwa. Baada ya kifo chake, alizikwa Betheli maeneo ya mwaloni. Eneo hilo alilozikwa Debora, lilipatiwa jina la Alon-bakuthi, yaani mwalo wa vilio (Mwanzo 24:59; Mwanzo 35:8).
            Kutokana na eneo alilozikwa Debora kuitwa Alon-bakuthi (mwalo wa vilio), hivyo inaonesha Debora alipendwa sana. Mungu alimuwezesha Debora kuishi kama alivyo chagua kwa uaminifu.

(b) Debora
             Debora huyu ndiye aliyejulikana zaidi, na kwa sehemu kubwa amezungumziwa katika kitabu cha Waamuzi sura ya 4 na 5 na Waebrania 11:32-34. Debora ni mwanake ambaye hakuwa na hofu katika uzalendo wa nchi yake. Alikuwa nabii mke na mke wa Lapidothi (Waamuzi 4:4). Baadhi ya wachambuzi wa mandiko hudai kuwa, mwanamke huyu anaonekana kuwa ni mwanamke mwelevu na mwenye akili kuliko wanawake wote wa agano la kale.
            Familia yake inaonesha ilikuwa katikati eneo la Betheli na Rama katika vilima vilima vya nchi ya Efraimu. Debora alipendelea kukaa chichini ya mtende wa Debora (Waamuzi 4:5). Alikuwa tu si kiongozi, bali alikuwa kiongozi  miongoni mwa viongozi watano wa juu (Waamuzi) katika Israeli. Muungu alimwinua juu ili kuwatoa watu wa Mungu (Israeli) katika ibada za sanamu. Hivyo, kwa matendo na maneno alitimiza majukumu yake kama Mwamuzi.
            Akiwa nabii mwanamke, alifaa sana kuamua mambo magumu kadiri ya mapenzi ya Mungu (Waamuzi 4:4-5). Debora pia alikuwa mpiganaji. Aliwahi kwenda kupigana ili kumuondoa mgandamizaji wa taifa la Israeli. Alikuwa pia Mwanamalenga ama mwandishi wa mashairi (Waamuzi 5:1-31). Anakumbukwa zaidi kwa kuongoza ushindi wa Waisraeli juu ya majeshi ya Sisera kaskazini ya Palestina.
            Akiwa pamoja na jemedari wake wa jeshi, Baraka, Debora aliongoza jeshi la Israeli juu ya mlima wa Tabori, kwa makusudi ya kuchokoza jeshi la magari ya Sisera liingie katika bonde la mto Kishoni chini yao (Waamuzi 4:6-10). Mvua kubwa zilinyesha na kufurisha bonde lote na magari yote ya Sisera yalikwama na hatimaye, Israeli walishinda vita.  

 Delila
            Huyu ni mwanamke aliyemsaliti mumewe kwa ajili ya fedha (Waamuzi 16:4-21). Maana ya jina Delila ni ‘nzuri’, ‘laini’, ‘nyororo’ au ‘dhaifu’. Kwa sababu ya hatia aliyoibeba, hajatokea mwanamke mwingine katika Biblia aliyeitwa jina hilo. Mwanamke huyu alitokea katika bonde la Soreki lililoanzia jirani ya Yerusalemu kwenda Mediterania.
            Kiujumla, hatuwezi tukamwelezea Delila bila kumwelezea Samsoni. Samsoni alikuwa imara kimwili lakini dhaifu kihisia. Japokuwa aliweza kupambana na simba, hakuweza kupambana na tamaa yake ya kimwili. Delila alimtumia samsoni na kumharibia mambo yake ya kiroho, hivyo, kumharibia nguvu zake pia.
            Delila alikuwa muongo na mdanganyifu, ila alikuwa na uwezo na nguvu ya kushawishi. Aliutumia uwezo wake wa ushawishi kwa malengo ya kujipatia pesa. Uzuri wake ulikuwa wenye roho mbaya. Alimsababishia Samsoni upofu, kifungo, mateso na kifo pia. Samsoni aliamini Delila anampenda, lakini Delila alimsaliti Samsoni kwa sababu tu alikuwa kinyume na watu waliokuwa kinyume na watu wa taifa la Mungu yaani Israeli.
            Samsoni alimdanganya Delila mara tatu kuhusu asili ya nguvu zake na mara ya nne alimwambia ukweli kuwa asili ya nguvu zake zipo katika nyele, na kisha ikawa hatima ya yeye kunyolewa na kukamatwa kisha kufungwa na kupatiwa mateso na Wafilisiti (Waamuzi 16:6-9, 11-12, 13-14, 15-21).   

 Dina
            Dina alikuwa binti wa Yakobo kupitia kwa mkewe aitwaye Lea. Huyu ni mwanamke ambaye kwenda kutembea na kuwaona binti  za watu wa mataifa kulimletea matokeo mabaya (Mwanzo 34). Maana ya jina hili ni ‘haki’ au ‘mtoa hukumu’. Jina hili walimpatia wazazi wake wakiamini katika haki ya kimbingu.
            Tamaa na udadisi wa kuyajua mambo ya kidunia kulimpelekea Dina kutamani kwenda kutazama binti za nchi ambako kulimletea madhara ya kushiriki uzinzi na mtoto wa mfalme Hamori, aitwaye Shekemu. Katika pitapita, mtoto wa mfalme alimwona Dina na akamtamani, alimchukua na kulala naye (Mwanzo 34:1-2).  Tukio la Dina kutolewa bikra yake, liliwauma sana kaka zake (hasa Simeoni na Lawi), na hatimae kufanya mauaji ya wanaume wote wa mji ule, akiwemo mfalme Hamori pamoja na mwanaye (Mwanzo 34:13-25). 
             Mauaji yaliyosababishwa na Simeoni na Lawi, yalipelekea baba yao, Yakobo afedheheke, na hatimae kuhama eneo hilo. (Mwanzo 34:30-31; Mwanzo 35:1-6). Simeoni na Lawi walitenda kinyume na Torati 22:28-29, isemavyo “Mtu mume akimwona kijana aliye mwanamwali ambaye hajaposwa, akamshika na kulala naye, wakaonekana; yule mtu mume aliyelala naye ampe baba yake yule kijana shekeli hamsini za fedha, kisha na awe mkewe, kwa kuwa amemtweza; hana ruhusa ya kumuacha siku zake zote”.

 Dorkasi
             Mwanamke ambaye utengenezaji wa nguo ulimfanya kuwa maarufu. Dorkasi ni jina la kwanza la Kiyunani (Kigriki) katika Biblia hasa agano jipya likiwa na maana ya Tabitha katika lugha ya Kiebrania. Biblia ipo kimya kuhusu wazazi ama familia aliyotoka Dorkasi. Mwanake huyu alikuwa amejaa matendo mema na alitoa sadaka za wema kwa wahitaji wa jamii iliyomzunguka (Matendo 9:36).
            Mwanamke huyu alikuwa Mkristo, na alitimiza agizo la  Yakobo 1:26, 27 lisemalo “Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai. Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa”.
            Jina Dorkasi, ama Tabitha humanisha ‘paa’. Huyu ni mwanamke aliyependwa sana na jamii yake, na alipokufa jamii hiyo ilimlilia sana, lakini pia aliweza kufufuliwa na Mtume Petro. Tukio hili la ufufuo wa Dorkasi, lilipelekea watu wengi wampokee Bwana (Matendo 9:37-42). Tendo hili la Petro kumfufua Dorkasi, linashiria uwezo na nguvu ya wale wote wamchao na kuyatenda matendo ya imani ya Yesu  Kristo, kwa kuwa yeye ni ufufuo na uzima (Yohana 11:41, 42; Mathayo 9:25 na Marko 5:40-41).
 
 Drusila
              Drusila ni mwanamke aliyependwa lakini aliipoteza fursa hiyo. Mwanake huyu alikuwa mke wa Feliki, na Biblia inamtaja kuwa alikuwa Myahudi (Matendo 24:24). Jina hili limetokana na neno la Kilatini “drusis” lenye maana ya ‘iliyomwagiliwa kwa umande’.
              Mwanamke huyu alikuwa mjukuu wa Herode Mkuu na binti mkubwa wa Herode Agripa wa kwanza ambaye alikuwa na mabinti wengine wawili. Mabinti hawa watatu wa Herode Antipa, mmoja aitwaye Salome ndiye aliyesababisha Yohana Mbatizaji kukatwa kichwa (Marko 6:22-29).
             Katika umri wa miaka 15, Drusila aliolewa na mfalme Azizi wa Emesa. Hakuwa mwaminifu kwa mumewe, hivyo aliamua kuachika na kuolewa na Gavana wa Kirumi ajulikanaye kama Feliki. Alitenda dhambi ya uzinzi maana aliolewa wakati hakuwa amepewa talaka na mumewe hakuwa amekufa. Drusila na Feliki walizaa mtoto waliyemwita Agripa.
             Drusila alikuwa mzuri zaidi ya dada yake aliyeitwa Bernike, kwa sababu hii, yeye na dada yake hawakupendana, na palikuwa na chuki kubwa baina yao. Cha ajabu, wote walitia aibu kutokana na matendo yao.

 Egla
             Mwanamke huyu alikuwa mke wa Daudi, na alimzalia mtoto wa kiume aitwaye  Ithreamu wakati Daudi akiwa bado yupo Hebroni (2Samweli 3:5; 1Nyakati 3:3). Hivyo, Egla alikuwa mmoja wa  wale wake wanane wa Daudi, na ambaye hajulikani sana. Lakini pia, alikuwa mama wa miongoni mwa watoto sita wa Daudi, wahati akiishi Hebroni. Maana ya jina hili ni ‘mtamba au mfarika wa mnyama’ au ‘gari la farasi’.

 Elisabeti
            Huyu ni mwanamke aliyezaa mtoto katika umri wa uzee, na mumewe alikuwa kuhani aliyeitwa Zakaria. Elisabeti ni mwanamke aliyepata bahati ya kipekee ya Kimbingu (Luka 1:46-56; linganisha na 1Samweli 2:1-10). Maana ya jina hili la Elisabeti humanisha ‘Mungu ni kiapo changu’. Jina lake linasadifu ucha Mungu wake, kwa maana alikuwa akimpenda na kumcha Mungu. Katika umri wa uzee, Elisabeti na Zakaria walimzaa Yohana Mbatizaji, mtangulizi wa huduma ya Yesu, kama matokeo ya maombi yao ya uhitaji wa mtoto (Luka 1:6-7, 13).
            Luka anamuelezea Elisabeti kuwa alikuwa miongoni mwa binti za Haruni, hivyo alitoka katika uzao wa Kikuhani (Kutoka 6:23). Alikuwa mke wa Kuhani Zakaria, aliyekuwa miongoni mwa seti ya Makuhani waliokuwa wakihudumu Sabato hadi Sabato (1Nyakati 24:10). Makuhani waliruhusiwa kuoa wake waliosafi na wasio najisi (Walawi 21:7). Hivyo, Elisabeti alikuwa mke safi kwa mumewe aliyekuwa kuhani. Elisabeti na Zakaria walijua kwamba mtoto wao angekuwa mtangulizi wa Masihi (Luka 1:13-17).
            Matukio mengine ya ajabu wakati wa kuzaliwa kwa mtoto yaliwasababisha hata wenyeji wa kijiji chao watambue kwamba mtoto yule amepangiwa mambo makubwa (Luka 1:57-66).  Elisabeti pia alikuwa jamaa wa Mariamu, mama yake Yesu (Luka 1:36). Elisabeti alipokuwa na mimba ya miezi sita, Mariamu alimtembelea na kumletea habari ya kuwa yeye Mariamu atakuwa mama wa Masihi aliyeahidiwa (Luka 1:36, 39-40). Elisabeti asiyekuwa na dalili yo yote ya wivu, alifurahi mno, naye alitafsiri kurukaruka kwa mtoto tumboni mwake ni dalili ya mtoto kufurahia jambo lile (Luka 1:41-45).

 Elisheba
             Elisheba alikuwa binti wa Aminadabu, dada yake Nashoni. Alikuwa mke wa Haruni aliyekuwa Kuhani mkuu wa taifa la Israeli. Kupitia kwa Haruni na Elisheba, walizaliwa Nadabu, Abihu, Eleazeri na Ithamari (Kutoka 6:23). Hivyo, Elisheba kuolewa na Haruni, alikuwa ameunganishwa moja kwa moja na familia ya Kikuhani. Haruni alikuwa kaka wa Musa na Miriamu. Maana ya jina hili la Elisheba linamanisha ‘Mungu ni kiapo chake’. Kwa upekee wake, mwanamke huyu alikuwa mzazi wa makuhani wote wa Kilawi.

 Efa
            Efa lilikuwa jina la suria wa Kalebu kiongozi katika kabila au taifa la Yuda, na alimzalia wana watatu waitwao Harani, Mosa, na Gazezi (1Nyakati 2:46). Maana ya jina hili ni ‘giza’ au ‘mwana wa mfalme’. Efa lilikuwa pia jina la wanaume wawili kama walivyobainishwa katika Mwanzo 25:4 na 1Nyakati 2:47. 

 Efrathi
              Mwanamke huyu alitwaliwa kuwa mke wa pili wa Kalebu baada ya mkewe aitwaye Azuba kufariki. Efrathi alimzalia Kalebu mwana aitwaye Huri (1Nyakati 2:19, 50). Huri mwana wa Kalebu na Efrathi, alikuwa na wana waitwao Penueli na Ezeri (1Nyakati 4:4).
             Kwa mujibu wa  Mwanzo 35:16, jina Efrathi limetajwa kama jina la mahali au mji ambao Raheli mke wa Yakobo aliposhikwa na utungu mzito wa kumzaa Benoni au Benyamini, kisha umauti ukamkuta baada ya kujifungua (Mwanzo 35:17-18). Maana ya jina hili ni ‘shamba la matunda’. Jina hili limetokana na maneno ya “efrata” na “efratani” yanayosisitiza wingi wa matunda (angalia Zaburi 132:6).

 Esta
            Esta ni mwanamke aliyeokoa taifa lake kutoka katika mpango wa mauaji. Esta alikuwa mwanamke wa Kiyahudi aliyeishi Uajemi (Persia). Esta lilikuwa jina lililotokana na asili ya Kiajemi “ester” lililo sawa na ‘nyota’ au ‘sayari aina ya Venasi’ likimanisha ‘bahati njema’ au ‘nyota njema’. Jina hili laweza kufasiriwa pia kama ‘nyota ya tumaini’,  ‘nyota ya furaha’ au ‘nyota ya ukuu’. Kwa maana hiyo ya jina, Esta alikuja akawa hivyo kwa jamaa zake.
            Esta alikuwa jamaa wa kabila la Benyamini na alitokana na familia iliyokuwa imechukuliwa mateka pamoja na nabii Nehemia miaka ya 600 K.K.  Alikuwa binti wa Abihaili aliyeishi Shushani mji mkuu wa Uajemi. Baada ya wazazi wake kufariki, Esta alibakia chini ya malezi na uangalizi wa Mordekai (Esta 2:6-7), aliyekuwa afisa katika Ikulu ya Ahasuero (aliyejulikana kwa jina la Xerxes wa kwanza, aliyetawala tangu mwaka 486 hadi 465 K.K).
            Habari za Esta zinaonekana katika kitabu kinachoitwa kwa jina lake. Kitabu chenyewe hakimtaji mwandishi wake. Kitabu cha Esta kinamtaja Mungu mara moja tu (nayo ni Esta 4:14). Hata katika kufunga kwao Wayahudi, haisemwi kwamba walimuomba Mungu (Esta 4:16), lakini kwa imani ndogo waliyokuwa nayo Wayahudi hawa wa Babeli (Uajemi ya zamani), Mungu alifanikisha kutoangamizwa kwao. Mfalme wa Uajemi alipotaka kumpata malkia mwingine, alimchagua Esta mwanamke aliyekuwa mtoto yatima wa Kiyahudi aliyelelewa na jamaa yake aitwaye Mordekai (Esta 2:5-7).
             Mordekai alikuwa na mchango mkubwa sana kwa Esta na alimlea kama binti yake wa kumzaa. Esta mara zote alikuwa mtiifu kwa Mordekai (mjomba wake), hata alipokuja kuwa Malkia, aliyaweka katika vitendo mashauri yote ya mjomba wake na alimwamini kama baba yake. Baada ya kifo cha Hamani, adui wa Wayahudi, Mordekai alikuja akawa Waziri mkuu badala ya Hamani. Kupitia kwa Esta, tunweza jifunza mambo yafuatayo:
a)      Kutafuta maelekezo ya Kimbingu katika nyakati ngumu (Esta 4:15-17)
b)      Kutumia maarifa yetu yote aliyotupatia Mungu ili kujua namna ya kufanya katika fursa finyu zinazopatikana ili kutuletea ukombozi na mafanikio hasa kama itakuwa sahihi.
c)      Wakati panapokuwepo na umuhimu wa kujitambulisha na kujiweka bayana – tufanye hivyo kwa mapenzi ya Bwana katika kuwaokoa wengine.
d)     Kuthamini na kutafuta ushirikiano kutoka kwa waumini wengine ili kufanya maombi ya pamoja kwa ajili ya jambo fulani.
e)      Kuwa na ujasiri katika Bwana na kutenda bila kupuuzia vitu vidogo vidogo.
f)       Cho chote unachopanga kiovu kwa wengine hugeuzwa na kuwa lipo kwako (mfano ni kwa Hamani).
g)      Yote mabaya tunayoyafanya kwa sababu ya madaraka na ukuu wetu hufika mwisho na nafasi huchukuliwa na wengine.

 Eunike
             Eunike alikuwa binti wa Loisi ambaye jina lake linaasiri ya Kiyunani. Loisi ambaye ni mama wa Eunike, alikuwa Myahudi, baba yake alikuwa Myunani. Huyu ni mwanamke ambaye mtoto wake wa kiume aitwaye Timotheo alikuja akawa mwinjilisti maarufu, aliyeingizwa katika kutenda kazi ya Bwana na Mtume Paulo (tazama Matendo 16:1-3).  Katika 2Timotheo 1:5, Paulo anamtaja Eunike kupitia kwa waraka wake kwa Timotheo, akisema “nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe unayo”.
            Jina hili la Eunike linamaanisha ‘ushindi ulio mwema’ au ‘kushinda kwema’ – huelezea furaha ya ushindi. Eunike aliliishi jina lake kwani alishinda katika kumrejesha mtoto wake kwa Mungu, maana alimfundisha na alimuombea ili atakaswe na Bwaba (1Timotheo 4:4-5).  Maandiko yamekaa kimya juu ya utambulisho wa baba yake Eunike. Mwanamke huyu wa Kiyahudi aliolewa na mtu wa mataifa na wakati Mtume Paulo anafanya mawasiliano na familia ya mwanamke huyu, mumewe alikuwa ameshafariki. 
            Baba yake Timotheo alikuwa Myunani na mama yake Myahudi. Alilelewa na kumjua Mungu angali bado mtoto mdogo, maana bibi yake na mama yake walimfundisha mambo ya Mungu wa Mbinguni (2Timotheo 3:14-15; 2Timotheo 1:5; Matendo 16:1).  Mtoto wa huyu mama ambaye ni Timotheo, anatajwa kuwa karibu sana na Mtume Paulo. Paulo alimwita timotheo mwanaye, na mara nyingi alisema habari za upendo wake kwa Timotheo na jinsi Timotheo alivyojitoa kwake  (1Wakorintho 4:7; Wafilipi 2:19-20; 1Timotheo 1:18).
            Japokuwa, Timotheo alitokana na baba asiyeamini, lakini yeye alitakaswa kwa sababu mama yake alikuwa ameamini. 1Wakorintho 7:14 inasema: “Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu”. Inaonesha ya kwamba, Paulo alifahamiana na Timotheo kwa mara ya kwanza alipotembelea miji ya Galatia ya Listra, Derbe, Antiokia na Ikonio katika safari yake kuu ya kwanza ya kueneza Injili (2Timotheo 3:10-11; Matendo 14:6, 7).

 Euodia
           Jina hili linamaanisha ‘safari ya mafanikio’, ‘safari njema’ au ‘safari salama’ huyu ni mwanamke pamoja na rafiki yake (Sintike) walikuwa wamenuia kumcha Bwana. Na Paulo katika Waraka wake kwa Wafilipi anamsihi Euodia na Sintike wawe na umoja katika Bwana (Wafilipi 4:2). Kule Filipi, mwanamke huyu alikuwa wa kwanza  kuisikia injili pamoja na Lidia mwongofu wa awali.
 Fibi
          Fibi ni mwanamke ambaye alivaa alama ya ukarimu. Anatajwa kuwa alikuwa mhudumu wa kanisa la Kenkrea (Warumi 16:1). Alikuwa ni mmwanamke aliyehitaji matokeo fulani katika Kazi ya Injili. Alijitoa kwa kusafiri safari ndefu kuelekea Rumi kwa matakwa yake na alijitoa kupelekewa watakatifu nyaraka za Paulo.  Umuhimu wake wa kwenda unaoneshwa na ombi la Paulo kwa Warumi, kumsaidia katika mambo yote (Warumi 16:2). Ukiangalia  Matendo 18:18, inaonesha, Paulo alikutana na Fibi kwa mara ya kwanza huko Kenkrea.

 Hawa
           Hawa ni mwanamke wa kwanza kuwa hapa duniani, baada ya Adamu kuumbwa kwanza Hawa alifuatia (1Timotheo 2:13). Jina la Hawa humanisha ‘mwanamke’ kwa sababu alitokana na mwanamume (Mwanzo 2:23). Maana nyingine ya Hawa ni ‘uhai’, ‘atoaye uhai’ au  ‘mama wa wote wenye uhai’. Mwanzo 3:20 inasema “Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai”.  
            Ni Adamu ndiye aliyemwita mkewe jina la Hawa baada ya kutoka katika bustani ya Edeni. Kabla ya  Hawa kuitwa jina hilo, alikuwa ni mwanamke aliyeitwa Adamu pia kama mumewe (Mwanzo 5:2). Hawa ni mwanamke mwenye utofauti mkubwa na wanawake wengine. Upekee wa Hawa unajibainisha katika mambo yafuatayo:
1)      Alikuwa mwanamke wa kwanza kuishi (kuwa) duniani (Mwanzo 2:18, 21-23).
2)      Hawa alikuwa mwanamke mzuri sana (zaidi) kuliko mwanamke aliyewahi kuishi hapa duniani.
3)      Hawa ni mwanamke aliyekuwepo kabla na baada ya dhambi kuingia duniani.
4)      Hawa ni mwanamke wa kwanza kudanganywa na Shetani hapa duniani (Mwanzo 3:1-6; 2Wakorintho 11:3).
5)      Hawa alikuwa mwanamke wa kwanza kutengeneza nguo (Mwanzo 3:7).
6)      Hawa alikuwa mwanamke wa kwanza kuzaa mtoto wa kiume aliyekuja kuwa muuaji (Mwanzo 4:8).
7)      Hawa alikuwa mwanamke wa kwanza kuitwa mke (Mwanzo 2:23; Mwanzo 3:20).
8)      Hawa alikuwa mwanamke wa kwanza kupokea unabii wa Kimbingu kuhusu ukombozi wa mwanadamu katika dhambi (Mwanzo 3:15).
9)      Hawa alikuwa mwanamke wa kwanza kumshawishi mumewe kutenda dhambi (Mwanzo 3:6 ). 
10)  Hawa ni mwanamke anayelaumiwa kwa kumpoteza Adamu kwa kuanguka katika dhambi (1Timotheo 2:14).

            Kupitia kwa Hawa, twaweza jifunza kuwa uhuru wa kibinadamu ni kufanya kitu cho chote tunachokitaka. Lakini Mungu anasema uhuru wa kweli unatokana na kutii na ufahamu wa kipi tusifanye. Lilikuwa kosa kubwa kwa Hawa kutaka kufanana na Mungu, hivyo Hawa alisadikishwa vibaya na Shetani. Kama ilivyo kwa Hawa, nasi tunamatamanio mengi katika malengo yetu, lakini  tunatumia njia zisizo ili kuyafikia matamanio yetu yaliyo kinyume na mapenzi ya Mungu.
           Utukufu binasi hutuongoza katika kumuasi Mungu, punde tu tunapoanza kumuacha Mungu katika mipango yetu, na hivyo tunajiweka sehemu sisi sehemu ya Mungu. Na hiki ndicho hakika Shetani alikihitaji kutoka kwa Hawa. Shetani alijaribu kumuhakikishia Hawa kuwa, dhambi ni nzuri na yakutamanika. Ujuzi ama ufahamu wa kujua mema na mabaya ilionekana si jambo baya kwa Hawa. Mara zote dhambi ni tamu na inapendeza machoni, hivyo tutegemee majaribu mengi ya Shetani yaliyo katika mivuto mizuri na yakupendeza, lakini ipo njia ya kutokea (1Wakorintho 10:13).
            Jaribu la kwanza la dhambi ya Hawa lilianzia machoni, kisha mikono na mdomoni na hatimaye kumshirikisha Adamu. Moja ya uhalisia wa dhambi ni kuwa, madhara yake husambaa. Na mara zote tunapofanya dhambi huwa tunajaribu kuwahusisha na wengine, ili tupunguze ukubwa wa hatia ya dhambi. Kama ilivyo sumu iliyowekwa kwenye mto, dhambi nayo huenea kwa haraka. Itambue dhambi kisha utubu kabla haijaenea kwa wengine. Ilimpasa Hawa akimbie katika yote yaliyosababisha mawazo mabaya ya kuitamani dhambi (2Timotheo 2:22).

 Gomeri
            Mwanamke huyu anatajwa katika kipindi cha huduma ya nabii Hosea (miaka 750 K.K).  Ni mwanake ajulikanaye kama ‘mwanake wa uzinzi’. Mungu alimwagiza nabii Hosea akamuoe mwanamke huyu wa uzinzi aitwaye Gomeri binti Diblaimu, na mwenye watoto wa uzinzi kama kielezo cha namna taifa la Isaraeli lilivyokuwa likifanya uzinzi wa kiroho (Hosea 1:2-3). Mwanamke huyu alikuja akamzalia Hosea watoto wawili (wa kiume na wa kike) waitwao Yezreeli na Lo-ruhama (Hosea 1:5-6).
            Kwa kuwa Agano kati ya Israeli na Yahweh (Yehova) lilikuwa sawa sawa na agano la ndoa, kushirikiana kwa Waisraeli na miungu mingine kulikuwa ni zinaa au uzinzi wa kiroho (Hosea 4:17; 5:4; 6:10; 7:16; 8:5-6). Kama kielelezo, Hosea aliona mfano hai kwa mke wake mwenyewe, Gomeri alipomwacha na kufuata wapenzi wengine. Hivyo Gomeri alikuwa kahaba (Hosea 1:2; 2:2). Kama jinsi Mungu ambavyo hakuacha kuwapenda Israeli, ndivyo hivyo Hosea hakuacha kumpenda mkewe aliyekosa, tena alimkomboa kutoka utumwani  (Hosea 3:1-3).
            Kama vile Gomeri, hata Israeli haikuwa na uaminifu kwa mumewe, Mungu (Hosea 2:2-23). Agano la Hosea la upendo wake kwa Gomeri lilitoa mfano wa Agano la upendo wa Mungu kwa watu wake. Kama gomeri kwa Hosea, na wao pia Israeli wangepelekwa kifungoni, lakini baada ya kusafishwa na ushirika wao wa zinaa na miungu ya Kikanaani, wangerudishwa na kuishi katika nchi yao tena (Hosea 2:17-20;3:4-5; 14:4-7).

 Hadasa
            Hadasa lilikuwa jina la Kiyahudi alilopewa Esta. Kama tulivyoona awali, Esta ambaye ni Hadasa alikuwa jamaa wa kabila la Benyamini na alitokana na familia iliyokuwa imechukuliwa mateka kwenda Babeli au Uajemi. Alikuwa binti wa Abihaili aliyeishi Shushani, mji mkuu wa Uajemi. Baada ya wazazi wake kufariki, Esta alibakia chini ya malezi na uangalizi wa Mordekai (Esta 2:6-7), aliyekuwa afisa katika Ikulu ya Ahasuero. Kwa habari zaidi zinazomhusu Hadasa, angalia kipengele kinachomzungumzia Esta.



 Hajiri
             Hajiri ni mwanamke aliyeishiwa maji kwenye chupa lakini akapata kisima cha maji. Habari za mwanamke huyu zinapatikana katika Mwanzo 16; Mwanzo 21:9-17; Mwanzo 25:12 na Wagalatia 4:24, 25. Jina la mwanamke huyu linatokana na lugha ya Kimisiri na kwa kiasi kidogo linataka kufanana na Lugha ya Kiarabu, hasa katika mzizi wa neno. Maana ya jina hili ni ‘pambana’, au jina hili laweza manisha pia  ‘aliyehamia’ au ‘mkimbizi’.
           Hajiri alikuwaa mjakazi wa Sara mkewe Ibrahimu mwenye asili ya Misri. Biblia ipo kimya juu ya familia yake na hakuna kumbukumbu ya familia au uzao aliotokea. Kunawakati Ibrahimu alihamia Misri kwa ajili ya kwenda kutafuta malisho ya mifugo yake, baada ya ukame kutokea Kanaani. Lakini mfalme wa Misri alimwona Ibrahimu ni mdanganyifu, na hivyo, alilazimishwa kuhama kutoka Misri kwa aibu (Mwanzo 12:10, 20; 13:1). Hivyo basi, yawezakuwa  Hajiri aliambatana na familia ya Ibrahimu kutoka huko Misri.
          Kutokana na Sara kukata tamaa ya kupata mtoto, alimshawishi Mumewe, Ibrahimu amjue Hajiri ili amzalie mtoto. Hajiri alimzailia Ibrahimu mtoto wa Kiume aliyeitwa Ishmaeli (Mwanzo 16:16; 25:12). Hajiri  pamoja na mwanaye walifukuzwa  kutoka katika familia ya Ibrahimu kwa sababu ya Ishmaeli alimzihaki Isaka katika karamu yake ya kuachishwa kunyonya  (Mwanzo 21:9-21).

 Hagithi
             Maana ya jina hili ni ‘sikukuu’, ‘sherehe’, ‘tamasha’, ‘mcheza dansi’ au ‘mcheza mziki’. Uhusika wa mwanamke huyu kwenye Biblia ni kwa kuwa mke wa tano wa Daudi  na mama wa  Adonia (2Samweli 3:4; 1Nyakati 3:2). Adonia mwana wa Hagithi alijiinua juu ili awe mfalme badala ya Baba yake alipokuwa katika hatua za mwisho za uzee katika ufalme wake. Alikuwa akiungwa mkono na amiri jeshi mkuu, Yoabu na kuhani mkuu, Abiathari (1Wafalme 1:5-7). Lakini Mungu alikuwa amemuonesha Daudi kwamba Sulemani awe mrithi wa kiti chake cha ufalme (1Nyakati 28:5), naye Sulemani aliungwa mkono na akida wa usalama wa mfalme, Benaya, kuhani mkuu mwingine, Sadoki, na nabii Nathani (1Wafalme 1:8).

 Hamolekethi
            Hili ni jina lefu  ni la mwanamke anayepatikana katika uzao wa Manase. Maana ya jina hili ni ‘malkia’ au ‘mtawala’. Mwanamke huyu alikuwa binti wa Makiri, dada wa Gileadi, mjukuu wa Manase na mama wa Ish-hodu, Abiezeri na Mala (1Nyakati 7:17-18). Kupitia kwa mwanamke huyu ndiko ulikotokea uzao wa Gidioni na Mala.

 Hamutali
           Mwanamke huyu alikuwa binti wa Yeremia wa Libna na mke wa mfalme na mama wa watoto wawili wa kiume ambao hawakumcha Bwana (Yeremia 52:1-2; 2Wafalme 23:31; 2Wafalme 24:18). Watoto wake hao ni Yehoahaki na Matania au Sedekia. Yaweza kuwa, ubovu wa tabia ya watoto hawa inasadikisha ushawishi wa mama huyu. Yeremia hakumtambua Sedekia kwa sababu ya uovu wake.  
 Hana
          Huyu ni mwanamke aliyesimama na kuwa mfano wa mama bora kwa kumtoa mwanaye kwa ajili ya kumtumikia Mungu. Ingawa Hana alikuwa mmoja wa wake wawili wa Elikana, lakini Hana alikuwa mke kipenzi wa Elika. Maana ya jina hili la Kiebrania humanisha ‘fadhili’, ‘neema’, ‘upendeleo’ au  ‘rehema’. Hana aliishi katika nyumba yenye huzuni na mafarakano yaliyosababishwa na mke mwenza. Mke mwingine wa Elikana aitwaye Penina, alikuwa akimdhihaki Hana kwa sababu hakuweza kupata watoto (1Samweli 1:2-8).
          Hana aliamini kuwa maneno yake katika maombi yangepata kibali machoni pa Mungu sawa sawa na Zaburi 19:14. Hivyo, Hana hakuchoka kumlilia Mungu ili apate mtoto, na aliweka nadhiri kuwa, kama Mungu angelimjibu ombi lake, yeye na Hana wangelimtoa mtoto huyo kwa ajili ya kumtumikia Mungu maisha yake yote. Mungu alimpatia mwana wa kiume naye alimwita Samweli (1Samweli  1:9-20). Samweli alipofikisha umri wa miaka kati ya miwili au mitatu, Hana alimpeleka katika hema la kukutania akamkabidhi kwa Mungu katika maisha yake yote.
            Sehemu ya shukrani ya sala yake Hana kwa Mungu zinaonekana pia katika sala ya shukrani ya Mariamu mama yake Yesu (linganisha 1Samweli 2:1-10 na Luka 1:46:-55).  Hana alimkabidhi Samweli kwa kuhani Eli aliyepaswa kumlea na kumfundisha ili awe mtumishi wa Mungu. Hana alimtembelea Samweli kila mwaka kwa ajili ya kumsalimia na kumpatia mahitaji yake (1Samweli 2:11, 18-20). Baada ya kumzaa Samweli, Hana alizaa watoto watano wengine (1Samweli 2:21).
            Hana anaonekana kuwa ni mwanamke ambaye si mlalamishi kitabia. Japokuwa huzuni yake ilisababishwa na kutopata mtoto, lakini mumewe alikuwa akimjali na kumfariji. Hana pia hakuwa mwanamke aliyeishi bila maombi, maumivu yake pia yalimfanya kuwa mtumwa katika maombi. Wimbo wake wa kusifu ama kutoa shukrani kwa Mungu unampambanua Hana kama mtunzi wa mashairi na nabii (1Samweli 2:1-10; Luka 1:46:-55). Hana alikuwa na roho ya kujitoa kwani alimtoa mwanaye kwa ajili ya kumtumikia Mungu.

 Haselelponi
            Mwanamke huyu alikuwa binti wa baba yake Etamu na dada wa Yezreeli, Ishma,  na Idbashi (1Nyakati 4:3). Maana ya jina la mwanamke huyu ni ‘niokoe Mugu wangu unayenijali’ au ‘niponye Mungu unayenijali’. Jina la mwanamke huyu limeundwa na maneno kama “El” likimanisha ‘Mungu’ na “zelel” sawa na‘kivuri’.

 Hela
            Mwanamke huyu alikuwa miongoni mwa wake wawili wa Ashuri, babaye Tekoa. Ashuri, mumewe Hela alikuwa mkuu wa familia katika kabila ya Yuda. Hela alimzalia Ashuri wana watatu waitwao Serethi, Ishari, na Ethnani (1Nyakati 4:5-7). Maana jina hili ni ‘uonjwa’, ‘mgonjwa’ au ‘kichefuchefu’.

 Hefziba
            Mwanamke huyu alikuwa mama wa Manase aliyekuja kuwa mfalme wa Yuda. Manase ambaye alikuwa mtoto wa Hezekia, alitawala kwa miaka hamsini na tano, kisha akafanya mabaya machoni pa Bwana (2Wafalme 21:1). Kama Isaya 62:4 inavyolitaja jina hili la Hefziba au Hefsiba, hivyo jina hili humanisha ‘Namfrahia’  au ‘Anipendezaye yupo nami’.

 Herodia
            Herodia alikuwa binti wa Aristobulo, mtoto wa kiume wa Herode Mkuu na Mariamme binti wa Mhasimonea, aliyekuwa Myahudi. Huyu ni mwanamke aliyesababisha kukamatwa na kuuwawa kwa Yohana Mbatizaji. Kwa chuki zake, Herodia alimshawishi binti yake (Salome) aombe zawadi ya kichwa cha Yohana Mbatizaji kutoka kwa baba yake, Herode Antipa  (Mathayo 14:3-12; Marko 6:14-24).
           Sababu ya Herodia kumchukia Yohana Mbatizaji ni kwa sababu Yohana Mbatizaji alikemea dhambi ya kuolewa na ndugu wa mumewe wa kwanza (Luka 3:19, 20) wakati hakuchukua wala kupewa talaka. Mume wake wa kwanza alikuwa Filipo wa kwanza, mtoto wa Herode Mkuu na Mariamme; hivyo, aliolewa na mjomba wake na binti yao ailiitwa Salome ambaye mama yake alimtumia ili kumuangamiza Yohana Mbatizaji (Marko 6:14-29).
            Kwa ufupi, wakati ambapo Herode Antipa alipotembelea Rumi, alivutiwa na Filipo na Herodia, Herode Antipa alimchukua na kumuoa mke wa ndugu yake. Mke wake aliyekuwa mtoto wa mfalme wa Uarabuni, alikuwa kikwazo kwa ndoa iliyokuwa haramu, hivyo alimpa talaka na Herodia kuolewa (na kuwa malkia) badala yake;  na baadaye binti yake (Salome) aliletwa Ikulu.
            Kisa cha Herodia na Yohana Mbatizaji ni sawa na kile cha Yezebeli kwa Eliya, kwa sababu Yezebeli na Herodia (wote) walifanikisha mauaji ya manabii wa Mungu.

 Hodeshi
            Hili ni jina la mwanamke aliyekuwa mke wa mmoja wa shina la Benyamini. Alikuwa mke wa Shaharaimu huko Bara-Moabu na aliolewa baada ya Shaharaimu kuwafukuza wakeze, Hushimu na Baara. Hodeshi alimzalia mumewe watoto (1Nyakati 8:8, 9).

 Hodia
            Mwanamke huyu alikuwa dada wa Nahamu na mke wa Meredi kati ya wake wawili, Yehodia au Myahudi na Bithia (1Nyakati 4:18, 19). Tafsiri zingine za Biblia huonesha kuwa, Hodia alikuwa mwanamume aliyemuoa dada wa Nahamu, lakini Nehemia 10:18 inaondoa utata wa jina na jinsia yake maana ni Hodia wawili tofauti. Kama wanavyodai wanazuoni wengine kuwa Hodia ndiye Yehudia. Hivyo Hodia huyu atakuwa ni mama wa watoto watatu wa kiume, Yeredi, Heberi na Yekuthieli. Jina hili la Hodia humanisha ‘uzuri wa Yehova’.

 Hogla
            Hili ni jina la mtoto wa tatu kati ya watoto watano waliozaliwa kwa Selofehadi kutoka kabila ya Manase. Ni miongoni mwa watoto watano wa kike waliodai haki ya kupatiwa urithi wa baba yao (maana baba yao hakuwa na mtoto wa kiume). Watoto hawa wa mzee Selofehadi walifanikisha kuipata haki yao ila kwa sharti la kuolewa na wanaume kutoka kabila lao na si kabila lingine katika Israeli (Hesabu 26:33; Hesabu 27:1-11; Hesabu 36:1-12; Yoshua 17:3).  

 Hulda
            Huyu ni mwanamke aliyeliokoa taifa na mabaya ambayo yangetokea hapo baadae. Jina hili la Hulda linatambulisha ‘mnyama mdogo kama kicheche’. Hulda alikuwa nabii mke kipindi cha mfalme Yosia na alikuwa mke wa  Shalumu. Wakati Kuhani Hilkia alipokipata kitabu cha sheria katika Hekalu, alimshirikisha mfalme Yosia, naye mfamle alikituma kwa Hulda nabii.
            Ujumbe wake Hulda wa kinabii kwa taifa, ulikuwa ni msisitizo wa kuzisoma sheria na kuzishika sheria za Mungu ili kuleta matengenezo na uamsho wa kiroho. Hivyo,  mfalme Yosia aliyapokea maelekezo ya nabii Hulda na alisimamia katika kuamsha maisha ya kiroho  na watu wote waliapa na kufuata mapenzi ya Mungu na kuwa waaminifu  katika sheria za Mungu. Tazama 2Wafalme 22:14-20 na 2Nyakati 34:22-33.

 Hushimu
           Maana ya jina la Hushimu ni ‘kuharakisha’ au ‘mtoto njiti’. Hushimu alikuwa mwanamke wa Kimoabu na alikuwa miongoni mwa wake wawili wa Shaharaimu, Mbenyamini ambaye alienda kuishi Moabu. Kabla hajaachika, alimzali mumewe watoto wawili wa kiume (1Nyakati 8:8, 11). Hushimu pia ni jina la kiume (tazama 1Nyakati 7:12).

 Iska
            Maana ya jina hili ni ‘yeye atatafuta’ au ‘yeye atatazama’. Hili ni jina linalomhusu binti wa Harani, mdogo wake na Ibrahimu. “............... na mkewe Nahori aliitwa Milka, binti Harani, ambaye alikuwa baba wa Milka na wa Iska” (Mwanzo 11:29).

 Kandake
           Maana ya jina hili ni ‘Malkia’ au ‘mtawala’. “.........; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; .....” (Matendo ya Mitume 8:27). Jina lake halisi la mwanamke huyu wa Kiethiopia (Kikushi) halikutolewa na Luka, maana Kandake lilikuwa jina la kiutawala au cheo na sio jina binafsi. Jina hili lilitumika kwa miaka mingi kwa malkia wote wa Kushi kama ilivyokuwa kwa jina la Farao kwa nchi ya Misri lilotolewa kwa Wafalme katika Misri ya zamani ama Kaisari kwa tawala ya Kirumi.

 Keren-hapuhu
            Hili ni jina la mtoto wa mwisho wa kike wa Mzee Ayubu baada ya wale binti watatu wa awali kufariki (Ayubu 1:2;  Ayubu 42:14). Jina hili linamanisha ‘mzuri sana’ au ‘pembe la rangi’; hivyo, jina la mwanamke huyu linaelezea ‘boksi la rangi’ ambalo lililokuwa  chombo kilichokuwa na kimiminika kilichotengenezwa au kutiwa katika pembe.

 Ketura
            Mwanamke huyu aliolewa na Mzee Ibrahimu baada ya mkewe kipenzi aitwaye Sara kufariki (Mwanzo 25:1-6). Sababu ya Ibrahimu kuoa tena imeelezewa katika 1Nyakati 1:32, 33. Maana ya jina hili ni ‘ubani’ au ‘udi’. Jina hili pia, ni sawa na ‘Kezia’, jina linaloelezea manukato. Mwanamke huyu alimzalia Ibrahimu watoto sita wa kiume, ambao ni Zimrani, Yokshani, Medani, Midiani, Ishbaki na Shua. Watoto hawa sita wa Ibrahimu ndiyo chanzo cha makabila sita ya Kiarabu yapatikanayo upande wa Kaskazini na Mashariki mwa Palestina.

 Kezia
           Jina la mwanamke huyu linapatikana katika Ayubu 42:14, likimanisha “cassia”. Kezia ni mtoto wa pili wa Ayubu (baada ya ya matatizo kupita) ambaye jina lake  linamanisha pia manukato sawa na ‘manemane’ au ‘udi’ (tazama Zaburi 45:8). Jina hili huelezea pia uzuri wake mwanake huyu.

 Kloe
            Mwanamke huyu anatajwa na Mtume Paulo katika waraka wake wa kwanza kwa Wakoritho (1Wakorintho 1:10-11). Maana ya jina hili ni ‘mti wa kijani’. Mti wa kijani katika lugha ya Kiyunani humanisha ‘sehemu ya kwanza ya kijani ya chipuo la mti’. Biblia haijasema cho chote juu ya mwanamke huyu wa Korintho kuhusu historia yake, isipokuwa inaonesha kuwa ni mlezi (matron) na kiongozi katika familia ya Kikristo.

 Klaudia
            Mwanamke huyu anayetajwa na Mtume paulo katika 2Timotheo 4:2 alikuwa anatokea familia maarufu huko Rumi. Maana ya jina hili ni ‘kilema’. Alikuwa miongoni mwa wanawake wanaoheshimika sana kutoka katika watu wa mataifa aliyeiamini Injili na kuongoka. Mwanamke huyu anaonekana kuwa na ukaribu na Mtume Paulo maana amemtaja katika salamu pamoja na washiriki wengine kupitia barua ya pili kwa Timotheo.

 Kozbi
           Jina la mwanamke huyu limetokana na lugha ya Kiebrania liloendana na tabia. Jina hili limetokana na neno “cazab” lenye maana ya ‘mdaganyifu’ au ‘udanganyifu’. Baadhi ya wanazuoni wa Biblia hudai kuwa jina hili aliitwa mwanamke huyu kwa sababu tu alizaliwa yeye badala ya mtoto wa kiume kama lilivyokuwa talajio la wazazi wake. Mwanamke au binti huyu alikuwa Mmidiani, binti wa Zuri, kiongozi katika familia iliyokuwa Midiani.
            Kwa sababu ya madhara ya uasherati, mwanamke huyu aliuawa pamoja na hawala yake (Muisraeli) aitwaye Zimri, mwana wa Salu, mkuu wa nyumba ya baba yake katika kabila ya Simeoni. (soma Heasbu 25:6-18). Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani ndiye aliyemuua Kozba na Zimri na kufanya hivyo, aliwaepushia Israeli na hasira ya Mungu ya kuwaangamiza (Hesabu 25:7-8; Zaburi 106:30-31). Lakini kabla ya hapo, Mungu alikuwa ameshaangamiza Waisraeli zaidi ya elfu ishirini na tatu (Hesabu 25:9; 1Wakorintho 10:8).
            Baalamu alitumia wanawake wa kigeni (akiwemo na Kozbi) ili kuwakosesha wanaume wa Israeli, na baada ya muda mfupi uasherati na ibada ya sanamu vilienea katika kambi ya Waisraeli. Mungu alipotuma maafa yaliyo waangamiza Waisraeli kwa maelfu, Baalamu bila shaka  alifikiri  kwamba maarifa yake yalisaidia, lakini ushujaa wa kuhani wa Israeli, Finehasi, uliiokoa Israeli na kuleta mauti juu ya Balaamu (Hesabu 25:1-9; Hesabu 31:16; Yoshua 13:22).

Lea
            Huyu ni mwanamke aliyekosa upendo kwa mumewe, lakini alikuwa mwaminifu. Yeye na mdogo wake waliolewa na mwanamume mmoja. Mwanzo sura ya 29 na 30 zinaelezea kuhusu Lea na Raheli. Hakuna maana ya moja kwa moja ya jina hili, ispokuwa baadhi ya wanazuoni wa Biblia hutoa maana ya Lea kuwa ni ‘aliyezimia kutokana na ugonjwa’, ‘aliyeolewa’ au ‘binti mkubwa katika familia’. Tafsiri nyingi za Biblia zinabainisha kuwa, Lea alikuwa na‘makengeza’ (Mwanzo 29:17).
            Lea alikuwa binti mkubwa wa Labani (mjomba wake na Yakobo) ambaye kwa udanganyifu, aliozeshwa kwa Yakobo na kumzalia watoto sita. Na kwa mjakazi wake aitwaye Zilpa, Lea alijiongezea watoto wawili wa kiume katika familia yake.
            Hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kama Lea alihusika katika udanganyifu wa baba yake ili aweze kuolewa na Yakobo kwanza badala ya mdogo wake aitwaye Raheli aliyekuwa mzuri kuliko yeye. Japokuwa alijua kuwa moyo wa mumewe ulimpenda sana mdogo wake, Lea alidumu kumpenda na kuwa mtiifu kwa mumewe mpaka alipomzika.
            Wakati ambapo Yakobo alikuwa amechanganyikiwa na uzuri wa Raheli, na kumpenda, hakuna panapoonesha naye Raheli alimpenda vilevile Yakobo. Raheli alikuwa na tabia ya ukali, wivu, mgomvi na mkaidi. Na nguvu ya chuki yake aliielekeza kwa dada yake (Lea).
            Watoto wake sita wa wa kiume ambao miongoni mwao waliunda kabila na taifa la Israeli: Reubeni wa kwanza, Simeoni wa pili, Lawi wa tatu, Yuda wa nne, Isakari wa tano, Zabloni wa sita na wa saba mtoto wa kike aitwaye Dina. Pamoja na tofauti zao, Lea na Raheli, wote kwa pamoja waliijenga nyumba ya Israeli  kupitia uzao wao (Ruthu 4:11).
          Mtoto wa kwanza wa Lea aitwaye Reubeni, alimkosea baba yake (Yakobo) kwa kulala na Zilpa ambaye alikuwa suria wa (sawa na mke) wa baba yake (Mwanzo 49:3). Reubeni alitenda kinyume na Kumbukumbu la Torati 27:20 inayosema: “Na alaaniwe alalaye na mke wa baba yake, kwa kuwa amefunua mavazi ya baba yake...”.  Kwa kosa hili, Reubeni aliondolewa katika orodha ya makabila kumi na mbili ya taifa la Israeli, badala yake waliwekwa watoto wawili wa Yusufu (1Nyakati 5:1). Hivyo basi, katika makabila kumi na mbili ya Isaraeli, Reubeni na Yusufu hawamo, maana nafasi zao walipewa wale watoto wawili wa Yusufu.

            Jambo la kujifunza hapa ni kuwa: Uchaguzi wa mwenzi usiangalie uzuri tu wa nje. Raheli alikuwa mzuri wa sura kuliko dada yake aliyekuwa mke mwenza kwa Yakobo, lakini Lea ndiye aliye mzaa Yuda na kupitia yeye katika uzao wake akazaliwa Masihi Yesu Kristo. Kutovutia kwake Lea kulisababisha kutopendwa sana na mumewe, lakini Mungu alivutiwa naye, labda kwa sababu ya uzuri wake wa ndani.
            Nyuma ya sura mbaya, kuna upendo mkuu unaozalishwa. Lakini Mungu haangalii juu ya uzuri na muonekano wa nje, ispokuwa ule uliopo katika moyo. Kuna aina mbili za uzuri: Upo uzuri ambao Mungu huutoa kwa kuzaliwa kwa mtu na huu hunyauka kama ua. Na upo uzuri ambao Mungu huutoa wakati ambapo kwa neema Yake wanadamu huzaliwa upya, na uzuri huu haupotei kamwe bali hustawi milele.

 Loisi
            Huyu alikuwa ni mwanamke wa kiyahudi ambaye alimfundisha binti yake na mjukuu wake wa kiume Maadiko Matakatifu katika agano la kale. Katika 2Tomotheo 1:5, Loisi ambaye ni  bibi yake na Timotheo na mama wa Eunike, anarejelewa na Mtume Paulo kwamba alikuwa mwanamke mwenye imani aliyoipanda kwa mtoto na mjukuu wake. Maana ya jina hili ni ‘inayokubarika’, ‘inayotamanika’ au ‘inayotarajika’.
            Familia yake iliishi Listra na kwa hakika yawezakuwa Paulo alitembelea huko, na katika kutembelea huko alifurahia kuwaongoza watu kwa Kristo...... akiwemo Loisi, Eunike na Timotheo (Matendo 14:6, 7; Matendo 16:1), hivyo Paulo akaandika juu ya imani yake imara izaayo matunda kwa watu wengine, ikianzia katika familia yake.
            Hakuna kumbukumbu yo yote ambayo inaelezea kuhusu baba wa Timotheo, ispokuwa anafahamika tu kuwa alikuwa mmataifa. Hivyo, mzazi mcha Mungu anaweza akamshawishi mtoto asiyemcha Mungu kumfuata Kristo (1Wakorintho 7:14; 2Timotheo 3:15). Paulo alijikita katika imani ya mama na bibi pekee katika maelekezo ya kiroho kwa Timotheo aliyekuja kuwa mtoto wake wa kiroho.

 Lo-ruhama
           Huyu mwanake alikuwa binti wa Hosea nabii kutoka kwa mkewe aitwaye Gomeri (Hosea 1:6, 8). Maana ya jina la mwanamke huyu ni ‘asiyehurumiwa’ au ‘asiyetia huruma’. Jina la mwanamke huyu, kipicha lilihusika na Israeli ambapo Mungu alikuwa ameondoa upendo wake kwa sababu ya uzinzi wao wa kiroho  (Hosea 2:1, 23; Warumi 9:25). 

 Lidia
           Lidia ni mwanamke katika agano jipya aliyekuwa mwenye bidii na juhudi katika biashara. Yeye na familia yake walikuwa wenyeji wa Thiatira, sehemu iliyokuwa koloni la Makedonia na alikuwa akifanya biashara ya kuuza raingi ya zambarau (Matendo 16:14). Kwa habari na sifa zinazomhusu Lidia, tazama Matendo 16:12-15, 40. Maana ya jina  hili ni ‘kupinda’ au ‘kuinama’. Mwanamke huyu alikuwa Myahudi maana alimwabudu Mungu wa Mbinguni.
           Kama tunavyofahamu kuwa, wafanya biashara huwa hawana muda na mambo ya dini, lakini Lidia alipata muda wa kufanya ibada katika imani yake ya Kiyahudi. Japokuwa, hakuwa Mkristo, alikuwa na shauku kubwa ya kuwa na uzoefu wa mambo ya kiroho.  Kutokuwa na uelewa, Lidia alijihudhulisha katika mikutano ya Paulo alipokuwa akifanya mdahalo katika mkusanyiko wa Wayahudi.
            Nuru aliyokuwa akiinena Paulo ilimgusa na moyo wake ulifunguka tayari kumpokea Yesu kama Mwokozi wake. Hivyo, imani ya Lidia ilitokana na kusikia ama kusikiliza neno la Mungu sawa na ilivyonenwa katika Zaburi 119:18, 130 na Luka 24:45. Kuongoka kwake kulikuwa kwa kukili hadharani, na wale wa nyumbani kwake aliwashuhudia jinsi alivyosikia na kilichotokea, na wanafamilia nao waliamini na kubatizwa na kuwa wanafunzi wa Mwokozi.
            Inasadikiwa kuwa Lidia huyu alikuwa mtu wa kwanza wa Ulaya aliyeongoka ili kumfuata Yesu Kristo wakati wa upelekwaji wa Injili wa Mtume Paulo. Biashara yake ilidumu kuwa salama, na Yesu alikuwa katika biashara yake, kwani kupitia biashara aliwasaidia watumishi wa Mungu katika kazi ya injili (Matendo 16:40). Pamoja na kuwa mfanyabiashara, Lidia alihudumu kwa ajili ya Bwana. Alidumu kuwa katika biashara yake huku akisaidia huduma ya Mungu katika Injili. Ukiwaondoa Paulo na Sila, Lidia alihudumia wengine wengi.
            Lidia alikuwa mkarimu, maana aliwapokea Paulo na Sila katika nyumba yake punde tu au baada ya kuachiliwa huru toka gerezani. Hakuona haya kuwapokea wafungwa, waliokuwa wakimtumikia Bwana kwani alikuwa akitimiza maandiko katia 1Timotheo 5:10; Waebrania 13:2; 1Petro 4:9. Baadhi ya wanazuoni hudhani pia, kati ya Euodia au Sintike aliyetajwa katika Wafilipi 4:2  ndiye Lidia. Na kama ndiyo hivyo, basi Lidia pia ni miongoni mwa wanawake waliofanya kazi pamoja na Paulo (Wafilipi 4:3).

 Maaka
           Maana ya jina hili ‘gandamiza’ au ‘dhulumu’. Jina hili liliitwa kama kidhihirisho cha mji mmojawapo wa Mesopotamia (1Nyakati 19:6-7; 2Samweli 10:8). Jina hili limetumika kama jina la mahali (2Samweli 10:6), na limetumika kwa wanaume pia (1Wafalme 2:39; 1Nyakati 11:43 na 1Nyakati 27:16). Wafuatao pia ni watu waliotumia jina la Maaka katika Biblia:
a)      Maaka mtoto wa kiume wa Nahori kwa suria wake aitwaye Reuma (Mwanzo 22:24).
b)      Maaka, mwanamke aliyekuwa suria  wa Kalebu, mtoto wa Hezroni (1Nyakati 2:48)
c)      Maaka, mwanamke kutoka kabila ya Benyamini aliyekuwa mke wa Makiri kutoka kabila ya Manase aliyekuwa baba wa Gileadi. Hivyo Maaka huyu alikuwa  mkwe wa Manase, kijana wa Yusufu. Maaka huyu alimzali Makili Pereshi na Shereshi (1Nyakati 7:12, 15, 16).
d)     Maaka, mke wa Yeieli, baba wa Gibeoni na mzao wa mfalme Sauli (1Nyakati 8:29; 1Nyakati 9:35).
e)      Maaka, binti wa Talmai, mfalme wa Geshuri. Maka huyu alichukuliwa vitani na Daudi na kuwa miongoni mwa wakeze nane na mama wa Absalomu (1Nyakati 3:2; 2Samweli 3:3).
f)       Maaka, mama wa Yeroboamu, binti au mjukuu wa  Absalomu. Mwanamke huyu alikuwa mjukuu wa Absalumu maana Absalomu alikuwa na binti mmoja tu, aitwaye Tamari ambaye aliolewa na Urieli wa Gibea (2Nyakati 13:2; 1Wafalme 15:1, 2; 2Nyakati 11:20-22).
g)      Maaka, binti wa  Absalomu mama wa Asa mfalme wa Yuda ambaye alifuata nyayo za  Daudi na kuonekana mwema mbele za Bwana (1Wafalme 15:9-13; 2Nyakati 15:16).

 Mahalathi
           Maana ya jina Mahalathi humanisha ‘ugonjwa’. Jina hili pia lilihusiana na huzuni, mashaka, uoga na wasiwasi (tazama Zaburi 53 baina ya Zaburi 88). Jina hili katika Biblia limetumika kwa wanawake zaidi ya mmoja kama ifuatavyo:
a)      Mahalathi, binti wa Ishimaeli, mtoto wa Hajiri na Ibrahimu. Alikuwa dada wa Nebayothi. Mwanamke huyu aliolewa na Esau na kuwa mke wa tatu (Mwanzo 28:9).
b)      Mahalathi, binti Yerimothi mwana wa Daudi. Alikuwa mke wa kwanza katika wale wake kumi na wanane wa mfalme Rehoboamu, mwana wa Sulemani au mjukuu wa Daudi (2Nyakati 11:18), ambaye pia alikuwa na Masuria sitini (2Nyakati 11:20). Ukifuatilia, utagundua Mahalathi na Rehoboamu ni ndugu waliokuja kuoana.

Mala
            Jina hili limetumiwa na wanawake zaidi ya mmoja katika Biblia na linamanisha ‘ambaye ni sawa na Yehova’. Baadhi ya wanazuoni wa Biblia hudai kuwa jina la Mala ni sawa na Mahalathi. Sanjali na kutofautiana maana kwa majina hayo mawili, wanazuoni wengine wa Biblia hupinga hoja hiyo maana muundo wa maneno katika majina hayo yanatofautiana. Mfano, muundo wa wa maneno matika jina la Mala ni Mah-lah na Mahalathi ni Ma-hala-th.Wafuatao ni baathi ya wanawake wanaotajwa kwa jina la Mala katika Biblia: 
(a)    Mala, mmoja kati ya binti za Selofehadi (Hesabu 26:33; Hesabu 36:11na Yoshua 17:3). Alikuwa miongoni mwa mabinti wa Selofehadi waliodai urithi wa ardhi wa baba yao katika nchi ya ahadi maana baba yao alifariki bila mtoto wa kiume (Hesabu 27:1-8).
(b)   Mala, binti wa Hamolekethi, dada wa Makiri na amepambanuliwa kama mjukuu wa Manase, mtoto wa  Yusufu (1Nyakati 7:17-18).

 Mara
            Ukirejea Kutoka 15:23, juu ya yale maji machungu, ambayo wana wa Israeli waliyaita mara, wakimanisha maji yale yalikuwa ni machungu, hivyo utagundua kuwa neno au jina hili la Mara linamanisha ‘uchungu’. Wakati Naomi akitoka Moabu na kufika Bethlehemu, alichagua jina  la Mara, kwa sababu Mungu alimtendea mambo machungu sana (Ruthu 1:20). Alijihisi kuwa, itakuwa sahihi kwake yeye akiitwa jina hili, maana alikuwa na hali mbaya ya kusikitisha. Kwa maana wakati alipokuwa Moabu, alifiwa na mumewe pamoja na watoto wake wawili wa kiume. Wakati wa kurejea Bethlehemu, alirudi akiwa na Ruthu pekee, mkwe wake badala ya kurudi kama alivyoondoka, akiwa yeye, mumewe na watoto wake. Kwa maelezo zaidi, tazama katika kipengele cha jina la Naomi.

 Mariamu Mama wa Yesu
            Wapo wanawake sita katika Agano Jipya waliotumia jina la Mariamu. Tofauti na Mariamu mama yake Yesu baadhi yao walikuwa mama yake Yohana Marko (Matendo 12:12), mwanamke mmoja wa kanisa la Rumi (Warumi 16:6) na mke wa Klopa ambaye pia ni mama wa wana wawili, yaani Yakobo na Yusufu (Mathayo 27:56; Marko 15:40, 47; Marko 16:1; Yohana 19:25). Jina hili linatokana na lugha ya Kiyunani sawa na Miriamu kwa lugha ya Kiebrania. Maana ya jina hili ni ‘uchungu’ (hasa utokanao na changamoto, huzuni ama maumivu).
            Mariamu mama wa Yesu, huyu ni mwanamke katika agano jipya aliyeheshimika kuliko wanawake wote. Yeye alibarikiwa kuliko wanawake wote, kwa sababu Mungu alimchagua awe mama yake Masihi (Luka 1:28, 32, 42-43). Habari zake zimezungumziwa sana katika Mathayo sura ya 1 na 2; Luka sura ya 1 na 2; Yohana 2:1-11; Yohana 19:25; Matendo 1:14. Mwanamke huyu alikuwa wa kabila ya Yuda katika uzao wa Mfalme Daudi. Aliolewa na Yusufu mtoto wa Heli kutoka katika kabila ya Yuda pia (Luka 3:23; Luka 2:7).  
            Aliishi mji wa Nazareti ya Galilaya, ambapo alichumbiwa ili aolewe na seremala wa huko aliyeitwa Yusufu. Mungu alimdhihirishia Mariamu kwamba, ingawa alikuwa bikra, angepata mimba kwa uwezo wa uumbaji wa Roho Mtakatifu moja kwa moja. Tofauti na kuchaguliwa na Mungu, namna ya ubebaji wa mimba kwa mwanamke huyu, ndiko kulikomfanya kuwa mwanamke wa pekee kabisa. Hivyo, Masihi ambaye angezaliwa kupitia mwanamke huyu angekuwa mwanadamu kamili, pia angekuwa mwana wa Mungu (Luka 1:30-35).
            Baada ya kupashwa habari za kuwa atabeba ujauzito wa Mwokozi, Mariamu alikubali mapenzi ya Mungu juu yake pasipo hoja wala ubishi (Luka 1:38). Alimsifu Mungu kwa kuwa alimchagua yeye, akiwa ni mwanamke wa kawaida tu aliyetoka katika familia (nyumba) ya hali ya chini, ili awe chombo ambacho kwa njia yake Mungu angeleta baraka yake duniani. Kwa njia ya mtoto wake, Mungu angetimiza ahadi zake kubwa alizowapa Ibrahimu na Daudi (Luka 1:46-56). Miezi mitatu iliyofuata, Maiamu aliishi kwa jamaa na rafiki yake Elisabeti katika nchi ya Uyahudi. Aliporudi Nazareti kwa hali ya kuwa na mimba, Yusufu alihangaika sana, hadi alipofunuliwa ukweli na Mungu na kisha kuyatii mapenzi yake matakatifu (Luka 1:56; Mathayo 1:18-25).   
            Miezi michache baadaye, Yusufu na Mariamu walihamia Bethlehemu ya Yuda kwa ajili ya sensa, na huko mtoto alizaliwa (Luka 2:1-7, 19). Kisha baada ya hapo, Yusufu na Mariamu walimpeleka mtoto Yesu Yerusalemu kwa ajili ya sherehe fulani za Kiyahudi, Mariamu alijifunza kidogo kuhusu mambo yaliyowakabili. Ingawa mwanaye angekuwa Mwokozi, pia angepingwa vikali, na mambo yale yangemletea Mariamu uchungu na masikitiko (Luka 2:22-23, 34-35). Kwa sababu ya vitisho na ukatili wa Herode, Yusufu na Mariamu walimtoroshea mtoto Yesu nchini Misri kwa ajili ya usalama na kuepuka kuwawa.
            Baada ya kufa kwake Herode, familia ile ilirudi Nazareti tena (Mathayo 2:13-14, 19-23). Yusufu na Mariamu walitimiza jukumu lao kwa uaminifu kama wazazi la kumlea Yesu awe mtiifu na kumfundisha mambo ya Agano la Kale (Luka 2:42-46, 51). Lakini hawakuelewa sana habari za uhusiano wa pekee ambao Yesu alikuwa nao  baina ya Yeye na Baba yake wa Mbinguni (Luka 2:49). Hata alipoanza huduma yake ya hadhara, Yesu aliona haja ya kumkumbusha mama yake namna ilivyompasa kuitumia nguvu yake ya mbinguni kufuatana na mapenzi ya Baba yake tu. Hivyo asingetumia wakati wo wote kwa ajili ya kuwafurahisha marafiki na jamaa zake (Yohana 2:3-4).
            Wapo watoto wengine waliozaliwa na Mariamu na Yusufu baada ya Yesu nao walikuwa ni Yakobo, Yusufu, Simoni, Yuda na yawezekana mabinti wawili pia (Matayo 13:55-56; Marko 6:3). Ndugu zake hawa, hawakumwamini Yesu wakati alipoanza huduma yake hadharani. Ndugu zake hawakumwamini kuwa Yeye ni Masihi. Na siku moja walisema mawazo yao wazi kuhusu Yesu mbele ya mama yao (Marko 3:21, 31-35; Yohana 7:3-5). Lakini Mariamu alikuwa na uhakika  kuhusu Umasihi wa mwanaye, naye alidumu kumwamini hata mpaka wakati wa kusulubiwa kwake (Yohana 19:25-27).
            Kufufuka kwake Yesu, kuliwabadilisha ndugu zake, kwa sababu katika siku baada ya kupaa kwake, wao pamoja na Mariamu walikuwa katika kundi la waamini wa Yerusalemu walioshirikiana katika maombi. Soma Matendo 1:14 ukihusianisha na 1Wakorintho 15:7. Twaweza hitimisha kuwa: Mariamu huyu alipewa neema kubwa na Mungu (Luka 1:28, 30), utabiri au unabii wa kuchaguliwa kwake ulianza tangu Agano la Kale (Isaya 7:14-16; Isaya 9:6-7; Mika 5:2, 3); Hakuwa na visingizio bali alijitoa kikamilifu katika kuukamilisha mchakato wa ukombozi kwa kubeba mimba ili kumzaa Mwokozi (Luka 1:31-35, 38); alimtukuza Mungu kwa kuchaguliwa kuwa mzazi au mama wa Mwokozi (Luka 1:46-55); alishiriki katika maombi ya siku kumi katika siku za pentekoste (Matendo 1:12-14); aliitwa mwenye heri (Luka 11:28), n.k.

 Mariamu Magdalene
             Mariamu Magdalene ni mwanamke aliyekuwa na mapepo saba. Mwanzoni mwa taarifa zake hakutajwa jina lake, aliitwa mdhambi ama mwanamke mmoja (Luka 7:37), hii ni kwa sababu alionekana kuvunja sheria za kiyahudi zijulikazo kama “Jewish Talmud”. Yaweza kuwa ni kweli, alihisiwa ama kubambikiwa kosa maana upande wa pili wa mkosaji (mwanamume) hakuonekana akishutumia kwa kuvuja sheria. Maana ya jina lake limetafasiriwa kutokana na eneo analotokea liitwalo ‘Magdala’ sawa na ‘mnara’ au ‘ngome’. Kama tulivyoona awali, jina la Mariamu humanisha ‘uchungu’ au ‘maumivu’.
            Kuhusu mwanamke huyu, hakuna kumbukumbu  inayohusu wazazi wake, ndoa na umri. Lakini pia Biblia haitaji cho chote kuhusu kazi aliyokuwa akifanya mwanamke huyu, isipokuwa anatajwa kuwa, alikuwa huru kumfuata Yesu katika safari zake zote. Biblia katika Agano jipya inaonesha siku moja Wayahudi walimpeleka  Mariamu Magdalene kwa Yesu ili amhukumu, na tukio hili lilikuwa mtego kwa Yesu kutoka kwa Waandishi na Mafarisayo (Yohana 8:3-6). Walitaka wajue Yesu kama atamhukumu au kumuachia. Na kama angewaambia wamuache huru, ingeonekana anapingana na Sheria na taratibu za Kiyahudi.
            Yesu hakufanya cho chote katika kesi ya Mariamu Magdalene, zaidi tu aliwaambia kama hawana dhambi basi wamponde mawe Mariamu Magdalene, na kisha aliandika chini katika mchanga na kila mmoja akajiona makosa yake na kuondoka (Yohana 8:6-9). Ikumbukwe kuwa Yesu  hakutoa hukumu kwa sababu alikuja kuokoa waliopotea na si kuhukumu (Yohana 3:17).  Ukiisoma Yohana 8:7-8, utagundua kuwa Yesu alijibu sawasawa na 1Wafalme 8:46,  Zaburi 14:3 na Isaya 53:6.
           Kwa mara nyingineYesu aliandika kwa mkono wake sawa na alivyoandika Amri Kumi na ile hukumu ya utawala wa Babeli kipindi cha mfame Belshaza (Danieli 5:5-6).  Lakini katika kosa la mwanamke huyu, Yesu aliandia dhambi za washitaki wake katika mchanga. Hivyo basi, Yesu huandika dhambi zetu sawa na alivyoandika katika mchanga ili iwe rahisi kufutika pale anapotusamehe, maana Yeye ndiye anayetusamehe na kutuhukumu pia (2Timotheo 4:1). Japo, Mariamu Magdalene alikuwa mdhambi, lakini ilimpasa Yesu amkomboe. Yesu anaichukia dhambi na si mdhambi. Hatuwezi kuishinda dhambi kwa nguvu zetu binafsi bali kwa msaada wa Mwokozi.
            Tunaposimama kama Mafarisayo na Waandishi kwa kuhukumu makosa ya wengine bila kuyaangalia makosa yetu, twaenda kinyume. Yatupasa Mwokozi atufunulie dhambi zetu ili tuziungame badala ya kuhangaika katika kuwashutumu wengine, yumkini dhambi zetu nyingi kuliko zao. Tunajihusisha na vibanzi ndani ya macho ya wengine bila kuona viboliti ndani ya macho yetu (Mathayo 7:3). Mariamu Magdalene alipelekwa mbele ya jaji kama mkosaji, lakini hakubaki mshitaki ye yote mbele yake (Yohana 8:9-10). Yesu alisimama na ataendelea kusimama kama hakimu mwaminifu. Na hakuna haja ya kuhukumiana maana sote tutasimama mbele ya huku ya Mungu (Rumi 14:10).
            Yesu alimwambia Mariamu Magdalene “...wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena” (Yohana 8:11). Yesu ana nguvu ya kumshindia dhambi mwanadamu (1Yohana 4:4). Fikiria, endapo Yesu angeruhusu tupondwe mawe kwa makosa na uvunjaji wa sheria, je, ni kiasi gani cha mawe yangelihitajika kutuadhibu kwa dhambi tutendazo? Kuna siku pia Yesu alimwondolea Mariamu Magdalene mapepo saba (Luka 8:2). Yafuatayo ni mambo yanayomhusu Mariamu Magdalene mpya aliyekombolewa kutoka katika dhambi:
1.      Alimpenda Yesu na kujisalimisha vyema kwake (Luka 10:38-42).
2.      Ni mwanamke pekee aliyeifuta miguu ya Yesu kwa nywele zake pamoja na kuipaka mafuta (Mathayo 26:6; Marko 14:3).
3.      Alishuhudia mateso na kufa kwa Yesu pale msalabani (Yohana 19:25; Luka 23:49; Marko 15:40, 47).
4.      Alikuwa wa kwanza na miongoni mwa wanawake walioshuhudia kufufuka kwa Yesu (Yohana 20:1-11; Luka 24:1-11; Mathayo 29:10; Luka 24:1-10).
5.      Alishiriki katika kuandaa mafuta ya kuupaka mwili wa Yesu ili kuuhifadhi (Luka 23:54-56; Luka 24:1).
6.      Akiwa pamoja na wanawake wengine na Mariamu mama yakeke Yesu, naye alishiriki katika maombi ya kumwagwa kwa Roho Mtakatifu  kipindi cha Pentekoste (Matendo 1:14).
7.      Shauku na huzuni ya kuukosa mwili wa Yesu kaburini kulimfanya awe wa kwanza kukutana na Yesu baada ya kufufuka kwake (Yohana 20:11-18)
8.      Alishiriki katika uenezaji wa injili, japo siyo moja kwa moja kama walivyofanya Mitume wa Yesu.

 Mariamu wa Bethania
            Huyu ni Mariamu ambaye anauhusiano na Martha, nasadiki walikuwa ndugu na habari zake katika Biblia zimeelezewa katika visa vya awali vya Martha. Maana ya jina hili, ni ile ile kama tulivyoona kwa Mariamu wengine.  Sanjali na kuwa na undugu na Martha, pia alikuwa na undugu na Lazaro aliyefufuliwa na Yesu. Watatu wote waliishi Bethania, si mbali sana na Yerusalemu, nao walikuwa marafiki sana wa Yesu (Yohana 11:1, 5).
             Mwanamke huyu alikuwa mwanafunzi mzuri wa mambo ya kiroho, hivyo mara nyingi ameonekana akiwa karibu na Yesu na alipenda kukaa kimya na kwa amani katika miguu ya Yesu. Tofauti ya Martha ndugu yake, yeye alichagua fungu lililo jema (Luka 10:38-42).
            Wanazuoni wa agano jipya hupishana katika kumfananisha Mariamu wa Bethania na Mariamu wa Magdala kuwa ni mwanamke mmoja au ni wawili tofauti. Wanazuoni wanaosema ni Mariamu wawili tofauti, yaani Mariamu wa Bethania na Mariamu Magdala aliyekuwa mdhambi, wanasimamia hoja zao kwa mafungu yafuatayo: Luka 7:36-50; Yohana 11:2 ;  Yohana 12:1-8. Marko 14:8.
            Mtazamo wangu nami, nachelea kuungana na wanazuoni wa agano jipya wanaodai kuwa Mariamu Magdalene na Mariamu wa Bethania ni mmoja. Ukiangalia Luka 7:37, Mariamu hatajwi jina, bali anatajwa kama mwanamke mmoja tena mdhambi. Katika Yohana 8:2-4 haitaji jina la Mariamu, bali inamtaja kama mwanamke aliyepelekwa kwa Yesu akiwa amefumaniwa amezini.
            Zifuatazo ni sababu baadhi zinazoonesha kuwa Mariamu Magdalene ndiye yuleyule Mariamu wa Bethania: wote hawakuwa wameolewa; wote walikuwa na pesa; wote; walikuwa na majina sawa; wote walikuwa na Yesu, lakini majina yao hayakutajwa  kwa wakati mmoja na wote taarifa zao za awali hazikuwa nzuri. Aya na mafungu yafuatayo, yanathibitisha kuwa, Mariamu Magdalene na Mariamu wa Bethania ni mtu mmoja na siyo wawili tofati: Mathayo 28:1 (Mariamu wa pili ni mama yao Yesu, Yakobo na Yuda);  Marko 15:40 na Mathayo 27:56.
            Nyakati fulani katika kifo cha ndugu yake, mwanamke huyu alikuwa katika huzuni kubwa (Yohana 11:28-37). Familia yake ilikuja ikawa kitovu cha uinjilisti baada ya Lazaro ndugu yake kufufuliwa na Yesu (Yohana 12:9-11). Alikumbuka kwenda kumshukuru Yesu baada ya kumuepushia kifo cha kupondwa mawe (Mathayo 26:6-13; Marko 14:3-9; Yohana 11:1; Yohana 12:1-13).

 Mariamu Mama wa Marko
            Mwanamke huyu alikuwa mama wa Marko aliyeandika injili ya pili ambaye jina lake la pili aliitwa Yohana (Matendo 12:12). Kwa kiasi fulani inasadikisha kuwa, Mariamu huyu alikuwa na hali nzuri ya uchumi katika familia yake, kwa sababu familia yake iliishi au ilimiliki nyumba kubwa na ilikuwa na wafanyakazi (Matendo 12:12-13). Bilashaka nyumba hii ilikuwa mahala ambapo Mitume na Wakristo wengine wa Yerusalemu walikutana mara nyingi, hii ni kwa sababu, baada ya Petro kutoka gerezani kimuujiza, alijua kwamba katika familia ya Mariamu angekutana na Wakristo wengine (Matendo 12:12).
            Kama ndiyo hiyo nyumba amayo Mitume walikutana mara kwa mara, basi ilikuwa ni nyumba yenye ‘chumba cha ghorofa’ ambamo kabla yake Yesu na wanafunzi wake walikutana (Luka 22:11-12; Matendo 1:13; tazama pia Yohana 20:19, 26). Mariamu huyu alikuwa ndugu au dada wa Barnaba (Wakolosai 4:10). Biblia haijatoa taarifa zo zote kuhusu wazazi ama mume wake, lakini twaweza sadiki kama wanazuoni wengine wanavyodai kuwa Mariamu huyu alikuwa Mjane kutoka katika familia kubwa. Biblia pia inamtaja Roda aliyekuwa mfanyakazi katika familia hiyo, na ndiye aliyemtambua Petro kuwa ni yeye aliyekuwa akibisha hodi baada ya kutoka gerezani kimwujiza. 

 Mariamu wa Rumi
            Mariamu huyu anapatikana katika salamu ya Mtume Paulo (Warumi 16:6). Katika waraka wa Paulo kwa Warumi, Paulo anamtambua Mariamu huyu kwa jina lake. Inaonesha mwanamke huyu wa Kirumi aliitwa jina hili kama jina la ubatizo (baada ya kuongoka na kubatizwa). Kama angekuwa ni Myahudi basi angelikuwa ni mfanyakazi wa mmoja wa watu wa juu huko Rumi – angekuwa masaliti kwa Wayakudi wenzie.

 Martha
            Martha ni mwanamke katika agano jipya aliyekuwa kivitendo zaidi katika utumishi wake wa Injili. Jina hili linamanisha Bwana sawa na neno ‘Maran-atha’ ambalo humanisha‘Bwana anakuja’ (1Wakorintho 16:22). Wanazuoni wengine hutafasiri jina hili kama ‘mwanamke’ au ‘mama’ (2Yohana 1:1). Mwanamke huyu alikuwa dada wa Mariamu na Lazaro. Hivyo, Martha, Mariamu na Lazaro waliishi katika kijiji cha Bethania, karibu na Yerusalemu (Yohana 11:1, 18).
            Yesu aliwajua watu wa nyumba ile vizuri (Yohana 11:5), kwa sababu alikuwa kwao  mara nyingi alipotaka kukwepa umati wa watu na kufurahia utulivu na ushirika. Inaonesha Martha alikuwa na tabia ya ukarimu (Yohana 11:20, 30; Yohana 12:1-2). Kwa pamoja, Martha na Mariamu walipendwa sana na Yesu (Yohana 11:5). Siku moja Yesu alimkemea Martha, alipokuwa akijishughulisha na maandalizi ya karamu ya pekee, ambapo Mariamu ndugu yake alikuwa ameketi na kuzungumza na Yesu bila kumsaidia Martha katika maandalizi ya karamu hiyo (Luka 10:38-42).
            Siku moja baada ya hayo, Lazaro alikuwa mgonjwa. Dada zake (Martha na Mariamu) walipeleka ujumbe kwa Yesu, lakini Yesu alipofika alimkuta Lazaro amekwisha kufa (Yohana 11:1-6, 17). Martha na Mariamu walikuwa na uhakika kwamba, endapo Yesu angelikuwepo, angeliweza kufanya jambo lo lote ili Lazaro asife (Yohana 11:10-21, 28-32). Hata baada ya Lazaro kufa, Martha bado aliamini kwamba Yesu alikuwa na nguvu ya kufanya jambo lo lote (Yohana 11:22), na kwa kujibu swali la Yesu, alithibitisha imani yake ya kuwa Yeye ndiye Masihi, Mwana wa Mungu  (Yohana 11:25-27).
            Tukio la Yesu kumfufua Lazaro lilimpatia umarufu na wafuasi wengi zaidi. Lakini kama Yesu alivyokuwa amekwisha sema, tukio la namna hii halikuwagusa watu waliodumu kumpinga. Waliendelea kumpinga, hata waliposhuhudia mwujiza wa mtu aliyerudi kutoka katika umauti akawa hai tena (Yohana 11:1-44, 46-50). Badala ya kumwamini, walifanya njama za kutaka kumuua Lazaro (Yohana  12:9-11).  Mwujiza huu ulianzisha uadui ambao katika muda wa juma (la mwisho) lililofuata  lilipelekea kifo cha Yesu (Yohana 11:53; Yohana 12:1, 17-19).
           Hivyo basi, tendo la Yesu kumfufua Lazaro halikuonesha mamlaka yake juu ya mauti tu, bali pia lilionesha umoja ambao Yesu alikuwa nao na Baba yake katika matendo yake yote hapa duniani na mbinguni (Yohana 11:41-44). Baada ya siku chache, Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakila pamoja na lazaro na dada zake, Mariamu alipaka miguu ya Yesu mafuta yenye thamani kubwa. Yesu aliliona jambo lile kama kama tendo la mfano wa kupakwa mafuta kwa maandalizi ya mazishi yake ambayo yangetokea baada ya siku chache (Yohana 12:1-8). Wakati wa siku chache kabla ya kusulubiwa kwake, Yeye na wanafunzi walipokwenda Bethania ili kulala huko usiku, labda nyumba ile ya akina-Martha ndipo mahali walipo lala (Marko 11:11-12, 19; Mathayo 21:17).
            Wachambuzi wa mandiko wa hivi karibuni hudhani kuwa, yaweza kuwa Martha alikuwa mke au mtoto wa Simoni aliyekuwa mkoma, hivyo baada ya kifo chake Martha alibaki kuwa mmiliki wa nyumba ya mumewe au baba yake (akiwa kama mtoto mkubwa) ambapo kufufuka kwa Lazaro kulisheherekewa. Wengine hudai kuwa Martha yawezakuwa, alikuwa ndugu wa karibu sana na Simoni ambaye alikuwa kama mwenyeji  wa watu waliofika katika nyumba hiyo. Na hoja ya msingi yawanazuoni hawa hujengwa katika tukio lile la Mariamu kuipaka miguu ya Yesu mafuta. Hivyo, kama tendo hilo lilikuwa lilelile lililoandikwa katika Mathayo 26:6 na Marko 14:3 basi yaweza kuwa ni kweli, Martha na Simoni walikuwa na ukaribu ama undugu. 

 Matredi
            Maana ya jina hili ni ‘kuamini mbele’, ‘utoaji’ au ‘ufukuzaji’. Jina hili lilikuwa jina la mama yake Mehetabeli, ambaye aliolewa na Hadadi (Mwanzo 36:39; 1Nyakati 1:50). Hivyo basi, Matredi alikuwa mama mkwe wa mfalme wa mwisho wa Edomu.
                                                                                              
 Mehetabeli
            Maana ya jina hili ni ‘ambaye Mungu humfanyia furaha’ au ‘mnufaika wa Mungu’. Mehetabeli alikuwa binti wa Matredi na mke wa Hadadi ambaye alikuwa mfalme wa mwisho wa Edomu (Mwanzo 36:39; 1Nyakati 1:50).  Kipindi cha Nehemia, jina hili limetajwa kama jina la kiume pia (Nehemia 6:10-13).

 Merabu
            Maana ya jina hili linamanisha ‘ongezeko’ au ‘maradufu’. Alikuwa binti wa Sauli, mfalme wa kwanza wa taifa la Israeli (1Samweli 14:49). Binti huyu ndiye binti ambaye mfalme Sauli aliahidi kumuozesha mtu ambaye angempiga au kumshinda Goliathi (1Samweli 17:25). Ni Daudi aliyempiga ama kumshinda Goliathi (1Samweli 17:50-51). Lakini japo Daudi alimshinda na kumuua Goliathi, Sauli hakutimiza ahadi yake ya kumuozesha Marabu kwa Daudi, bali alimpa kazi nyingine kwa hila ya kupigana vita ndipo amuozeshe Merabu (1Samweli 18:17, 18).
            Daudi alivipiga vizuri vita vya Bwana, lakini Sauli hakumuozesha Daudi binti yake, badala yake  Merabu aliozeshwa kwa Adrieli, Mmeholathi (1Samweli 18:19). Wanazuoni wengine wa Biblia hudai kuwa, Merabu alikufa akiwa kijana na watoto wake alipewa dada yake aitwaye Mikali ambaye hakuwa na watoto na aliwalea kama wanawe (2Samweli 6:20-23; 2Samweli 21:8).

 Meshulemethi
            Meshulemethi alikuwa binti  wa Haruzi wa Yotba, na alikuwa mama wa Amoni, aliyekuja kuwa mfalme wa Yuda (2Wafalme 21:19). Maana ya jina hili ni ‘whote walipao’ au  ‘kupatiliza’. Aliolewa na Manase, kijana wa Hezekia. Mwanaye alitenda maovu mbele za Bwana katika utawala wake. Hakuna ushahidi wa moja kwa moja, kuwa Meshulemethi alichangia katika matokeo ya uovu wa mwanaye.

 Mikali
            Mikali alikuwa binti wa Sauli, mfalme wa kwanza wa Israeli (1Samweli 14:49). Alikuwa binti mdogo wa Sauli aliyekuwa mfalme wa kwanza wa Israeli. Mama yake aliitwa Ahinomu. Kwa kuwa Mikali alimpenda sana Daudi, na baba yake aliamua kumuozesha kwa Daudi (1Samweli 18:20-28). Kutokana na hila za baba yake aitwaye katika kutaka kumuua Daudi, kunasiku moja alimdanganya baba yake ili kumuepushia mumewe na kifo (1Samweli 19:11-17). Jina hili inatokana na neno “Michaih” na “Michael” ambapo maana yake ni sawa na ‘Yeye aliye sawa au anafanana na Yehova’ .
            Mikali ndiye mke wa kwanza wa Daudi. Japo awali alikuwa ametolewa kwa Falti, kijana wa kiume wa Laishi wa Galimu kwa muda (1Samweli 25:44; 2Samweli 3:13, 14). Kama mama mdogo wa watoto wa dada yake aitwaye Merabu. Mikali aliwalea watoto wa dada yake baada ya dada yake kupatwa na umauti. Sifa ya pekee ya Mikali kwa mumewe ni kuwa: Aliolewa na Daudi, alimpenda Daudi, alimwokoa Daudi, (1Nyakati 13:31), hakupenda Daudi atende mambo ya ajabu ajabu (2Samweli 6:16-23; 1Nyakati 15:29)

 (a) Milka
            Milka ni jina lililo na maana ya ‘malkia’ au ‘mshauri’. Milka alikuwa binti wa Harani aliyekuja kuolewa na baba yake mkubwa aitwaye Nahori ambaye pia ni mdogo wake na Ibrahimu (Mwanzo 11:26-29).  Milka alimzalia Nahori watoto wa kiume, na  mdogo kabisa aliitwa  Bathueli aliyekuwa baba wa Rebeka na Labani (Mwanzo 22:20, 23; Mwanzo 24:15, 24, 47). Katika Milka huyu twasadiki kuwa, yeye ndiye bibi wa wote kupitia kwa Rebeka na kuendelea. 

(b) Milika
            Mwanamke huyu alikuwa miongoni mwa binti watano wa Zelofehadi na alishirikiana na ndugu zake katika kudai haki ya urithi wa baba yao (Hesabu 26:33; Hesabu 27:1; Hesabu 36:11 na Yoshua 17:3). Baadhi ya nyaraka za wanazuoni hudai kuwa, jina hili ni kifupisho cha jina ‘Bethmilea’ na ni jina la Kijiografia zaidi kuliko jina la mtu. 

Miriamu
            Huyu ni mwanamke ambaye, wivu wake ulisababisha hukumu. Jina hili ni la Kiebrania lenye maana sawa na Mariamu linalomanisha ‘uchungu’. Kwa sababu ya wivu wake na Haruni juu ya Musa, alijikuta katika uchungu. Wivu wao kwa Musa ulikuwa juu ya mamlaka yake makubwa  aliyokuwa amepewa na Mungu katika taifa la Israeli (Hesabu 12:1-2). Miriamu alipata lawama zaidi katika jambo lile la kumsema vibaya Musa, na Mungu alimwadhibu kwa ugonjwa wa ukoma uliotokea ghafla. Lakini Musa alipomwombea msamaha alipona, na baada ya kupona, alitengwa kwa siku saba (Hesabu 12:9-15; tazama Walawi 14:8). Kumbukumbu la torati 24:9 inasema “Kumbukeni na BWANA, Mungu wako, alivyomtenda Miriamu katika njia mlipotoka Misri”.
            Miriamu alikuwa binti katika familia yenye wazazi wamchao Mungu. Alikuwa mtoto wa kwanza wa Amramu na Yokebedi (Hesabu 26:59) na dada wa Haruni na Musa. Huyu ndiye dada hapo awali asiyetajwa kwa jina na aliyemwangalia mtoto Musa (Kutoka 2:1-8). Yeye na kaka zake wawili, walipewa kazi ya maana na Mungu katika kuimarisha Israeli kuwa taifa jipya na huru (1Nyakati 6:3; Mika 6:4). Miriamu alikuwa nabii wa kike, na baada ya kuvuka Bahari ya Shamu, alioongoza  maandamano ya wanawake katika kusherehekea makuu ya Mungu katika kuwashindia kutoka kwa Wamisri (Kutoka 15:19-21).
            Inaonesha kuwa, Miriamu alikuwa mke wa kiongozi mmoja katika Israeli aliyeitwa Huri, miongoni mwa Waamuzi watatu wakati wa Musa (Kutoka 24:14). Alikuwa bibi wa Zazaleeli, msanifu maarufu wa ujenzi wa Hema (Kutoka 31:2).  Wachambuzi wengine wa Biblia hupendekeza kuwa, Miriamu aliishi bila kuolewa katika maisha yake yote. Miriamu alikufa jangwani kati ya Misri na Kanani na alizikwa Kadesh-barnea (Hesabu 20:1). Kupitia Miriamu tunayakujifunza yafuatayo:
a)      Alikuwa mwangalizi wa mtoto Musa ili ajue nani atamchukua katika safina iliyokuwa imewekwa katika mto Nile (Kutoka 2:4). Alikuwa mlezi na mlinzi wa Musa na alikuwa mwaminifu kwa kuhifadhi siri juu ya uhusiano wa Musa na Waebrania kwa miaka kumi na mbili, tangu Musa akiwa amezaliwa.
b)      Ni mwanamke wa kwanza anayethibitishwa na Biblia kuwa alipewa karama ya unabii katika Bahari ya Shamu (Kutoka 15:20, 21).
c)      Ni mwanamke au dada mwenye wivu, na alimpinga kaka yake kwa nafasi aliyokuwa nayo katika kuliongoza taifa la Israeli. Miriamu na Haruni, waliongea kinyume juu ya Musa kuhusu uoaji wake (Hesabu 12:1-2). Kutokana na kumuongea vibaya Musa, Miriamu alipigwa ugonjwa wa ukoma na Mungu. Alijutia makosa na aliombewa msamaha na kaka yake kisha kutengwa kwa siku saba (Hesabu 12:12). Adhabu ya ukoma kwa Miriamu ilikuwa fundisho na kumbukumbu kwa vizazi vingine  (Kumbukumbu la Torati 24:9).
d)     Yaweza kuwa alikufa kama mtakatifu na alizikwa Kadeshi (Hesabu 20:1).

            Katika 1Nyakati 4:17 anatajwa Miriamu mwingine. Ambaye ameorodheshwa kama mke wa Ezrahi (Biblia ya “King James” inamtaja Ezrahi kama Ezra, hivyo wachambuzi wengine hudai Miriamu huyu alikuwa dada wa Ezra) wa kabila ya Yuda. Baadhi ya wanazuoni wengine wa Biblia hawaonesha kama Miriamu huyu alikuwa ni mwanamke au Mwanamume kulingana na maana. Katika Biblia yetu ya Kiswahili, inampambanua kuwa ni mwanamke, na alimzalia Ezrahi watoto, Shamia na Ishba.    

 (a) Naama
            Jina hili ni miongoni mwa majina ya wanawake wa kale yaliyowekwa katika kumbukumbu za maandiko matakatifu. Mwanzo 4:22 inamtaja Naama huyu kama binti wa Sila na umbu lake Tubal-kaini. Mwanamke huyu anatokea katika uzao wa Kaini (ukoo au uzao wa wana wa wanadamu).  Maana ya jina hili ni ‘uzuri’ au ‘utamu’. Hivyo, Naama ni jina la kike linalotokana na neno “naam”. Jina hili siyo sawa na jina la mtoto wa Kalebu aitwaye Naamu (1Nyakati 4:15), japo jina la Naama na Naamu yanatoka katika nenono moja la ‘naam’. Yoshua 15:41, inalitaja jina hili kama jina la mji pia.

(b) Naama
            Hili lilikuwa pia ni jina mmoja wa wake wa Sulemani. Alikuwa mama wa Rehoboamu mwana wa Sulemani, amabaye alimrithi Sulemani baba yake ufalme. Rehoboamu ndiye mfalme wa mwisho katika muunganiko wa taifa la Israeli. Mwanamke huyu alitoka katika kabila teule za maadui za Isaraeli (1Wafalme 14:21, 31; 2Nyakati 12:13). Waamoni na maovu yao yalikuwa ni chukizo mbele za watu wa Israeli. Mwanamke huyu alimwongoza Sulemani katika njia ya upotevu. Kwa kuwa alikuwa mke mkuu wa mfalme Sulemani,  alichagua eneo kwa ajili ya madhabahu ya mungu wake, aitwaye ‘Moleki’ au ‘Milkom’.

                                                                    Naara
           Naara humanisha ‘binti au mwana wa mtawala mkuu’. Naara huyu alikuwa ni mmoja kati ya wake wawili wa Ashuri, baba yake na Tekoa na alimzalia watoto (1Nyakati 4:5, 6). Pia hili ni jina la mji ambao pia ulijulikana kama ‘Naara’ (Yoshua 16:7; 1Nyakati 7:28).

 Naomi
           Naomi ni mwanamke aliyeonja kikombe cha uchungu. Rejea katika maandiko matakatifu katika kitabu cha Ruthu. Jina hili linamaanisha ‘furaha yangu kuu’ au ‘furaha ya Yehova’. Ni jina linaloashiria uchangamfu, wenye kukubalika  au wenye kuvutia. Naomi alikuwa na uungwana ambao ulimpa haiba na mvuto imara. Japokuwa sifa zake zilikuja kufunikwa na kuongozwa na maumivu baada ya kufiwa mume na watoto wake (Maloni naKilioni). Jina la mumewe ni Elimeleki, wote walikuwa Waebrania.
            Naomi na Elimeleki ni watu wa Bethlehemu ya Yuda na kwao walizaliwa watoto wawili wa kiume. Kwa sababu ya njaa kali wakati wa utawala wa Waamuzi, iliyoonekana kama adhabu iliyowaijia watu baada ya kutenda dhambi (Walawi 24:14, 16), Naomi na Elimeleki, Muefraimu wa Bethlehebu waliamua kuhama pamoja na familia yake kwenda nchi nyingine palipokuwa na chakula cha kutosha, hivyo walisafiri kutoka Yuda na kwenda kukaa kwenye vilima vya nchi ya Moabu.
            Maana ya Elimeleki ni ‘Mungu wangu ni Mfalme’. Kwa kumshawishi mkewe, waliicha Bethrehemu yaani ‘nyumba ya mikate’ na kwenda Moabu inayomanisha ‘uchafu’ au ‘si chochote’. Naomi alijikuta katika nchi ya ugeni, na watoto wake walioa wanawake wa Kimoabu, ingawa taratibu za Mungu hazikuruhusu kuoa nje ya kabila za Israeli. Wakwe zake waliitwa Ruthu na Orpa. Japokuwa Elimeleki, mume wa Naomi alikimbia kufa kwa njaa, umauti ulimpata hukohuko alikokimbilia. Naomi naomi alibakia huko Moabu akiwa mjane.
            Baada ya kifo cha mumewe, Naomi alipoteza tumaini la kuendelea kuishi Moabu. Akiwa katika huzuni na majonzi ya kufiwa na mume wake, Naomi alifiwa na  watoto wake wote wawili. Na wakati huu umri wake ulikuwa umesonga na hakuwa na msaada tena zaidi ya binti wajane waliokuwa wake wa watoto wake (Ruthu na Orpa). Kwa hali hiyo, ilimbidi Naomi kurudi katika nchi yake, maeneo ya Bethlehemu palipokuwepo na ndugu zake na marafiki zake (Ruthu 1:1-22). Aliamua kurejea akiwa katika hali ya machungu kutokana na maswaibu yaliyomkuta kule Moabu.
            Orpa alibakia Mobu, lakini Ruthu aliambatana na mkwewe Naomi katika nchi ya Yuda. Naomi na Ruthu walikuwa na dhiki, na hivyo Ruthu alikwenda kuokota masazo ya wavunaji ili apate chakula cha yeye na mkwe wake. Ruthu hakujua kwamba mtu ambaye katika shamba lake alikuwa akiokota  masazo alikuwa Boazi, jamaa wa karibu sana na marehemu Elimeleki. Baada ya Boazi kupata habari za Ruthu za wema aliokuwa amemfanyia Naomi, yeye naye alimwonyesha wema wake (Ruthu 2:1-23). Kwa kuwa Naomi alijua kwamba Boazi alikuwa jamaa wa karibu wa Elimeleki aliyesalia na hajaoa, alimshauri Ruthu amwombe Boazi amzalie mtoto ambaye, kufuatana na desturi za Kiebrania, angehesabiwa  kuwa mtoto wa mume aliyekufa.
            Mtoto yule angekua na kuchukua jina na urithi wa marehemu  mume wa mjane huyo. Boazi alikuwa tayari kufanya vile kama alivyokuwa Ruthu ameomba, lakini akiwa mtu mkweli na mwaminifu, Boazi alimwambia  Ruthu kwamba  alikuwepo jamaa aliyekuwa wa kariku kuliko yeye (Ruthu 3:1-18). Jamaa huyo baada kujuzwa, inaonesha alikuwa na wajibu mwingine kuliko kuzaa na kulea mtoto kwa niaba ya Elimeleki marehemu. Mtu yule pia angepaswa kukomboa mali ya familia ile ya Elimeleki, ambayo Naomi alipaswa kuiuza kwa sababu ya ugumu wa maisha.
            Kwa njia hii angelihifadhi urithi wa Elimeleki na mwanawe. Kwa kuwa mtoto ambaye angezaliwa baadaye angelithi mali ya familia hiyo, jamaa wa karibu zaidi alimwomba Boazi atimize wajibu huo wa jamaa badala yake yeye. Boazi alifurahi, kwa sababu alipenda kumuoa Ruthu, naye aliridhia kumzaa mwana na mrithi kwa njia yake. Mwana yule alikuwa babu wa mfalme Daudi na mzazi mmojawo (bibi) wa Yesu aliye Masihi (Ruthu 4:1-22; Mathayo 1:1, 5-6).

 Nehushita
            Jina hili linamanisha ‘kipande cha shaba nyeupe’. Mwanamke huyu alikuwa ni binti wa Elinathani, mtu aliyejulikana Yerusalemu, na aliolewa na Yehoyakimu asiye mtu wa dini, kijana mkubwa wa Yosia. Alikuwa pia ni mama wa Yekonia (au Yehoyakini), mfalme aliyeanza kutawala akiwa na umri wa miaka kumi na minane (2Wafalme 24:8). Kipindi mfalme Nebukadreza alipouangusha ufalme wa Yehoyakini (Yekonia), mama yake Nehushta alimfuata utumwani Babeli. Hakuna kitu kilichosemwa juu ya tabia ya mama wa Malkia huyu, kwa kuwa mwanae alifuata njia mbaya za baba yake.

  Noadia
            Jina hili humanisha mtu ambaye ‘Bwana alijifunua kwake’. Alikuwa ni nabii wa uongo na alisimama kinyume na Hulda ambaye alikuwa nabii aliyevuviwa na Mungu. Noadia alikuwa ni mwanamke wa pekee lakini hatali sana kutokana na ushawishi wake. Noadia anatajwa kama rafiki na huenda ndiye mhamasishaji wa Sunbalati na Tobia katika kumpinga Nehemia ambaye walijaribu kumuogopesha (Nehemia 6:14). Noadia pia ni jina la Kilawi kipindi cha Ezira (Ezira 8:33).

 Noa
            Jina hili humanisha ‘pumziko’ au ‘utulivu’. Huyu ni miongoni mwa binti watano wa Selofehadi aliyeungana ndugu zake wa kike kudai haki ya urithi wa baba yao kwa Musa (Hesabu 26:33; Hesabu 27:1-7). Katika matoleo ya Biblia za Kingereza Noa (ambaye ni Nuhu kwa lugha ya Kiswahili) ni jina pia la mtoto wa kiume wa Lameki (Mwanzo 5:30).

Oholibama.
            Mwanamke huyu alikuwa miongoni mwa wakeze Esau. Alikuwa Mkanaani na anajulikana kama binti Ana. Kupitia yeye, alimzalia Esau wana watatu wa kiume, waitwao Yeushi, Yalamu na Kora (Mwanzo 36:2, 5, 14, 25, 41; 1Nyakati 1:52).

 Orpa.
             Orpa ni mwanamke ambaye aliikataa fursa yake. Habari zake zinaanza kutajwa katika Ruthu 1:3-4. Jina hili limetafsiriwa kwa namna tofautitofauti kwa kubadiri heru zake. Lakini maana yake bila kubadilisha herufi zake ni ‘mtoto wa paa’  au ‘swala mdogo’. Kutokana na tabia yake ya kuwa na nia mbili, jina lake la weza manisha ‘mwenye nia mbili’ (sawa na ilivyonenwa katika Yakobo 1:8). Wanazuoni wengine hutetea kuwa, Orpa ametokana na neno la Kiebrania lenye maana ya ‘shingo’ linalosadifu tabia yake  ya kuwa na shingo ngumu au sumbufu kwa sababu alirudi nyuma na kuacha kufuatana na wajane wenzake, Naomi na Ruthu (Ruthu 1:4-16).
            Kuhusu familia yake, hakuna cho chote kinachozungumziwa zaidi tu ya kuolewa na Kilioni, mwana wa Elimeleki na Naomi wakati walipokuwa wamehamia Moabu. Baada ya Naomi kupoteza wanawe wawili wa kiume, Ruthu na Orpa walibakia kuishi katika nyumba ya Naomi mkwe wao. Wakati Naomi akirudi katika nchi yake, aliwasihi, Orpa na Ruthu kurudi makwao. Ruthu aliambatana na Naomi mkwewe, lakini Orpa alirejea kwao maana hakuhitaji cho chote kutoka kwa Yehova, Mungu Waisraeli. Baada ya yeye kubakia Moabu, habari ama taarifa zake hazikutajwa tena katika Biblia.

 Penina
            Jina hili humanisha ‘marijani’ au ‘tumbawe’. Alikuwa miongoni mwa wake wawili wa Elikana. Hakuna kumbukumbu yo yote ya nyuma zaidi ya kuwa aliishi Rama na alikuwa mke wa Elikana aliyemzalia watoto. Penina alikuwa akimdhihaki na kumchokonoa mke mwenza (Hana) kwa maneno kwa sababu hakuweza kupata watoto (1Samweli 1:2-8). Pamoja na dhihaka na maneno yake ya chinichini kwa Hana, kulimuimalisha Hana katika kumtii, kumlilia na kumuomba Mungu. Hatimaye Mungu alijibu ombi la Hana la kupata mtoto, Mungu alimfuta maumivu ya dhihaka ya Penina. Baada ya Hana kumzaa Samweli, alizaa wana wengine tena (1Samweli 2:21).

 Persisi
            Persisi anaonekana kutajwa na Mtume Paulo katika salamu yake ya utambuzi ndani ya Waraka wake kwa Warumi (Warumi 16:12). Jina hili limechukuliwa  kutoka nchi ya Uajemi (Persia), likiwa na maana ya ‘mtu abebwaye na dhoruba’. Japo hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kuwa Mkristo huyu wa kike, mtumishi katika kanisa la awali huko Rumi (Roma), alikuwa  na asili ya Uajemi.

 Prisila (Priska)
            Prisila ni jina la kike lenye kivumishi cha Priska likimanisha ‘isiyotaabika’ ‘stahimilivu’, isiyobadilika, enyethamani’ au ‘heshimika’. Huyu ni mwanamke ambaye alikuwa mbele zaidi katika utumishi wa Injili. Mafungu yafuatayo katika Agano Jipya yanamtaja Prisila kwa namna kadha wa kadha: Matendo 18:2, 18, 26; Warumi 16:3; 1Wakorintho 16:19; 2Timotheo 4:19.  
            Mara kadhaa Prisila ametajwa na Mtume Paulo katika barua zake, na hizo zote alimtaja sambamba na Akila. Jina hili pia linatajwa katika muundo wa familia baina ya Priska na Akila katika waraka wa pili wa Paulo kwa Timotheo (2Timotheo 4:19). Hivyo, Akila na Prisila walikuwa mke na mume kama ilivyo thibitishwa katika Matendo 18:2. Paulo na akila walishiriki kazi pamoja ya kushona mahema (Matendo 18:3).
             Biblia inapowataja mume na mke, Akila la Prisila (Priska), mara nyingi inamtaja Prisila kabla ya mumewe (Matendo 18:26; Warumi 16:3; 2Timotheo 4:19). Jambo hili siyo la kawaida, lakini Biblia haisemi sababu yake. Labda Prisila alikuwa na bidii zaidi na alijulikana zaidi kuliko Akila katika kazi ya Injili ambayo siku zote wote wawili walijitoa kwa moyo wote. Prisila na Akila waliishi mjini Rumi wakati ambapo Warumi hawakuwa wameanza kuwachukia Wayahudi.  
            Kaisari alipowafukuza Wayahudi wote kutoka Rumi, Prisila na Akila walihamia mjini Korintho  katika mkoa wa Akaya, sehemu ya kusini ya Ugiriki ambapo walikutana na Paulo. Inawezekana kwamba wakati huo waliupokea Ukristo (Matendo 18:1-3).  Baada ya miezi 18, Paulo alipoondoka Korintho, Prisila na Akila walisafiri pamoja naye, wakabaki Efeso. Paulo alipoendelea na safari yake (Matendo 18:11, 18-19). Yaweza kuwa walisaidia pia kuanzisha  kanisa la Efeso.
            Zaidi ya yote, wao waliweza kumsaidia Apolo, mwalimu wa Kiyunani aliyekuwa ameongoka muda mfupitu, naye alikuwa amefika kutoka Misri (Matendo 18:24-26). Walibaki Efeso wakimsaidia Paulo baada ya kurudi kwake alipofika na kuishi mjini huko kwa muda wa miaka mitatu (Matendo 19:1 na 20:31). Wakati Paulo akiandika Waraka wa kwanza kwa Wakorintho, kanisa lilikuwa likitumia nyumba ya Prisila na Akila kwa ajili ya mkusanyiko (1Wakorintho 16:19).
            Baada ya Wayahudi kuruhusiwa kurudi Rumi tena, Prisila na Akila walirudi na kuishi huko kwa muda huku wakizidi kumtumikia Mungu na huko pia. Kama ilivyokuwa Efeso, nyumba yao ilikuwa mahali pa kukutania kanisa (Warumi 16:3-5). Baada ya miaka mingi, Prisila na Akila waliishi Efeso tena, na yawezekana walimsaidia Timotheo katika kazi ngumu ambayo Paulo alimwachia. Salamu ambazo Paulo aliwatumia muda mfupi kabla ya kufa kwake, zilikuwa ni neno la mwisho kwao (2Timotheo 4:19 na 1Timotheo 1:3).
            Priska na Akila walipata kuheshimiwa na kupendwa sana na rafiki za Paulo. Kwa utukufu, walifanya kazi pamoja katika utumishi wa kanisa. Walikuwa wamoja katika furaha na upendo; Walikuwa wamoja katika Bwana na Walikuwa wamoja katika kazi (Matendo 18:3; Matendo 20:34, linanganisha na 1Wathesalonike 2:9 pamoja na 2Wathesalonike 3:8). Walikuwa pamoja katika urafiki wao kwa Paulo (Warumi 16:3; 2Timotheo 4:19).  Walikuwa wamoja katika ujuzi wao wa maandiko matakatifu (Matendo 18:25, 26). Walikuwa wamoja pia katika utumishi wa kanisa.

 Pua
            Maana ya jina hili ni ‘kuzaa mtoto’ au ‘furaha ya mzazi kuzaa’. Mwanamke huyu alikuwa miongoni mwa wakunga (wazalishaji) wa Waebrania wakati wakiwa utumwani Misri. Kutokana na tishio la ongezeko la Waebrania nchini Misri, Pua na mwezake waliagizwa na Farao kumuua kila mtoto atakayeonekana ni wa kiume wakati watapokuwa wakiwazalisha wanawake wa Kiebrania (Kutoka 1:15-16). Kwa kuwa Pua na mwenzie walikuwa wakimucha Mungu, hawakutekeleza agizo la Farao hata walopoitwa na kuulizwa utekelezaji wa jambo hilo (Kutoka 1:17-21).  

 Raheli
            Jina hili la Raheli humanisha ‘kondoo jike’ au ‘mwana kondoo’. Raheli alikuwa binti mdogo wa Labani, mwana wa Bethueli na kaka yake Rebeka. Yakobo alipoenda Padan-aramu ili atafute mke, alimwona Raheli, mtoto wa mjomba wake na kumpenda. Yakobo alifanya kazi kwa muda wa miaka saba kama malipo ya mahari kwa Raheli, siku ya harusi alibabaishiwa kwa kupewa binti mkubwa, Lea, badala ya Raheli. Baada ya sherehe za harusi kuisha, Labani alimwambia Yakobo afanye kazi kwa miaka saba mingine kama malipo ya mahari kwa Raheli kuwa mkewe. Labani alimpatia kila binti yake mjakazi kama zawadi ya harusi yao (Mwanzo 29:1-30).
            Lea, dada yake na Raheli alikuwa wa kwanza kumzalia Yakobo wana wanne, Raheli yeye alikuwa bado hajapata mtoto. Kwa kuona kuwa hatazaa, alimshawishi Mumewe azae na kijakazi wake aitwaye Bilha, Yakobo alikubaliana na ombi la mkewe na kujipatia mtoto kwa Bilha. Lea naye alifanya vivyo hivyo, kwa kumpatia Yakobo mjakazi wake aitwaye Zilpa ili azae naye. Baada ya Yakobo kuwa na wana kumi wa kiume na mmoja wa kike, ndipo Raheli naye akapata mwana wa kwanza, aitwaye Yusufu (Mwanzo 29:31-35; Mwanzo 30:1-24).
            Raheli alikufa wakati wa kumzaa mtoto wake wa pili aitwaye Benyamini, mwana pekee wa Yakobo aliyezaliwa Kanaani. Baada tu ya kujifungua, alimwita mwanaye jila la Benoni, lakini baada ya  kufa, Yakobo alimwita Benyamini mtoto huyo. Raheli alizikwa karibu na Rama, katika njia itokayo Betheli kuelekea Bethlehemu (Mwanzo 35:16-20; 1Samweli 10:2; Yeremia 31:15; Mwanzo 48:7). Baada ya karne kadhaa, Yeremia aliona mfano wa Raheli akiomboleza na kuwalilia watoto wake kuwa hawako, wakipelekwa kifungoni  katika nchi ya mbali (Yeremia 31:15; Mathayo 2:16-18). Hivyo basi, kwa ufupi twaweza jifunza mambo yafuatayo kutoka kwa Raheli:
1.      Raheli alikuwa mke wa pili wa Yakobo na mama wa vijana wawili wa kiume (Yusufu na  Benyamini). Yeye na dada yake, Lea, waliolewa na mume mmoja.
2.      Alikuwa mzuri kwa asili kuliko dada yake ambaye alikuwa na makengeza (Mwanzo 29:17).
3.      Kukutana kwake, yeye na Yakobo kulikuwa ni maongozi ya utukufu wa Mungu mwenyewe  (Mwanzo 28:15; Mwanzo 29:6)
4.      Alidanganywa kikatili na baba yake, badala ya kuozesha yeye, aliozeshwa kwanza dada yake (Mwanzo 29:20-23).
5.      Alipendwa sana na mumewe (Mwanzo 29:18, 20, 30).
6.      Alikuwa hazai, lakini mwisho wake alizaa na kutokuwa mgumba tena (Mwanzo 29:31; Mwanzo 30:1, 22-24; Mwanzo 46:19).
7.      Kabla ya kuongoka alikuwa muabudu sanamu wa siri (Mwanzo 31:34; Mwanzo 35:2-4).
8.      Alikuwa alama ya kukumbukwa (Mathayo 2:16-18).
9.      Kutokana na uchungu mkali, aidha na umri kuwa mkubwa, alikufa baada ya kujifungua  (Mwanzo 35:16-18).

 Rahabu
            Rahabu ni mwanamke aliyechukuliwa na Mungu bila yeye kustahili. Aliitwa na Mungu kutoka katika kilima cha uchafu (ukahaba). Jina la Rahabu, kwa mara ya kwanza linatajwa katika kitabu cha Yoshua. Konsonati na irabu ya kwanza, anmbayo ni  ‘ra’ katika jina la Rahabu inamanisha mungu wa Kimisiri aitwaye “Ra”. Hivyo, Rahabu maana yake ni ‘kali sana’, ‘ufidhuli’ au ‘ukali’. Akiwa kama Muamori, Rahabu alikuwa katika jamii inayoabudu miungu (sanamu). Habari za mwanamke huyu zimetajwa katika Yoshua 2:1-3; Yoshua 6:17-25; Mathayo 1:5; Waebtrania 11:31;  Yakobo 2:25, kwa kutaja baadhi.
            Kabla Yoshua hajaishambulia Kanaani, alitumia wanaume wawili ili waupeleleze mji wa kwanza ambao wangeukuta, yaani Yeriko. Hapo Yeriko, wapelezi wale walifikia katika nyumba ya kahaba, Rahabu. Aliwaficha wapelelezi wale wasije wakakamatwa na walinzi wa mji, na kwa shukrani yao aliwaomba wao wamhifadhi yeye na famlia yake wakati ambapo Waisraeli wangeishambulia Yeriko. Kwa kuwa Rahabu alikuwa amesikia habari za kutosha kuhusu Mungu wa Israeli, hata aliogopa nguvu yake, lakini vile vile aliamini kwamba neema Yake ingeweza kumwokoa (Yoshua 2:1-14; Waebrania 11:31).
            Rahabu pia alionesha imani yake alipotii maelezo aliyopewa na wapelelezi. Aliwaficha kama alivyoombwa, naye alifanya vile alivyoambiwa kama maandalizi ya Mashambulizi ya Waisraeli. Kwa kuwa Yeriko ulikuwa ni mji mchafu wa Waamoni, hivyo  Mungu alimuamuru Yoshua auangamize  pamoja na wakazi wake. Yoshua alipoingia katika mji aliitii amri ya Mungu, ila alikumbuka na kutii ahadi ya Rahabu iliyoletwa na wapelelezi. Kwa makubaliano ya Rahabu na wapelelezi, Waisraeli walimhifadhi pamoja na familia yake pale mji wa Yeriko walipouteka. Yeye na familia yake  walipokelewa na kuwa sehemu ya taifa la Israeli (Yoshua 2:15-24; Yoshua 6:17, 22-25; Yakobo 2:25).
            Baadaye Rahabu aliolewa na Salmoni na kumzalia Boazi, aliyemuoa Ruthu ambaye mtoto wao Obedi alimzaa Yese, baba yake Daudi ambako ndiko shina  alikozaliwa Yesu Kristo (Mathayo 1:5-6). Baadhi ya wanazuoni wa Biblia hudai kuwa Salmoni aliyemuoa Rahabu alikuwa miongini mwa wale wapelelezi wawili kama shukrani au malipo aliyoyastahili kama upendo wa kweli baada ya kuokoa uhai wa wale wapelelezi. Kwa hiyo, Rahabu aliingia kwenye orodha ya miongoni mwa bibi zake Yesu Kristo.
            Kama alivyoahidiana na wale wapelelezi, Rahabu alitumia ishara ya kamba nyekundu  kama wokovu wa yeye na ndugu zake. Sifa ya kamba nyekundu, ilikuwa iwekwe nje ya dirisha ili Yoshua na watu wake waione. Pamoja na hivyo, ilikuwa lazima watu walio ndani ya mji wasiione – kwa ajili ya usalama zaidi. Kamba nyekundu ilikuwa kiashiria cha usalama na kafara ya Yesu Kristo (Waebrania 9:19, 22); kama mchakato wa ishara ya wokovu. Kama ilivyokuwa kwa Waisraeli, Rahabu pamoja na ndugu zake  wasingeweza kuhisi amani  ndani ya nyumba, lakini ahadi ileile ya Kutoka 12:13 inayosema “Nitakapoiona damu, nitapita juu yake” iliishi.
            Yapo mambo mengi ya kujifunza kutoka kisa kizima cha Rahabu, ambapo Mungu alimtumia kama kiumbe dhaifu ili kukamilisha mpango wake. Mambo yafuatayo twaweza jifunza kutoka na kupitia kwa Rahabu:
           1. Rahabu anatukumbusha kubadilika mioyo pamoja na maisha yetu. Mara tatu, Biblia inamrejerea Rahabu kama kahaba – ambapo neno kahaba kwa Kiebrania ni “zoonah” na Kiyunani ni “porne”. Habari njema ni kuwa, Rahabu aliamua kubadilika na kuwa mtu mwema na mpya.
            2. Rahabu aliwatambua wale wapelelezi kuwa siyo watu wa zinaa, ni watu wamchao Mungu, hivyo aliwahifadhi na akawatengenezea njia na kuwapatia usalama wa kutoroka.
           3. Mbele za Mungu wa Israeli, Rahabu aliuweka pembeni uzalendo wa nchi yake ili kufanikisha mpango wa Mungu kwanza. Kufanya kwake jambo hilo la hatari, Rahabu alikuwa amesikia habari za ukuu wa Mungu wa Israeli (Yoshua 2:9-11).
           4. Rahabu alizijua vyema mbio zake juu ya hukumu ya Mungu kwa dhambi zake, hivyo, alitamani kuachana na mtindo huo wa maisha na jamaa za nchi yake wenye maisha ya zinaa na ibada kwa miungu ili tu atambulike naye kuwa ni mtu wa miliki ya Mungu.
          5. Alithubutu kwa kujitoa muhanga kwa kuwahifadhi na kuwaficha wapelelezi, ambalo lilikuwa kosa la jinai au uhaini, na kosa hilo lingemsababishia adhabu ya kifo.
          6. Alimdanganya mfalme wa Yeriko. Chini ya sheria za kivita, Rahabu hawezi akalaumiwa katika kusema uongo ili kulinda watu wenye haki dhidi ya uovu, ile ilitumika kama mbinu ya kivita.
          7. Biblia inamuelezea Rahabu katika agano jipya jinsi alivyokuwa mwenye hadhi ya juu na mfuasi mwaminifu wa Mungu; kutoka dhambini na kuwa miongoni mwa watakatifu hata kuwa sehemu ya shina (ukoo)  aliozaliwa Yesu  (Mathayo 1:5).
           8. Imani yake ilimponya pamoja na ndugu zake. Paulo katika Waebrani 11:31 anasema kuwa: “Kwa imani Rahabu, yule kahaba, hakuangamia pamoja na hao walioasi; kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi kwa amani”. Hivyo, Rahabu alipewa hadhi sawa na watakatifu kama Henoko, Nuhu, Ibrahimu, Yusufu, Musa, Daudi n.k. Kwa mujibu wa Mtume Paulo, Rahabu alidhihirisha ya kuwa: “Haki kwa imani pekee ni imani iliyokufa bali imani itendayo kazi kwa upendo”. Rahabu aliamini kwa moyo wake wote na kukiri kwa kinywa chake sawa na Warumi 10:9, 10.
            9. Rahabu alihusika na wokovu wa watu wengine – Rahabu aliomba familia yake iokolewe (isiangamizwe). Mwanamke huyu anatukumbusha kuwa, tufanye maombezi ya wokovu kwa watu wa familiwa na wengine ili nao wapate kutakaswa na damu ya Kristo, ili wawe nyota katika taji zetu. Lakini pia, Rahabu anatukumbusha kuwa, tumeipata nuru ili nawengine tuwaambukize nuru hiyo ili nao waokolewe.
            10. Ambapo wanawake wengine katika Yeriko hawakuona uthamani na uzuri wo wote kwa Rahabu ili awe sehemu ya rafiki zao, ila kupitia imani, Rahabu akawa shujaa wa Mungu na kuwadhihirishia makahaba na wadhambi wengine kuwa wanaweza kuurithi uzima wa milele na kuingia katika ufalme wa Mungu endapo wataamua kubadilika kikamilifu (Mathayo 21:3).  

            Kwa kuhitimisha habari za Rahabu, wakati mwingine jina hili huhusika na mnyama wa ajabu wa baharini (Ayubu 9:19; 26:12; 38:8-11; Zaburi 89:9-10) ama ni jina lingine la Misri (Zaburi 87:4; Isaya 30:7).

 Rebeka
            Rebeka ni mwanamke ambaye upendeleo wake  kwa mwanaye ulileta huzuni. Jina hili humanisha ‘kitanzi’ au ‘kamba ya kufungia wanyama’. Jina hili limehusishwa na ‘kumfunga mwanakondoo au ndama’. Maana nyingine ya jina hili ni ‘kiungo cha kitanzi’. Biblia inamtaja Rebeka kuwa, alikuwa mzuri sana wa uso na bikra (Mwanzo 24:16; Mwanzo 26:6). Rebeka alikuja akawa mke wa Isaka, na kipindi Isaka amemchukua Rebeka kama bibi harusi, alisahau kuhusu huzuni ya mama yake aliyefariki. Isaka na Rebeka, waliishi kwa furaha kwa miaka ishirini bila kuwa na watoto. Baadaye walizaa watoto wawili (mapacha),  Hesau akiwa kulwa  na Yakobo akiwa ni doto (Mwanzo 25:20-26).
            Rebeka alikuwa wa muhimu sana katika mipango ya Mungu ya kujipatia taifa kufuatana na ahadi aliyompa Ibrahimu (Mwanzo 22:15-18; Mwanzo 24:3-4, 67). Kuhusu familia yake, Rebeka kwa mara ya kwanza ametajwa kama mzaliwa katika kizazi cha Nahori ndugu yake Ibrahimu (Mwanzo 22:20-24). Bethueli, ambaye ndiye baba yake na Rebeka alikuwa miongoni mwa watoto wa Nahori na alikuwa na mke ambaye hakutajwa jina, hivyo, Rebeka alikuwa dada yake Labani (Mwanzo 24:29).
           Kwa kuwa Ibrahimu alikuwa kinyume na ibada za sanamu, alimuongoza mwanaye Isaka asioe binti wa Kikanaani maana walitokana na jamii inayofanya ibada kwa sanamu. Ibrahimu alimwagiza mtumishi wake amtafutie Isaka mke kwa jamaa zake na Ibrahimu (Mwanzo 24:3-4). Kupitia mtumishia wake Ibrahimu, Isaka alimuoa Rebeka. Kwa muda wa miaka ishirini, Rebeka alikuwa hana mtoto na alielewa juu ya ahadi ya Mungu kwamba, agano lililofanyika kipindi cha Ibrahimu hawezi Mungu kuacha kulitimiza. Na Isaka mumewe, aliamini kuwa ipo siku mkewe atabeba mimba.
           Baadaye iridhihirika kuwa, Mungu anawakati wake katika kujibu mahitaji ya wanadamu. Rebeka alibeba mimba na alijifungua watoto mapacha walioitwa Esau na Yakobo (Mwanzo 25:19). Rebeka alimpenda Yakobo zaidi kuliko Hesau, si vinginevyo, bali ni kwa mapenzi ya Mungu (Warumi 9:13; Waebrania 12:16). Ingawa Mungu alikuwa amemwambia Rebeka kwamba Agano lingetimizwa kupitia kwa mtoto wake mdogo (Mwanzo 25:23; Warumi 9:10-13), hakuwa na haki ya kufanya mbinu za hila ili kumdanganya Isaka mumewe. Mungu angetimiza mpango wake, bila yeye kufanya jambo lo lote ili kwamba Yakobo apate baraka ile (Mwanzo 27:6-29).
           Japokuwa Rebeka alikuwa mzuri, mwenye imani, mchapa kazi, kilichofunika haiba ya uzuri wake wote ni uongo na kuonesha upendeleo wa wazi kwa mtoto mmoja ulio kinyume na mapenzi ya Mungu (Mwanzo 27:46-28:1-7; Warumi 3:8, Yakobo 1:20; 1Petro 2:1). Kwa sababu ya upendeleo wake, Esau alipanga kumuua Yakobo, laini yeye Rebeka alifanya mpango wa kumlinda kwa kumtuma Yakobo kwa mjomba wake (kaka yake Rebeka) aliyeishi Padan-aramu. Wakati huo alimdanganya Isaka, mumewe kuwa amemtuma Yakobo ili akatafute mke miongoni mwa jamaa zake  (Mwanzo 27:41-28:5).
            Hatukupata ushahidi wo wote kama Rebeka alimwona mwanae mpendwa tena wakati mwingine hadi ulipomkuta umauti wake. Rebeka alipokufa alizikwa katika eneo la makaburi ambalo Ibrahimu alikuwa amelinunua kwa ajili ya familia yake (Mwanzo 49:31).

 Reuma
           Hili ni jina la kwanza la mwanamke katika Biblia kutajwa kama suria. Maana ya jina hili ni ‘aliyetukuka’. Hakuna cho chote kilichosemwa katika kutukuka kwa huyu mwanamke. Alikuwa mke (suria) wa pili wa Nahori, ndugu yake Ibrahimu. Reuma alikuwa mama wa watoto wanne waitwao Teba, Gahamu, Tahashi na Maaka (Mwanzo 22:24).

Roda
            Roda ni binti ama mwanamke aliyeitwa kichaa. Hili ni jina linalotoka katika lugha ya Kiyunani. Maana ya jina hili ni ‘uwa’ au ‘waridi’. Roda alikuwa kijakazi wa Mariamu (mama yake na Marko). Watakatifu wa Mungu waliokutana katika Nyumba ya Mariamu wakimuombea Petro alipokuwa amefungwa gerezani walimwita Roda “manias” sawa na ‘mwanamke mwenye wazimu’ (Matendo 12:12-16). Kama kijakazi mtumwa, hajaelezewa chimbuko la familia yake.
            Ilikuwa ni usiku wa manane, wakati Petro alipofika katika nyumba ya Mariamu na Roda aliye kijakazi katika familia ya Mariamu akaitikia wito wa hodi yake, hivyo inaonesha kuwa Roda alikuwa akiwajibika katika majukumu yake hata kwa muda wa ziada hasa nyakati za usiku. Kwa hili, Mariamu alijifunza kitu juu ya Roho kuhusu Bwana alivyofanya kazi kwa kijakazi wake, namna alivyoitambua sauti ya Petro alipokuwa akibisha hodi, ambapo wao walimdhihaki.
           Roda alijua kuwa ‘hutakiwi kumfungulia mtu mlango wakati wa usiku mpaka umemtambua yeye ni nani’, hivyo Roda aliitambua sauti ya Petro, kuwa ni yeye abishaye hodi. Roda alimuamini Mungu pamoja na nguvu ya maombi na hivyo hakuwa na shaka na sauti ya Petro, kuwa ni yeye na ameachiwa baada ya maombi ya watakatifu kusikilizwa na Mungu wa Mbinguni. Kuachiliwa huru kwa Prtro kulimfurahisha sana Roda, akaenda kuwapasha habari watakatifu wa Mungu waliokuwa wakimwombea Petro (Matendo 12:14). 

Rispa
           Jina hili linamaanisha ‘enye joto’ au ‘jiwe linalookwa’. Rispa alikuwa binti wa Aya, na alikuwa suria wa Sauli aliyemzalia watoto wawili (2Samweli 3:7). Jina la Aya limetajwa pia katika  Mwanzo 36:24; 1Nyakati 1:40,  (ambalo hatukuweza kulithibitisha kama ndilo jina la baba yake Rispa) akitokea upande wa Esau na alikuwa mtoto wa Sibeoni. Sifa ya pekee ya mwanamke huyu, alilinda  maiti za watoto wake waliouwa kwa kutundikwa na mfalme Daudi (2Samweli 21:8-11). Hivyo, Rispa alidhihirisha hisia na sifa za moyo wake safi wenye uvumilivu wa kuilinda maiti za watoto wake waliouliwa ili isiharibiwe na ndege ama wanyama. Mwanamke huyu aliaksi kile kilichonenwa katika Isaya 49:15 kuwa, “Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? .....”
Ruthu
             Huyu ni mwanamke aliyeinuka kutoka kwenye umasikini (giza) hadi utajiri (nuru). Mwanamke huyu anaelezewa katika kitabu chote cha Ruthu na Mathayo 1:5. Jina hili limetokana na neno “reuth” ambalo humanisha ‘kuona’. Ruthu ni mwanamke ambaye jina lake limebeba jina la kitabu cha Ruthu. Ruthu alikuwa ni binti wa Kimoabu aliyeolewa katika familia ya Kiebrania. Habari zake zilitokea wakati wa Waamuzi. Ruthu alikuwa mke wa mtoto wa Naomi na Elimeleki (rejea katika habari za Naomi). Baada ya Elimeleki na baadaye hata wana wawili walipokufa, Naomi na Ruthu walirudi Israeli. Walihamia mji wa nyumbani kwao Naomi, yani Bethlehemu (Ruthu 1:1-22).
             Kwa kuwa walikuwa na dhiki, Ruthu alikwenda kuokota masazo ya wavunaji ili apate chakula cha yeye na Naomi. Shamba alilokuwa akiokota lilikuwa ni la Boazi, jamaa wa karibu na marehemu mkwewe (Elimeleki). Boazi alipata habari za wema ambao Ruthu amemtendea Naomi, hivyo naye alimtendea wema (Ruthu 2:1-23). Tunakukumbusha kuwa, Boazi ni mtoto wa yule mwanamke aliyetajwa kuwa alikuwa kahaba aitwaye Rahabu, aliyekombolewa na Waisraeli wakati wakiuangamiza mji wa Yeriko. Ni Rahabu yule yule ambaye jina lake limeonekana katika orodha ya wazazi wa Yesu, Boazi alitokana naye (Yoshua 6:17; Ruthu 4:18-22; Mathayo 1:1, 5).
             Kwa kuwa Boazi alimcha Mungu, alifanya bidii  ya kumpa Ruthu thawabu kwa kuwa naye alimfanyia  wema mkwewe ambaye pia alikuwa mjane (Ruthu 2:11-12). Alimlinda na vijana wa mahali pale (Ruthu 2:8-9, 22), alimpa chakula na kinywaji wakati wa kazi yake ya mchana (Ruthu 2:9, 14), alimpa nafasi ya kuokota masazo ya wavunaji (Ruthu 2:16-22) na kumpa ziada ya  ya riziki ya nafaka (Ruthu 3:15). Boazi, hakuonesha ubaguzi wa kikabila, kwa kuwa Ruthu alikuwa Muamoni, ambao tangu na tangu palikuwepo na uadui wa kijadi baina ya Waisraeli na Waamoni (Ruthu 2:6, 10).
            Naomi alimshauri Ruthu amwombe Boazi amzalie mtoto ambaye, kufuatana na desturi angehesabiwa kuwa mtoto wa mumewe aliyekufa. Hivyo, mtoto yule angekuwa na kuchukua jina na urithi wa mume wa mjane huyo. Ruthu alitii ushauri wa mkwewe na alipomuomba Boazi ahifadhi jina la mumewe aliyefariki kwa njia ya kutimiza wajibu wa jamaa wa karibu, Boazi aliitikia vizuri. Boazi alifurahi, kwa sababu alipenda kumuoa Ruthu, naye alilidhika kumzaa mwana na mrithi kwa njia yake. Hivyo basi, Ruthu aliolewa na Boazi na mtoto aliye mzalia alikuja akawa babu wa mfalme Daudi na mmojawapo wa wazazi wa Yesu aliye Masihi (Ruthu 4:18-22; Mathayo 1:1, 5).
           Ruthu aliyemhusika mkuu katika kitabu cha Ruthu, kupitia yeye, Boazi na Naomi, kitabu cha Ruthu katika Biblia kinatoa dondoo nyingi za kujenga katika ufahamu mpana wa mahusiano ya uchumba na ndoa kwa Wakristo. Kama alivyoelezewa katika kitabu cha Frank P. Karoli, katika kitabu kinachoitwa “Mwongozo katika Uchumba na Maisha ya Ndoa” na “Mwongozo katuka Urafiki na Uchumba” kuwa, yapo mambo kadhaa ya kujifunza katika kitabu cha Ruthu, kuhusu masuala ya uchumba ili kuielekea ndoa ndoa:
1.      Mchumba mwema ni yule mwenye tabia ya kutii na kufuata maelekezo ya wazazi au walezi yaliyo na tija (Ruthu 3:1-12).
2.      Mchumba wa kweli lazima aoneshe nia ya kuoa au kuolewa naye huyo mchumba (Ruthu 3:8-9).
3.      Mchumba mwema ni yule mwenye kuonesha tabia ya kujali watu wengine (Ruthu 2:5).
4.      Mchumba mwema ni yule mwenye tabia ya kuhurumia na kusaidia wengine (Ruthu 2:8).
5.      Mchumba yampasa awe na tabia ya kuheshimu na kuonesha unyenyekevu (Ruthu 2:10).
6.      Mchumba mwema ni yule mwenye tabia ya ukarimu (Ruthu 2:14, 16).
7.      Mchumba mwema ni mwenye kumtumainia Mungu kwa kila jambo katika maisha yake (Ruthu 2:20).
8.      Mchumba mzuri ni yule aliye msafi na nadhifu na sio kwa sababu ya mapambo (Ruthu 3:3).
9.      Mchumba mzuri ni yule mwenye washauri wema ili kufanikisha uchumba na siyo kuubomoa (Ruthu 3:1-2).
10.  Uchumba wa kweli hauhusishi ngono kabla ya ndoa (Ruthu 3:7-9).
11.  Mchumba mwema ni yule aliye mwaminifu na watu wamshuhudie hivyo pia (Ruthu 3:11).
12.  Uchumba wa kweli hauangalii vitu, talanta ama mali bali upendo ulio wa dhati (Ruthu 3:10).
13.  Uchumba lazima uwe wa wazi kwa ndugu, jamaa na marafiki (Ruthu 4:9-11).
14.  Uchumba wa kweli wenye uaminifu, huzaa ndoa yenye mibaraka (Ruthu 4:13).

            Kwa kuhitimisha habari za Ruthu, twaweza sema kuwa, Ruthu alikuwa: mwenye upendo na ukarimu kwa wengine, mwaminifu, asiye mbinafsi, mjane aliyekuja kuolewa, alijitambua, alimcha Mungu, mnyenyekevu na mwanamke au mama aliyekuja kupata heshima kubwa (Ruthu 1:16, 17; Torati 7:3; Ruthu 2:11-12, n.k.)

(a) Salome
            Jina hili ni lakike linalofanana maana na jina la Sulemani, limetokana na muundo wa neno katika lugha ya Kiyunani la ‘Shalomu’ ambalo humanisha ‘amani’. Salome huyu ni mwanamke ambaye kucheza kwake kulisababisha kifo cha Yohana Mbatizaji (Mathayo 14:6-11, Marko 6:22-28). Jina lake halijulikani sana, maana ni kana kwamba halikutajwa moja kwa moja. Lakini katika kumbukumbu za utawala wa Kirumi, jina hili lipo bayana. Hivyo, kuhusu familia atokayo, alikuwa binti wa Herodia kutoka kwa mume wake wa kwanza  aitwaye Filipo, mwana wa Herode mkuu.
            Kama tulivyoona katika habari za Herodia huko mwanzo, nikuwa, wakati ambapo Herode Antipa alipotembelea Rumi, alivutiwa na Herodia aliyekuwa mke wa Filipo ndugu yake. Herode Antipa alimpa talaka mke wake na kumuoa Herodia mke wa ndugu yake bila kupewa talaka. Katika kuikemea dhambi hii Yohana Mbatizaji, ilimsababishia kutupwa gerezani, (Marko 6:17-18). Kwa hiyo, wakati Herodia anamuacha mumewe wa kwanza aitwaye Filipo, alikuwa amezaa naye mtoto wa kike aitwaye Salome na aliletwa na mamaye kuishi Ikulu ya Herode.
            Siku ya sherehe ya kuzaliwa kwake Herode, Salome binti Herodia, Salome alicheza vizuri sana na alimfurahisha Herode, baba yake asiye wa kufikia. Herode alimwambia aombe zawadi yo yote, mama yake alimshawishi Salome aombe zawadi ya kichwa cha Yohana Mbatizaji, na Herode kwa shingo upande akafanya hivyo (Marko 6:21-28;  Mathayo 14:6-11).

(b) Salome
             Jina hili linatajwa katika Marko 15:40-41 na Marko 16:1-2. Huyu ni mwanamke ambaye watoto wake (Yohana na Yakobo) walitaka mema kutoka kwake, walimuomba aende kuwaombea cheo kwa Yesu atakapokuwa mfalme (Mathayo 20:20-24; Marko 10:35-40). Maandiko matakatifu yapo kimya kuhusu uzao ama familiya aliyotokea mwanamke huyu. Zaidi kinachofahamika ni kuwa, alikuwa mke wa Zebedayo, mvuvi aliyefanikiwa na alikuwa ameajiri wafanyakazi (Marko 1:19; Mathayo 4:21). Yeye na familia yake waliishi pwani ya Ziwa Galilaya ambo mumewe na wanae walifanya kazi ya uvuvi wa samaki
            Tunathitisha kuwa, Salome ndiye mama yao wana wa Zebedayo au mama yao na Yohana na Yakobo, ambaye pia alikuwa mke wa Zebedayo.  Salome anaye tajwa katika Marko 15:40, ndiye aliyetajwa kama mama yao wana wa Zebedayo katika Mathayo 27:56. Inaonesha Salome alijitoa kikamilifu kwa Yesu na alikuwa miongoni mwa wale aliomfuata Yesu kule Galilaya na alionekana akiwa na Mitume wa Yesu tangu mwanzo wa huduma ya Yesu katika hadhara ya watu (Marko 15:40, 41; Mathayo 27:56). 
            Inaonesha kama Salome alikuwa dada au ndugu yake na Mariamu, mama wa Yesu (Mathayo 27:56; Marko 15:40; Yohana 19:25-27). Salome pamoja na mumewe, waliwaandaa watoto wao kwa ajili ya kumfuata Yesu. Salome alikuwa pia miongoni mwa wale wanawake waliokuwa wamekwenda kuupaka mafuta mwili wa Yesu, na badala yake hawakuukuta mwili wa Yesu. Walikutana Malaika, akawambia, Yesu amekwisha fufuka nao wakazipeleka taarifa kwa Mitume (Luka 24:1-12).
            Watoto wake walikuwa wenye hasira kali, Yesu mwenyewe mara nyingi alikuwa akiwataja kama “wana wa ngurumo” (au boanerge), labda kwa sababu mara nyingine hawakuweza kuvumilia katika bidii yao (Marko 3:17; Marko 10:35-40; Luka 9:49-56). Kutokana na tabia hiyo,Yesu aliwakanya (Luka 9:51-65). Kwa kuwa Yesu alikuwa amesha wajuza Yohana na Yakobo kuwa wangeweza kutazamia  aina ya mateso  kama yeye alivyokuwa akitazamia. Kwa Yakobo, jambo hili lilitokea baada ya miaka michache, ambapo Herode Agripa alipomkata kichwa (Mathayo 20:20-24; Matendo 12:1-2).

Safira
            Jina hili ni la Kiebrania linalomanisha ‘kito cha thamani’. Safira ni mwanamke aliyekufa kwa sababu ya udanganyifu wa yeye na mumewe na alikuwa mwanamke wa kwanza kutotii kipindi cha kanisa la awali la Kikristo. Wakati wa kuanza kwa kanisa la awali lililokuwa chini ya Mitume, waumini walikuwa wakijitolea na kuuza mali zao ili kulitegemeza kanisa na watenda kazi wake. Vitu vyote vya waumini wa awali vilikuwa ni shirika.
           Tofauti na alivyofanya Barnaba, Safira na mumewe baada ya kuuza walificha sehemu ya fedha, hivyo kwa udanganyifu wao umauti uliwakuta (Matendo 4:32-34: Matendo 5:1-11). Yeye na mumewe walikuwa watu wenye nia mbili (Yakobo 1:8; Tito 2:10); walifanya sawa sawa na Akani aliyechukua vitu baadhi  vilivyotiwa wakfu kwa ajili ya Bwana (Yoshua 7:1).

Sara (Sarai)
           Sara ni mwanamke aliyekuja kuwa mama wa mataifa mengi. Kuhusu familia atokayo, Sara alitokea Uru wa Wakalidayo (Babeli au Mesopotamia), na jina lake la Sarai lilimanisha ‘binti mfalme’, hivyo yawezakuwa alitokea katika familia yenye ufahari fulani. Wanazuoni baadhi wa Biblia hudai kuwa, Sara alikuwa binti wa Tera na dada asiye wa kufikia wa Ibrahimu (upande wa mke mwingine wa Tera, asiye mama yake na Ibrahimu). Hivyo, Ibrahimu alimuoa Sara aliyekuwa mtoto wa mama yake wa kambo. Wanazuoni hao huitumia Mwanzo 11:29, kuwa tera naye alimuoa Milka aliyekuwa binti wa ndugu yake wa baba mmoja (Tera).  Ibrahimu aliyekuja kuwa mumewe, alimzidi Sara miaka kama kumi hivi (Mwanzo 17:17).
            Sara alipoolewa na Ibrahimu katika nchi ya Mesopotamia, jina lake lilikuwa Sarai na jina la Ibrahimu mumewe lilikuwa Abramu. Mungu aliwapa majina mapya, Abramu aliitwa Ibrahimu, na Sarai aliitwa Sarai. Ibrahimu maana yake ‘Baba wa mataifa mengi’, na Sara maana yake  ‘Binti mfalme’ au  ‘mama wa mataifa’. Mungu aliwaita majina haya ili ithibitike kuwa  wangekuwa wazazi wa taifa kubwa, yaani Israeli (Mwanzo 11:29; Mwanzo 17:5-6, 15-16; Isaya 51:2). Kutoka Mesopotania Mungu aliwangoza Ibrahimu na Sara mpaka nchi ya kanani, yaani nchi aliyowaahidi kwamba ingekuwa makao maalumu ya Waisraeli (Mwanzo 12:1, 5-8).
           Mungu alikuwa amewaahidi Ibrahimu na Sara kwamba, watapata mtoto, ingawa kwa miaka mingi hawakumpata. Kwa kadri walivyoendelea kuzeeka, ndivyo ilivyoonekana vigumu zaidi kwa Sara  kuzaa mtoto, na hivyo Sara alimshauri Ibrahimu kuwa amjue kijakazi wao, Hajiri ili wajipatie mtoto kupitia yeye. Mtoto alizaliwa, lakini Mungu alimwambia Ibrahimu hakuwa mwana aliyekuwa amemuahidi (Mwanzo 16:1-4, 15; Mwanzo 17:18-19).  Sara aliona ni vigumu kwa yeye aliye mzee kuweza kuzaa  mwana, na hivyo Mungu alituma wajumbe (Malaika) kutoka mbinguni ili wamwaminishe, kwa maana Sara ilimpasa kushiriki imani ya mumewe (Mwanzo 18:10-14).
            Mwaka uliofuata, Ibrahimu akiwa na miaka mia moja na sara miaka tisini hivi, Sara alimzaa Isaka, mwana ambaye Mungu alikuwa amemwahidi (Mwanzo 17:17, 19, 21; Mwanzo 21:1-5). Hivyo, imani ya Ibrahimu na Sara ilikuwa imepimwa kwa muda wa Miaka ishiri na tano (Mwanzo 12:4), nayo ilionekana kuwa imara na yenye uvumilivu (Warumi 4:17-21; Waebrania 11:11-12).  Hapo nyuma migogoro ilitokea baina ya Sara na Hajiri (Mwanzo 16:4-9), lakini iliisha. Ilipotokea tena, Sara alimwambia Ibrahimu amfukuze Hajiri na mwanaye kutoka nyumbani kwake (Mwanzo 21:10).
            Japokuwa Sara alimheshimu Ibrahimu kama mkuu wa familia yao, pia alikuwa na neno  maalumu katika maamuzi ya kifamilia, na ndiyo maana Mungu alimwambia Ibrahimu afanye kadri ya maneno ya Sara (Mwanzo 21:12, linganisha na 1Petro 3:6). Isaka peke yake alitakiwa awe mrithi wa ahadi ambazo Mungu alizitoa  kuhusu wateule wake na nchi yao. Sara aliishi mpaka alipoweza kumwona mwanaye akikua na kuwa kiongozi mwenye madaraka. Isaka alipokuwa na umri wa miaka 37 hivi, sara alikufa (Mwanzo 32:1, 19). Yafuatayo ni mambo kadhaa muhimu ya kutazama kwa Sara:
            Upekee wa Sara: Kupitia kwa mumewe, Sara alikuwa mwanamke wa kwanza kuitwa Muebrania, hivyo akajichukulia nafasi ya kuwa mwanamke mhimu katika historia hasa katika chanzo cha Waebrania. (Mwanzo 14:13). Neno Muebrania humanisha ‘aliyehamia’ (tazama Mwanzo 11:31; Isaya 51:2). Baada ya dhambi kuingia duniani, Sara atajwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwa na imani juu ya Mungu na anafuatiwa na Rahabu (Waebrania 11:11, 31), na wote waliishi na kufa katika kuamini (Waebrania 11:13).
            Uzuri wake: Sara alikuwa mzuri kuliko kawaida  (Mwanzo 12:11, 14). Hata katika umri wa miaka tisini, bado Sara aliku mzuri, na ndiyo maana Ibrahimu aliogopa kumtambulisha  kwa mfalme  (Farao) kuwa Sara ni mkewe maana alidhani mfalme angempenda, hivyo Ibrahimu aliye mumewe angeuliwa (12:12-20).
            Huzuni yake: Kutokana na utasa aliokuwa nao Sara, ulimletea huzuni kubwa, na hivyo imani ikamtoka kwa kuwa aliona hatazaa kabisa. Kutokana na hali hiyo, alimshawishi mumewe ajipatie uzao kwa kijakazi wao, Hajiri  (Mwanzo 11:30; Mwanzo 16:1-8).
            Tunajifunza kuwa: Mungu ndiye mwenye uweza wa kuwapa watoto hata walio vikongwe endapo tumaini la mtu lipo juu ya Mungu (Mwanzo 17:15-17). Fikara za mwanadamu hukoma, lakini Mungu Yeye ni muweza wa yote. Mungu hutupatia hitaji zetu pale tunapokuwa tumeshindwa katika kutumia maarifa, nguvu na uweza wetu binafsi ili tu utukufu tumulejeshee Yeye. Mtoaji wa watoto kwa wanandoa ni Mungu na si vinginevyo. Pale wanandoa wanapokosa mbaraka wa watoto, wavumilie na wadumu katika kumuomba Mungu.
            Umri wake: Sara alikuwa ni mwanamke wa kwanza na miongoni mwa wanawake wachache waliotajwa umri wao katika Biblia. Mwanamke ambaye ni binti mdogo aliyetajwa umri yupo katika Luka 8:42. Sara alijiita mwenyewe kuwa ni mzee kipindi akiwa na umri wa miaka themanini na saba (Mwanzo 18:12), lakini alifariki akiwa na miaka miamoja ishirini na saba (127) na Ibrahimu mumewe  alifariki akiwa na umri wa miaka mia moja sabini na tano.
            Mfano wake: Ukipitia kwa kina mafungu yaliyo katika mabano, utaona namna Sara au Ibrahimu mumewe alivyotumika kama kielelezo kwa mambo kadhaa ya imani, kiroho na utimilifu wa unabii (Wagalatia 4:21-31, Waebrania 11:11, 12; Warumi 4:11; Wagalatia 3:7; Mwanzo 18:12;1Petro 3:6).

Sera
            Jina hili linamaanisha ‘tele’ au ‘wingi’. Huyu alikuwa binti wa Asheri, na mjukuu wa Yakobo kupitia kwa kijakazi wa mke wake Lea aitwaye Zilpa (Mwanzo 46:17; 1Nyakati 7:30). Kwa hiyo, Asheri alikuwa mtoto wa Yakobo kwa Zilpa, kijakazi wa Lea mkewe Yakobo. Na Asheri alizaa wana wa Kiume wa nne na wakike mmoja aitwaye Sera.

(b) Shelomithi
           Jina hili limetokana na neno “shelomi” likimanisha ‘amani yangu’ (Hesabu 34:27).  Neno shelomithi au shelumiel humanisha ‘Mungu ni amani’ (Hesabu 1:6; 7:36).  Hivyo basi, jina hili humanisha  ‘mwenye amani’. Kwa mujibu wa Mambo ya Walawi 24:10-14, jina hili lilikuwa ni jina la binti yake Dibri wa kabila ya Dani katika kipindi cha Musa aliyeolewa na mwanamume wa Kimisiri ambaye hakutajwa jina kwa sababu isiyostahili, labda ni kwa sababu iliyopo katika  2Wakorintho 6:14, 15.  Binti wa mwanamke huyu alipondwa mawe akafa kwa sababu ya kulikufuru jina la Mungu kwa kujiapiza ndani ya marago (Mambo ya Walawi 24:11-12, 14).

 (b) Shelomithi
            Mwanamke huyu alikuwa ni binti wa Zerubabeli, hivyo Shelomithi huyu, alikuwa umbu (dada) wa Meshulamu na Hanania (1Nyakati 3:19). Zerubabeli ambaye ni baba wa mwanamke huyu siyo Zerubabeli mkuu au Mfalme aliye waongoza Wayahudi kurudi nyumbani, wakitokea uhamishoni Babeli (Mathayo 1:12; Luka 3:27). Jina hili pia ni jina la kiume (1Nyakati 23:18; 23:9; 26:25, 28; Ezra 8:10). Na Shelomithi ambaye ni mtoto wa Maaka anayetajwa katika 2Nyakati 11:20, haijulikani kamba ni wa kike au wa kiume.

Sheera
            Jina hili linamaanisha  ‘uhusiano wa mwanamke kupitia damu’. Sheera alikuwa ni binti wa  Ifraimu, ambaye yaweza kuwa alikuwa na nguvu nyingi (ya kimwili au kiuchumi au kiutawala), aliyejenga vijiji (miji) vitatu na kisha alivipokea kama urthi na alijipanua kifamilia kwa sababu fulani (1Nyakati 7:23-24). Yaweza kuwa miji miwili aliyoijenga mwanamke huyu ilikuja ikatekwa au kuchakaa, na katika utawala wa Sulemani alienda kuikomboa au kuijenga upaya (2Nyakati 8:5).  


Shimeathi
            Maana ya jina hili humanisha ‘umaarufu’. Shimeathi alikuwa ni mama wa Yozakari au Zabadi aliyekuwa mmoja kati ya wahudumu wa nyumba ya mfalme Yoashi, ambao walitenda fitina ya kumuua Yoashi. Mwanamke huyu alikuwa Muamoni, yumkini uovu wake waweza kuwa ulichagiza kummbadilisha hata mtoto wake wa kiume (2Wafalme 12:21; 2Nyakati 24:26).

Shifra
            Maana ya jina hili ni ‘zaa’ au ‘kuzaa sana’. Kupitia kwa Pua, tunamuona mwanamke huyu aliyekuwa mkunga, na kupitia kushiriki kwake alihatarisha maisha yake katika kuokoa watoto wa kiume waliozaliwa na  wanawake wa Kiisraeli nchini Misri. Shifra pamoja na Pua walikuwa mstari wa mbele katika kuzalisha ili kuokoa uhai wa vichanga toka tumboni mwa mama zao (Kutoka 1:15).

Shomeri (Shimrithi)
            Shomeri na Shimrithi ni majina mawili yanayotumika kwa mtu mmoja katika sehemu tofauti katika Biblia, Agano la Kale. Jina hili linamanisha “mtunza’ au ‘aliyelindwa na Bwana’. Mwanamke huyu alikuwa Mmoabu na mama wa kijana mmoja wa Kimoabu aitwaye Yehozabadi, ambaye pamoja na Zabadi, mtoto wa mwanamke aitwaye Shimeathi walimuua kwa upanga mfalme Yoashi alipokuwa amelala kitandani (2Wafalme 12:21; 2Nyakati 24:26).
Shua
            Jina hili la Shua linaasiri ya Kikanaani likimanisha ‘tajiri’, ‘mashuhuri’ au ‘mafanikio’. Shua alikuwa binti wa Heberi, mjukuu wa kiume wa Asheri na pia alikuwa dada wa Jafteti, Shomeri na Hothamu. (1Nyakati 7:32). Shua mwingine  ni yule mke wa Yuda, aliyekuwa Mkanaani (Mwanzo 38:2, 12; 1Nyakati 2:3). Shua ni jina pia lililotumiwa na wanaume kadhaa katika Biblia, Agano la Kale.

Susana
            Maana ya jina hili ni ‘eupe pee’ au ‘iliyo safi kabisa’.  Susana alikuwa miongoni mwa wanawake ambao Yesu aliwaponya kimwili na kiroho na kuamini kwao walimfuata Yesu pamoja na wanafunzi wake. Katika tukio hili ndipo Mariamu Magdale alipotolewa mapepo saba. Paoja na Mariamu Magdalene, wanawake wengine waliotajwa majina yao na Luka katika tukio hili la uponyaji la Yesu ni Yoana mkewe Kuza na Susana mwenyewe. Wanawake wote walioponywa na Yesu katika tukio hili, walikuwa wakimhudumia Yesu kwa mali zao (Luka 8:2, 3). 
Sintike
            Maana ya jina hili ni ‘bahati njema’. Sintike ni mwanamke aliyekuwa miongoni mwa watumishi wa kanisa la awali huko Filipi. Kama siyo  msisitizo wa kudumisha umoja wao, labda yaweza kuwa Sintike na Eudia walikuwa wametofautia katika utumishi na ndiyo maana Paulo katika waraka anawasihi wawe na nia moja katika Bwana (Wafilipi 4:2). Paulo anaendele kusisitiza kuwa, wanawake hao wasaidiwe kwa kuwa waliishindania Injili pamoja na yeye (Wafilipi 4:3).

Serua
            Maana ya jina hili humanisha ‘ukoma’. Mwanamke huyu alikuwa mama yake Yeroboamu, aliyekuja kuwa mfalme wa kabila kumi za Israeli kwa kutumia nguvu ya uasi baada ya Sulemani kufariki. Serua aliolewa na Nebati wa Sereda, ambaye alikuwa mtumishi katika utawala wa Sulemani. Ametajwa pia kama mwanamke mjane, baada ya mumewe kuuliwa kwa sababu watoto wake walienda kinyume na mfalme (1Wafalme 11:26).   

Seruya
            Jina hili humanisha ‘dawa kutoka kwa Yehova’. Seruya alikuwa dada yake Daudi, alikuja akawa mama wa Abishai, Yoabu na Asaheli ambaye mara zote hurejerewa kama  “mtoto wa kiume wa Seruya”. Watoto wa Seruya walitaka kuonekana katika historia ya Waisraeli kipindi cha utawala wa Mfalme Daudi (2Samweli 17:25; 1Nyakati 2:16).

Sibia
            Mwanamke huyu alijulikana kama Sibia wa Beer-sheba. Jina hili humanisha ‘swala jike’. Sibia alikuwa binti wa mfalme wa Yuda, na jina lake lilibeba mkitadha wa neema au uzuri. Sibia aliolewa na mfalme Ahazia na kumzalia mtoto aitwaye Yehoashi au Yoashi ambaye aliokolewa katika kuuliwa kipindi cha utoto wake. Yoashi naye alikuja akawa mfalme wa Yuda na alitawala kwa miaka arobaini, kipindi hicho Yehoyada akiwa kuhani (2Wafalme 12:1; 2Nyakati 24:1).

Sila
            Maana ya jina hili ni ‘kivuli cha giza’ au ‘kivuli cha ulinzi’. Sila alikuwa mke wa pili wa Lameki (mzaliwa wa tano kutoka kwa Kaini), na ndiye mama wa Naama. Naama ni mtoto wa kike wa kwanza kutajwa jina lake kwenye Biblia. Maana ya jina hili la Naama ni  ‘upendo’. Sila pia ndiye mama wa Tubai-kaini aliyekuwa mgunduzi wa kwanza wa uhunzi (ufuaji wa vyuma na shaba) na mtengeneza vifaa vitokanavyo na vyuma na shaba (Mwanzo 4:19-22).

Sipora
            Maana ya jina hili la Sipora ni ‘ndege mdogo’ au ‘shomoro’. Sipora alikuwa miongoni mwa mabinti saba (yeye akiwa binti mkubwa) wa Yethro aitwaye pia Reueli na Regueli (Kutoka 2:18; Hesabu 10:29). Ni katika familia atokeayo binti huyu ambapo Musa alifikia (na kuishi) akiwa mwenye umri wa miaka arobaini alipokuwa amekimbia kutoka Misiri. Wakati Musa akitokea Misri (baada ya kuua huko) alikutana na binti saba wa Yethro (na Spora alikuwepo), wakichota maji na Musa akawasaidia (Kutoka 2:11-20). Baba yake aitwaye Yethro  alikuwa Kuhani wa Midiani. Sipora alikuja akaolewa na Musa na kumzalia watoto wawili wa kiume, Gershomu na Eliezeri (Kutoka 2:21-22; kutoka 18:2-4)

Tapenesi
            Tapenesi ni jina linalomanisha ‘mkuu wa enzi’ au ‘mkuu wa zama’ au ‘mkuu wa kizazi’. Jina hili ni la malkia au mke wa mfalme wa Misiri (Farao) katika zama za utawala wa mfalme Sulemani. Dada yake Tapenesi aliolewa na Hadadi mzao wa mfalme wa Edomu alipokuwa amekimbilia Misri. Baada ya Hadadi kutoka Misri alikuja akawa mfalme wa Edomu pia. Dada huyu wa Tapenesi ambaye hakutajwa jina, alikufa wakati akijifungua  na Tapenesi akawa mlezi wa huyo mtoto aitwaye Genubathi. Alimlea na kumkuza kama mwanaye wakuzaa (1Wafalme 11:19, 20).

(a) Tamari
            Huyu ni mwanamke mwenye historia inayotia ukakasi kulingana na njia aliyotumia ili kujipatia mtoto. Jina hili la Tamari humanisha ‘mtende’. Kama ilivyo thamani ya mtende kuliko miti yote ipatikanayo mashariki ya kati, katika kufikirika, yaweza kuwa uzuri wa Tamari ulisadifu uzuri na thamani ya mtende. Ukiachana na umuhimu wa jina hili, kuna mambo mengi ya muhimu ya kufahamu kwa Tamari huyu. Biblia ipo kimya kuhusu familia ambayo Tamari ametokea, zaidi tu ya kumtaja kama Mkanani na aliolewa katika familia ya Yuda.
            Mara ya kwanza Tamari aliolewa na Eri, mtoto wa kwanza wa Yuda kwa Shua. Tamari hakuendelea kuwa mjane kwa muda mrefu, kulingana na taratibu za Kiebrania  aliolewa na mtoto wa pili  (katika familia hiyo) wa Yuda ili aweze kuendeleza uzao wa ndugu yake aliyefariki.  Hivyo, Onani alikuwa mume wa pili wa Tamari, na hakutimiza takwa kwa kaka yake aliyekufa katika kumuendelezea uzao wake kwa mke aliyemuacha. Kushindwa  kwa Onani kutimiza agizo la kisheria la Kiebrania hivyo alipatwa na umauti kwa kosa hilo. Na Shela akishakuwa mkubwa, alitakiwa awe mume wa tatu wa Tamari kama sheria ilivyohitaji (Mwanzo 38:6-11; Torat 25:5-6; Mathayo 22:24).
            Baada ya Yuda kufiwa mkewe na Tamari kuona kwamba, Shela amekwisha kukua na wala hakuozwa ili awe mumewe, Tamari alitengeneza mazingira ya kulala na mkwewe (Yuda).  Siku moja Tamari alipojua kuwa mkwewe atapitia njia fulani akiwa anaenda kukata manyoya ya kondoo zake maeneo ya Timna, alitoa nguo zake za ujane, akavaa nguo zingine kisha akajifunika kwa ushungi usoni mwake. Kwa sababu ya tamaa zake za kimwili na bila kujua kuwa ni Tamari mkwewe (akidhania ni kahaba), Yuda alilala na Tamari. Kwa kuwa Yuda alimwahidi kumpatia mwana-mbuzi mwanamke wakati wa kurudi kutoka Timuna, hivyo alimwachia rehani ya pete yake ya muhuri, kamba yake na fimbo yake (Mwanzo 38:12-19).
            Yuda alimchulia yule mwanamke mwana-mbuzi ili akakomboe vitu vyake alivyomuachia. Alipofika maeneo hayo, hakumkuta yule mwanamke. Aliulizia wenyeji wa eneo hilo, ikaonekana hakuna anayemfahamu kahaba yule. Baada ya miezi mitatu, Yuda akapewa habari ya kuwa mkwewe anaujauzito uliotokana na uzinzi. Kabla ya kuuwawa, kwa maagizo ya Yuda, Tamari alijieleza, na kutoa vile vitu vya Yuda mkwewe kama vielelezo vya ushahidi vya mtu aliyelala naye na akampatia mimba. Yuda alikiri mbele ya kadamnasi kuwa, alifanya kosa la kutomwozesha kwa Shela kama alivyokuwa amemwahidi hapo mwanzo (Mwanzo 38:20-26). Tamari alijifungua watoto mapacha waitwao Peresi na Zera (Mwanzo 38:27-30; 1Nyakati 2:4; Mathayo 1:3).
            Japokuwa kisa kizima cha Tamari ni chenye fedheha, aibu, udanganyifu, hila na uvunjifu wa sheria za Mungu, Rehema ya Mungu ilichukuwa mkondo wake baina ya Yuda na Tamari. Na kupitia miongoni mwa watoto waliozaliwa kati ya Yuda na Tamari, Peresi alikuja akawa shina la kuzaliwa kwa Yesu Masihi (Mathayo 1:3). Hivyo, Tamari ni mwanamke wa kwanza miongoni mwa wanawake wachache waliotajwa na Mathayo katika kitabu cha ukoo wa Yesu, kama bibi zake na Mwokozi wetu Yesu Kristo (Matayo 1:3, 5, 6, 16).   
(b) Tamari
            Huyu ni mwanamke aliyetendewa sivyo na kaka yake wa kambo. Tamari huyu alikuwa binti mzuri wa Daudi na Maaka (1Nyakati 3:9), na dada wa Absalomu na dada wa kambo wa Amnoni aliyekuwa mtoto wa Daudi kwa mke mwingine aitwaye Ahinoamu. Kutokana na uzuri aliokuwanao Tamari, kaka yake wa kambo aitwaye Amnoni alimtamani kimapenzi. Kwa kuchochewa na ushauri mbaya wa rafiki yake aitwaye Yonadabu, Amnoni alimhadaa Tamari amletee chakula akijifanya anaumwa kisha akalala naye kwa nguvu. (2Samweli 13:1-21).
           Kutokana na kosa hilo, Daudi alishindwa kutekeleza matakwa ya sheria kwa kosa alilolitenda Amnoni kwa dada yake sawa na Mambo ya Walawi 18:9, 11. Absalomu alimchukia Amnoni kwa kumlazimisha Tamari dada yake kulala naye. Baada muda Absalomu alilipiza kisasi kwa kumuuua Amnoni (2Samweli 13:22, 28-32).

(c) Tamari
            Tamari huyu anayetajwa kuwa alikuwa mzuri wa uso ni binti wa Absalomu na mjukuu wa Daudi (2Samweli 14:27). Absalomu alimwita binti yake jina hili kama kumuenzi dada yake mzuri aliye twezwa kwa nguvu na Amnoni. Tamari huyu alikujakuolewa na Urieli wa Gibea, na alimzaa Maaka, aliyekuja kuolewa na Rehoboamu, mfalme wa Yuda, akamzalia mwana aitwaye Abiya aliyekuja naye kuwa mfalme wa Yuda (1Wafalme 15:2; 2Nyakati 11:20-22; 2Nyakati 13:2). Tamari pia ni jina la mahali au mji kama ulivyotajwa na nabii Ezekieli (Ezekieli 47:19; Ezekieli 48:28, angalia pia 1Wafalme 9:18; 2Nyakati 20:2).

Tafadhi
            Maana ya jina hili ni ‘tone la manemane’. Tafadhi ni miongoni mwa majina machache katika Biblia yaliyohusianishwa na manukato. Huyu ni mwanammke pekee aliye na jina hili. Tafadhi alikuwa binti wa Sulemani ambaye aliolewa na mtoto wa Abinadabu aliyekuwa akida katika Nafath-dori yote (1Wafalme 4:11).

Timna
            Maana ya jina hili ni ‘kizuizi’ (restrait).   Biblia inawataja wanawake wawili wanaotumia jina hili. Timna wa kwanza ni suria wa Elifazi, mtoto wa kiume wa Esau, ambaye alikuja akawa mama wa Amaleki. Inasadika kuwa, alichukuliwa kama mateka kipindi cha vita ya Waedomu na Wahori. Anajulikana kama dada yake na Lotani (Mwanzo 36:12, 22; 1Nyakati 1:39). Timna wa pili ni mwanamke aliyekuwa binti wa Timna ya zamani.
Tirsa
            Jina hili la Tirsa linamanisha ‘kupendeza’. Tirsa alikuwa miongoni mwa binti za Zelofehadi waliodai urithi wa baba yao kwa Musa, kwa kuwa baba yao hakuwa na mtoto wa kiume ambaye angestahili kuchukua urithi (Hesabu 26:33). Jina hili pia ni jina la mji uliotwaliwa na Yoshua katika (Yoshua 12:24).

Trifaina na Trifosa
            Majina haya yanatokana na mzizi au muundo wa neno wa aina moja, hivyo humanisha‘laini’, ‘nyororo’, ‘dhaifu’, au ‘tepetevu’. Kwa jinsi ambavyo Paulo amewaunganisha pamoja wanawake hawa wa Kikristo, unaweza ukadhani kuwa ni mwanamke mmoja. Labda yaweza kuwa ni mapacha wa kuzaliwa au kuzaliwa katika Kristo, au walikuwa ndugu miongoni mwa familia yenye heshima huko Rumi. Wanawake hawa walifanya pamoja kazi ya kanisa la awali huko Rumi na ndiyo maana Paulo hakuweza kuwatenganisha katika kujitoa kwao kwa ajili ya Bwana (Warumi 16:12).
           Inaonesha ya kwamba, wanawake hawa waliishi kiudhaifu dhaifu labda kwa sababu ya maisha ya anasa waliyokuwa nayo ama matatizo ya kimwili.

Vashti
            Kwa kuzaliwa, Vashti alikuwa mtoto wa mmoja wa mfalme wa Uajemi. Jina hili la Vashti linamaanisha ‘mwanamke mzuri’. Mwandishi wa kitabu cha Esta anamtaja Vashti kuwa “alikuwa mzuri wa uso”. Yawezakuwa jina lake lilisadifu uzuri wake aliokuwanao (Esta 1:11). Vashti alikuwa malkia na mke wa mfalme Ahasuero, na ni mwanamke aliyetukuza uzuri na urembo wake. Biblia inamtaja Vashti kuwa alitia mgomo kwa kukataa kuitikia wito wa mumewe katika karamu aliyokuwa ameiandaa. Malengo ya kuitwa kwake na mumewe (mfalme) ilikuwa ni kuwaonesha watu au wageni uzuri wa mkewe. Kwa kulinda heshima yake, Vashti alikataa kwenda kwani mumwe na watu au wageni hao walikuwa wamelewa sana (Esta 1:5-6, 9-12).
            Wanahistoria wa Biblia wanadai kuwa, Vashti alikuwa malkia mzuri kuliko wanawake wote  katika ufalme huo na yaweza kuwa  uzuri wake ndio ulisababisha kujiamini kwake. Kwa sababu ya kutoitikia wito wa mumewe, mumewe alitumia mamlaka ya kifalme kwa kutaka ushauri kutoka kwa wenye hekima na walio na elimu na kujua nyakati. Kupiti mashauri, ilionesha Vashti ameuaibisha ufalme wote kwa kuwa mfano mbaya kwa wanawake wengine. Kwa ukubali wa mfalme, hukumu ilipitishwa juu ya Vashti ya kuvuliwa umalkia wake na apewe mwanake mwingine mwema kuliko yeye. Na baada ya maamuzi hayo, ilibidi atafutwe mwanamke atakayekidhi vigezo vya kuwa malkia, na aliyeonekana kufaa ni Esta (Esta 1:13-2:17).
                                          
Yaeli
            Mwanamke huyu alikuwa mke wa Haberi, Mkeni. Yaeli ni mwanamke anayetajwa katika kisa cha Debora nabii kwenye kitabu cha waamuzi, na ni mwanamke aliyemuua mwanamume wakati akiwa amelala katika hema yake. Mwanamume huyo  aliyeuliwa na Yaeli alikuwa akiitwa Sisera (aliwatesa Waisraeli kwa muda usiopungua miaka ishirini). Wakati akiwa amemkimbia Baraka na jeshi lake, Sisera alienda kujificha kwa hema ya Yaeli, ndipo Yaeli akamtia kigingi katika paji ya uso wake. (Waamuzi  4:17-22). Katika wimbo wa Debora na Baraka, Yaeli anatajwa na kusifiwa kutokana na tukio la kishujaa alilolifanya la kumuua Sisera aliyekuwa mtesi wa Waisraeli (Waamuzi 5:6, 24-27).

Yekolia
            Mwanamke huyu alikuwa akikaa Yerusalemi na alikuwa mama wa Uzia (au Azaria), mfalme wa Yuda, aliyeanza kutawala akiwa na miaka kuumi na sita (2Wafalme 15:2; 2Nyakati 26:3). Jina hili la Yekolia, maana yake  ni‘mwenye nguvu’.  Yaweza kuwa mazuri yote ya utawala wa mfalme Uzia nikutokana na maongozi mazuri ya mama huyu yaliyomletea heshima mwanaye (Isaya 6:1-3).


Yedida
            Mwanamke huyu alikuwa binti wa Adaya wa Bozkathi, mfalme muovu aliyeuawa na watumishi wake. Yedidia ni mama yake na Yosia aliyekuja kuwa mfalme wa Yuda, ambaye alitenda mema sawa na Daudi. Wakati Mumewe aitwaye Amoni (mfalme) akiwa muovu, yeye alikuwa mcha Mungu na alikuwa muongozo bora kwa mwanaye (2Wafalme 22:1, 2). Maana ya jina hili ni ‘mpenzi wa Yehova’. Jina hili la Yedida, wengi hulichanganya na kudhani ndilo jina sawa na Yedidia, lililokuwa jina la kuzaliwa la Sulemani linalomanisha ‘aliyependwa na Yehova’ (2Samweli 12:24-25).

Yehoadani
            Maana ya jina la mwanamke huyu ni ‘Yehova ni pambo langu/lake’. Yehoadani aliolewa na mfalme Yoashi aliyeokolewa na Yehosheba akiwa na umri wa miaka sita (au chini ya umri huo). Mumewe akiwa mgonjwa, aliuliwa na watumishi wake. Alikuwa mama wa Amazia aliyefanikisha kuchukua kiti cha ufalme wa baba yake aliyeuliwa. Ingawaje mtoto wake alianza kwa kutawala kwa haki, baadaye aliingiza ibada ya sanamu katika nchi kama alivyofanya baba yake, hivyo na yeye aliuliwa (2Nyakati 24:24-27; 2Wafalme 14:2; 2Nyakati 25:1, 14, 2-28).

Yehosheba (Yehoshabeathi)
            Maana ya jina hili ni ‘Yehova ni kiapo’. Mwanamke huyu alikuwa binti wa Mfalme Yehoramu au Yoramu, kwa mke wake wa pili, dada asiye wa kufikia (half-sister) wa Ahazia. Mwanamke huyu aliolewa na Kuhani mkuu, hivyo kuwa binti pekee wa Mfalme aliyeolewa na Kuhani. Alikuwa pia mwanamke mwenye shime aliyemficha mpwa wake aitwaye Yoashi ili asiweze kuuawa na Athalia kama walivyouliwa wazaliwa wengine wa kifalme (2Wafalme 11:2; 2Nyakati 22:11).

Yehodia
            Mwanamke huyu anajulikana kwa jina lingine maarufu la Myahudi. Hivyo, mwanamke huyu alitambulika kama mke wa Kiyahudi wa Meredi akitofautishwa na yule mke wake mwingine wa Kimisri aitwaye Bithia (1Nyakati 4:18).

Yemima
            Mwanamke huyu huelezewa na wachambuzi wengi wa Biblia kama miongoni mwa watoto wa kike wa Ayubu, waliozaliwa baada ya kurejeshewa afya na mali zake. Yemima alikuwa binti wa kwanza kati ya watatu wa mzee Ayubu. Yemima akiwa miongoni mwao, Biblia inathibitisha kuwa, hapakuwepo na wanawake wazuri kama hao wana wa Ayubu katika nchi hiyo  (Ayubu 42:14, 15).

Yeriothi
          Yeriothi alikuwa miongoni mwa wake wa Kalebu, mwana wa Hesroni (1Nyakati 2:18). Maana ya jina la mwanamke huyu ni ‘pazia za hema’. Jina hili pia linafanana na jina la mtoto wa kiume wa Hesroni. Baadhi ya wachambuzi wengine wa Biblia, hudhani Yeriothi aliitwa pia, ama alijulikana kama Azuba.

Yerusha
Mwanamke huyu alikuwa mtoto wa Sadoki. Maana ya jina hili ni ‘milikiwa au ‘olewa’. Yerusha aliolewa na mfalme Uzia ambaye alifariki kwa ukoma, na  ambaye kifo chake kwa kina kimetajwa na Isaya nabii (Isaya 6:1). Familia ya Uzia na Yerusha, ilikuwa familia inayomcha Mungu. Mwanamke huyu, alimzalia Uzia mtoto wa kiume (aitwaye Yothamu) aliyekuja kuwa mfalme wa Israeli (2Wafalme 15:33; 2Nyakati 27:1-6).

Yezebeli
            Yezebeli ni mwanamke aliyekuwa na matendo ya Kishetani: alikuwa muabudu sanamu, muovu, mpotoshaji wa mumewe, mpenda anasa na mapambo, muuaji, mchawi, n.k (2Wafalme 9:22; Mathayo 7:16-20). Kuhusu maana ya jina hili, sikuweza kupata maana ya moja kwa moja, bali asili ya jina hili nila-kifoinike. Yezebeli alikuwa binti wa Ethbaali, mfalme wa Wasidoni na kwa pamoja alihusika kama mfalme na kuhani wa ibada ya Baali (1Wafalme 16:3).
            Yezebeli alipoolewa na mfalme Ahabu wa Israeli ya kaskazini alisaidia kuunganisha nchi za Fonike na Israeli ziwe na umoja kisiasa na kidini (Yezebeli alikuwa na uwezo mkubwa wa kummiliki mumewe). Yezebeli alikuwa binti wa mfalme na kuhani wa miji ya Fonike ya Tiro na Sidoni, naye alifanya bidii sana kufanya Ubaali wa Fonike uwe dini rasmi ya Israeli. Ahabu alisaidiana naye akajenga hekalu la kifalme la Ubaali katika mji mkuu wa Israeli, Samaria (1Wafalme 16:29-33).
            Lakini baada ya muda mfupi, Yezebeli na Ahabu walipata upinzani kuto kwa nabii wa Mungu, Eliya (1Wafalme 18:17-18). Huduma za manabii Eliya na Elisha zilikuwa na makusudi maalumu ya kuhifadhi ibada ya kweli ya Yahweh (Yehova) katika Israeli ambapo Ubaali wa Yezebeli ulitishia kuondoa ibada hiyo kabisa.
            Katika muda mfupi, Yezebeli alikuwa ameua manabii wengi wa Mungu na kuweka manabii wa kwake kwa wingi wa mamia mahali pao (1Wafalme 18:4. 19). Eliya alipowapima na kuwaua manabii wa Baali katika Mlima Karmeli, Yezebeli alijaribu kumwua, lakini aliwahi kukimbia (1Wafalme 18:40; 1Wafalme 19:1-3).
            Yezebeli alionesha udhalimu wa tabia yake alipomshawishi Ahabu kujitwalia shamba la mizabibu ya Nabothi. Aliweka watu walioshuhudia mashitaka  ya uongo dhidi ya Nabothi, kisha, baada ya kuuawa kwake Nabothi, alitwaa shamba lake (1Wafalme 21:1-6). Kwa tukio hilo, Eliya alitangaza hukumu kali juu ya nasaba ya ufalme wa Ahabu, na hasa juu ya muuaji Yezebeli (1Wafalme 21:20-25).
            Baada ya kufa kwake Ahabu, Yezebeli aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya Israeli. Kwa miaka kumi na nne iliyofuata wanawe wawili, yaani Ahazia na Yehoramu, walitawala kwa mfululizo wa enzi zao wakapendekeza siasa ya dini ya mama yao (1Wafalme 22:51-53; 2Wafalme 1:17; 2Wafalme 3:1-3). Yeye pamoja na mwanaye Yehoramu waliuawa Yezreeli siku moja katika maasi ya kumwagika damu yaliyoendeshwa na Yehu. Yezebeli akiwa na kichwa kigumu mpaka siku ya mwisho, alitaka kukutana na muuaji wake katika heshima yake yote ya malkia (2Wafalme 9:22-37).
            Wakati wa Agano Jipya, kanisa la Thiatira katika Asia Ndogo lilisumbuliwa na mwanamke ambaye  jina lake la utani au la mfano lilikuwa Yezebeli. Alikuwa nabii wa uongo ambaye ilikuwa ni sawa na ile ya Yezebeli wa kwanza. Imani yake ilikuwa na ishara ya zinaa na ibada ya miungu (Ufunuo 2:18-23).    

Yoana
           Yoana ni wanamke aliyemtukuza Kristo baada ya kumponya. Maana ya jina hili ni ‘Yehova ameonesha fadhila’ au ‘Bwana ni neema or Bwana hutoa hisani’. Yoana alikuwa mke wa Kuza, wakili wa Herode (Luka 8:1-3). Luka anampambanua Yoana kuwa alikuwa miongoni mwa wanawake waliohuzunishwa na kifo cha Yesu pale msalabani. Pamoja na Yoana, wanawake hao walifanya maandalio ya kuupaka mafuta mwili wa Yesu baada ya Sabato kuisha (Luka 23:55-56). Lakini pia ni miongoni mwa wanawake waliofurahia na kutangaza habari za kufufuka kwake Yesu Kristo (Luka 24:1-12). Yoana ni jina pia la kiume (Luka 3:27).

Yokebedi
            Yokebedi ni mwanamke ambaye watoto wake walikuja kuwa wakuu sana. Alikuwa mke wa Amramu na mama wa Musa, Haruni na Miriamu. Jina la mwanamke huyu linatajwa katika kitabu cha Kutoka 6:20; Hesabu 26:59; Waebrania 11:23 n.k. Lakini kisa kizima cha mwanamke huyu kinaanzia Kutoka 2:1-11. Maanaya jina hili ni ‘utukufu wa Yehova’ au ‘Yehova ni utukufu wake/wetu’. Kuhusu familia aliyotokea, ametajwa tu kama binti wa Mlawi aliyeolewa na Mwanamume kutoka familia ya Mlawi (Kuto 2:1). Kitu ambacho chaweza shangaza, aliolewa na ndugu yake (mtoto wa kaka yake). Ndoa ya aina hii, haikuwa makosa kabla ya kutolewa kwa sheria za Musa.
           Mwanamke huyu aliweza kuishi maisha ya kumlinda na kumtunza mtoto wake wa kiume kinyume na agizo la Farao, lililokuwa linataka watoto wote wa kiume wa Kiisraeli wauawe punde tu baada ya kuzaliwa (Waebrania 11:23; Matendo 7:20). Mwanamke huyu alipopata nafasi ya pili ya kumlea mwanaye, Musa toka kwa bitinti Fara, nafasi hiyo alikuwa akiitumia vyema, alikuwa akimfundisha na kumsisitiza mwanaye kuwa yeye siyo Mmisri  yeye ni Mwebrania. Hata Musa alipokabidhishwa katika Ikulu ya Farao, alijua kuwa yeye ni Mweburania na siyo mtoto wa binti Farao (Kutoka 2:2-11).

Yudithi
            Maana ya jina hili ni ‘aliyesifiwa’. Mwanamke huyu alikuwa binti wa Beeri, Mhiti na alikuja akawa mke wa kwanza wa Esau (Mwanzo 26:34). Kwa kumuoa Yudithi, Esau alivunja agano la Ibrahimu babu yake kwa kuoa Binti anayetokea katika kabila la kipagani. Ikumbukwe kuwa, Ibrahimu alimkataza Isaka, mwanaye (ambaye ni baba yake Esau) kuoa binti za Kanani ambao walikuwa waabudu miungu pia (Mwanzo 24:3). Kwa maamuzi ya Esau kumuoa Yudithi, baba na mama yake waliumia mioyo yao sana (Mwanzo 26:35).

Yulia
            Mwanamke huyu anatajwa na Mtume Paulo katika Warumi 16:15, alikuwa miongoni mwa wacha Mungu walioipokea Injili kupitia kwa Paulo huko Rumi. Maana ya jina hili ni ‘mwenye nywele za mawimbi, kunjamana, singasinga’. Inaonesha alitokea katika familia maarufu ya kale huko Rumi. Twaweza dhani kuwa, Yulia alikuwa mke au dada wa Filologos, na yaweza kuwa waliishi au walitoka familia moja, aidha mume na mke au mtu na kaka yake. Yulia ni tofauti na Yulio, mwanamume aliyetajwa katika kitabu cha Matendo ya Mitume 27:1, 3.
Zebida
            Maana ya jina hili la Zebida ni ‘kuzawadia’ au  ‘zawadi’. Zebida alikuwa binti wa Pedaya wa Ruma, alikuwa mama wa Yehoyakimu au Eliakimu, mfalme wa Yuda (2Wafalme 23:36). Zebida alikuwa mke wa Yosia, mfalme wa Yuda katika miaka ya 609 K.K.  Mwanaye alikuwa miongoni mwa wafalme wa Yuda waliotenda mabaya. Aliwatoza wananchi wake kodi kubwa na kuwalazimisha wafanye kazi miradi yake binafsi bila kuwalipa.
Zereshi
             Maana ya jina hili la Zereshi ni ‘nyota ya heshima’, ‘nyota ya upendo’, ‘nyota ya  kusujudu’ au ‘nyota ya dhahabu’. Zereshi alikuwa mke wa Hamani ambaye alikuwa adui wa Wayahudi na alikuwa Waziri mkuu  chini ya mfalme Ahasuero wa Uajemi (Persia) aliyejulikana kama Xerxes wa kwanza. Huyu ni mwana mke aliyepitia uzoefu mgumu. Alimshuhudia mumewe akifa akiwa ametundikwa juu ya mti. Aina ya kifo alichokufa mumewe, ni kifo alichokuwa amempendekezea mumewe amfanyie Mordekai, hivyo mumewe alikufa kifo alichokuwa amemtengenezea Mordekai (Esta 5:10, 14; Esta 6:13).
            Kifo cha Hamani, mumewe Zareshi kilitimia sawa na Isaya 54:17, kuwa: “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa, na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa makosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana”.

Zilpa.
            Jina hili linamaana ya ‘isiyohalisi, isiyohakika, isiyorasmi, isiyoaminika au isiyothabiti’. Zilpa alikuwa msichana mtumwa ambaye Labani alimpa binti yake (Lea) ili awe kijakazi wake. Kwa kuzaa na Yakobo, Zilpa alichangia katika kukua kwa Israeli kama taifa. Baada ya Lea kukoma kuzaa, alimtoa Zilpa kwa Yakobo ili aweze kuongeza uzao wake, hivyo, Zilpa alikuja akawa mama wa watoto wawili wa kiume, waitwao Gadi na Asheri. Watoto hawa walikuja wakawa sehemu na mchango kwa taifa la Israeli, miongoni mwa makabila kumi na mawili (Mwanzo 29:24; Mwanzo 30:9, 10; Mwanzo 35:26; Mwanzo 37:2; Mwanzo 46:18).

Comments

Popular posts from this blog

MFANO WA MPANGO KAZI

SOMO: MADHARA YA KUKATAA KUMTII MUNGU