‘A’ HADI ‘Z’ ZA KUZINGATIA KWA MCHUMBA ANAYEPASWA KUWA MWENZI WA MAISHA
Kumekuwapo na changamoto nyingi sana za
ndoa, na hizo changamoto zimesababishwa na kufanya makosa kwa wanandoa hapo
awali katika suala nzima la uchaguzi wa wenzi au wachumba wao katika hatua za
uchumba kabla ya ndoa kuja. Changamoto mojawapo katika ndoa imesababishwa na
mitazamo tofauti na utashi binafsi wa watu katika kuingia kwenye ndoa.
Kutokufahamu umuhimu wa ndoa kwa Wakristo
baadhi kumepelekea kuvunjika kwa ndoa baadhi, maana wanandoa hao wameoana kwa
kuangalia vitu, kazi, mali, sura, kipaji, mvuto, umaarufu au cho chote kutoka
kwa mchumba kama kigezo cha kumvuta na kuiingia katika mahusiano ya uchumba ili
kuifikia hatua na adhima ya ndoa.
Ndoa (kama tasisi) ni takatifu, na Mungu aliiasisi
ndoa kwa makusudi matakatifu. Ndoa ya kwanza iliasisiwa na Mungu mwenyewe
katika bustani ya Edeni kati ya Adamu na Hawa (mume mmoja na mke mmoja). Hivyo
basi, mchakato mzima wa kumpata mwenzi wa maisha kunahitaji kumshirikisha Mungu
ili akupatie mwenzi mwema wa maisha wa kufanana nawe. Vijana wa kike na wa
kiume wanaotegemea kuingia katika ndoa, wanatakiwa wajue kuwa, kunahitajika uangalifu
mkubwa sana ili kumpata mchumba na mwenzi sahihi wa ndoa.
Hivyo; ni vyema kutambua ni kipi cha
kuzingatia ili kumpata mchumba anayefaa kuwa mke au mume mwema. Mithali 2:11 inatuambia kuwa: “Busara
itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi”. Kwa hiyo, sehemu yote ya sura hii
itatoa elimu, busara ufahamu ambao vijana wa kike na wa kiume utawahifadhi kwa
kufuata hatua zitakazokuwa za msingi katika kujipatia mchumba anayestahili kwa
ajili ya ndoa yenye furaha daima:
‘A’Azima
ya Kuingia Kwenye Ndoa Itambuliwe
Azima na nia ya kuingia kwenye ndoa
yampasa mtu aitambue. Jambo
la kuwa katika ndoa halikwepeki, muda ukifika wakufanya hivyo yampasa mtu
kuazimia kwa dhati kabisa. Biblia inasema kwenye
kitabu cha Mhubiri 3:1 “Kwa kila jambo kuna
majira yake na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”. Kunuia kwa mtu na kuwa tayari kutamwandaa
kisaikolojia pamoja na kujipanga kwa ajili ya azima hiyo. Kwa namna nyingine,
kuingia kwenye ndoa sio suala la kuigiza wala kujaribu, bali kunahitaji azima
ya kuingia kwenye ndoa moja kwa moja.
‘B’Bidii
ya Kazi
Mchumba anayefaa ni yule mwenye bidii
katika kazi na siyo alichonacho, mali alizonazo, kazi aliyonayo nk. Mtu mwenye
bidii katika kutafuta anauhakika wa kufanikiwa, hivyo mchumba huangaliwa katika
kufanya kazi kwa bidii na mipango thabiti kwa ajili ya kuyatafuta mafanikio kwa
njia halali. Mithali 10:4 na Mithali 12:27; mafungu haya
yamesadiki juu ya bidii katika kazi. Kulingana na mfumo wetu wa elimu (miaka 16
na zaidi hutumika kwa ajili ya elimu toka chekechea hadi chuo kikuu). Kumpata
kijana aliyefanikiwa kuwa na funguo tatu yaani nyumba, ofisi na gari ni nadra
sana. Mara nyi watu hupata funguo tatu uzeeni na umri wa kuoa unakuwa umepita.
Hivyo, angalia mchumba aliye na bidii katika kazi, ili muyatafute maendeleo
katika ndoa kwa pamoja.
Hivyo kwa wale wanaotafuta wenzi wenye
funguo tatu hasa kwa kijana, yampasa amtafute mtu mzee, mtu aliyefiwa na mwenzi
wake au kwa binti aingie katika ndoa ya mitara. Mchumba mvivu na tepetevu na
asiyejibidisha hafai kuwa mke au mume kwani dunia ya sasa inahitaji kusaidiana
katika kutafuta ili kuyafikia malengo mapema. Huu ni ushauri wangu mwenyewe,
maana uzoefu unaonesha madhara yake. Mfano baba ambaye ni mtafutaji pindi anapofariki
au kupata ulemavu wa kudumu au ugonjwa wa kudumu, familia huyumba na
kusambaratika. Hili jambo lipo hata kwa upande wa wanaume, maana wapo
wasiotafuta wala kujibidisha katika kutafuta hivyo kutegemea mahitaji yaliyo
mengi kutoka kwa wake zao (ambapo sio salama pia).
‘C’Chunguza
Tabia
Kipengele hiki ni nyeti sana maana ndipo
kiini cha mchumba anayefaa kuwa mke au mume. Kipengele hiki kinabeba muktadha
mzima wa mchumba mwema atokaye kwa Mungu. kupitia tabia ndipo unaweza kupata mke
mwema. Wasifu wa nje wa mtu kuutambua ni
rahisi sana kuliko wasifu wa ndani wa mtu; vivyohivyo tabia za ndani na tabia
za nje kwa mchumba. Ukikosea kuchunguza tabia ya mchumba katika kipindi cha
urafiki, ni vigumu kuzibaini tabia katika uchumba maana atazificha ili kulifikia
lengo la kuolewa au kuoa.
Tabia ni sawa na ngozi, kuibadirisha ni
vigumu sana (Yeremia 13:23). Usijipe
moyo kwa kusema na kufikiri “ngoja anioe
au nimuoe kisha nitambadirisha tabia yake”. Japo pia mwenye uwezo wa
kumbadirisha mtu tabia ni Mungu, hivyo itahitaji maombi mengi na ya dhati kwa
kumuombea mchumba au mume au mke. Mafungu yaliyo katika Mithali 7:10-12, Mithali 11:16 na
Mithali
12:4 yanaeleza juu ya tabia bainishi zinazofaa na zisizofaa kwa mtu
anayemwabudu na kumcha Mungu wa mbinguni. Kuna aina kuu mbili za tabia na mfano
wake:
1. Tabia zinazojipambanua kwa nje: Tabia
za nje zinajipambanua katika matumizi ya
ulimi wakati wa kuongea, mitindo au
aina za mavazi anazo pendelea kuvaa (Mwanzo
3:7, Kumb 22:5, 1pet 3:1-6), kujipamba kwake kwa sura au mwili na manukato (Hosea 2:13, Wimbo 1:3, Ezekiel 23:40), vyakula na vinywaji apendeleavyo (Mithali 23:20-21). Tabia zote za nje kuzibaini hazihitaji muda
mrefu sana, mfano, si vigumu kumbaini mtu mchafu au msafi.
2. Tabia zinazojipambanua kwa ndani: Tabia
hizi hazionekani kwa urahisi maana ni za ndani mno; mfano wa hizo ni wivu,
upole, uchoyo, kutojali, dharau, mtazamo kwa kutaja baadhi. Tabia za ndani
huchunguzwa kwa muda mrefu sambamba na matendo ya huyo mtu. Warumi
3:12 imezungumzia tabia njema zinatakiwa kuwa hata za moyoni. Ugunduzi
wa tabia hizi juu ya mtu, kunahitaji kiwango na ujuzi mzuri wa saikoloji.
Kubadilika kwa tabia hizi za ndani kunahitaji uwezo wa Roho Mtakatifu na utayari
wa mtu baada ya kugundua udhaifu na mapungufu yake.
‘D’Dini
au Dhehebu
Dini au dhehebu katika mahusiano ni
kipengele cha kuzingatia na kutilia maanani zaidi. Inapendekezwa kuwa, wale
wanaotarajia kuwa wenzi ni vyema ukawepo ufanano wa dini au dhehebu. Kila dini
na dhehebu kuna mafundisho yake (doctrines) ambayo yanapishana kutoka dhehebu
au dini moja kwenda dhehebu au dini nyingine.
1Wakorintho 1:10 na 1Wakorintho 1:12 aya hizi zinatoa
umuhimu na faida za wanandoa kuwa wenye dini au dhehebu moja, maana hawatapishana
katika misingi ya mafundisho bila kuwagawanya watoto katika imani za
mafundisho. Ukitaka familia iwe chini ya kiwango katika mambo ya kiroho, jaribu
kuchanganya dini mbili tofauti miongoni mwa wanandoa katika ndoa.
‘E’Elimu
Kuna elimu ya kweli ambayo inahusu uelewa
na maarifa juu ya Mungu wa kweli wa mbinguni na elimu ya kidunia ambayo
tunaipata shuleni kupitia mitaala ya masomo mbalimbali. Nitazungumzia juu ya
elimu ya kidunia ambayo inaweza ikaleta utofauti kwa wachumba watakapo kuwa
katika maisha ya ndoa. Inashauriwa kuwa wachumba wanaotarajia kuoana
wasipishane sana viwango vya elimu au walingane viwango vya elimu ili kuleta
uwiano katika mitazamo, uelewa na tafakari.
Sanjali na viwango vya elimu kuwiana au
kutotofautiana, kigezo cha elimu lazima kipewe nafasi ili kila mmoja kati ya
wachumba kuridhia wao kwa wao, endapo mmoja hajui kusoma wala kuandika au
hajaenda vidato katika elimu. Suala la elimu pia laweza kutatuliwa kwa wenzi
kukubaliana katika kuendelezana katika masuala ya elimu. Mafungu yafuatayo
yanaelezea juu ya elimu ya kweli na elimu dunia: Mithali 4:13, Waefeso 5:22 na
Esta
1:22.
‘F’Familia
Atokayo (Historia yake)
Suala la ufahamu wa historia na familia anayotoka
mchumba ni vyema kuifahamu bayana na kujiridhisha kwayo. Kuifahamu familia anayotoka
mchumba ni jambo jema sana, kwani itasaidia kujua endapo kuna magonjwa ya
kurithi, malezi mabaya na tabia mbaya za wazazi au walezi wa mchumba ama sivyo.
Mara nyingi tabia ya wazazi au mzazi (walezi au mlezi) hubainisha tabia ya
mchumba, hususani binti kama anavyoelezwa katika Ezekieli 16:44.
Mafungu mengine yanayoelezea juu ya
umuhimu wa kuijua historia ya familia anayotoka mchumba ni Hosea 2:4-5 na 2Samweli 13:8-12.
Yapo matendo yaliyofanywa na wazazi na kupelekea matokeo yake kuendelea
kuandama vizazi vinavyofuata (Kutoka 20:5) hivyo ni bora
kujiridhisha kabla ya kuoa au kuolewa.
‘G’Gharama
ya Mahali kwa Mchumba
Kila jambo halikosi kuwa na gharama aidha
muda au pesa. Zipo gharama kwa mchumba, hivyo ni vyema (kijana wa kiume)
akazitambua ili kujua endapo atazimudu ama sivyo. Ipo gharama kubwa ambayo huwa
inawakabili vijana wa kiume ni lazima aipitie ili kuifikia hatua ya kumuoa
mchumba aliyempata.
Gharama hiyo huhusisha mahali pamoja na
viambata vya zawadi (Mwanzo 24:48-53). Suala la mahali
linatofautiana tamaduni na tamaduni, sehemu na sehemu, imani moja kwenda imani
nyingine.
Nionavyo mimi: ifike wakati Wakristo
tuachanane na suala la mahali ili tuepukane na tamaduni katika mchakato wa
ndoa. Mahali sio kitu kizuli maana taratibu zake zimejaa upagani mwingi. Suala
la mahali kuwa ghali, limekuwa kikwazo kikubwa katika jamii ya Wikristo
hususani kwa kusababisha vijana wasioane; hivyo, vijana kuoana bila kufuata
taratibu za Kibiblia, mabinti kutoolewa
na mwisho wa siku kuzaa watoto nje ya ndoa aidha wakiwa bado nyumbani kwa
wazazi wao.
Aidha, kwa upande wa kijana wa kiume
lazima aangalie gharama za maisha ya binti kulingana na familia anayotoka ili
kujua kama ataweza kumhudumia katika ndoa. Zipo familia ambazo zipo vizuri
kimaisha (kiuchumi), hivyo kunamaisha ya hali ya juu ambayo mtoto wa kike amekuwa
akiyaishi na kila alichohitaji alikipata. Kijana anaetarajia kuoa binti atokaye
katika familia tajiri lazima ajiandae kumhudumia kama alivyokuwa akiishi
nyumbani kwao. Kwa mtazamo wangu pesa sio tiba ya kuleta upendo bali upendo wa
dhati unatoka moyoni mwa mtu husika. Soma Mithali15:16-17.
‘H’Hiari
ya Mchumba Kuishi Naye
Upendo wa kweli hauhitaji shuruti wala
kulazimisha, bali upendo huandamana na hiari juu kuridhia toka moyoni. Hivyo,
mchumba ni vyema akakubali yeye mwenyewe ili kuingia ndani ya ndoa. Uhuru
katika kukubari hakuleti majuto hapo baadae ndani ya ndoa, maana mtu ameamua
mwenyewe. Sio salama sana kutumia ushawishi wa kipesa, mali au misaada yo yote
ili kutengeneza mazingira ya mchumba kukubali, kwa sababu vitu au pesa vyaweza
kuwa mvuto bandia badala ya upendo wa kweli kutoka moyoni.
Rushwa yenye ushawishi katika uchumba si jambo
jema, maana hapo baadae kwa wenzi, kunaweza kukatokea upungufu au ukosefu wa
upendo wa dhati ndani ya ndoa. Kunajambo zuri la kujifunza katika Mwanzo
24:54 ambapo Rebeka alihiali yeye mwenye kwenda kuungana na mume wake
baada ya kutolewa zawadi na mahali.
‘I’Imani
Kipengele hiki ni sawa na kile kipengele
cha dini au dhebu, lakini
kinautofauti kidogo. Suala la imani nalo ni jambo nyeti sana sawa sawa na kile
kipengele cha “D” juu ya umuhimu wa
wachumba kufanana kwa dhehebu au dini kabla ya kuoana. Yapendeza wachumba
wanaotaka kuoana wawe wa imani moja, maana kutofautiana imani huzaa migogoro
katika ndoa.
Zipo imani ambazo huruhusu kula vyakula
vyote, kuoa na kuacha (kutalakiana), kunywa pombe, kuoa wake wengi na kuvuta
sigara, hivyo mwingine akiwa na masharti katika hivyo vipengele, kutaleta
migogoro mikubwa ndani ya ndoa. Sambamba na hayo, hata taratibu za ibada kupisha
kati ya imani moja na nyingine kwa wenza husababisha makwazano miongo mwa
wanandoa.
Suala lingine la msingi katika imani ni
juu ya kiwango cha kiroho cha mchumba. Inapotokea wachumba ni wa imani moja,
suala la kiwango cha kiroho (imani) kwa mchumba lafaa kuzingatiwa pia ili hapo
baadaye wachumba hao watakapooana waweze kuwa na familia yenye kiwango kizuri
cha kiroho pamoja na malezi mazuri ya kiroho kwa watoto wao.
Sio salama pia kutumia silaha ya
kumtangazia mtu (mchumba) kuwa nitaolewa au nitakuoa wewe endapo utabadiri
imani yako na kuja kwenye imani yangu; kwa sababu mchumba aweza kukubali
kubadiri imani yake ili aolewe au kuoa kwa sababu ya kukidhi hitaji lake na
siyo kwa kuikiri imani.
Kitabu cha 1 Wafalme 11:4 kinasema
hivi: “Maana ikawa, Sulemani
alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala
moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba
yake.” Ni vyema wachumba wanaotarajia kuoana wawaze pamoja, wanuie pamoja,
watende pamoja, waamini pamoja katika imani ili kuondoa mpasuko hapo badae
wawapo kwenye ndoa yao.
‘J’Julisha
Wazazi
Uchumba wa “Yusufu na Mariam”
ulitambulika nyumbani kwao na jamii inayowazunguka. Wakati mwingine hata
urafiki utambulike kwa wazazi ili wazazi nao wapime uaminifu wa rafiki huyo kama
ilivyotokea kwa Musa (Kutoka 2:16-21). Wachumba wanaotarajia
kuoana ni vyema wakazijulisha pande zote mbili za wazazi wao ili kuweka uwazi
na kulinda uchumba wao ili kuepuka usaliti kama ambavyo wangekuwa wawili kwa
uchumba wa siri.
Huwa ni moja ya heshima kubwa sana kwa
wazazi kujulishwa juu ya uchumba wa binti au kijana wao endapo amefikisha umri
wa kufanya hivyo ili nao wapate ya kushauri au kutoa baraka zao kwa ajili ya
hatua nyingine kuelekea katika ndoa.
‘K’Kasoro
Alizonazo Mchumba Zibaini Mapema
Kubaini kasoro alizonazo mchumba ni vyema na
ni vizuri ili kujipima kama zitaweza kuvumilika au kubadirika kama ni za
kufanyiwa mabadiriko haraka kabla ya kuamua kuingia kwenye ndoa. Biblia
inamzungumzia “Lea” kasoro yake ya kuwa na makengeza lakini Yakobo alimkubali
kwa kasoro yake hiyo (Mwanzo 29:17). Lea huyo huyo mwenye
kasoro na asiyependwa alibarikiwa kupata mtoto mapema kuliko “Raheli”. (Mwanzo
29:31).
Hakuna mtu ambaye hakosi kasoro, labda awe
malaika. Lakini, ni vyema kufahamu kuwa; kasoro ambazo sio za kimaumbile bali
ni za kitabia huachwa na si za kuvumiliwa. Ukizibaini kasoro zako pia yakupasa
kuziacha.
‘L’Linganisha
Umri wenu
Nionavyo mimi: jambo la msingi kutambua
katika umri; wanawake hukomaa kiakili mapema, kuliko wanaume; lakini pia wanawake
hukua kiumbo haraka, lakini hawazeheki mapema, bali wanaume hawakui haraka ila
huzeeka mapema. Hivyo basi ni vyema mwanamke awe chini kidogo ya umri wa
mwanamume kutokana na kukua kwao haraka.
Ulinganifu wa kiumri ni mzuri ili kubaini
umri sahihi wa kuzaa pamoja na kuweza kusimamia majukumu ya kifamilia. Kiafya
inashauriwa kuwa, mwanamke asiendelee kuzaa afikishapo umri kati ya miaka 34
hadi 36, hivyo ili mwanamke aweze kuzaa watoto watatu wenye kutofautiana miaka
mitatu; akichelewa sana mwanamke aanze kuzaa akiwa na umri wa miaka 25 hadi 26
ili ukijumlisha miaka tisa ya tofauti ya watoto watatu, hivyo atakoma kuzaa akiwa
au kabla ya miaka 36. Jambo la kusisitiza ni kuwa si wote wanaoweza kutendewa
miujiza kama Sara alivyo zaa katika umri wa uzee (Mwanzo 17:17).
Sio
vizuri pia kwa mwanamume kuchelewa kuoa, maana haipendezi kulea watoto katika
umri wa uzee, hivyo angalau mtu akichelewa sana miaka 32 awe ameoa. Sanjali na
hayo, kwa mtazamo wangu: umri wa miaka 18 hadi 25 kwa wanawake huwa ni umri wa
mabadiriko makubwa ya kimaumbile, na wengi wao hunenepa kutoka umbo la awali
kwa sababu ya mabadiliko ya kihomoni na maumbile. Umri wa miaka 25 na kuendele
ndio umri sahihi wa kutambua umbo la mwanamke maana atakuwa amepitia hatua zote
za mabadiriko ya kimakuzi.
‘M’Miliki
Alizonazo Mchumba Zitambulike
Vijana wengi huwa hawana mali kwani huwa
katika hatua za utafutaji wa mali. Endapo kuna mali au miliki aidha za kurithi
au kupewa na ndugu au jamaa; kunatakiwa kuwepo
ukweli na uwazi kwa wachumba juu ya mali na miliki walizonazo kwa kila mmoja
kabla ya kuoana.
Kukosekana kwa uwazi juu ya miliki au mali
alizonazo mchumba kwa weza sababisha kutoaminiana endapo siku moja miongoni
mwao katika ndoa atabaini kuwa hakuwekwa wazi. Kumficha mchumba juu ya miliki
na mali hupelekea kupotea endapo mmoja atafariki ghafla wakati wawapo katika
ndoa. Uwazi wa miliki utawaweka huru wachumba wote wanaotaka kuoana hapo baadae
ili kurahisisha mipango ya maendeleo yao mapema.
Wakati mwingine mali alizonazo mchumba
hujulikana bila hata kumuuliza mhusika, kama ilivyokatika kisa cha kitabu cha Ruthu,
ambapo Ruthu alitambua mali za Boazi kwa kumuona katika usimamizi wa hiyo
miliki yake (Ruthu2:3-4). Jua kuwa: Boazi
alikuwa mzee katika umri, hivyo mali zake alikuwa amezitafuta tangu enzi za
ujana wake, hivyo ni tofauti na vijana wengi ambao huwa hawana mali, kwani huwa
katika mchakato wa kutafuta mali.
‘N’Ndoto
za Mchumba Katika Maisha yake
Kila mwanadamu aliye na akili timamu na mwenye
uwezo wa kufikiria japo hata kidogo huwa hakosi kuwa na ndoto za maisha anazotarajia
kuzitimiza katika kipindi cha muda fulani ndani ya maisha yake. Ni vyema ndoto
za wachumba zibainike kwa kila mmoja, ili waweze kuona namna na jinsi yakuweza
kuzitimiza aidha ndani ya ndoa au kabla ya ndoa.
Aidha, mmoja wao kati ya wachumba anaweza
akawa na mpango wa kufikia kiwango fulani cha elimu, mfano shahada ya kwanza
katika taaluma fulani ndipo aoelewe, hivyo ni vyema mwingine kuvuta subira ili
lengo la mchumba wake litimie katika ndoto ya maisha yake. Endapo itakuwa ni
vigumu kusubiri, basi huyo asiyeweza kusubiria amuache mchumba wake na awe huru
kutafuta mwingine aliyetayari kuingia katika ndoa bila kupoteza muda mwingi.
‘O’Onesha
Hali Halisi ya Maisha Yako
Kitendo cha kuonesha hali halisi ya maisha
hata kabla ya uchumba na ndani ya uchumba ni jambo jema na salama sana. Inawapasa
wachumba kuepuka maisha ya kuigiza tofauti na jinsi walivyo, maana ni mojawapo
ya udanganyifu na huleta migogoro hapo baadaye katika ndoa. Unakuta kijana
anaazima gari, nguo ili aonekane ni wa maisha ya juu sana na kushawishi wale wa
karibu yake waone kuwa ni mtu wa maisha mazuri.
Ukiazima gari, eleza kuwa umeazima na
kuazima nguo kumepitwa na wakati na hakufai kabisa. Kitendo cha kuigiza hali ya
maisha yasiyo “Ruthu” alikishinda, zaidi alionesha hali ya maisha yake jinsi
yalivyo toka moyoni hadi nje ya maisha aliyokuwa akiyaishi; angalia Ruthu
1:16-17, Ruthu 3:10. “Esta” naye katika nchi ya ugenini
pia naye alifanya vivyo hivyo hadi kupata fursa ya kuolewa na mfalme, maana
mabinti wengi walienda kwa kujipamba, kuvaa vito na mavazi ya thamani sana wakati
siyo hali ya maisha yao; Esta yeye alienda jinsi alivyo (Esta 2: 15-17).
Tabia ni uchaguzi mtu anaweza
akaibadirisha endapo akinuia kufanya hivyo kwa dhati. Vijana wa kiume na wakike
yawapasa kuishi katika kweli na ukweli mtupu ili ukweli uwaweke huru. Katika
uchumba wamo matapeli wengi sana, ndiyo maana wengi huumizwa sana punde
ibainikapo kuwa mchumba huyo sivyo alivyokuwa akimdhania na kujitumainisha
kwake.
‘P’Pima
Uaminifu wa Mchumba
Uaminifu hauwezi ukaondolewa na mazingira,
sababu fulani wala changamoto inayomkabiri mchumba. Kuanza uhusiano (kuoa na
kuolewa) na mtu ambaye hujajihakikishia upendo na uaminifu wake juu yako ni
kujipalia moto hapo badae; maana wapo ambao huanzisha mahusiano na mtu fulani
kwa kutimiza haja zao za matamanio au kuchuma kitu fulani kwa huyo mtu.
Kwa wale wanaoelekea katika safari ya maisha
ya ndoa na ambao bado wanatafuta; kipindi salama cha kumchuguza tabia mtu, ni
kipindi cha urafiki na kidogo kipindi cha uchumba. Kijana wa kiume akimtamkia
binti kuwa anataka kumuoa (yaani awe mchumba), matarajio ni kuwa, huyo binti
ataficha tabia ake mbaya alizonazo ili aolewe. Vivyo hivyo kwa binti
anapomkubalia kijana wa kiume kuingia naye uchumba, ategemee pia kijana huyo
atazificha tabia zake mbaya ili aweze kufanikisha kumuoa. Wote hao; kijana wa
kie na wa kiume wakifika kwenye ndoa hujibainisha tabia zao zote mbaya, ambapo
kuzirekebisha kunahitajika hekima ya kimbingu ya wanandoa na Mungu aingilie
kati.
‘R’Ruhusa
ya Wazazi
Ruhusa toka kwa wazazi huwa ni jambo la
msingi sana kwa wachumba ili kuweza kuoana. Mbaraka wa wazazi ni bora na mhimu
kwa wachumba katika safari ya kuoana na kuanzisha familia. Tena ni vyema pande
zote za wazazi zikaridhia ili wachumba kuendelea na mchakato wa kufanikisha
ndoa. Kuridhia kwa wazazi hutengeneza upendo kila upande wa wazazi wa wanandoa katika
familia (soma Mwanzo 29:21-23).
Japo kunawakati pia wazazi hupinga
kulingana na mila, wakati mwingine utashi wao au imani, hivyo mtii baba na mama
katika misingi ya Kibiblia na sio misingi iliyo nje na neno la Mungu. Hekima ya
wachumba katika kushauri itumike pale inapoonekana kuwa wazazi hawako sahihi
kwa yale wanayolazimisha kulingana na neno la Mungu linavyo elekeza, na pia
mazuri yaliyo mema ya wazazi wachumba wayafuate na kuyatii.
Samsoni
mnadhiri wa Mungu alipingwa na wazazi wake kwa jambo jema kabisa; yeye mwenyewe
alikengeuka kwa utashi wake mwenyewe. Ukisoma “Waamuzi 14:1-4” inaonesha
kuwa wazazi wake Samsoni walimpinga kwa ombi lake baya. Maamuzi yake Samsoni
yalikuwa kinyume na imani kama mnadhiri wa Mungu hivyo ilimgharimu mateso na
hadi kifo akiwa mateka katika himaya ya Wafilisti waabudu miungu.
‘S’Sura
na Umbo la Mchumba
Ni vyema kuchagua mchumba utakayempenda
daima wakati wote wa maisha ya ndoa kwa kuzingatia uzuri wa tabia kwanza na
uzuri wa umbo. Kila mtu ni mzuri kwa asili yake, kulingana na muonekano wa nje
au tabia za ndani. Biblia inazungumzia sana uzuri wa asili na uzuri wa tabia na
sio uzuri wa kununua au mapambo ya gharama na vito vya thamani. Katika lugha
yetu ya Kiswahili ni vyema ukatofautisha uzuri na urembo au ulimbwende.
Uzuri ni wa asili, urembo au ulimbwende ni
mapambo na muonekano wa mavazi katika mwili. Japo uzuri na urembo huenda pamoja
na huwezi ukautofautisha kwa uharaka; maana wapo wazuri kwa sababu ya mapambo
na mavazi, na wapo wabaya kwa sababu ya kukosa mapambo na mavazi nadhifu.
Soma mafungu yafuatayo: Esta
1:19 inazungumzia ukarimu, Mwanzo
26:7 inazungumzia uzuri wa Rebeka, Wimbo 2:14 inazungumzia uzuri wa
umbo na sauti, Wimbo1:15 inahusu uzuri wa mwanmke, Wimbo 5:10 inasifu rangi
na umashuhuri na Esta 2:7 inasadiki
uzuri wa sura na tabia njema.
‘T’Tamaduni
Zenu Zisitofautiane Sana
Suala la tamaduni huleta changamoto na
tofauti nyingi sana na hupelekea kutokea kwa migogoro katika ndoa; hivyo ni
vyema pia kwa wachumba kabla hawajaoana lazima waliangalie hili ili lisije
likawa changamoto aidha wao kwa wao au kutoka kwa ndugu zao (angalia Mwanzo
28:2 na Waamzi 14:1-3). Kwenye biblia hasa agano la kale, suala la
utamaduni limejitokeza katika mgongo wa imani kama inavyotanabaishwa katika
mafungu tajwa hapo juu. Agano jipya halitilii sana mkazo wa tamaduni bali imani.
Endapo Imani ni moja, suala la utamaduni
halipo. Hakuna tamaduni iliyobora kuliko nyingine, isipokuwa ni mitindo tu ya
maisha ndiyo huleta tofauti ya tamaduni moja na nyingine. Watu wa imani moja si
sawa kulishupalia suala la utamaduni maana huleta utengano na ubaguzi. Kwa sasa
kutokana na kuingiliana, kuoleana na msingi wa utamaduni wetu upo juu ya tabia
ya Yesu Kristo; tamaduni zetu hazina nafasi tena, bali hoja ya msingi ni imani
hazitakiwi kutofautiana kama ilivyonenwa katika Mwanzo 24:3-4.
‘U’Ukarimu
na Uvumilivu wa Mchumba
Kipengele hiki kitamhusu sana mwanamke na
kiasi mwanamume, maana mwanamke ndio muhimili mkuu wa familia japo baba ndiye
kichwa cha familia. Mwangalie mchumba wako Je, anaweza kuvumilia katika shida
bila kusaliti anapoishiwa? Mwanamke katika ndoa na familia yake, awe na moyo wa
ukalimu, huruma, kutoa na kusaidia wengine walio wahitaji (soma Mithali
31:20). Baadhi ya wanawake
wana roho mbaya na hawana hata tone moja la ukalimu na moyo wa kusaidia
wengine; wakati mwingine huwabagua wale wasio wa upande wa familia yake (suala
hili lipo hata kwa wanaume pia).
Mwanamke anayemcha Mungu ni sehemu ya
kimbilio na msaada kwa jamii na wanafamilia wanaomzunguka. Moyo wa kutoa,
kusaidia wahitaji na masikini pamoja na kuwakalimu wageni ndizo funguo za
baraka ya familia. Roho mbaya na ukali hukimbiza wageni katika familia, na
kupelekea kufunga milango yote ya baraka kutoka kwa Baba wa Mianga. Mwanamke
mwanandoa mtarajiwa lazima ajenge tabia ya kuvaa viatu vya matatizo ya wengine,
ahurumie na kukumbuka kuwaombea walio katika shida na changamoto.
Mwanamke ambae ni mke mtarajiwa yampasa
kuwa mwangalifu ili kujipatia mume mwenye tabia njema. Katika 1Samweli
25:1-42, mtumishi wa Mungu Daudi alipanga kumwangamiza Nabali kwa
sababu ya kukosa hekima ya maneno na fadhira juu ya yale Daudi aliyomtendea
katika kumlindia mifugo yake, lakini Abigaeli
mkewe Nabali alijishusha kwa Daudi; kwa kutumia hekima na maneno mazuri alifanikisha
kumuepushia mumewe na upanga wa Daudi.
‘V’Vumilia
Mapungufu Aliyonayo Mchumba Ikiwezekana
Kama tulivyoona kwenye kipengele cha kubaini kasoro za mchumba, kuwa hakuna
mwanadamu aliyekamilika asilimia mia. Ukimpata asiyekuwa na kasoro au hana mapungufu,
tegemea malaika pekee na ambapo hapa duniani hayupo. Yapo mapungufu mengi
ambayo yanaweza kujipambanua kutokana na silika ya dhambi kwa mwanadamu.
Mapungufu hayo yanaweza kuwa yaliyo katika nyanja kuu mbili, yaani mapungufu
yatokanayo na wasifu wa nje (mapungufu ya kimaumbile) na mapungu yatokanayo na
wasifu wa ndani (matendo ya kiroho zaidi, mfano uchoyo, hasira, kiburi n.k).
Suala la kumvumilia mchumba kutokana na
mapungufu yake ni kanuni ya kimbingu kama jinsi Mungu anavyotuvumilia kwa hali
ya juu. Kuvumilia pekee hakutoshi, bali muombee, mwelekeze kwa upole na
kumfundisha kwa moyo wa upendo. Kwa mtazamo wangu; tabia ni uchaguzi tofauti na
kalama ambapo Mungu humpatia mtu.
Mungu anasehemu kubwa sana ya
kutubadirisha kuliko tunavyoweza kufikiri na kufanya kwa uwezo wetu.
Tukimshirikisha Yeye aweza kutubadirisha na kuwa nuru au chumvi ya ulimwengu.
Mungu alimbadirisha Petro, Paulo; hivyo tukimwomba kwa nia ya dhati
atatubadirisha au kubadirisha tabia ya mchumba usiyoipenda.
‘W’Wasilianeni
Mara kwa Mara
Kuwasiliana ni mojawapo ya kanuni
inayoweza kufanikisha kudumu kwa uchumba endapo wawili miongoni mwa wachumba
wako mbali kimazingira. Kuwasiliana mara kwa mara kunasaidia kujenga uhusiano
na kutambuana mapungufu au matatizo, hata kukuza upendo wa wachumba. Uchumba waweza
vunjika kwa sababu ya kukosekana kwa mawasiliano ya karibu na ya mara kwa mara.
Bila mawasiliano kutokana na umbali, mchumba
anaweza kumsahau yule wa mbali endapo atajitokeza anayeonesha kujari kwa
ukaribu na kumjulia hali au kuzungumza naye mara kwa mara. Zipo njia nyingi za
kuwasiliana kwa ulimwengu wa sasa; kuwasiliana kwa weza kuwa katika kuombeana,
kuwasiliana kwa kutumia simu, barua kwa njia ya posta, barua pepe na mitandao ya
kijamii.
Mfumo wa maisha wa sasa haulingani na
mfumo wa maisha ya babu zetu wa zamani, vivyo hivyo uvumilivu na uaminifu bila
kuvunja uchumba kwa hivi sasa hauwezekani kwa sababu ya kukosa mawasiliano kwa
dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia. Kuwasiliana kunakumbusha kutunza ahadi
ya wachumba ili kulifikia lengo lao la kuoana. Kuwasiliana pia kunaonesha
upendo katika kumjali mchumba ili aonekane kuwa ni wa thamani, pamoja na
kutiana moyo ili kuvishinda vishawishi.
‘Y’Yakinisha
Pendo la Mchumba
Kwa mujibu wa 1Wakorintho 13:4-13; upendo
ni uwazi, upendo ni uvumilivu, upendo hauchoshi, upendo huwafanya wapendao kubebeana
matatizo na shida, upendo ni furaha, hivyo upendo haujifichi. Ni vyema mchumba
akaangalia nakuchunguza kweli ya upendo wa mchumba wake. Mchumba aliye na upendo
wa kweli, atamuweka mchumba wake kama muhuri moyoni mwake.
Katika kitabu cha Waamuzi sura ya 16, upendo
wa “Delila”
kwa Samsoni”
haukuyakinisha upendo wa kweli ukiachana na suala la uzinzi na uasherati kabla
ya ndoa. Upendo wa Adamu kwa Hawa ni upendo wa kuigwa kwa
wachumba (ila si kwa kumuasi Mungu kama alivyofanya Adamu). Kisa hiki cha Hawa
na Adamu wengi hukichukulia juu juu; unajua haikuwa rahisi sana kwa Adamu
kufanya kosa la kula tunda alipoletewa na Hawa. Adamu alikubali kula tunda kwa
sababu ya upendo kwa mke wake, kuwa asiangamie peke yake (Mwanzo 3:6).
Tufanye nini maana Yesu ameturejeshea kile
tulichokipoteza kutoka kwa wazazi wetu kwenye bustani ya Edeni maana ni upendo
mwingine waajabu wa agape, Yesu
kukiacha kiti chake cha enzi ili atufie siye tusiostahili. Hivyo, upendo ulilipwa
kwa upendo wa juu zaidi. Naamini kuwa; kuoa au kuolewa na mtu usiyempenda kwa
dhati toka moyoni hupelekea migogoro katika ndoa na kuingia katika dhambi ya
kuchukiana na kuishi kwa kuvumiliana.
‘Z’Zuia
Kufanya Ngono Kabla ya Ndoa
Uchumba wa Yusufu na Mariamu
ulikuwa katika kanuni ya kujizuia kufanya ngono hadi ndoa itakapofungwa. Mariamu
alikuwa bikira safi hakuwa ameguswa na mwanamume, na Yusufu alijua kanuni ya
uchumba kuwa kufanya ngono nje ya ndoa ni kujichumia dhambi ya uzinzi (Mathayo
1:18-24 inaleza kisa chote). Kumekuwepo na ushawishi mkubwa wa utandawazi
na makundi rika yanayoharibu maana ya uchumba, kwa kusababisha vijanawengi
kufanya ngono kabla ya ndoa, hivyo kushiriki dhambi ya uzinzi.
Mwonja asali haonji mara moja, akionja
huchonga mzinga daima. Samson alionja mara moja na ikabidi ajenge mzinga (Waamuzi
16:1, na Waamzi 14:7). Thamani ya mwanamume au mwanamke hupotea kwa
mchumba wake endapo wachumba hao watakutana kimwili kabla ya ndoa. Kuruhusu
ngono kabla ya ndoa husababisha uchumba kuvunjika, maana ile shauku ya kuoana
hupotea kwa sababu wachumba wameshajuana tayari, hivyo hufanyika mchakato wa
kutafuta mchumba mpya.
Ngono kabla ya ndoa husababisha maambukizi
ya magonjwa ya zinaa, mimba za nje ya ndoa, au kuwa na watoto wengi kwa baba au
mama tofauti. Nivyema wachumba wakawa waaminifu hadi ndoa ifungwe ili washiriki
zawadi yao kwa uhuru.
Wataalamu wa mahusiano katika misingi ya Kibiblia,
hawashauri uchumba uzidi mwaka mmoja kama hakuna kipingamizi kwa wachumba
kuoana. Uchumba wa muda mrefu mara nyingi huvunjika, au husababisha wachumba kufanya
ngono babla ya ndoa. Jambo hilo husababisha upendo kupungua au kutoweka kwa
sababu Shetani anakuwa ameweka himaya yake, na kupelekea uchumba uvunjike.
Ndoa ni takatifu, ndoa ni kielelezo cha
uhusiano wa mwanadamu na Mungu, au Mungu na kanisa, hivyo ndoa iheshimiwe na
watu wote. Shetani huharibu utukufu wandoa ili afanikishe kuharibu familia,
kanisa na jamii kwa ujumla; hivyo, yawapasa wachumba kuwa waangalifu daima
katika hatua zao za uchumba, na haina haja ya kuchelewa kuoana kama hakuna
kipingamizi cha kuwachelewesha.
Comments
Post a Comment
Thanks for viewing and passing through NMEE blog. Keep following the blog