FAIDA ZA KUTOFANYA UZINZI AU NGONO HADI WAKATI WA NDOA




     Yampasa kijana wa kike au wa kiume aliye Mkristo ajiepushe kushiriki ngono. Ni vyema vijana wakahakikisha kutunza usafi wa miili yao na kuheshimu utukufu na usafi wa tendo la ndoa. Vijana wa kike na wa kiume wafanye mambo yafuatayo ili kuepuka kujamiiana kabla ya ndoa:
1. Waepuke kuwa katika mazingira hatarishi yanayoshawishi kufanya zinaa, mfano sinema na sehemu zingine za starehe.
2. Waepuke marafiki wabaya katika kundi rika ambao wanamatendo mabaya.
3. Waepuke utembeaji wa usiku bila sababu zo zote katika mazingira yasiyo salama kwao.
4. Waepuke kuangalia au kusoma vitu vinavyohusu mapenzi na ngono ili wasiziamshe hisia zao.
5. Waoe haraka kama umri umefika ili kuiepuka zinaa.
6. Wajihusishe na programu za kanisa juu ya ibada na kumtumikia Mungu ili muda wote waufikirie utukufu wa Bwana.
7. Wapende kusoma na kulitafakari neno la Mungu ili Roho wa Mungu akae ndani ya maisha yao.
8. Wajue kufanya ngono kabla ya ndoa ni dhambi na wanavunja amri ya saba ya Mungu inayokataza kufanya uzinzi.
9. Wajiheshimu katika mavazi, mazungumzo na mienendo mizima ya maisha yao ili wasimpe nafasi Shetani.
10. Wapende kufanya mazoezi hususani ya viungo vya mwili ili kuondoa hisia na mawazo mabaya katika fikra zao.

Faida za Kujilinda Bila Kutenda Ngono Hadi Wakati wa Ndoa
     Kujitunza na kujilinda bila kutenda tendo la ndoa kwa vijana wa kike na wakiume kunafaida zifuatazo:

1. Kuwa mwenzi unayefaa katika ndoa.
2. Huamsha ari na hisia za kujithamini.
3. Ni kipimo kizuri cha uwezo wa kuzuia au kuzimudu hisia.
4. Hujenga uwezo wa uvumilivu wa kihisia.
5. Hutoa nafasi ya kujikita katika mambo na malengo ya msingi ya maisha bila kuingiliwa na tamaa za mapenzi kabla ya ndoa.
6. Hujenga taswira na msingi wa uaminifu kwa kijana.
7. Huepusha maumivu ya mapenzi kwa vijana kabla ya ndoa.
8. Husaidia kutunza via vya uzazi mpaka vikomae ili kuwa tayari kwa ajiri ya kushiriki tendo la ndoa na kuzaa pindi kijana awapo ndani ya ndoa.
9. Huepusha kuharibu hisia na ubongo katika kufikiria mapenzi kabla ya ndoa.
10. Huepusha utumwa wa ngono kabla ya ndoa kwa vijana.
11. Huepusha utoaji wa mimba zitokanazo na kushiriki tendo la ndoa bila malengo ya kuzaa.
13. Huondoa hofu kwa vijana juu ya kuhisi maambukizi ya magonjwa ya zinaa na Virusi Vya Ukimwi kwa kushiriki ngono kabla ya kuoa au kuolewa.
14. Huwaepusha vijana dhidi ya kupata mimba katika umri mdogo.
                                                                                                                           
Nini cha Kufanya Endapo Kijana Ameshiriki Uzinzi (ngono) Kabla ya Ndoa?
     Kijana wa kike au kiume endapo atakuwa ameshiriki ngono aidha kwa makusudi au bahati mbaya (ni mara chache sana bahati mbaya hujitokeza) yampasa afanye mambo yafuatayo ili awe safi mbele za Mungu na kujipanga kwa ajili ya kushiriki awapo ndani ya ndoa tu:

1.      Fanya toba ya dhati kwa Mungu kisha acha kabisa.
2.      Badirisha mienendo na mitindo yako ya maisha iliyokuwa inakuvuta kufanya uzinzi.
3.      Epuka makundi rika yaliyo maovu na makundi yenye tabia mbaya na hatarishi kwako.
4.      Jilinde na vitu vinavyosababisha kuleta hisia za kimapenzi mfano sinema, tamthiliya, program za TV za mapenzi, majarida na vitabu vya mapenzi.
5.      Epuka kutembelea mazingira yenye ushawishi mkubwa wa kubadili hisia zako na kutamani kufanya mapenzi.
6.      Tenga muda mwingi kwa ajili ya kujifunza neno la Mungu kwa kusoma Biblia na kushiriki ibada na programu mbalimbali za kanisa.
7.      Pambana kuzidi kuwa safi siyo kwa uweza wako pekee bali mkabidhi tatizo linalokusumbua Yesu Kristo aliye mshindi wa dhambi na hutushindia pia.
8.       Chunga mdomo wako katika mazungumzo na aina ya mavazi unayovaa maana kwayo huashiria urahisi na husadifu tabia ya mtu.
9.      Achana na tabia ya kuangalia picha na mikanda ya watu walio uchi au nusu uchi maana huathiri ubongo na hisia.


Madhara ya Kuharakisha Ngono Kabla ya Ndoa
     Mtumishi wa Mungu Gibsoni Ezekieli yeye anasema “vijana wote wa kike na wakiume yawapasa kujua kuwa hakuna mstari unaotenganisha kutoka ujana kwenda utu uzima. Namna unavyofanya mambo yako ukiwa kijana huathiri utu uzima wako. Tabia unazoendekeza wakati wa ujana zitakufuata utakapokuwa mtu mzima. Vijana wengi wamekuwa na tabia ya kuwa na mazoea mabaya, hususani juu ya kutoheshimu na kutilia umakini suala la tendo la ndoa. Mazoea ya kubadirisha wasichana na wavulana kama nguo kwa kujiaminisha kuwa wataacha kufanya hivyo endapo wataoa au kuolewa na kuwa katika ndoa zao”.

     Anaendelea kusema kuwa “Mazoea mabaya ni muuaji anayeonekana hana hatia mwanzoni, na vijana hujifariji nitakapooa au kuolewa kwa sababu nitakuwa na mtu wa kunipoza haja zangu nitaacha uzinzi na uasherati. Hawajui ya kuwa utegemezi au uraibu (addiction) humfanya aliyezoea kuhitaji kufanya hivyo mara kwa mara. Pia husababisha kitu ambacho wataalam wa saikolojia hukiita Objectification of women and men, yaaani mwanamke au mwanamume anakuwa kama ni kitu tu cha kumridhisha mwanamume au mwanamke. Mwanamke au mwanamume anakuwa si mtu bali kitu cha kutuliza haja za kingono katika maisha”.

     Kama tulivyoona katika nukuu ya maelezo ya mtumishi wa Mungu Gibson Ezekiel; hivyo basi, mazoea ya ngono kabla ya ndoa kwa wasichana na wavulana huleta athari badaye katika nyanja zifuatazo:
     1. Kutokana na mazoea ya kubadirisha badirisha au kufanya ngono mara nyingi na kwa hali ya juu kabla ya ndoa, mwanamke au mwanamume huonekana kama “sex machine” katika ndoa kwa sababu tendo hilo limejengeka katika mawazo na fikra kama starehe na haja ya msingi kila wakati. Inapoonekana mke au mume hawezi kuwa tayari muda wote kutenda tendo la ndoa kwa mara nyingi inavyotakiwa kufanya kama miongoni mwa mmoja wa wanandoa kama alivyozoea kufanya mara kwa mara hapo kabla ya ndoa, mmoja hutoka nje ya ndoa ili kukidhi haja yake ya tendo la ndoa.
     2. Yawezakuwa mke au mume huyo aliyepatikana kuwa tofauti na wale aliowazoea kushiriki nao ngono hapo awali. Kwa ufupi unaweza ukaoa au kuolewa; mkeo au mumeo asikupe ushirikiano kama ilivyotazamiwa kutokana na mazoea. Uhitaji mwingi kati ya mmoja wa wanandoa itapelekea kuchepuka kwa sababu ya kushindwa kuvumilia hisia endapo mwezi ameonekana kulegalega na kutokukidhi haja ya tendo la ndoa aidha, kwa sababu ya majukumu na uchovu wa kazi au ugonjwa au ujauzito kwa mwanamke. Ndiyo maana wanandoa wengi huendeleza tabia zilezile za kuwa na wenzi wengine wengi hata baada ya kuoa au kuolewa, kwani hitaji lake lipo juu sana. Kwa sababu hiyo, tabia ya uzinzi hujitokeza kwa wanandoa walio wengi.
     Jambo la kuzingatia: Imeandikwa kuwa mume au mke kwa pamoja wasinyimane, tena mume ana mamlaka juu ya mwili wa mkewe na mke ana mamlaka juu ya mwili wa mumewe. Lakini Paulo akaonya ya kwamba, wanandoa wafanye tendo la ndoa kwa kiasi ili wasije wakajaribiwa na Shetani katika hilo na kutenda dhambi (1Wakorintho 7:1-5).

Comments

Popular posts from this blog

MAJINA YA WANAWAKE KATIKA BIBLIA ‘A’ HADI ‘Z’

SOMO: MADHARA YA KUKATAA KUMTII MUNGU

MFANO WA MPANGO KAZI