FALSAFA YA MUNGU KATIKA NDOA



Fungu: Wimbo Uliobora 5:16 “Kinywa chake kimejaa maneneo matamu, Ndiye mzuri sana pia. Ni huyu mpendwa wangu, Ni huyu rafiki yangu, Enyi binti za Yerusalemu”


01: UTANGULIZI
Ufafanuzi wa fungu kuu: Fungu kuu limebeba mkitadha wa mambo makuu matano (5) yafuatayo:
1.     Maneno ya hekima, busara, staha, faraja, upendo, shime na kutia moyo.
2.     Msistizo juu ya uzuri: 1. tabia na mwenendo, 2. umbo na muonekano, 3. usafi na unadhifu.
3.     Upendo usiokuwa na chembe ya ubinafsi.
4.     Uwazi na ukweli.
5.     Urafiki miongoni mwa wapendanao.

Ombi:

02: KIINI CHA SOMO
Sambamba na hivyo vipengele vitano (5) juu ya muktadha mzima wa fungu letu kuu (Wimbo Uliobora 5:16), leo tutaangalia kwa kina kipengele kimoja tu kinachohusu, urafiki miongoni mwa wanandoa (wapendanao).

“Ili Mkristo ye yote aweze kuifikia ndoa lazima aanze na hatua mama mbili, ambazo ni urafiki na uchumba.   Bila hatua hizo mama, itakuwa ni ndoa iliyotokana na utashi wa watu wengine nje na wale wawili (wachumba)  wanaotazamia  au wanandoa waliooana. Ndoa inayopatikana bila urafiki na uchumba, ni ndoa iliyofanikishwa na watu wengine bila adhima ya wawili (mke na mume) kukubaliana kisha kuridhiana wao kwa wao. Urafiki na uchumba ndiyo barabara sahihi inayompeleka mtu katika ndoa.....”  [Maelezo ya Frank P. K. Katika kitabu chake cha “Uchumba na maisha ya ndoa katika misingi ya Kikristo” toleo la tatu 2019] .

Ndoa kutokuwa na furaha haisababishwi na ukosefu upendo, bali husababishwa na ukosefu wa urafiki miongoni mwa wanandoa wenyewe. Ndiyo maana wale wote walioachana siyo kwamba hawakupendana, rahasha walipendana sana tu; hivyo, upendo pekee hauwezi ukaleta amani katika familiya bila mizizi ya kina ya urafiki kwa wanandoa.

Urafiki miongoni mwa wanandoa huzalisha umoja ambao huleta upendo. Hivyo, kukosekana kwa urafiki husababisha kukosekana kwa umoja katika ndoa. 
  

Umoja Miongoni Mwa Wanadoa
Kwa mujibu wa falsafa ya Mungu “umoja katika ndoa ni kuwa mwili mmoja”; Kama Mungu alivyosema katika Mwanzo 2: 24, kuwa “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja”.

Kuwa mwili mmoja katika ndoa ni kufahamiana, kupendana, kuumia wakati mwingine anapoumizwa, kufurahi wakati mwingine anapofurahi. Kuwa mwili mmoja kunaongeza uwajibikaji na huchochea mahusiano/mahaba (Mwanzo 26:8).

Yeyote anayeingia katika ndoa, amekubali kushiriki uzoefu na kutimiza mpango wa awali wa Mungu. Umoja wa kimwili hutupa hisia za ukaribu juu ya wenzi wetu na hututiajoto, shime na kuhakikisha uwepo wa ulinzi.

Katika umoja wa kimwili ndipo mume na mke hushirikiana katika mawazo, hisia, matamanio, ndoto, malengo, uhuru, furaha na makwazo katika mazingira salama. Umoja huo wa kimwili ndiyo Mungu alioukusudia katika ndoa zetu na hicho huwasukuma mke na mume kuoana.

Umoja wa kimwili (yaani ndoa) hutengeneza uhalali wa kumilikiana na kushikamana kwa wanandoa.  Umoja wa kimwili hutupatia fursa ya kutodai nini tunaweza kupata bali nini yatupasa kutoa kwa wenzi wetu; maana upendo katika ndoa siyo hisia tu baali ni maamuzi pia.

Hivyo basi, twaweza sadiki kuwa, umoja katika mwili ndiyo falsafa ya ndoa aliyoiasisi Mungu (rejea kwa kusoma Mwanzo 2:22 – 23; Mwanzo 5:2).

Nyanja Nne (4) za Umoja katika Mwili kwa Wanandoa
Umoja katika mwili kwa wanandoa upo katika Nyanja kuu nne (4) zifuatazo: umoja wa kimwili katika hisia, umoja wa kimwili katika akili, umoja wa kimwili katika tendo la ndoa na umoja wa katika mambo ya kiroho.

1.     Umoja wa Kimwili katika Hisia
·        Ni wakati ambapo mwenzi anaweza akaongea kwa uwazi na uhuru juu ya hisia na matamanio yake.
·        Ni wakati ambapo wenzi hushirikishana, huthaminiana, hushiriki adha na furaha na huaminiana wao kwa wao.
·        Tafiti zinaonesha kuwa, mara nyingi baada ya honeymoon wanandoa hupoteza mvuto wa kuwa pamoja kihisia.
·        Zingatia mambo machache yafuatayo katika suala la hisia baina ya mwanamke na mwanamume:

1.     Wanawake huongea huku wakisikiliza kwa wakati mmoja, lakini mwanamume hawezi kusikiliza na kuongea kwa wakati mmoja.

2.     Mwanamke anaweza akamuacha mwenzi wake kwa sababu hamtimizii hitaji la hisiazake. Na mwanamume anaweza akamuacha mwenzi wake kwa sababu ya kuona mwenzi huyo hana furaha kwa sababu ya mahitaji anayotoa.     
     
3.     Mwanamume hapendi kukosolewa au kuonekana amekosea kwa sababu hujihisi kuwa hajafanya jukumu lake impasavyo. Na hii ndiyo sababu ambayo humfanya mwanamume kuwa mgumu kusema ‘samahani’ maana huona kama anajihukumu moja kwa moja kuwa  anamakosa na ameshindwa.

4.     Mwanamume huficha hisia zake akimanisha kutoonesha wazi wazi udhaifu wake. Mwanamke huweka wazi matatizo yake  kwani hujihisi ahueni kutoka kwenye msongo.

5.     Wanawake hawahitaji utatuzi wa matatizo yao, bali wanahitaji kuongea matatizo yao na kusikilizwa tu. Mwanamke kushiriki tatizo lake na mtu mwingine ni kuonesha ishara ya uaminifu katika urafiki au uhusiano.

6.      Mwanamume anapokuwa na msongo hawezi akaongea. Wanaume huongea kwa ndani kwa sababu ubongo wao  (wa kulia) hauna sehemu imara ya mazungumzo kama ilivyo kwa wanawake.

7.     Katika hisia, mwanamke ni mwongeaji na mwanamume ni mfikiriaji.

8.     Wanawake hulia zaidi kuliko wanaume, kwa sababu ubongo wa wanawake umeunganisha na hisia za ubongo mwingine.

2.     Umoja wa Kimwili katika Akili
·        Huu ni umoja unaohusisha mitazamo, maamuzi na fikra.
·        Hapa wanandoa hushirikishana ama hushirikiana katika mitazamo, mawazo na maamuzi yao.
·        Katika umoja huu si kwamba ndoa inawahakikishia wanandoa kukubaliana mara-zote, rahasha.
·        Wanandoa wanaweza wakauchochea umoja huu katika akili zao kwa kusikilizana, kuheshimiana na kutiana moyo.
·        Umoja huu hauwezi kuishi (kudumu) endapo mazingira wanandoa yametawaliwa na kupishana kauli, mitazamo na kushushana viwango.
·        Wakati mwingine inawezaikatokea wanandoa wasikubaliane kabisa.

3.     Umoja wa Kimwili Katika tendo la ndoa
·        Hii ndiyo zawadi nzuri ambayo mungu aliwapatia wanandoa yaani waliooana tu.
·        Umoja huu wa kimwili hufanyika vizuri endapo upendo uliopo si wamashariti (1Wakorintho 13:4-5).
·        Katika umoja huu, wanaume huona ni hitaji lao la kwanza kuliko wanawake (ambapo wanawake hitaji lao la kwanza ni lile la ummoja wa kimwili katika hisia).
·        Endapo umoja wa kimwili katika tendo la ndoa na ule wa kihisia kwa pamoja ukikuza (kustawishwa), wanandoa watapitia uzoefu mzuri usio na changamoto nyingi katika mahusiano yao ya kindoa.
 

4.     Umoja wa katika  Mambo ya Kiroho
·        Umoja huu ndiyo msingi wa yote katika umoja wa kimwili.
·        Umoja huu umejikita zaidi katika kushiriki mambo ya kiroho, yaani imani na kukua katika Kristo.
·        Umoja huu ndio huzalisha familiya imara kama wanandoa watajikabidhi kwa Mungu mmoja mmoja na kwa pamoja kama wenzi.
·        Umoja huu ndiyo unakamilisha kusudio zima la wenzi “kuwa mwili mmoja”.
·        Umoja huu, husaidi wanandoa katika kutiana moyo na kukua zaidi kiroho hata katika nyakati ngumu (mrejee mke wa Ayubu katika Ayubu 2:7-10).
·        Umoja huu, hutokea pia wakati ambapo mmoja wa wanandoa kudumu katika kuomba na mwingine kukata tama (au kuwepo hali ya kukatishana tama).
·        Wakati (ambapo) wanandoa wanapokuwa vizuri katika mambo ya kiroho, huwa rahisi kufanya toba au kukubali kosa ama kutoa msamaha na kusameheana.
·        Katika umoja huu, safari zetu za kindoa huwa ni njia kuu katika safari zetu za kumwelekea Mungu.
·        Yatupasa kutambua kuwa, misukosuko katika ndoa ni misukosuko katika mambo ya kiroho, hivyo, kadri tunavyomsogelea Mungu, ndivyo tunavyokuwa karibu kwa kila mwanandoa katika ndoa zetu. Na kadri tunavyojitenga na Mungu ndivyo hivyo tunavyotengana katika ndoa.
·        Mungu ni mwaminifu, hatatuacha kamwe kama tulianza naye, atatushindia katika miisho ya maisha ya ndoa zetu.

03: HITIMISHO
Kila mwanadamu amepewa wa kufananaye (Mwanzo 2:28). Upendo wa wanandoa lazima utokane ama ushikamanishwe na upendo wa Kristo (upendo wa agape). Tutumie kanuni ya Waefo 5:25 – 29:
·        Jitoe kwa ajili ya mwenzi wako kama Kristo alivyojitoa (vs. 25)
·        Mpende mwenzi wako maana utakuwa umeupenda mwili wako (vs. 28–29)
·        Mthamini mwenzi wako maana utakuwa umeuthamini mwilili wako (vs. 29)

Mungu awabariki Sana: Amina!



Comments

Popular posts from this blog

MAJINA YA WANAWAKE KATIKA BIBLIA ‘A’ HADI ‘Z’

MFANO WA MPANGO KAZI

SOMO: MADHARA YA KUKATAA KUMTII MUNGU