MWIKO KUVUNJIKA CHUNGUNI

Salamu nawasalimu, Amani nawatakia,
Niishikapo kalamu, swali nawaulizia,
Si fumbo la kitalaamu, ni hoja nawapangia,
Umevunjika chunguni, mwiko wangu, mwiko wangu!
Kupika ninavyopika, nikipika vinalika,
Vinalika na kulika, na vidole kulambika,
Mwiko ninaposhika, Vitu vinakorogeka,
Umevunjika chunguni, mwiko wangu, mwiko wangu!
Viungo nikiongeza, chumvi na mdalasini,
Na ndimu nikinyunyiza, kolienda na komuni,
Utamu nikikoleza, harufu tamu chunguni,
Umevunjika chunguni, mwiko wangu, mwiko wangu!
Sasa nashindwa kupika, mwiko umevunjikia,
Nilipokuwa napika, chunguni kumegukia,
Mwiko wangu wa hakika, mwingine sitamania,
Umevunjika chunguni, mwiko wangu, mwiko wangu!
Maana yake ni nini, mwiko kunivunjikia,
Niambieni asilani, mizimu imechukia?
Nichinje mnyama gani, mkosi kufukuzia,
Umevunjika chunguni, mwiko wangu, mwiko wangu!
Nawauliza watani, na watani wa watani,
Hili jambo ni la nini, kuvunjikia chunguni,
Kama ni zuri ni nini, niambieni jamani,
Umevunjika chunguni, mwiko wangu, mwiko wangu!
Swali nimewauliza, beti zangu nazifunga,
Msiseme nawakwaza, imenibidi kulonga,
Mwenzenu naona kiza, nashindwa tena kusonga,
Umevunjika chunguni, mwiko wangu, mwiko wangu!

Comments

Popular posts from this blog

MAJINA YA WANAWAKE KATIKA BIBLIA ‘A’ HADI ‘Z’

SOMO: MADHARA YA KUKATAA KUMTII MUNGU

MFANO WA MPANGO KAZI