NGUVU YA MSAMAHA


Katika injili ya Marko 11:25-26 kusameheana kumesisitizwa kama ifuatavyo: 25”Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili Baba yenu aliyembinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. 26”Lakini kama ninyi hamsamehi, wala Baba yenu aliye Mbinguni hatawasemehe ninyi makosa yenu”

Kwa Nini ni Muhimu Kusamehe?
Zipo sababu nyingi za kusamehe, zifuatazo ni miongoni mwazo:

1.      Kusamehe ni tabia ya Mungu, na wamchao: Mwanadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu (Mwanzo 1:26). Mwanadamu amchae Mungu kwa kweli yote, lazima awe na tabia ya Mungu kwa maana Mungu ni kielelezo cha kwanza cha kusamehe kwa mwanadamu (Isaya 43:25. Isaya 1:18, 1Yohana 1:9).

2.      Kusamehe ni hali ya Upendo: Kama tunda la roho ni upendo vivyo hivyo kusamehe ni tunda la upendo (1Wakorintho 13:4-7). Tabia ya mtu amchae Mungu ni upendo kwa wengine hata kama atakwazwa. Mungu ni pendo, hata mwanadamu pia yampasa awe na upendo utokanao na Mungu. Kusamehe ni ishara na kielelezo cha upendo, kwa hiyo mtu anayesamehe anakiwango kikubwa cha upendo (Yohana 3:16. 1Yohana 4:8. Yeremia 29:11).

3.      Ni kufanya kama Mungu anavyotusame: Kama Mungu anavyomsamehe mwanadamu bila kuchoka binadamu pia yampasa kusamehe wengine vivyohivyo bila kuchoka (Yohana 1:12-13).

4.      Hakuna mwanadamu aliyemkamilifu asilimia 100: Endapo mtu atagundua kuwa, hakuna aliyemkamilifu asilimia zote, basi atakuwa anajua nini maana ya kutoa msamaha kwa wengine. Mwanadamu yeyote hukosea na kukosewa pia. Sio salama mwanadamu kujihesabia haki kuliko mwingine; maana hata yeye akikosea huhitaji kusamehewa pia. (Warumi 3:10, 23).

5.      Kusamehe kunaondoa mawazo ya kulipiza kisasi: Mwanandoa asipojenga tabia ya kusamehe hujenga mawazo ya kisasi; kutosamehe na kuwaza jambo baya juu ya mwingine ni sawa na yule aliyetenda kwa vitendo. Kisasi ni kile unachokirejesha kwa mtu; mfano kumnunia mtu, kutopokea simu yake, kumchongea na kumsema vibaya, kuua au kupanga njama za kuua mtu, kuchawia au kuloga, kumpiga mtu (Warumi 12:19.Yakobo 4: 12).

Madhara Yanayoweza kumpata Mtu Asiposamehe
Tabia ya kutoweza kusamehe hujenga hali au tabia ya kulipa kisasi. Kuwaza kulipa kisasi ni sawa na kutenda katika kulipa kisasi, hivyo mawazo au hatua za kisasi huwa na hasara zifuatazo kwa mmoja au wanandoa wote:

1.      Kunapelekea kujitenga na uwepo wa Mungu: Roho Mtakatifu hawezi kukaa mahali palipo na machafuko au Mungu hawezi akashikamana na mdhambi ambaye anawaza maovu bila kutubu. Kutosamehe kwa mtu huondoa uwepo wa Mungu kwa mtu huyo (Warumi 12:17, 21).

2.      Hupelekea matatizo mengine juu ya mlipa kisasi: Mtu asiyesamehe hutengeza ongezeko la majaribu mengine kumwandama maana mkono wa Mungu unapotoweka Sheteni huweka makazi ili kuzidi kumpoteza mtu huyo. (Mithali 17:13).

3.      Hupelekea kutenda au kuchuma dhambi ya mauaji (1Yohana 3:15, 1Yohana 3:11-12,  Mathayo 5:21-22): Kumuwazia mtu  mwingine babaya, hujenga moyo wa visasi hivyo, kujichumia dhambi ya mauaji maana dhambi hutendeka katika fikra (moyoni) matendo hufuata.

4.      Mtu alipaye kisasi hujiongezea uadui au maadui: Tabia ya kulipa kisasi haitatui tatizo bali huongeza matatizo na maadui

Namna ya Kufanya ili Mtu Aweze Kusamehe
Kusema “nimekusamehe lakini sintosahau” ni kutojua maana ya kusamehe, ili mwanadamu aweze kusamehe, yampasa kusahau kabisa juu ya kosa au baya alilotendewa. Mkristo amchaye BWANA yampasa ajue, kufuata, kufanya na kuyaishi mambo yafuatayo yatakayopelekea kusamehe na kusahau:

1. Ajue kuwa yeye ni mtoto wa Mungu hivyo yampasa kusamehe na kusahau kama Mungu awasameheavyo wanadamu na kufuta makosa yao (1Petro 1:18-19).
2. Ajitahidi kuwaombea mema na kuwapenda adui zake siku zote na siyo kulipa baya kwa baya (Mathayo 5:44-45), hivyo awawazie mema adui zake siku zote (Warumi 12:20-21)
3. Ajue kuwa yeye siye mwenye kujipigania, bali Mungu ndiye huwapigania walio wake, hivyo vita vyote si vyake bali ni vya Mungu mwenyewe na mwanadamu yampasa kumkabidhi Mungu matatizo yake (Ayubu 19:25, 2Nyakati 20:15).
4. Mwanadamu atambue kuwa, vita vyake si juu ya damu na nyama, bali ni ya kiroho zaidi maana pambano kuu bado linaendelea kati ya wema na ubaya yaani Shetani na Kristo (Waebrania 12:2-3, Wagalatia 4:7).
5. Ajuwe kuwa si mtu amkoseae au kumtendea mabaya bali ni Shetani anamtumia mwanadamu kutenda yaliyo maudhi.

Comments

Popular posts from this blog

MAJINA YA WANAWAKE KATIKA BIBLIA ‘A’ HADI ‘Z’

MFANO WA MPANGO KAZI

SOMO: MADHARA YA KUKATAA KUMTII MUNGU