UJASIRIAMALI NA BIASHARA KATIKA FAMILIA NA NDOA



     
     Uchumi imara wa familia (kwa wanandoa) hurahisisha upatikanaji wa mahitaji ya msingi ya familia pamoja na uhakika wa kuhudumia mahitaji ya watoto. Lakini pia, familia yenye uchumi mzuri inaweza ikasaidia kusukuma au kuendeleza na kukuza huduma ya uinjilisti na utume ulimwenguni kwa njia ya kumtolea Mungu zaka na sadaka pamoja na kuchangia programu mbalimbali za kazi ya utume ulimwenguni au katika kanisa mahalia.

     Pale wanandoa au wanafamilia wanapoitegemeza kazi ya Mungu, Mungu huwabariki na kuwapatia cho chote kile wanachokiomba, kama vile Mithali 16:3 inavyosema kuwa: “Mkabidhi BWANA kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika”. Maana imeandikwa pia kuwa: “Ni heri kumkimbilia BWANA kuliko kuwatumainia wanadamu” (Mithali 118:8).

     Hivyo basi, ni vizuri wanandoa kujituma katika kutafuta na kuzalisha ili kukuza kipato cha familia kupitia kazi za mikono yao maana Mungu hatawaacha kuwabariki kwa kujituma kwao na kufanya kazi kwa bidii. Bidii na jitihada ya kazi kwa wanando, iende sambamba na kumwomba Mungu (Luka 11:9-10); maana imeandikwa kuwa: “Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? Au akimwomba yai, atampa nge?” (Luka 11:11-12). 

     Hata hivyo, ukiwa na Mungu atakupa uwezo wa kuthubutu kuanzisha biashara au uzalishaji kama alivyothubutu Daudi katika kumkabili Goliathi kwa jina la BWANA (1Samweli 17:32, 45). Katika sura hii tutaangalia vipengere kadhaa vya muhimu juu ya kufanikisha kuanzisha biashara (hususani ujasiriamali) kwa wanandoa ili kukuza vipato vyao. 

A: Wazo la Biashara
     Biashara yo yote huanza na wazo la biashara. Wazo la biashara ni maelezo mafupi na fasaha yanayohusu uendeshaji wa shughuli ya biashara iliyokusudiwa. Wazo la biashara ni vyema likajikita katika gharama, bidhaa, huduma, mahitaji ya watu, bei, matakwa ya watu, ujuzi na uzoefu [Philemon Frank, 2016. Secrets of Success in Entrepreneurship].

     Biashara yenye ufanisi ni ile inayokidhi mahitaji ya wateja wake. Pia, biashara lazima iwapatie watu au wateja kile wanachohitaji au wanachotaka; hivyo basi, wazo la biashara litakuambia: aina ya bidhaa au huduma zitakazotolewa na biashara yako, nani watakuwa wateja wa biashara yako, jisjinsi au kipi biashara yako itakavyouza bidhaa zake au kutoa huduma zake na namna biashara yako itakayokidhi mahitaji ya wateja.

Jinsi ya Kutafuta Mawazo Mazuri ya Biashara
     Zipo namna mbalimbali za kutafuta mawazo mazuri ya biashara. mawazo yanayotokana na rasilimali zilizopo, shughuli iliyopo na uliyonayo, mahitaji Mawazo mazuri ya biashara yaweza patikana kwa vyanzo au njia zifuatazo:na shauku za watu juu ya kipi wakipate, kutoka fursa za biashara zinazoonekana au zilizo hai, mahitaji ya wateja talajali pamoja na ujuzi, ufahamu au uzoefu wa mtu husika. Sambamba na sababu hizo, Mungu anatakiwa apewe kipaumbele ili kuyanyosha mapito yote ya wazo la biashara (angalia katika Mithali 3:6).

Mambo Yanayounda Wazo Zuri la Biashara
     Unapohitaji kupata wazo bora au zuri la biashara (kutoka miongoni mwa mawazo mengi ya biashara), ni lazima ufahamu mambo yanayounda wazo zuri la biashara. Wazo zuri la biashara ni lile linalozingatia mambo yafuatayo: bidhaa au huduma inayotakiwa na wateja, biadhaa au huduma unayoweza kuuza kwa bei ambayo wateja wako wanaweza kuinunua na ambayo itakupatia faida, maarifa na ujuzi ulio nao au unaoweza kuupata ili kufanikisha uendeshaji wa biashara hiyo na mwisho rasilimali au fedha unazoweza kuwekeza katika biashara husika.

Ubunifu wa Wawazo la Biashara
     Wakati wa kutoa mawazo ya biashara ni vizuri uweke mawazo yako wazi kwa kila jambo. Fikiria mawazo mengi kadri uwezavyo na kuyaorodhesha kadiri uwezavyo juu ya biashara ambayo unaweza kuifanya. Biashara yenye mafanikio msingi wake ni wazo zuri la biashara. Ni muhimu kuwa na muda na kufanya juhudi, kufanya kazi kwa bidii katika kutambua mawazo ambayo yanastahiki na yenye kufaa sawa na neno la Mungu linvyosema: “Nanyi jipeni nguvu, wala mikono yenu isilegee; kwa maana kazi yenu itakuwa na ijara” (2Mambo ya Nyakati 15:7).

     Mawazo ya biashara yanaweza kupatikana kwa: kupeana mawazo (kukoleza bongo), kutembelea eneo lako la biashara, kuchunguza mazingira yako, kutumia uzoefu ulionao na kuazima orodha kutoka kwa wengine.
  1. Kukoleza Bongo
     Hii ni njia ya kufungua au kuweka wazi mawazo yako na kukusaidia kufikiri mawazo mengi tofauti. Unaanza na neno au mada halafu andikika kitu kinachokuja katika mawazo yako. Kupeana mawazo ya kunafanya kazi vizuri unapobadillishana mawazo na mtu mwingine au na kikundi cha watu, lakini pia waweza kujaribu mwenyewe peke yako. Makampuni mengi yanatumia njia hii kupata mawazo mapya ya biashara; njia hii husaidia kutoa maono mapya kwani pasipo maono, watu huacha kujizuia (Mithali 29:18).

     Anza na neno moja (mfano mbao, kuku). Badala ya kuanza na neno la kubahatisha tu unaweza ukaanza na bidhaa maalumu, halafu unajaribu kufikiria biashara zote zinazohusika nayo, mfano: zile zinazohusika katika uuzaji, zile zinazohusika katika utengenezaji, zile zisizohusika moja kwa moja (faida ya ziada) na zile zinazohusika katika kutoa huduma.

  1. Orodha ya Mawazo
     Anza na orodha ya mawazo kwa biashara yako, rudia shughuli za awali ulizokwisha kuzifanya hadi sasa. Chagua mawazo yo yote ambayo yanaweza kuwa mawazo ya biashara ya kufaa na yaandike.Tenga karatasi yako katika pande mbili, kulia (mawazo) na kushoto (maoni).

  1. Ziara Katika Eneo la Biashara
     Tazama eneo lako unaloishi, tafuta aina za biashara ambazo zinafanyika katika eneo lako, angalia kama unaweza kuona mapengo katika soko. Kama ni kijiji au mji mdogo, zunguka mji wote na kama ni jiji tembelea eneo la viwanda, soko na maeneo ya madukani. Tenga karatasi yako ya utafiti katika orodha ya sehemu nne yaani; wafanya biashara wa rejareja, wauzaji au wafanya biashara wa jumla, wazarishaji wa kubwa na wadogo na watoa huduma; kisha chambua mapengo na fursa zilizopatikana.
  1. Kuchunguza Mazingira Yako
     Kama orodha yako ilihusisha eneo kubwa la soko lako, yumkini unaweza kuona ni aina gani ya viwanda au huduma ambayo uchumi wa eneo lako unategemea. Itakuwa vizuri kufikiri kupata mawazo mazuri ya biashara kwa kuzingatia nyenzo na taasisi zote zilizopo katika eneo lako. Kwa mfano, fikiria kuhusu: nyenzo za asili (vifaa vya asili), uwezo na ujuzi wa watu, taasisi, viwanda, bidhaa mbadala zinazoagizwa, uchapishaji na maonesho ya biashara na maonesho ya bidhaa.
  1. Kutumia Uzoefu
     Zingatia uzoefu wako pamoja na uzoefu wa watu wengine ili kutoa huduma, uzalishaji au kufanya biashara kulingana na wazo la biashara.

Namna ya kuchagua Wazo Linalofaa katika Orodha ya Mawazo Yako
     Ukiwa umepata mawazo machache yanayotekelezeka kuanzisha biashara yako angalau matano au zaidi ya matatno; hivyo, kazi inayofuata ni kuchukua orodha yako ya mawazo na kupunguza katika mawazo matano na kubakiwa na yanayofaa zaidi. Inawezekana kuwa kuna mambo mengi usiyofahamu kuhusu kuendesha biashara ambayo iko katika orodha yako; maswali maswali yafuatayo yanaweza yakakusaidia kuchagua wazo bora la biashara miongoni mwa mawazo mengine:

1.                  Unafahamu kwa kiasi gani kuhusu bidhaa au huduma katika biashara hii? (Aina ya hiyo huduma).
2.                  Una uzoefu gani utakaokusudia kuendesha biashara?
3.                  Una elimu na ujuzi gani ambavyo vitakusaidia kuendesha biashara hii?
4.                  Unaweza kupata wapi ushauri na taarifa kuhusu biashara hii?
5.                  Unajuaje kuwa biashara hii inahitajika katika eneo lako?
6.                  Wateja wa biashara yako watakuwa ni akina nani?
7.                  Je, watakuwepo wateja wa kutosha?
8.                  Je, wateja wataweza kudumu kununua bidhaa au huduma?
9.                  Je, hii itakuwa ndio biashara pekee katika eneo lako?
10.              Kama kunabiashara zinazofanana na hiyo utawezaje kushindana na wengine bila kushindwa?
11.              Utawezaje kuuza idadi kubwa ya bidhaa bora na huduma wanazohitaji wateja?
12.              Kwa nini unafikiri biashara hii itakuletea faida?
13.              Je, biashara hii inahitaji vifaa, jengo au wafanyakazi wenye sifa?
14.              Je, unafikiri unaweza kupata fedha kupata vitu vinavyohitajika?
15.              Utatoa wapi vifaa vya kuanzishia biashara hii?
16.              Unaweza kufikiria wewe mwenyewe kuendesha biashara hii katika kipindi cha miaka kumi ijayo?
17.              Unadhani una sifa na uwezo wa aina gani unaokufanya wewe uweze kuendesha biashara hii?
18.              Je, unavutiwa kiasi cha kutosha katika kuendesha biashara ya aina hii hadi kuthubutu kutumia muda na nguvu zako ili ifanikiwe?

Kulikubali au Kulikataa Wazo Lako la Biashara
          “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kumalizia?” (Luka 14:28). Kwa vile umepunguza mawazo yako ya biashara kufikia matatu ambayo unadhani ndio yanayofaa zaidi, unahitaji kupata taarifa zaidi kuhusu soko kwa ajili ya mawazo yako. Lengo lako ni kuangalia mambo yatakayo kusaidia kukubali au kukataa wazo la biashara. Kulikubali au kulikataa wazo la biashara zingatia njia mbili (2) zifuatazo kuchambua mawazo yako: Utafiti katika maeneo na uchambuzi wa UMAFUTI (SWOT).
  1. Utafiti katika Eneo
     Utafiti huu unatokana na kuzungumza na wateja, wasambazaji na jamii inayoishi katika eneo hilo la biashara. Unaweza ukakusanya taarifa nyingi za kufaa kuhusu mambo yanayoathiri mawazo yako ya biashara. Ziara hizo zitachukua muda mrefu, lakini kwa kufanya utafiti wa aina hii, tayari umekwisha anza kufanya kazi kama mfanyabiasha mwenye mafanikio na mawasiliano unayofanya wakati wa ziara hizi, yatakuwa ya manufaa kwako utakapoanza biashara yako.


Watu wa kuzungumza nao.
     Zungumza na wateja muhimu kama vile matajiri, wazee maskini, vijana, wanaume au wanawake. Zungumza na wasambazaji au watoa huduma; zungumza na wazalishaji; zungumza pia na viongozi wenye hoja wa kiserikali, wa taasisi na wa makampuni (wakiwa kama wahojiwa muhimu).
Jinsi ya kuendesha mahojiano yako.
     Eleza wazo lako kwa matumaini, na eleza kwa nini unafikiri kuwa ni biashara ambayo wateja wako wanahitaji. Andaa karatasi kwa ajili ya kuandikia taarifa utakazozipata toka kwa mtoa taarifa. Acha mada moja izae mada nyingine wakati wa mazungumzo.  Usiulize maswali yanayohitaji majibu ya ndiyo au hapana bali uliiza maswali yaliyowazi ukitumia “nini?” “nani?” “kwa nini?” “wapi?” “lini?” “vipi?” “namna gani?”.

     Usiogope kuuliza swali baada ya swali; uliza swali moja moja. Jitahidi kusrudia maelezo watu wanayokueleza kuhakikisha umeelewa walichosema.

  1. Uchambuzi wa UMAFUTI (Swot Analysis).
     Njia nyingine ambayo watu wengi wanaitumia kuchagua wazo la biashara linalofaa zaidi ni uchambuzi wa UMAFUTI (SWOT). Uchambuzi huu husaidia kuona maeneo yanayoweza kuwa na matatizo na faida kwa kila wazo. Angalia kirefu na maana yake kwa lugha ya Kiswahili na Kingereza:

              U   = Uwezo                                                            S = Strengths
              MA = Mapungufu/madhaifu                  au               W= Weaknesses
               FU = Fursa                                                            O = Opportunties
               TI   = Tishio                                                            T= Threats

     Jambo la kuzingatia, kumbuka kuwa, uchambuzi wa UMAFUTI unategemea sana mambo yafuatayo ili kupata wazo la biashara lililo bora na sahihi:
 
              JA = Jamii                                       S= Social factors
              SE = Serikali                   au             P = Political factors
              MA = Mazingira                              E = Environmental factors 
              TE = Teknolojia                  T= Technological factors.

Uchambuzi wa UMAFUTI Ndani ya Biashara
     Zingatia kuwa ni mambo gani katika mazingira ya ndani ya biashara unayotegemea kuianzisha yataleta faida katika na yapi yatakayoleta hasara. Kuchambua uwezo na udhaifu wa wazo la biashara unaangalia katika biashara iliyokusudiwa kwa kuzingztia mambo yafuatayo:

     Uwezo: Uwezo ni mambo muhimu yanayoleta matumaini ambayo yataifanya biashara yako kuwa na manufaa kuliko biashara nyingine zilizopo na washindani wengine. Inawezakuwa umependekeza kuuza bidhaa bora zaidi au kuwa na mahari ambapo ni rahisi kwa wateja kufika.

     Mapungufu: Ni mambo ambayo biashara yako itashindwa kuyamudu. Pengine bei ya bidhaa zako itakuwa kubwa kwa sababu biashara yako ipo mbali na wasambazaji na itakubidi ulipie zaidi kwa ajili ya usafiri au gharama za ushururu, leseni na pango.

Uchambuzi wa UMAFUTI Nje ya Biashara
     Kuchambua fursa na tishio la biashara uliyodhamiria kuianzisha, yakupasa uangalie nje ya biashara; yaani mazingira ya nje. Zingatia kuwa ni mambo gani katika mazingira ya nje yataleta faida na yapi yatakayoleta hasara katika biashara hasa katika vipengele vifuatavyo:

     Fursa: Fursa ni maendeleo muhimu yanayotokea katika sehemu yako. Inawezekana kuwa, mahitaji ya bidhaa unayokusudia kuitengeneza yataongezeka kwa sababu ya vyuo vingi kuongezeka au kumiminika kwa watalii.

     Tishio: Tishio ni mambo yanayoweza kuleta athari mbaya katika biashara yako. Kwa mfano wazo la biashara linaweza likawa rahisi mno kiasi kwamba watu wengine wakaanzisha biashara kama hiyo katika eneo lako na kukupunguzia soko maana wateja kwa idadi ni wale wale.

     Zingatia: Baada ya uchambuzi wa UMAFUTI katika wazo lako la biashara, jiulize maswali yafuatayo na kujibu ndio au hapana: Je, uwezo ni mwing kuliko mapungufu? Je, kunafursa nyingi kuliko tishio. Kama kunamapungufu, basi ni vyema kujua ni jinsi gani ya kuyashughulikia mapungufu hayo.

Ufupisho wa Wazo la Biashara
     Baada ya kumaliza hatua ya kujitayarisha kuanzisha wazo lako la biashara, sasa unaweza kufanya ufupisho wa wazo lako la biashara kwa kuandaa muhtasari kwa kufuata vipengele vifuatavyo:

1.      Wazo langu la Biashara …………………… (Jumla au rejareja).                         
2.      Aina ya biashara ……………….… (Biashara ya uzalishaji au utoaji huduma).
3.      Bidhaa au huduma yangu itakuwa ………………………….…………..…………….
4.      Wateja wangu watakuwa ………………………………………..……………..………
5.      Mahitaji ya wateja yatakayotimizwa ni ………………….………….……………….
6.      Ujuzi na uzoefu wa elimu niliyonayo katika aina ya biashara ni ………………….
7.      Nimechukua wazo hili la biashara kwa sababu ……….…………………………….

Mashaka Juu ya Wazo la Biashara
     Kama unamashaka na huna uhakika juu ya wazo lako la biashara litakalokufaa, yakupasa uchague ni jambo gani litakufanya usiwe na uhakika: Je, ni kuhusu uchaguzi huna uhakika kama unafaa kuanzisha biashara? Je ni kwa sababu tu hufurahii mawazo yako matatu ya biashara uliyochagua?

     Endapo utabaini ya kuwa, huna ujuzi, uwezo wala ufahamu juu ya kufanya biashara yako mwenyewe fanya yafuatayo ili kuboresha sifa na uwezo wako (kutoka kwenye udhaifu kwenda kwenye uhodari):  Zungumza na watu walio katika biashara ya aina hiyo ili ujifunze kutoka kwao, pata mafunzo ya muda mfupi kwa kusoma masomo maalumu juu ya biashara hiyo.

     Aidha, tafuta kazi kama msaidizi au mwanafunzi wa mtu aliyefanikiwa katika biashara hiyo, soma vitabu na vyanzo mbalimbali vitakavyokusaidia kuongeza ujuzi wako katika biashara hiyo, fikiria na changanua kuhusu matatizo ya biashara hiyo na njia zake za kutatua matatizo hayo ili kujidhatiti na kuiepuka hofu ya kuthubutu katika kuianzisha biashara.

     Zaidi na zaidi, ili kuboresha uwezo (ujuzi) juu ya biashara yako unayotarajia kuianzisha, fanya na zingatia yafuatayo: fanya mazoezi ya kujadili faida na hasara ya wazo lako la biashara, ongeza msukumo wako kwa kutengeneza mpango mkakati wa baadaye, wasome na kuwafuatilia kwa makini wafanyabiashara waliofanikiwa, elewa kuwa mafanikio yako yanategemea sana juhudi zako mwenyewe na msaada wa Mungu pekee, Jenga uwezo wa kuangalia na kukadiria tatizo na jaribu kubahatisha, fikiria na jifunze jinsi ya kufanya vizuri katika kubabiliana na hali ya matatizo.

     Zungumza na familia yako kuhusu matatizo ya kuendesha biashara yako na washawishi wakusaidie, uwe wazi zaidi na kukubali mawazo mapya na maoni ya watu wengine, wakati mambo yanapokwenda vibaya chunguza chanzo cha tatizo na boresha uwezo wako wa kujifunza kutokana na makosa na ongeza juhudi yako katika kufanya kazi na tambua kuwa kufanya kazi kwa bidii ndiko kunakoleta mafanikio.

     Fahamu ya kuwa, watu wengi hawafai kuwa na biashara zao wenyewe na wapo watu wanazo sifa nyingi za kufanya biashara zao na wanaweza kufanikiwa. Kama wewe ni dhaifu, tafuta mshiriki mwenza anayekamilisha uwezo, badala ya kuanza biashara peke yako na ukaikomeshea njiani au kupata hasara.
Kuchunguza Uwezo na Uzoefu
     Uzoefu huja kwa kutenda mwenyewe; “Tena mjitahidi kutulia, na kutenda shughuli zenu, na kufanya kazi kwa mikono yenu wenyewe …….” (1Wathesalonike 4:11). Kabla hujaanza kutekeleza wazo lako la biashara, angalia na zingatia mambo yafuatayo: uzoefu wako wa kazi, uwezo wa kiufundi, utendaji kazi katika biashara, ushirikiano na watu, historia ya familia utokayo na uliyonayo, mvuto na mambo unayopenda, shughuli unazofanya nyumbani kwako nje na bishara, kazi ya kuajiliwa au kujiajili. 

Aina ya Biashara Uitakayo
     Kuna aina kuu nne (4) za biashara: uuzaji wa rejareja, uuzaji wa jumla, uzalishaji na utoaji huduma. Lazima ujiulize kuwa, je, ni aina gani ya biashara unaipenda na unaweza ukaimudu kutokana na wazo au mawazo ya bishara uliyonayo? Hivyo, ni lazima kuwe na sababu za msingi za kuipenda au kuichagua aina hiyo ya biashara ukusudiayo kuifanya.

B: Njozi, Tunu na Malengo Katika Biashara.
     Katika mafanikio na maendeleo yo yote ya biashara ni lazima kuwepo hitaji la vitu vine, ambavyo ni vya muhimu sana kwa mfanya biashara ye yote, ambavyo husimama kama daraja na msingi wa mafanikio na maendeleo ya biashara. Vitu hivyo vinne ni pamoja na:


a)      Njozi au ndoto
b)      Mkakati au mikakati
c)      Thamani au tunu
d)     Malengo.


Njozi au Ndoto
      Ni picha pana ambayo mfanya biashara (mjasiliamali) hutegemea kuwa katika mafanikio yake ya biashara. Ni hitaji la baadae ambalo linaongoza maisha ya sasa (yaliyopo) ya mtu, biashara au taasisi kama inavyohitajika kuwa hapo baadae kwa miaka kadhaa ijayo.

     Njozi inapatika kutoka katika tunu au thamani ya mtu, biashara, kampuni au tasisi inavyotaka kuwa. Mala zote thamani au tunu zinapatikana kutokana na hisia za mtu mwenyewe kuhusu au biashara inavyotakiwa iwe hapo baadae.

Mikakati au Mkakati
     Ni mbinu au harakati juu ya jambo au kitu kinachotegemewa kutimizwa katika ndoto. Mkakati unaundwa na lengo moja au zaidi.
Malengo
     Ili kupima maendeleo ya biashara, ni muhimu kuwa na malengo uliyopanga awari.  Malengo husadia kufahamu ni kwa kiasi gani biashara yako imefanikiwa. Sifa ya Malengo ni lazima: yawe maalumu, yawe yenye kupimika, yaweze kufikirika au kupatikana, yawe katika muda maalumu na yaweze kutekelezeka kirahisi.

Jinsi ya Kupata Fursa katika Biashara
     Ili kuzipata fursa za biashara yako ukiwa kama mfanyabiashara au mjasiliamali, zingatia na fuata yafuatayo: panua wigo wa kufahamiana na watu, kuwa msomaji wa vyanzo mbali mbali vya habari, angalia hitaji la watu au wateja wa hiyo biashaya, kuwa mwanafunzi wa mazingira kila wakati ukijifunza na kuyasoma mazingira ya biashara yako, hudhuria maonesho na semina mbalimbali za biashara na ujasiriamali, Jitazame, je, wewe unanini ndani yako (uwezo wako), fuatilia matangazo na mabandiko ya kijamii na kiuchumi ili kujua mambo mapya katika ulimwengu wa kibiashara.
Vyanzo vya Mtaji
     Wengi hushindwa kuanzisha biashara kwa sababu tu hawana mtaji wa kuwekeza katika biashara. Ili kutafuta mtaji waweza anzia hatua ndogo kabisa kisha kuyafikia malengo ya kuanzisha biashara unayoitaka. Vyanzo vya mtaji wa biashara ni kama: rasilimali zako mwenyewe ulizo nazo waweza ziuza au kuzitumia kama mtaji, mkopo binafsi (kutoka kwa watu wa karibu), kufanya kazi kwa kuajiliwa au kama kibarua, program za maendeleo ya kibiashara na misaada ya kijamii iliyokusudiwa kuwawezesha wafanya biashara. “Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuuzi hana ufahamu” (Mithali 12:11)

Vikwazo na Mafanikio Katika Kukua Kwa Biashara
     Biashara yo yote haikosi kukumbwa na changamoto kadha wa kadha, maana biashara ili iendelee kukua kupitia hatua kadhaa. Zifuatazo ni baadhi ya changamoto zinzoweza kukwamisha biashara yako isiendelee au kukua: miundo mbinu mibovu ya kiuchukuzi na usafirishaji, ufahamu mdogo wa kibiashara, kutolifahamu soko na wateja wake, uhaba wa taarifa na vyanzo vya fursa, kukosekana kwa vyanzo vya ziada vya fedha, uhaba wa mtaji, kukosekana aina bora ya wafanyakazi katika biashara na kuwepo ushindani mkali juu ya aina hiyo ya biashara.

     Ili mfanyabiashara (mjasiliamali) afanikiwe, anahitaji mbinu zifuatazo: kutunza na kujali muda, kauli nzuri na kumjali mteja, uaminifu na uvumilivu, kununua na kuuza bidhaa halali na bora, kuwa mtafiti wa biashara (juu ya manunuzi, bei na masoko), kubana matumizi; usafi katika eneo la biashara, usafi binafsi na usafi wa bidhaa na huduma; kuwa na leseni na kulipa kodi ya mapato, Awe na vyanzo vya pesa na kuweka akiba yake benki. Kuweka akiba benki humsaidia mfanyabiashara kuweka pesa wa ajiri ya matumizi ya baadae, kuweza kupata mikopo ya kibiashara kirahisi na kuepuka upotevu na matumizi mabaya ya pesa yasiyo na tija.

Utunzaji wa Kumbukumbu
     Suala la msingi katika biashara, ni kuweka kumbukumbu ili mali isipotee bila kujua. Kuna namna nyingi ya kutunza kumbukumbu kwa mifumo tofauti tofauti. Kumbukumbu za biashara zinaweza zikatunzwa kielektroniki, fomu maalumu zilizoandaliwa na kuwekwa katika mafaili pamoja na madaftari. Yafuatayo ni aina ya madaftari ya kutunzia kumbukumbu: daftari la matumizi, daftari la mauzo, daftari la stoo, daftari la wadaiwa, daftari la manunuzi, daftari la matumizi binafsi (yasiyo ya kibiashara), daftari la kibiashara na daftari la hasara ya biashara.

     Zingatia: Wanandoa na wanafamilia yawapasa kutambua kuwa, katika jitihada zote za kutafuta mafanikio, Mungu apewe nafasi ya kwanza kwa ajili ya wokovu wa maisha yao, maana imeandikwa kuwa, “….utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa (Mathayo 6:33).

Comments

Popular posts from this blog

MAJINA YA WANAWAKE KATIKA BIBLIA ‘A’ HADI ‘Z’

SOMO: MADHARA YA KUKATAA KUMTII MUNGU

MFANO WA MPANGO KAZI