YALIYOMO KATIKA KITABU CHA MWANZO


1.    UTANGULIZI
Kitabu cha Mwanzo ni miongoni mwa Vitabu vitano vya Musa (Mwanzo, Kutoka, Mambo ya Walawi, Hesabu na Kumbukumbu la Torati). Hapo awali kabisa, vitabu hivi vitano vya Musa vilikuwa kitabu kimoja, na baadaye kilitenganishwa na kuwa vitabu vitano kama tulivyo navyo siku hizi katika Biblia. Kwa ujumla, vitabu hivi vitano vinajulikana kwa jina la Pentatuki (maana yake, vitabu vitano).

 Jina hili la Pentatuki linatokana na maneno mawili ya Kiyunani (Kigiriki), yaani “penta” maana yake ‘tano’ na “teuchos” maana yake ‘kitabu’. Waebrania walimanisha Pentatuki yote ni “sheria” au “torati” (2Nyakati 17:9; Nehemia 8:14, 18; Mathayo 5:17; Mathayo 11:13; Mathayo 12:5; Luka 24:44).

Majina ya vitabu hivyo katika tafsiri ya kale ya Kiyunani ya Septuaginta yalikuwa Genesis kwa kitabu cha Mwanzo, Exodus kwa kitabu cha Kutoka, Leviticus kwa kitabu cha Walawi, Numeri kwa kitabu cha Hesabu na Deuteronomium kwa kitabu cha Kumbukumbu la Torati.

Mapokeo ya Kiebrania ya kale pamoja na yale ya Kikristo yalimtambua Musa kuwa ndiye mwandishi wa Pentatuki, ingawa Pentatuki yenyewe haimtaji mwandishi wake. Sehemu mbalimbali  katika Biblia inataja kazi ya uandishi wa Musa. Aliandika sheria ambayo Waisraeli waliipokea kutoka kwa Mungu (Kutoka 24:4; 34:27; Kumb 31:9, 24), aliandika historia ya Israeli  (Kut 17:14; Hes 33:2) naye alitunga nyimbo na mashairi (Kut 15:1; Kumb 31:22, 30).

2.    KUHUSU KITABU CHA MWANZO
Watu waliotafsiri kitabu cha Mwanzo kwa mara ya kwanza kutoka lugha ya Kiebrania kwenda Kiyunani, walikiita  “Genesis”, wakimaanisha ‘Mwanzo’ au ‘Asili’. Kitabu cha Mwanzo kinafungua kumbukumbu kuhusu asili ya ulimwengu wetu, asili na historia ya mwanadamu. Kitabu cha Mwanzo kinahusu kisa na mpango wa mpango wa Mungu juu ya uumbaji na chanzo cha vitu na viumbe wote katika dunia yetu.

Kwa kuwa kitabu cha Mwanzo ni kitabu cha kwanza, hivyo kinafunua hatua mbali mbali katika Biblia. Kinaifunua asili ya Mungu na mamlaka ama uwezo wake, Akiwa Ndiye Muumbaji, Mtoaji, Muhukumu, Mrudhuku na Mkombozi. Thamani na utambulisho wa mwanadamu umetokana na mfano wa Mungu katika uumbwa kwake.

Kitabu cha Mwanzo kinahusu pia anguko la mwanadamu na madhara ya dhambi yaliyosababisha utengamano wa mwanadamiu kwa Mungu, na ahadi ya ukombozi wa mwanadamu kupitia kwa Masihi ambaye atatuhakikishia wokovu kwa njia ya agano na kutusamehe dhambi zetu (Mwanzo 3:15).  Kutotii kwa Adamu na Hawa, uhusiano wetu na Mungu ulivunjika, na uovu kuanza kuchukua hatamu katika uharibifu wake.

Panapoanzia kitabu cha Mwanzo tunaona uumbaji wa Mungu unavyofanyika kwa namna kujidai ya uwezo na malengo ya uumbaji Wake, na kwa jinsi ya pekee Anamuumba mwanamume na mwanamke kwa mfano Wake (Mwanzo 1:26, 27). Lakini kitambo kidogo, dhambi ikaingia duniani, na Shetani akajidhihirisha nia yake mbaya kwa wanadamu.

Kuanguka dhambini kwa wazazi wetu wa kwanza, tunasoma kitabu cha Mwanzo na kuona namna Adamu na Hawa walivyofukuzwa kutoka kwenye bustani nzuri ya Edeni, na mtoto wao wa kwanza wa kiume anageuka kuwa muuaji, uovu ukazaa uovu mpaka Mungu alipoamua kuiangamiza dunia kwa gharika ispokuwa familia ya watu wa chache iliyoongozwa na Nuhu, ambaye alikuwa mtu pekee aliyekuwa amebakia akimcha Mungu.

Pamoja na hayo, mafungu makuu katika kitabu cha Mwanzo ni 1:27 na 12:2, 3, na wahusika wakuu pia katika kitabu cha Mwanzo ni   Adamu, Hawa, Nuhu, Ibrahimu, Sara, Isaka, Rebeka, Yakobo na Yusufu. Ni kwa Ibrahimu, ndipo Mungu alipoanzisha agano kama msingi wa mpango Wake wa kuwaokoa wanadamu: wokovu huja kwa njia ya kuamini, uzao wa Ibrahimu utakuwa wa watu wa Mungu na Mwokozi wa ulimwengu atakuja kupitia taifa lililoteuliwa na Mungu.

Watu tunaowasoma katika kitabu cha Mwanzo ni watu wa kawaida sana, lakini kupitia hao Mungu alifanya mambo makuu. Nahuu ni mfano hai wa kuwa Mungu anaweza akatumia watu wowote ili kukamilisha mpango wake – na hata watu kama sisi. Hivyo, penda kukisoma kitabu cha Mwanzo ili uhamasike. Maana kwacho kunatumaini, haijalishi kunagiza gani katika ulimwengu huu, Mungu anampango na sisi.

Haijalishi namna gani tunajihisi kutofaa au kutoheshimika, Mungu anatupenda na anahitaji kututumia katika mpango wake. Haijalishi ni wadhambi kiasi gani na tumetanga mbali na Mungu, wokovu Wake upo kwa ajili yetu – tusome kitabu cha Kwanzo ili tupate tumaini la maisha yetu.  
 
3.    MUHTASARI WA KITABU CHA MWANZO
Ufuatao ni jumla ya muhtasari wa kitabu cha Mwanzo, kuanzia uumbaji hadi wakati wa kifo cha Yakobo na Yusufu nchini Misiri:

1.    Kisa cha uumbaji (Mwanzo 1:1-2:3):
·         Adamu na Hawa
·         Kaini na Abeli
·         Uzao wa Adamu (wana wa Mungu)

2.    Kisa cha Nuhu (Mwanzo 6:1-11:32):
·         Gharika
·         Ueneaji wa watu baada ya gharika
·         Mnara wa Babeli

3.    Kisa cha Ibrahimu (Mwanzo 12:1-25:18):
·         Ahadi ya Mungu kwa Ibrahimu ya kuwa taifa
·         Ibrahimu na Lutu
·         Ahadi ya Mungu kumpatia Ibrahimu motto
·         Sodoma na Gomora
·         Kuzaliwa na kutaka kutolewa sadaka Isaka
·         Isaka anamuoa Rebeka
·         Kifo cha Ibrahimu

4.    Kisa cha Isaka (Mwanzo 25:19-28:9):
·         Yakobo na Esau (mapacha)
·         Isaka na mfalme Abimeleki
·         Isaka anambariki Yakobo badala ya Esau

5.     Kisa cha Yakobo (Mwanzo 28:10-36:43):
·         Yakobo kuanzisha familia
·         Kurudi nyumbani kwa Yakobo

6.    Kisa cha Yusufu (Mwanzo 37:1-50:26):
·         Yusufu kuuzwa katika utumwa
·         Yuda na tamari
·         Yusufu kufungwa gerezani
·         Yusufu kufanywa mkuu Misri
·         Yusufu kukutana na kaka zake Misri
·         Yakobo na familia yake kuhamia Misri
·         Kifo cha Yakobo na Yusufu Misri

4.    UJUMBE MKUU KATIKA KITABU CHA MWANZO
Kitabu cha Mwanzo kinajumbe au mafundisho muhimu saba, kama yalivyobainisha kwa maelezo machache:

1.    Asili na Mwanzo
Kitabu cha Mwanzo kinaelezea na kutoa mwanga wa chanzo na asili ya chochote katika ulimwengu, hivyo kuweka uhalisia bayana.  Fumbo la asili na chanzo cha ulimwengu, dunia, watu, dhambi na mpango wa Mungu wa kuwaokoa wanadamu linateguliwa katika kitabu cha Mwanzo.

Kitabu cha Mwanzo kinatufundisha ya kwamba dunia na vitu vyake vilitengenezwa kwa ufanisi mzuri na kupendeza. Na kwa namna ya pekee, Mungu akamuumba mwanadamu. Tunajifunza kuwa, Mungu huumba na kutoa uhai kwa viumbe vyote.

2.    Ukengeufu wa kutotii
Mara zote wanadamu hujikuta katika chaguzi mbalimbali. Kama ilivyo kwa Adamu na Hawa, kutotii hutokea wakati ambapo watu huwa na nafasi ya kufanya uchaguzi, hivyo kuchagua kutofuata mpango wa Mungu katika maisha yao. Kitabu cha Mwanzo kinaelezea kuwa, kwa nini watu ni waovu: kwa sababu walichagua kukosea. Hata mashujaa katika Biblia walianguka kwa kutomtii Mungu.

3.    Mafanikio
Mafanikio ni neon na jambo pana zaidi ya umiliki tu wa vitu tu. Mafanikio ya kweli ni yale yatokanayo na matokeo ya kumtii Mungu. Wakati ambapo wanadamu wanakuwa wamemtii Mungu katika mafanikio yao, huwa wanakuwa na amani kupitia Kwake, pamoja na wengine na wao pia.

4.    Ahadi
Mungu hufanya au hutoa ahadi ili kusaidia na kuwalinda watu wake. Moja wapo ya ahadi za Mungu ni lile linaloitwa ‘agano’. Mungu hutunza na kutimiza ahadi Zake, na Anatimiza hadi/hata sasa. Aliahidi kutupenda, kutukubali, kutupokea na kutusamehe.  

5.    Utii
Kinyume cha utii ni dhambi, na kinyume cha dhambi ni utii. Kumtii Mungu huturejeshea mahusiano yetu na Yeye.  Njia pekee ya kufurahia ahadi za Mungu ni kumtii Yeye.

6.    Israeli
Mungu alilianzisha taifa la Israeli kwa ajili ya kuwatenga watu kwa ili kupata: 1. Kuzifanya njia Zake kuwa hai katika ulimwengu huu, 2. Kuutangazia ulimwengu namna jinsi Mungu alivyo, na 3. Kuuandaa ulimwengu huu kwa ajili ya kuzaliwa kwa Masihi.   

Mungu Anawatafuta watu waweze kumfuata ili wautangaze ukweli na upendo Wake kwa mataifa yote, na siyo kwa mapenzi yao wenyewe. Hivyo, sisi kama Israeli wa kiroho yatupasa  kuwa waaminifu ili kuibeba misheni ambayo Mungu ametupatia kwayo.  
7.    Dhambi
Dhambi imevuruga na kuharibu maisha ya watu. Na hii hutokea pale tunaposhindwa kumtii Mungu. Kuiishi njia ya Mungu hufanya maisha yetu yawe yenye maana na kutimiza mipango ya Mungu juu ya kusudi la kumuumba mwanadamu. 




ITAENDELEA....................... 


Comments

  1. Nashukuru kwa walio tafsiri maandiko kutoka matakatifu na kuchambua vema luhga vizuri

    ReplyDelete

Post a Comment

Thanks for viewing and passing through NMEE blog. Keep following the blog

Popular posts from this blog

MAJINA YA WANAWAKE KATIKA BIBLIA ‘A’ HADI ‘Z’

MFANO WA MPANGO KAZI

SOMO: MADHARA YA KUKATAA KUMTII MUNGU