MANENO YANA NGUVU (WORDS ARE POWERFUL)


MANENO YANA NGUVU.                                                                                                                                


Naanza kwa kuandika kuwa; “Nayajua mengi kwa kuwa nimempa kila mtu nafasi ya kuwa mwalimu wangu, kila mtu hunifunza kwa yale atakayo. Huwa naheshimu kauli na mawazo ya wote kwa uzito sawa, LAKINI UELEWA NI JUU YANGU”

Jua ya kwamba; “Ulemavu wa fikra tulizonazo juu ya maisha na juu yetu wenyewe huzaa mawazo mpauko yasiyoakisi umuhimu na umaana wa utu wetu na malengo yetu. Kuna muda tunafikiri kuwa watu wa aina fulani ndio wawezao kufanya mambo ya maana na yenye maendeleo kwa wao wenyewe, na sisi kujiweka nyuma kwa miakisio ya ubovu wa uteuzi wa fikra sahihi dhidi ya fikra mtambuka. Tunawaza zaidi kuliko kufikiri juu ya hatima ya uzio wa upeo wetu na malengo yetu. Akili zetu hutuongoza katika mwambao wa kukata tamaa na kutojikubali. Tunahangaikia kuona kuliko kutazama na kuyafanya ya mwisho kuwa ya kwanzo. Sisi ni zao la umakini hafifu wenye kichefuchefu cha kutambua tunapotaka kwenda na njia tupitayo. Ukungu wa fikra potofu huyasonga mawazo machachu tuliyonayo juu ya yale tuyaaminiyo kwenye maisha ya wengine. MABADILIKO NI WEWE “WEWE NI SERIKALI YA AKILI YAKO.”

Tambua kuwa; “Kitu pekee kidogo na cha thamani unachoweza kufanya katika maisha yako ni kutafuta nini unachokitumainia, na kikubwa unachoweza kufanya ni kuishi ndani ya matumaini hayo. Sio tu kuyakubali kwa mbali ila kuyaishi kwa undani wake. Matumaini yanaweza kuwa nguvu kubwa yenye msukumo. Inawezekana kabisa kusiwe na miujiza ndani yake, ila ujuapo unachotumainia sana na ukakikumbatia kama mwanga ndani yako basi unaweza kutenda jambo na kuyafanya mambo
yatokee kama miujiza…yafanye matumaini yako yaishi...JUKUMU MOJA WAPO LA BINADAMU NI KUFIKIRI KWA NIABA YAKE MWENYEWE”

Elewa kwamba; “UKOSEFU WA FIKRA HURU NDIO UZAAO UTUMWA WA MAWAZO NA MATAZAMIO HAFIFU. kijana mwenye fikra mpauko huwa na mawazo mgando na mitazamo mdebwedo, hufikiri kwa lugha fulani na kutenda kwa utamaduni wenye kilema cha utashi...huwaza kwa kwenda mbele yake na kutenda kwa yaliyonyuma yake…ukubwa wa ubovu wake ni mkondo hasi wa ayaaminiyo…hufikiri kwa fikra tata za wengine na kupambanua kwa mawazo mtambuka ya wasiojikubali, muhimu kwake ni jioni kila ianzapo asubuhi, ahueni ya maisha yake ni mkono unyooshwao ili kumbeba na sio kumuonyesha njia”…..

Fahamu kuwa; “Kitu kikubwa kinachotuogopesha si kwamba tuna mapungufu au kwamba hatujakamilika. Woga wetu mkubwa ni kwakuwa tuna nguvu kupita kawaida. Huo ni mwanga wetu, na wala sio giza linalotuogopesha muda wote. Muda mwingine tunajiuliza ‘mimi ni nani mpaka niwe mwenye kipaji, nguvu, mwerevu au mwenye akili nyingi?’ lakini tunasahau kujiuliza kwani ‘mimi ni nani mpaka nisiwe vyote hivyo?’ maisha ni kwa wale waaminio uzuri wa ndoto zao, ni kwa wale waotao na kufanya juhudi ya kuzibadili ndoto zao kuwa kweli. Unaweza kama Ukiamua, WEWE NDIYO WA KUJIPANGIA MAMBO MENGI UYATAKAYO.

Ukifahamu kuwa; “Maisha hutupa changamoto ili kupima ujasiri wetu na utayari wetu wa kubadilika, katika muda huo, hakuna nafasi ya kujifanya kwamba hakuna linalotokea au kusema kuwa hauko tayari kuipokea hiyo changamoto. CHANGAMOTO HAZISUBIRI UTAYARI WAKO. Maisha hayaangalii nyuma, ni kama sheria mpya inayotungwa juu ya jambo fulani, huwainaanzia pale iliposainiwa. Wiki moja ni zaidi ya muda wakutosha tunaohitaji ili kuamua kama tunakubali mwisho wetu kuupanga au la!” Japokuwa unaweza pia kuhitaji kwenda mbele kwenye maisha yako, lakini unaweza kukuta umeweka mguu mmoja kwenye ‘break’.
Nini thamani ya maisha kama tunaamua kwenda mbele kwa mashaka ya kukanyaga breki. Ili uwe huru, lazima ujifunze kusahau na kuacha mambo mengine yaende. Acha kuumizwa na machungu yaende, sahau. Tupa woga kulee, achana na kuzisumbukia na kukumbuka maumivu yako ya zamani. Nguvu unayotumia kujihusisha na maumivu yako na maisha yako ya zamani ndiyo inayokuvuta nyuma na kukufanya usisonge mbele. KUBALI KUANZA UPYA.

Elewa kwamba; “Kushindwa kupanga ni kupanga kushindwa. Kanuni ya mafanikio katika lolote binadamu afanyalo huwa ni KUWA NA MPANGO THABITI, mpango hukueleza ni wapi unataka kufika na kwa kiasi gani. Mipango ya mafanikio yetu hupangwa na vichwa vyetu pamoja na fikra tulivu zinazotawala mioyo yetu, ukiwa na mpango kinachofuata ni MKAKATI, hii huwa ni njia ya utekelezaji wa mpango wako. Ukijua uendako ni rahisi sana kupata njia ya kukupeleka huko, hata kama utachelewa kiasi gani lakini ni rahisi sana kufika huko. Maisha hayana kanuni maalumu wala haikuhitaji uwe na elimu kubwa sana ili ufanikiwe katika
maisha, unachotakiwa tu ni kujitambua, kuweka mipango, kutafuta mkakati, kuweka vipaumbele, kujiamini na kusimamia unayoyaamini, UKIMALIZA YOTE HAYO KIKUBWA NI UWE NA HAMU KUBWA YA KUFANIKIWA INAYOZIDI WOGA WAKO WA KUSHINDWA. MAISHA MAZURI NI WEWE TU KUYATAFUTA.”

Kumbuka daima; “Kulisha mbwa wote chakula sawa kwakuwa hujui yupi atakuokoa wakati wa hatari. Inawezekana katika kuwalisha mbwa ukawa ukimpendelea mmoja au hata kuwa pendelea wa aina fulani tu, lakini katika kuenenda kwako ukakutana na hatari ukiwa na mbwa wote. Wale uliowalisha na kuwapendelea wakanenepa na kunawiri wakakukimbia kwakuwa walikuwa na nguvu za kukimbia, uliwalisha mpaka wakawa wajinga na wavivu wa akili yao, hawakujua tena kuwa wakila wanatakiwa wakulipe kwakuwa walinzi wako na watetezi wako. Wale ambao hukuwalisha, hukuwapendelea au kuwajali wakabaki na wewe wakitamani kukutetea, lakini kwakuwa walikonda kwa upendeleo wako uliowanyanyapaa na kuwatenga, wakawa hawana tena nguvu hata ya kukupigania na kukutetea. UTAKUFA HAPO. Majuto ni mjukuu, ni mjukuu ambaye hutokea wakati wa dakika za mwisho kabisa za Tumaini finyu lililobaki kwenye mishipa ya damu. Kumjua mtu au kutokumjua hakukupi sababu ya kumdharau au japo kumuamini sana. Maisha ni kitendawili ambacho wachache hukitegua kwa wakati husika. USIMDHARAU MTU KWA KILE ULICHONACHO AMBACHO YEYE HANA. KILA MTU NI MUHIMU KWAKO, NI MUDA TU HAUJAFIKA WA KUONA UMUHIMU WAKE
KWAKO”

Maishani mwako; “Usidhani yanayokutokea sasa, au yale uliyoyapitia ndiyo yatakayoonesha wewe utakuwa mtu wa aina gani hapo baadaye. Haijalishi umetoka kwenye familia ya aina gani na wala haijalishi maisha yako ya sasa yakoje. Lakini uamuzi wako utakaoufanya sasa juu ya nini unataka kukitilia mkazo na nini maana ya vitu fulani kwako, aina ya mafanikio uyatakayo na jinsi ambavyo utafanya ili kuyafikia ndicho kitakachokupa mwanga wa mtu wa aina gani utakuwa. Kila kitu duniani chenye mafanikio kilianzishwa na mtu mmoja tu. Wazo huwa kichwani kwa mtu mmoja nayeye anaposhirikisha wengine bado tunahesabu kuwa yeye ndiye aliyeleta jambo hilo. Kila mtu mwenye mafanikio alikuwa na ndoto kabla, akazichambua ndoto zake na kuziishi huku akifanya kila njia kuzileta kwenye uhalisia. WEWE UNANAFASI YA KUFIKA PALE UTAKAPO KAMA UTAACHA KUJIDHARAU.”

Kumbuka; “Kifo ni hatua ya mwisho wa muda wa binadamu katika dunia, haijalishi ni muda gani utachukua hapa duniani ila jua tu kwamba ipo siku na wewe utakufa. Cha kujiuliza ni kitu gani katika maisha kitakutambulisha baada ya kifo chako? Ni kitu gani kitamfurahisha muumba wako pale utakapokuwa ukifanyiwa hesabu ya
mema uliyoyafanya kama shukrani ya pumzi kwa muumba? Kuna muda wa kila kitu, kuna starehe za ujana na shida za uzeeni. Kufa Hakuhitaji uwe mgonjwa au upate ajali, ili ufe inahitajika SIKU YAKO IWE IMEFIKA. Inaumiza sana kufiwa na mtu uliyempenda au mtu aliyewahi kukufanya ucheke ama kujifunza kitu. Lakini hiyo haitufanyi tusahau kuwa wote tutakufa. Muda wetu katika dunia hii una kikomo, na huwa kifo ni mshangao kwetu hasa afapo mtu ambaye hatukutegemea. Ni kama kupanda ngazi usiku wa giza nene, ufikapo sehemu na kudhani kuwa kuna ngazi nyingine mbele lakini unashangazwa na kujikuta ukitembea hewani na kuanguka, giza litakufumba macho na hutaamka tena. KILA MUDA NI MUDA WA KUJIWEKA SAWA KWA MUUMBA. TAFUTA KITU CHA KUIFANYA JAMII YAKO IKUKUMBUKE, TAFUTA KITU CHA KUMFANYA MUUMBA WAKO AJISIKIE FARAJA KUKUPOKEA.”

Fahamu ya kuwa; “Watu waliofanikiwa zaidi ni wale walioyajua matatizo, waliozijua harakati za maisha yao, waliokumbana na misukosuko na taabu, waliokutana na kukata tamaa na majaribu lakini mwisho wa siku waliyakabili na kusonga mbele. Lolote ambalo haliwezekani leo, unaweza kulifanya liwezekane kesho, hiyo ni kama tu utaamua juu ya mustakabali wa njia uipitayo.”

Hakika; “Umaskini wa fikra ni mbaya zaidi kuliko umasikini wa kipato. Fikra sahihi kwa wakati sahihi ndio njia ya kupata suluhu ya kila limfikalo mwanadamu.”

Si vyema; “Ukalala kwa kujiachia kama bado mafanikio yanakukimbia. Amka panga namna ya kuyakabili matatizo yako kwakuwa matatizo yameshapanga namna ya kukukabili. Amka na ujiulize utalala mpaka lini na kuamka ukiwa na hali ile ile na mawazo yaleyale? Jiulize ulivyokuwa mwaka jana na ulivyo mwaka huu. Je kwanini hamna tofauti ya mafanikio yako wakati kuna ongezeko la umri??? GUNDUA KIPAJI CHAKO…KITUMIE…ELIMU YAKO SI KITU KAMA ITASHINDWA KUKUTATULIA CHANGAMOTO ULIZONAZO.”

Tambua; “Kuna sababu ya kila kitu kinachotokea kwenye maisha yako hutokea kwa sababu, ingawaje kuna muda kwa upeo wa fikra zetu au kwa ukungu wa uelewa wetu mdogo, tunajikuta tukilaani kutokea kwa kitu hata kama sababu yake inakuwa yenye manufaa kwetu. Upendo wetu juu ya wengine hutufumba macho na kutufanya tusahau kuwa tuna jukumu la kujitazama wenyewe pia pale wengine wanaposhindwa kujali hisia na machozi yetu.”

Fahamu; “Mtu DHAIFU hawezi KUSAMEHE, kitendo cha kusamehe ni cha watu JASIRI wenye uwezo wa kupuuzia machungu nakuamua kuonyesha kutojali kwao. Ni mpaka utakapo samehe na kuasahau ndipo utaweza tena kuendelea na maisha yako. Kwa kushindwa kusamehe unaweza tengeneza tatizo kubwa kuliko lile alilotengeneza aliyekukosea.”


WEWE NA MIMI NDIYO WENYE HATIMA YA MWISHO YA KULETA MAFANIKIO NA MAENDELEO BINAFSI NA TAIFA LUTU KWA UJUMLA. © 2O16

Comments

Popular posts from this blog

MAJINA YA WANAWAKE KATIKA BIBLIA ‘A’ HADI ‘Z’

MFANO WA MPANGO KAZI

SOMO: MADHARA YA KUKATAA KUMTII MUNGU