MISINGI YA UFUGAJI WA KUKU WA ASILI.





  1. FAIDA ZA UFUGAJI WA KUKU WA ASILI
(1)   Ni chanzo cha haraka cha pesa
(2)   Nyama ya kuku ni protein tosha
(3)   Kinyesi cha kuku ni mbolea
(4)   Maganda na manyoya ni mapambo

            Qn. Je wewe unajua faida zingine? Basi Zitaje.

  1. MAHITAJI MUHIMU KWA UFUGAJI KUKU WA ASILI
(1)   Mahali pa kuwaweka
(2)   Mahali pakupata huduma na ushauri
(3)   Mahali pakupata kuku wa kufuga (waliochanjwa dhidi ya mndonde)

  1. NYUMBA YA MALAZI YA KUKU WA ASILI
(a)    Nyumba iwe mahali penye kivuli
(b)   Paa liwe Refu kuruhusu kuingia mtu mzima
(c)    Nyumba iwe na uwezo wa kupitisha hewa
(d)   Mlango uangalie Kaskazini kupingana na jua(Mlango uruhusu mtu mzima kuingia )
(e)    Iwe na mlango madhubuti na kufuli kudhibiti vibaka.

NDANI YA NYUMBA YA KUKU KUWE NA NINI?
        (1)Vichanja vya kulala kuku wakati wa usiku
        (2)Viota vya kutagia na kuatamia
        (3) Weka bembee ndani ya nyumba ya kuku
        (4)Dawa au majivu ya kuulia wadudu (utitili)

AINA ZA NYUMBA ZA KUKU.
(1)   Nyumba ya tope
(2)   Nyumba ya matofali ya udongo au kuchoma
(3)   Nyumba ya kuinuliwa.

Kibanda cha kuku wagonjwa na wageni katika banda
-          Kuku wageni na wagonjwa wawe na nyumba yao maalumu (wageni wawekwe peke yao kwa wiki moja )
-          Safisha kibanda baada ya kutoa kuku wagonjwa na wageni.
               
Vifaranga
      -     Baada ya kuanguliwa vifaranga , wawekwe pamoja na mama yao katika siku za kwanza.
      -     Weka Gazeti, majani, pumba za mchere sakafuni wakati wa baridi.

KUMBUKA
(1)   Jenga nyumba ya kuku kwa kutumia vifaa vinavyopatikana katika mazingira yako ili kupunguza gharama
(2)   Nyumba ya mbao ni budi inyanyuliwe juu na kuweka wavu au fito kama sakafu ili kuruhusu kinyesi kudondoka.
(3)   Madirisha yawekwe wavu kuzuia wanyama pori paka na kunguru na wezi
(4)   Weka vichanja ndani ya nyumba na ziwe na muundo rahisi kutolewa nje na kusafisha.
(5)   Weka viota kwa ajiri ya kutagia.
(6)   Vifaranga na mama zao wawekwe nyumba tofauti na kuku wengine wakubwa.
(7)   Hakikisha nyumba ya kuku inaingilika na kusafishika

Sehemu ya kupata ushauri na msaada wa kitaalamu kuhusu ufugaji wa kuku .
(1)   Wataalamu wa mifugo
(2)   Duka la dawa za mifugo
(3)   Tembelea wafugaji wengine waliofanikiwa
(4)   Jielimishe juu ya ufugaji wa kuku kwa kusoma na kusikiliza

(4) CHAKULA NA LISHE YA ZIADA KWA KUKU WA ASILI
Kwa nini kuku wapewe chakula cha ziada?
-Kuku wa asili wanauwezo mkubwa wa kujitafutia chakula
-Mahitaji ya lishe ya kuku hubadilika kutokana na umri na kama anataga au hapana .
-Vifaranga wanaokuwa huwa wanamahitaji makubwa ya protini ili hali wale wanaotaga huhitaji Sana madini ya chokaa
-Vilevile msimu wa kiangazi kuku hukosa vitamini “A” kwa kukosekana kwa majani mabichi, hivyo huathiri vifaranga.
-Wapatie vifaranga nyongeza ya protini kwa kuwapa unga wa dagaa au wadudu kama mchwa kuongeza protini.
-Changanya kikombe kimoja cha unga na dagaa (au vichwa vya dagaa vilivyotwangwa) na vikombe vitano vya pumba na uwape kuku kama ziada.
-Kuongeza chokaa, wapatie kuku chokaa ya dukani au maganda ya mayai yaliyotwangwa baada ya kubanikwa kwenye moto, au mifupa ya samaki iliyotwangwa baada ya kubanikwa kwenye moto. Weka katika chombo tofauti na chakula kingine Ili kuku wale kadri wanavyojisikia.
-Waweza wapa kuku vitamini “A” ya kununua dukani wakati wa kiangazi kirefu . Vinginevyo hakikisha kuwa wanapata majani ya kijani au mchicha mara kwa mara

JINSI YA KUTENGENEZA KILO 1 YA CHAKULA.
-Tumia kikombe kimoja cha chai (kile kidogo) ni sawa na gramu 200 za uzito kikijazwa hadi juu. Vikombe vitano vya namna hii huweza kutoshereza kilo moja ya uzito.

(a) Pumba au mahindi ya kuparaza ni vikombe 4(+) unga, dagaa kikombe kimoja = changanya hadi dagaa wasionekane kabisa
(b) Vifaranga vidogo umri wa wiki 8 (+) weka nusu ya kikombe cha chai kwa siku kwa vifaranga 10 katika wiki ya kwanza ongeza polepole hadi kufikia vikombe viwili ifikapo wiki ya nane (8)
(c) Kuku wanaokuwa wiki 9 hadi 20 (+) vikombe viwili kwa siku kuku 10 au ongeza au punguza kutegemeana na wingi wa kuku.
(d) Kuku wakubwa (+) vikombe viwili na nusu kwa kuku 10 kwa siku. Ongeza au punguza kutegemeana na upatikanaji wa chakula cha kujitafutia.

Note– Uchanganuzi uliopo juu ni kwa kuku wanaojitafutia chakula.kama kuku wanafungiwa      ndani ongeza chakula mara mbili ya kilichopendekezwa hapo juu. Kama una kuku wengi zaidi, ongeza kwa kilo kwa uwiano ulioonyeshwa hapo juu. Viazi na mihogo vimenywe na kukatwa vipande vidogo ili kuku waweze kudonoa
(NI LISHE NJEMA NI AFYA NJEMA – NILISHE NIKULISHE)

Vyombo vya maji na chakula.
-Tumia vyombo maalumu kulishia kuku ili kuepuka upotevu wa chakula.
-Tumia mbao, mabanzi ,mabati kutengenezea vyombo vya maji au kulishia kuku




Jinsi ya kutengeneza mchwa kwa ajili ya kulisha kuku.
(1)   Changanya kinyesi cha ng’ombe na majani makavu, mabua ya mahindi au maranda ya mbao
(2)   Mwagia maji kila kilichomo kilowane kisha weka katika chombo kama chungu au boksi.
(3)   Chukua chombo chako na ukiweke katika njia ya mchwa.
(4)   Acha kwa masaa 24.
(5)   Baada ya muda huo mchwa wengi watakuwa wameota ndani ya chombo hicho.
(6)   Wape kuku waanze kula mara moja.

Zingatia
(a)    Tumia vyakula vinavyopatikana katika mazingira yako kuwapa kuku chakula cha ziada
(b)   Zingatia bei na kiasi kinachohitajika kama ziada hili usipate hasara.
(c)    Punguza idadi ya kuku wakati wa upungufu wa chakula kupunguza hasara .
(d)   Usiweke chakula chakula cha ziada kwa muda mrefu kikaharibika
(e)    Weka vyakula mbali na ndege pori na panya kuepuka magonjwa .

5. UZALISHAJI WA VIFARANGA
- Chagua jogoo na tetea bora kuwa ndiyo wazazi wa vifaranga wako.
-Utunzaji bora wa mayai unaweza kukuongezea idadi ya vifaranga

Sifa za jogoo bora
1.-Awe mkubwa
2 -Awe na uzito mzuri usioangukia upande mmoja
3- Awe mchangamfu
4- Awe anapenda kuwa na himaya yake (utamjua kwa kumjazia wapinzani atakuwa anapigana badala ya kufuata matetea!
5- Muweke yeye na matetea 10.

Tetea mzuri ni yupi
1-Awe na umbo kubwa
2-Awe na uwezo wa kuatamia
3- Awe na uwezo wa kulea vizuri
4- Awe na uwezo wa kutaga mayai ya kutosha.

 Nifanyeje Kama sifa za tetea ninazotaka zimegawanyika kwa tetea zaidi ya mmoja?
- kama kuku mmoja ni muatamiaji mzuri lakini umbo lake ni dogo na mwingine ana umbo kubwa(mfano kuku aina ya kuchi ) linalofaa kibiashara,lakini sio mlezi mzuri .
Ufumbuzi.
- Mtumie kuku muatamiaji mzuri kuatamia mayai ya kuku mkubwa .Au waweza tumia mayai ya kuku mkubwa. Au waweza tumia mayai matatu au manne kila muatamio ili uzao wa kuku unaohitaji usipotee.

Utunzaji wa mayai

(1) Mayai mengine huwa hayaanguliwi kwa sababu zifuatazo
  (a) Kumpa tetea mayai mengi kuliko uwezo wake wa kuatamia
  (b) Kumpa kuku mayai yaliyokaa muda mrefu zaidi ya siku 15 baada ya kutagwa .
  (c) Mayai yalitunzwa sehemu  isiyo na hewa ya kutosha
  (d) Kuatamia mayai yaliyovunjika au machafu.
(2) Hakikisha kuku wako anataga mayai kwenye viota ulivyowawekea katika nyumba yao.
(3) Okota mayai kila siku na kuyahifadhi mahali safi penye hewa ya kutosha, Wakati wa kuatamia ukifika chagua mayai kuanzia la mwisho liwe la kwanza
(4) Kila ukiokoteza yai lililotagwa siku hiyo liandike namba kwa kalamu ya risasi, ndipo ulihifadhi
(5) Acha yai moja la kumuitia kuku aje atagie hapohapo kesho yake.
(6) Yai lihifadhiwe ile sehemu butu ya yai itazame juu na sehemu iliyochongoka itazame chini.
(7) Mayai yahifadhiwe kwenye kasha la kuhifadhia mayai la dukani au boksi lilojazwa mchanga mkavu na msafi. (Boksi likatwe kupunguza urefu na mchanga ujazwe hadi juu.

(8) Safisha mayai yaliyochafuka kwa kinyesi kwa kutumia kitambaa chenye spriti kidogo au kitambaa kikavu. Usisafishe mayai kwa kutumia maji

Vifaranga wakae vipi na kwa muda gani na mama yao?
- Mara baada ya kuanguliwa vifaranga ni lazima wakae na mama yao, nawatafutie chakula na kuwalinda na wadudu wa mchana na usiku, pia kuwafunika usiku ili wasipate baridi.
- Hakikisha hawapigwi jua wala kunyeshewa mvua .Na wakati wa usiku lazima walale pamoja na mama yao.
- Wapatie chakula na maji.
- Watenge na mama yao baada ya miezi miwili ili kumsaidia mama yao aanze tena kutaga. Muweke mama mbali nao ili waweze kuzoea kujitafutia chakula na kuishi peke yao.

Kuatamiza mayai mengi kwa mpigo.
- Huu ndio msingi wa ujasiliamali katika sekta ya ufugaji wa kuku wa asili

(1)   Kumbuka kuku huweza kuatamia mayai ya kuku mwingine, sio lazima yawe ya kwake .Pia kuku huatamia mpaka vifaranga vitotolewe.
(2)   Kama unataka kuku watano watamie na kutotoa kwa mpigo, fanya yafuatayo.

(a)    Kuku wa kwanza akianza kuatamia mwekee mayai viza au mayai yasiyo na mbegu mafano mayai ya kuku wa kisasa au kuku asiye na jogoo.
(b)   Rudia zoezi hilo hadi utakapofikisha kuku watano kisha wawekee kuku wote mayai yenye mbegu.
(c)    Kama hutakuwa na mayai ya kutosha labda uliyonayo yameshakwisha kaa zaidi ya wiki, unaweza kununua mayai mazuri kutoka kwa mfugaji unayemuamini.
(d)   Mpe kila kuku kati ya mayai 10-12
   
       (3) Wakitotoa wote utapata vifaranga kati ya 35-50 ambao baada ya miezi 6 au 8               watakuwa tayari kuuzwa.

ZINGATIA
(1)   Kuandaa majike kwa ajili ya uzalishaji
(2)   Tengeneza sehemu ya faragha kwa ajili ya kutagia mayai (kiota)
(3)   Weka utaratibu wa kuondoa mayai toka kwenye kiota na kuyaifadhi mahali pa wazi, penye hewa ya kutosha.
(4)   Zingatia matunzo bora kwa kuku watagao kwa kuwapa chakula cha ziada na maji ya kutosha (Dagaa pumba n.k )
(5)   Wakati wa kuatamia ukifika, chagua mayai yaliyotagwa mwishoni, yasiyo na nyufa masafi na mwekee kuku idadi ya mayai (8-12) kadri ya mwili wake.
(6)   Zingatia matunzo ya vifaranga, kuvipatia chakula cha ziada kuwaepusha na ajali na wanyama wakali.
(7)   Ongeza idadi ya kuku kadri ya uwezo na nafasi yako. Zingatia idadi ya majogoo isiwe kubwa sana (jogoo 1 kwa matetea 8- 12)
(8)   Chagua watoto wa kuku walio bora kuwa wazazi wa baadae wa zizi lako.

6. UDHIBITI WA MAGONJWA YA KUKU.
-          Utafiti unaonesha kuwa udhibiti wa magonjwa haya huzuia vifo vya kuku na kuongeza kipato cha mfugaji.

Msingi wa afya bora na kuzuia magonjwa kwenye kuku.

(1)   LISHE
(a)    Lishe bora huzuia magonjwa. wape kuku chakula bora na maji safi
(b)   Ongeza virutubisho vinavyoweza kupungua kama ilivyoelezwa katika somo la lishe
(c)    Safisha vyombo vya chakula na maji kila mara ili kupunguza vimelea vya magonjwa .

(2)   USAFI
(a)    Safisha banda la kuku kila mara kuondoa mlundikano wa kinyesi.
(b)   Hakikisha hakuna kinyesi ndani ya banda ili kuuwa mazalia ya vimelea.
(c)    Paka chokaa ya kujengea ukutani ili kuua vimelea baada ya mlipuko wa magonjwa. Au mara moja kwa mwaka kama hakuna ugonjwa. Chokaa huuwa vimelea vya magonjwa, changanya na maji na zipake kama rangi.

Magonjwa Hatari Na Dalili Zake Kinga Na Tiba.
-Kuku huweza kuathiriwa na magonjwa mengi sana, lakini utafiti umeonyesha kuwa magonjwa ya mdonde, ndui, koksidosisi, upungufu wa vitamini “A” huongeza kuua kuku wa asili.

(1) MDONDO
- Huathiri kuku wa umri wowote na huweza kuua kuku wote kijijini.
- Dalili zake ni.
(a) kuku huacha kula
(b) Kuku hupumua kwa shida
(c) Kuku huarisha
(d) Kuku hutoa kamasi na machozi
(e) Kupooza na kuzungusha kichwa
(f) Kutembea kinyume nyume.

(02) NDUI YA KUKU
- Huathiri sana vifaranga wanaokua hasa wakati wa mvua
- Husababisha uvimbe katika uso, kishungi, shingo na chini ya mdomo wa kuku.
- Ugonjwa huu husababishwa na virusi na hamna tiba.
- Chanjo inapatikana , na ikitumika ipasavyo huzuia kabisa ugonjwa.

(03) UKOSEFU WA VITAMINI “A”
- Huathiri zaidi kuku wadogo wanokua
- Dalili zake ni
    - Macho huvimba na kutoa uchafu mzito kama sabuni ya kipande iliyolowana.
    - Kuku wenye dalili hawaponi na hatimaye hufa.
- Ugonjwa huu mara zote hujitokeza baada ya kipindi kirefu cha kiangazi
- Kinga ni kuwapa kuku mchicha au majani mabichi mara kwa mara.
- Wape kuku wote dawa ya vitamini za kuku kutoka dukani kuzuia kujitokSeza kwa ugonjwa.

(04) KIKSIDISISI
- Huathiri kuku wa umri wote lakini zaidi vifaranga na kuku wanaokuwa.
- Kuku hudhoofika, manyoya huvurugika na kuku huwa kama wamevaa koti
- Kuku huarisha damu au kinyesi cha kahawia

MINYOO, VIROBOTO, CHAWA NA UTITIRI
-          Minyoo hukaa tumboni na ikizidi huweza kusababisha kuku kupunguza kutaga, kuharisha na kuku hupoteza uzito.
-          Viroboto hushambulia kichwa na kunata huku vikinyonya damu. Viroboto huuwa vifaranga
-          Chawa na utitiri hughasi kuku hadi wakashidwa kutaga na kuatamia.
-          Mwaga majivu katika banda na viota vya kutagia kama kinga kwa kuku wako. Tumia dawa za kuuwa wadudu kama “akheri power” au “sevin dust” au zinginezo utakazoshauriwa na wataalamu.
-          Tumia unyoya mmoja wa kuku ulioloweshwa na mafuta ya taa na utumie kupaka katika viroboto kwenye kuku walioshambuliwa

Chanjo Zipi Zitolewe Kwa kuku wako?

(1) CHANJO YA MDONDO.
   - Hii ni lazima kwa kuku wote
   - Chanjo itolewe mara kwa mara, (yaani kila baada ya miezi 3)
   - Kwa vifaranga waliozaliwa nje ya wakati wa chanjo wapewe chanjo wakati wowote katika wiki ya tatu halafu waendelee kuchanjwa na kuku wengine.

- Wafugaji wenye kuku wachache wajiunge pamoja na kuchanja pamoja, hii itapunguza gharama kwani chanjo nyingi za madukani zimetengenezwa kwa ajiri ya kuku elfu moja.

(2) CHANJO YA NDUI
- Itolewe tu pale ambapo ndui inaonekana kuwa ni tatizo kwani bei ya chanjo hii ni ghali.
- Chanjo itolewe mara moja kwa miezi sita (6)
- Chanjo hii hutolewa kwa njia ya sindano kwenye bawa na inapaswa ifanywe na mtaalamu wa mifugo
- Wafugaji watengeneze ushirika wa kuchanja pamoja ili kupunguza gharama

(3) DAWA ZA MINYOO.
- Minyoo hutibiwa kwa kuweka dawa za mnyoo katika maji ya kunywa.
- Tibu minyoo mara moja au mbili kwa mwaka na usafishe mabanda na vyombo kupunguza maambukizi

Utaratibu wa kinga na chanjo za magonjwa katika kuku wa asili.
-          Magonjwa huweza kukingwa kwa usafi wa nyumba, mabanda na vyombo vya kulia. Pia kinga na dawa za kuzuia huhitajika kwa magonjwa yasiyoweza kuepukika kwa usafi pekee.
-          Chanjo hupatikana katika maduka ya dawa za mifugo au kupitia kwa wataalamu wa mifugo wa serikalini.
-           
UGONJWA
CHANJO   /  KINGA
Mdonde
-Chanjo ya mdonde kila baada ya miezi mitatu
 -vifaranga wafikishe wiki tatu ndio wachanjwe
Ndui
-Chanjo ya sindano itolewe na wataalamu mara 1 kila miezi 6
-chanjo itolewe kabla ya mvua ndefu.
Upungufu wa vitamini A
-wapatie kuku majani mabichi au mchicha mara kwa mara
- au wape kuku dawa ya vitamini A Kotoka dukani kwa muda wa siku 3 hadi 5
Koksidiosisi
-Usafi wa mabanda kila siku
-wape kuku kinga ya dawa aina ya ‘salfa’ au aruprolion” kwa siku tatu mfululizo na vifaranga mara wafikishapo siku 7 tokea watotolewe. 



Viroboto / chawa / utitiri
-          Mwaga majivu katika banda hasa kwenye viota vya kutagia au tumia dawa za mfano akheri power’ na sevin dust’ kumwagia kuku mwilini na katika mazingira
-          Paka mafuta ya taa kwenye viroboto vinavyoonekana.
Minyoo
-          Tibu minyoo ya kuku kwa dawa za dukani mara moja au mbili kwa mwaka, ikiwezekana wiki mbili kabla ya kutoa chanjo ya mdonde.
-           

USIFANYE  HAYA.
(1)   Kuleta kuku wapya Bila kujua Historia ya chanjo walipotoka
(2)   Kuchinja kuku wagonjwa
(3)   Kuacha Banda chafu
(4)   Kuficha ugonjwa Bila kutoa taarifa kwa mganga wa mifugo kijijini
(5)   Kuuza kuku wagonjwa
(6)   Kununua kuku wagonjwa
(7)   Kutembelea zizi lenye ugonjwa bila kuchukua tahadhari
(8)   Kutupa kuku waliokufa porini
(9)   Kununua chanjo zinazotembezwa barabarani na wauzaji wasio Rasmi

7. MAFUA MAKALI YA NDEGE
- Ugonjwa wa homa ya mafua ya ndege ni hatari kwa afya za kuku na husababisha vifo kwa kuku.
- Ugonjwa huu husababishwa na Virusi vya influenza aina ya ‘A’ vinavyoweza kuambukiza wanadamu na nguruwe
- Zipo takribani aina 144 za virusi vya homa ya mafua makali ya ndege ila kwa sasa  ni aina ya H5N1 ndiyo inayosumbua ulimwengu.
-Ndege jamii ya bata pori na wanyama pamoja na ndege waishio kandokando ya bahari, maziwa na mito huweza kuhifadhi aina  zote hizi za virusi wakati mwingine bila wao kuonyesha dalili za ugonjwa .

Njia ya kusambaa kwa ugonjwa wa mafua ya ndege.
(1)   Njia ya hewa (chafya)
(2)   Njia ya chakula (kula vitu vilivyochafuliwa kwa virusi)
(3)   Kugusa macho ,pua na mdomo kwa vitu vilivyochafuliwa kwa virusi

Vyanzo vya mafua ya ndege
(1)    Kinyesi,damu, mayai, makamasi na majimaji kutoka kwa kuku wagonjwa huwa vimejaa virusi .
(2)    Maambukizi pia hupatikana katika mazingira yaliyochafuliwa kwa virusi
(3)    Maambukizi pia huweza kupatikana katika mazingira yaliyochafuliwa kwa virusi.
(4)    Maambukizi pia huweza kupatikana kwenye mavazi, vifaa vya kubebea kuku, magari n.k vilivyochafuliwa kwa virusi.



Jinsi ya kuzuiya maambukizi ya mafua ya ndege.
(1)   Fanya usafi wa mazingira na mabanda kwa ujumla .
(2)   Kunawa mikono kwa sabuni kila baada ya kugusa kuku wagonjwa au waliokufa.
(3)   Kukaa mbali na kuku wagonjwa au waliokufa kwa ugonjwa huu
(4)   Kijihadhari wakati wa kuchinja na kutayalisha kuku kwa ajiri ya kitoweo

Maambukizi ya mafua ya ndege kwa watu.
-          Hadi sasa maambukizi ya homa ya mafua makali ya ndege ni kidogo, isipokuwa ni nusu ya watu walioambukizwa wamepoteza maisha.
-          Maambukizi kati ya mtu na mtu bado hayajathibitishwa.
-          Mafua ya ndege huambukizwa kutokana na kula nyama au mayai yasiyo iva sawa sawa.
-          Pia kugusa kuku wagonjwa au waliokufa kwa ugonjwa huu au wakati wa kuchinja na kutayalisha kuku kwa kitoweo
-           
Mbinu za kukinga kuku dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa mafua ya ndege.
(1)   Usifuge kuku na bata katika nyumba moja
(2)   Chanja kuku dhidi ya ugonjwa wa mdondo kurahisisha utambuzi wa ugonjwa.
(3)   Kuondoa kuku wote wenye dalili za ugonjwa na waliokufa na kuwazika au kuwachoma moto
(4)   Usafi
(5)   Kudhibiti nyendo za kuku wasikutane na ndege pori
(6)   Usirudishe nyumbani kuku waliopelekwa sokoni wakakosa soko kwani wanaweza kuleta ugonjwa.
(7)   Wajenge kuku wageni takribani wiki mbili kabla ya kuwachanganya na kuku wako.

Mbinu za kukinga maambukizi haya kwa watu.
(1)   Kunawa mikono kwa maji na sabuni
(2)   Kukaa umbali zaidi ya mita moja kutoka pale kuku wagonjwa au waliokufa kwa ugonjwa
(3)   Kula kuku aliyepikwa akaiva
(4)   Zuia kuguswa kwa damu, kujishika machoni, mdomoni na puani wakati wa kutayalisha kuku, kushika nyama ya kuku au kinyesi cha kuku n.k.

Dalili za ugonjwa wa mafua ya ndege kwa kuku
-          Ugonjwa huu unadalili sawa na zile za ugonjwa wa mdondo, ndio maaana ni muhimu chanjo ifanyike dhidi ya mdondo kama mbinu ya kupambana na homa ya mafua makali ya ndege.
-           
Fanya yafuatayo katika kuzuia maambukizi Kwa kuku na watu
1. Toa taarifa panapohusika ukion vifo vya kuku au nde pori wengi hasa unapokuwa umechanja dawa dhidi ya ugonjwa wa mdondo kwa kuku.
2. Nenda haraka katika kituo cha afya ukiona dalili za mafua na homa kali mahali ambapo kuku wanaumwa au kufa.
3. Usiokote, usinunue wala usile ndege pori waliokufa.

8. KUKU WA ASILI KAMA MRADI WA KUINGIZA KIPATO .
Hebu linganisha wafugaji hawa wawili.
       Mmoja anauza kuku mmoja shilingi elfu 8 na wapili anauza kuku 10 kwa shilingi elfu 5 kila mmoja

  • Je ni nani mjasiliamali kati ya hawa?
  • Ye ni nani atapata pesa nyingi zaidi?
  • Ni yupi anayeuza kuku na kurudi kununua saruji kwa ajiri ya kusakafia ukuta?
  • Ni yupi anayeuza kuku kwa ajili ya kupata pesa ya kununua sabuni dukani tu?
  • Jew ewe uko upande gani?
-Kujua kuku wa asili ni njia moja wapo ya kuweza kujiingizia kipato.
- Je utauza kuku mmoja mmoja au utauza kuku wengi kwa pamoja kama wapo?


Unaweza kuuza mazao gani kutoka kwenye kuku?
-          Kuku kama majogoo ni zao muhimu la kuuza. Uza majogoo wasiohitajika pale wanapofikia ukubwa utakaokupa bei mzuri. Uza kuanzia miezi sita. Jogoo mmoja anatosha kuhudumia majike hadi 12, hauhitaji kuwa na majogoo wengi.
-          Uza kuku kwa makundi ili uweze kupata hela ya kushikika kuliko kuuza kuku mmoja mmoja.
-          Uza matetea yasiyohitajika kwa uzalishaji. Haya huweza kuuzwa yakifikisha miezi 8
-          Uza majike waliozeeka na wasiotaga mayai.
-          Uza mayai mapema baada ya kutagwa kama hayahitajiki kwa ajili ya kuatamia. Kama una matetea ya kutosha uza mayai sokoni mara kwa mara ili uweze kujenga jina wanunuzi wakufahamu.
-          Uza mayai ya kuatamiza kwa wanakikundi wenzako ili kufanikisha uatamizaji wa makundi
-          Boresha zizi lako la kuku uwe na kuku wazuri ili uweze kuuza mayai ya kuatamiza ambayo yanaweza kuwa na bei kubwa zaidi.

KUMBUKA. -  Kutafuta masoko ya kuku ,mayai kwenye mahoteli, mgahawa na sehemu za  
                         Kuuzia vyakula sehemu za vijijini na mijini
                      -  Kujitambulisha kuwa unafuga kuku na ueleze idadi unayoweza kuwauzia na kwa
                          Muda gani.Jitahidi kutoa bei ya ushindani

BAAADA YA KUUZA KUKU FANYA YAFUATAYO.
-          Mfano umeuza kuku 15 kwa bei ya shilingi elfu 5000 kila mmojana umepata jumla ya shilingi elfu 75. Je, gharama yao ilikuwa ni kiasi gani? (Utakuwa unajua). Je, uzitumie fedha hizo? (Najua mahitaji ni mengi sana japo huwezi kuyamaliza). Kwa kuwa mahitaji yako ni mengi na huwezi kuyamaliza kwa kiasi cha pesa ulichopata ,basi fanya yafuatayo.
-          Jua kwamba shughuli yoyote ya kijasiliamali ni kwa ajili ya kuongeza kipato kwa matumizi ya kila siku.
-          Tumia fedha kununua vitu unavyohitaji kila siku.(fikiria kuboresha nyumba yako , kadri kipato kinavyoongezeka )
-          Tumia thelusi moja kwa fungu hili, yaani kama mapato ni 75 elfu, tumia 25 elfu kwa fungu hili.
-          Mradi wowote wa kijasiliamali unamsemo wa kwamba “Nitunze ni kutunze /Tutunze tukutunze”, hivyo tumia thelusi nyingine kuboresha mradi wako.
-          Imarisha banda la kuku, nunua dawa na chanjo za kuku, na vifaa vya kutumika katika nyumba yao. Hata ikibidi kwa kupata mbegu zingine ama kwa kununua kuku au mayai yenye mbegu bora.
-          Tunza thelusi nyingine kwa matumizi ya baadaye (kumbuka akiba haiyozi).
-          Kipato kikiongezeka kwa nini usiweke hela Benki (fungua akaunti kama hauna )
-          Mgawanyo wa theluthi ya mapato yako baada ya kuuza kuku yawe kama ifuatavyo.
(i)                 Pesa kwa ajili ya matumizi
(ii)               Pesa kwa ajili ya mradi wa kuku
(iii)             Pesa kwa ajili ya akiba

Jinsi Ya Kutunza Kumbukumbu.
-          Mali bila daftari hupotea bila habari” Usemi huu unamaana yakinifu katika shughuli yoyote ya  kijasiliamali
-          Katika mradi wa kuku pia ni vema kutunza na kuweka kumbukumbu kila siku (au angalau mara moja kwa wiki).
-          Kila siku waangalie kuku wako kuwaona wanahali gani na ni wangapi waliopo, hapo utaelewa kama kuna mgonjwa wa kutibu au tahadhari gani zichukuliwe .
-          Weka kumbukumbu za matetea,majogoo,umri wakati wa kutaga na kuangua vifaranga .
-          Weka kumbukumbu za kiasi, bei na siku ya kununua vyakula, kuku au mayai.
-          Chakula cha ziada unachotumia kiandikwe kwenye kitabu cha kumbukumbu .
-          Andika tarehe ulizochanja kuku dhidi ya mdonde na magonjwa mengineyo.
-          Andika idadi, tarehe na bei ulizouzia kuku wako .

-          Kurasa za kumbukumbu katika daftari la kutunzia kumbukumbu ziwe.

(i)                 – Kurasa za kumbukumbu za kuku
(ii)               –Kurasa za kumbukumbu za vyakula
(iii)             –Kurasa za kumbukumbu za vifaa
(iv)             –Kurasa za kumbukumbu za chanjo na dawa

SAMPULI ZA KARATASI ZA KUMBUKUMBU

1. KUMBUKUMBU ZA KUKU NA UZALISHAJI

Jina la mfugaji
Wiki /Tarehe
Wiki /Tarehe








#
Kumbukumbu
Idadi
Thamani
Maoni ya ziada
Idadi
Thamani
Maoni ya ziada
1.
Tetea






2.
Jogoo






3.
Vifaranga wadogo






4.
Vifaranga wakubwa (miezi 2-6)






5.
Kuku waliokufa






6.
Mayai yaliyototolewa






7.
Mayai yaliyowekwa kuatamia






8.
Vifaranga vilivyoanguliwa






9.
Jogoo waliouawa






10.
Tetea waiouawa






11.
Vifaranga wadogo waliouzwa






12.
Vifaranga wakubwa waliouzwa






13.
Mayai yaliyoalibiwa






14.
Kuku walioliwa /kuuzwa






15.
Kuku waliotolewa zawadi









2. KUMBUKUMBU ZA CHANJO NA AFYA MWAKA 200-

Tarehe za chanjo
UGONJWA
Chanjo ya I
Chanjo ya II
Chanjo ya III
Chanjo ya IV
1.MDONDE




(a) idadi ya waliochanjwa
(b) idadi ya wasiochanjwa
(c) maelezo









2. NDUI




(a) idadi ya waliochanjwa
(b) idadi ya wasiochanjwa
(c) maelezo














Tiba mbalimbali
Minyoo



Vitamini A



Koksisisi



Mengineyo




  1. KUMBUKUMBU YA VIFAA NA VYAKULA.
#
Kifaa
Idadi
Thamani /Bei ya kununua /Maoni
Tarehe.
1.





2.





3.





4.





5.





6.






Vyakula na dawa.
1.





2.





3.





4.





5.





6.





7.







 Tengeneza nakala za kutosha.


Mambo ya kukumbuka ili uandae mpango wa uzalishaji biashara.

(1)   Jogoo mmoja anaweza kumudu tetaa 8-12. Unaweza ukapanga uzalishaji na uuzaji wako kwa idadi hiyo.
(2)   Tetea anauwezo wa kutaga mayai mpaka 30 akilishwa vizuri na kama mayai yatakuwa ya kuondolewa kwenye kiota
(3)   Kwa Uatamiaji na utotleshaji mzuri, mpe tetea mayai 10 mpaka 12
(4)   Matunzo mazuri kinga za magonjwa na ajali zitakuhakikishia kuwa vifaranga angalau 8 kati ya 10 walioanguliwa hadi kufikia uzito wa kuuzwa.
(5)   Ukiwa na tete watano unaweza kuuza hadi kuku 30 kwa mwaka. Hivyo tetea 10 watakuwezesha kuuza hadi kuku 60 kwa mwaka.

Zingatia yafuatayo ili upate faida
(1)Lenga soko katika sikukuu za mwisho wa mwaka na zinginezo ambapo kuku huuzwa zaidi.
(2) Tafuta soko ili ujenge jina kwa wanunuzi Wakubwa
(3) Jiunge au shirikiana na wenzako kuunda kikundi cha wafugaji kuku ili muweze.-
       (a) Kuchanja chanjo pamoja ili kupunguza gharama.
       (b) Kutafuta masoko pamoja
       (c) Kupasiana wateja Kama hauna /hana kuku wakati huo
       (d) Kuweza kujitambulisha kwa masoko kwamba kuna kuku wa kuuzwa kibiashara.
       (e) Kuwa na sauti moja katika kupanga bei.


_________    END_________________________ END________________________________


REJEA.

SUA (2008), Mwongozo wa ufugaji bora wa kuku wa asili vililini.










Comments

Popular posts from this blog

MAJINA YA WANAWAKE KATIKA BIBLIA ‘A’ HADI ‘Z’

SOMO: MADHARA YA KUKATAA KUMTII MUNGU

MFANO WA MPANGO KAZI