ELIMU BORA NA UFAULU WA WANAFUNZI WA KIDATO CHA PILI NA NNE KWA SHULE ZA SEKONDARI ZA SERIKALI



1.0.            Utangulizi
Hakuna nadharia ya moja kwa moja iliyopendekezwa na kukubaliwa kiulimwengu na kuteuliwa ili kuelezea nini maa ya elimu. Mwl. Nyerere yeye alitoa maana ya elimu kuwa “ni mchakato (transformation) wa kuhamisha maarifa kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine”. Kuna haja kubwa ya kuhusisha ufaulu na ubora wa elimu wanayoipata wanafunzi. Idadi kubwa ya ufaulu si kiashiria sahihi cha ubora wa elimu. Ubora wa elimu hupimwa kwa uthamani (quality) wake na siyo kwa idadi (quantity) ya wanafunzi kufaulu tu. Hivyo, kabla ya kuingia katika kiini cha andiko hili, ni vyema nikagusia kuhusu ubora wa elimu kwa msaada wa nukuu chache.

Elimu bora ndiyo njia yenye ufanisi zaidi katika kujenga maadili, mitazamo, tabia na maarifa muhimu kwa watu binafsi ili waweze kutumika kwa manufaa katika jamii iliyotangamana (Haki Elimu, 2011). Kumekuwa na changamoto katika kuinua ubora wa elimu na mafunzo kutokana na mitaala katika ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo kutokidhi mahitaji ya mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na teknolojia  na hivyo kutoa wahitimu ambao hawana umahiri wa kutosha kuhimili ushindani katika ulimwengu wa kazi (Sera ya elimu, 2014). Utoaji wa elimu bora ni jambo muhimu katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Dira ya Maendeleo ya Taifa (2025) inataja kwamba elimu bora ni muhimu ikiwa taifa litakubali kikamilifu kupambana na changamoto za maendeleo zinazolikabili. Mitihani ya Taifa ni kiashiria muhimu cha kupima wanafunzi wamejifunza kiasi gani, nayo ni chanzo muhimu cha taarifa kwa wazazi pindi wanapofanya maamuzi kuhusu watoto wao. Elimu bora imehusishwa pia na utoaji na ustadi wa waalimu (Oduro, Dachi & Fertig, 2008). Oduro na wenzie wanadai kuwa mabadiliko katika elimu barani Afrika yamelenga zaidi kuongeza idadi ya watu wanaopata elimu, huku ubora wa elimu inayotolewa ukipewa umakini mdogo.

2.0.            Changamoto ya Kuifikia Elimu Bora na Ufaulu Mzuri wa Wanafunzi
Mosha (2011) amewahi kueleza kwa muhtasari sababu za wanafunzi kufeli katika mitihani yao ya taifa, sababu hizo alizibainisha katika makundi makuu mawili, ambayo ni: sababu za kimazingira na sababu za vitendea kazi. Kwa mujibu wa Mosha, sababu za kimazingira hujumuisha mazingira ya kisiasa, kiuchumi, kisheria, kidemografia, kiutamaduni na kimataifa. Sababu za vitendea kazi hujumuisha uongozi duni katika taasisi, ufadhili duni kwa sekta ya elimu, hali duni ya miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, walimu wenye sifa duni na matatizo ya mitaala. 

2.1.            Changamoto ya Miundombinu
Uhaba na ubovu wa miundombinu katika shule za sekondari za serikali ni mojawapo ya kikwazo cha kufanikisha upatikanaji wa elimu bora na ufaulu mzuri kwa wanafunzi wa kidato cha pili na nne. Sababu za kuwepo kwa hali duni ya elimu na kushuka kwa ufaulu wa wanafuzi wa kidato cha pili na nne katika mitihani yao ya Taifa, tafiti mbalimbali zimekuwa zikidai zaidi kuwa zinachagizwa na kuwepo kwa miundombinu isiyorafiki na isiyofaa ya kufundishia na kujifunzia. Siwezi kubeza jitihada za serikali katika kukarabati na kujenga miundombinu mipya katika shule zetu, lakini pawepo na usimamizi mzuri.

Haiji akilini, jengo halijamaliza hata mwaka tangu kujengwa au kukarabatiwa linaanza tena kuhitaji ukarabati. Kwa hili lazima TAMISEMI au Wzara ya Elimu iwe na timu maalumu ya kufuatilia juu ya matumizi sahihi ya pesa (value for money) katika ujenzi na ukarabatiji wa miundombinu mashuleni. Timu hii yaweza pia husika katika kufanya uthaminishaji wa pesa zilizotumika na ubora wa jengo lililojengwa au kukarabatiwa. Lazima tujiulize, kwa nini majengo ya Mkoloni yapo katika ubora hadi sasa, wakati yanayojengwa sasa, ndani ya miaka mitano yanakuwa hoi – tabani.



2.2.            Changamoto ya Walimu
Kumekuwepo na tafiti chache sana zinazozungumzia ubora wa waalimu na ari yao ya kuwajibika kikamilifu na kujitolea ili huleta mafanikio katika utoaji wa elimu bora na kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule za sekondari za serikali. Katika programu mbalimbali za zamani katika elimu zilizoasisiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinaonesha, miongoni mwa mambo mengine, kumekuwepo kwa msisitizo mdogo sana kwa waalimu kama sehemu muhimu katika kuleta mabadiliko katika mfumo wa elimu, hususani linapokuja suala la kuboresha ustawi na weledi wao.
HakiElimu katika ripoti yao ya ‘utafiti kuhusu sifa za waalimu kitaaluma, hamasa na moyo walio nao katika kufundisha na athari zake katika kutoa elimu bora’ inaeleza kuwa, “kati ya maeneo 39 ya programu zilizopewa kipaumbele katika Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II), ni programu mbili tu zinazogusia kwa mbali suala la kuboresha ustawi na weledi wa walimu”. Walimu ni sehemu muhimu katika kuleta elimu bora na kufaulisha pia. Elimu bora na kufaulisha wanafunzi kunahusiana moja kwa moja na ufundishaji na ujifunzaji bora.
Kuna mambo kadhaa kwa walimu yanayohafisisha ufundishaji bora, miongoni mwayo ni kukosa sifa na uzoefu, kiwango kidogo cha hamasa katika kazi waliyo nayo, kukosa ari na moyo wa kujituma, kukosa hisia za kupenda kufundisha na kuyapenda mazingira ya kazi. Tafiti pia zinaonesha kuwa pindi waalimu wanapokuwa na hamasa na hisia za kuipenda kazi ya ualimu, wanafunzi nao huwa na hamasa ya kujifunza na hujifunza maarifa yanayofundishwa na waalimu wao kwa ufanisi zaidi (Caprara na wenzie, 2006). Hivyo basi, ni muhimu kuwatia hamasa waalimu kama hatua mojawapo ya kushughulikia tatizo la kushuka kwa ubora wa elimu na ufaulu wa wanafunzi.
2.3.            Changamoto ya Ufanisi wa Uongozi wa Shule
Ufanisi mzuri wa uongozi wa shule waweza kuwa ni chachu kwa walimu kufanya kazi vizuri na wanafunzi kufaulu vyema, hivyo kuinua ubora wa elimu.Tafiti za masuala ya ufanisi wa shule zinaonesha kuwa, wakuu wa shule wamekuwa kiini cha mafanikio ya shule.  Tafiti hizo zinaonesha kuwa, ubora wao hufikiwa na kuonekana pale wanapotimiza majukumu yao ya kuhakikisha vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana kwa wakati na vya kutosha, kueleza kwa uwazi dira na mikakati ya shule, kuelezea kwa uwazi na usahihi kile wanafunzi wanachotegemea kukipata wakati wa mafunzo yao, kuwa na mawasiliano rafiki ya mara kwa mara kati ya mkuu wa shule na walimu, wanafunzi, wafanyakazi wasio walimu, wazazi na jamii inayoizunguka shule.

Mkuu wa shule hana budi kutengeneza mazingira rafiki ya kufikiwa kwa urahisi na bila ya vikwanzo pale mwalimu, mwanafunzi, mzazi au mwanajamii anapolazimika kuwasiliana naye ana kwa ana, hususani katika suala zima la kiunua taaluma na ufaulu wa wanafunzi. Wakuu wa shule wanaposhindwa kuwa wasimamizi bora wa mambo ya kiutawala, kwa kuwafanya walimu na wanafunzi kuyafikia malengo ya kufanikisha ufaulu mzuri wa wanafunzi, ndipo ubora wa elimu na kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi huonekana kwa shule za sekondari za serikali. Lazima wakuu wa shule waweke pembeni ubinafsi, upendeleo, ubaguzi, usiri na kutojali bali wawe watu wa njozi na malengo ambayo yatafikiwa kwa mshikamano wa walimu, wanafunzi na wadau wengine wa elimu.

2.4.            Changamoto ya Wazazi na Jamii
Wazazi na jamii inayozunguka shule husika inamchango mkubwa katika kuipatia shule mafanikio (Asia na Ogula, 2013). Wajibu wa wazazi na jamii ni kuisaidia shule kufanikisha kuyatimiza malengo ya elimu ya Taifa yaliyokusudiwa kwa wanafunzi. Ikumbukwe kuwa, wazazi na wanajamii wanaweza kushiriki katika uhamasishaji wa wanafunzi (watoto wao) kujisomea pale wawapo nyumbani baada ya masaa ya shule au likizo. Mbali na mambo hayo, wazazi na jamii pia ina wajibu wa kuhakikisha inawaandaa vyema watoto wao ili waweze kupokea vyema yale wanayofundishwa shuleni.

Wazazi, walezi na jamii hainabudi kuhakikisha watoto wanapatiwa lishe ya kutosha, malazi bora, mavazi bora (zikiwamo sare za shule), vifaa muhimu vya kujifunzia na kuhakikisha wanakuwa na afya njema wakati wote. Wazazi, walezi na jamii imekuwa na mchango mkubwa wa kutofanikisha wanafunzi kufaulu na kujipatia elimu bora. Hii ni kwa sababu ya mtazamo hasi juu ya umuhimu wa elimu ya sekondari, hivyo kutotimiza wajibu wake katika kuwatia moyo, kuwashauri, kuwapa hamasa, kuwahudumia, kuwalinda na vishawishi mbalimbali wanafunzi. 

Wazazi, walezi na jamii imekuwa ikiwashawishi wanafunzi (watoto wao) wa sekondari kuwa na utoro wa rejareja, wa muda mrefu au kuacha kabisa shule ili waweze kuolewa, kulima, kufanya biashara, kujihusisha na shughuli za uvuvi na uchimbaji wa madini mbalimbali ili tu [wazazi na walezi] wajipatie ridhiki kupitia watoto wao. Wakati mwingine ili kufanikisha adhima ya watoto wao kutoendelea na masomo ya sekondari, wamekuwa wakiwaambia watoto wao waandike majibu yasiyo sahihi katika mitihani ya Taifa ili wafeli na wasiweze kuendelea na madarasa au ngazi zingine za elimu.

2.5.            Changamoto ya Uwezo wa Wanafunzi katika Kujifunza.
Wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza katika shule za sekondari wengi wao huwa hawana umahili wa lugha ya Kingereza ambayo hutumika kama lugha ya mawasiliano katika kujifunza na kufundishia kwa shule za sekondari. Kwa mwanafunzi kuwa mahili wa lugha ya Kiingereza hutegemea na jitihada zake mwenyewe na mkazo wa shule na walimu kwa mwanafunzi kujifunza ili kuimudu lugha hiyo. Ukiachana na changamoto ya umahili wa lugha ya Kiingereza, mwanafunzi mwenyewe ni sehemu muhimu ya kuboresha au kushusha ufaulu wake.

Yapo mambo ambayo huweza kuathiri ufaulu wa mwanafunzi kwa shule za sekondari. Mambo hayo ni pamoja na kukosa utayari wa mwanafunzi mwenyewe katika kujifunza maarifa na stadi mpya, mtazamo hasi kuhusu shule, na walimu wake, hali duni ya uchumi wa nyumbani kwao, mahudhurio hafifu ya darasani, umbali kati ya shule na aishipo mwanafunzi, nidhamu mbovu ya mwanafunzi (shuleni na nyumbani). Nidhamu mbovu za wanafunzi husababisha walimu kupoteza vipindi vyao kwa ajili ya kukaa vikao vya kujadili nidhamu za wanafunzi au mwanafunzi mtovu wa nidhamu kutumia muda mwingi kufanya adhabu/kazi za nje ya darasa, hivyo kuathiri ufanisi wa ujifunzaji na ufundishaji kwa shule za sekondari.

2.6.            Changamoto ya Matumizi Mazuri ya Muda
Matumizi mazuri au mabaya ya muda kwa mwanafunzi awapo nyumbani na shuleni katika kujisomea husadifu hali ya ufaulu wake katika mtihani wa Taifa. Katika nchi za ulimwengu wa tatu (zinazondelea), imeonekana kuwa, kuna uhusiano mkubwa kati ya mafanikio ya mwanafunzi kielimu na matumizi mazuri ya muda katika kujifunza. Na tafiti pia zinaonesha kuwa, wanafunzi wanapotumia siku nyingi za mwaka wakihudhuria shuleni huku wakijibidisha katika kufanya kazi zilizoandaliwa na kuratibiwa vizuri na walimu wao, hufanya vizuri zaidi katika mitihani yao.

Utoaji wa kazi nyingi za kufanyia nyumbani nje na masaa ya shule, humfanya mwanafunzi autumie muda wake vizuri katika kujisomea awapo nyumabani kwao. Pia, utimizaji mzuri wa vipindi vya darasani kwa mwalimu wa kila somo kwa shule za sekondari kumeonekana kuzaa matunda katika kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi. Katika utumiaji mzuri wa muda kwa shule za sekondari za serikali kumekuwa hakuko vizuri, maana kumekuwa na uvunjwaji wa vipindi mara kwa mara (kwa ajili ya shughuli mbali mbali na vikao vingi), hivyo kuharibu ratiba ya vipindi ambayo mwanafunzi alipaswa kujifunza ili kupata maarifa na sitadi mpya.

2.7. Changamoto ya Siasa katika Sekta ya Elimu
Siasa na viongozi wa siasa kuingilia taaluma ya ualimu na elimu kumepelekea ufaulu duni wa wanafunzi kwa shule za sekondari za serikali. Kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wanasiasa kutoa matamko na maagizo ya vitisho kwa walimu na watendaji wa elimu, hivyo kupunguza ari na moyo wa kufanya kazi kwa ufanisi katika shule za sekondari zilizo chini ya serikali. Wanasiasa na siasa pia imechangia kushuka kwa ubora wa elimu hususani kwa kutathimini ukuaji wa elimu kwa kuangalia wingi wa wanafunzi na siyo ubora wa elimu unaotolewa (kwa kuhesabu hata daraja la IV kuwa ni ufaulu kwa kidato cha nne, na mwanafunzi wa kidato cha pili kumpasa apate ufalu kuanzia ‘D’ mbili katika masomo yote).

 Mtazamo wa wanasiasa kujali kuongeza miundombinu pekee bila kuzingatia uongezaji wa vitendea kazi vya kujifunza na kufundishia, pamoja na kuongeza walimu kwa shule za sekondari za serikali. Kweli kabisa, kunaongezeko la wanafunzi kwa shule za sekondari kwa sababu ya ongezeko la watoto kwa njia ya kuzaliana kunako hitaji ngezeko la miundombinu, ila pia ni muhimu, ongezeko la miundombinu likaenda na kasi ya upatikanaji wa vitendea kazi na utoshelevu wa walimu.  Pia alama za ufaulu wa kuingia kidato cha kwanza kushushwa sana kumesababisha udahiri wa wanafunzi wengi walio na uwezo mdogo kiakili na hivyo kusababisha ufaulu wa kidato cha pili na nne kushuka.

2.8. Changamoto ya Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.
Madhara ya Sayansi na Teknolojia kwa wanafunzi ni makubwa na yanapelekea ufaulu duni. Wanafunzi wamekuwa wakitumia muda mwingi kutizama runinga (sizoni, miziki, mieleka, n.k.), na kuangalia mambo yasiyo ya kitaaluma kupitia simu na kompyuta zenye viunganishi vya internet. Katika hili, limeteka akili za wanafunzi wengi, hivyo kukosa muda wa kujisomea. Kuiepuka changamoto hii ni vyema serikali, wazazi na jamii isimamie na kuelekeza namna bora ya matumizi sahihi ya Sayanzi na Teknolojia kwa wanafunzi. Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kwa upande wa pili ni msaada kwa wanafunzi wanaojua kuitumia ili kuinua ufalua wao katika mitihani ya Taifa (maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yamerahisisha ujifunzaji wa mwanafunzi).

3.0. Hitimisho
Ili kunyanyua ubora wa elimu na kuongeza ufaulu wa wanafunzi kwa shule za sekondari za serikali, ni muhimu mambo yafuatayo yakazingatiwa: Halmashauri zianzishe mifuko maalumu ya elimu ambayo itasaidia kutatua changamoto za dharula za kielimu kwa wakati pindi zinapotokea kuliko kusubiri na kuomba pesa serikali kuu. Kuimarishwe ukaguzi wa shule kwa ngazi za wilaya ili kuwafanya wahusika kuwajibika zaidi na kufanya shule zitekeleze adhima iliyokusudiwa kwa ufanisi. Kuanzisha mitihani ya ujirani mwema ili kuongeza ushindani miongoni mwa wanafunzi. Katika shule za sekondari za serikali pia kuanzishwe “Special Program for Solving Past Papers” ili wanafunzi wawe na ufahamu na uzoefu wa namna ya kujibu maswali ya masomo mbalimbali.  Shule, wilaya na mikoa ianzishe maazimio ya mipango mikakati (kazi) ya muda mrefu na muda mfupi ili kufanikisha kuongeza ufaulu wa wanafunzi kwa shule za sekondari za serikali.

Mfano wa baadhi ya maazimio ya muda mrefu katika mpango mkakati yaweza kuwa:  Kutumia walimu wa sayansi wachache waliopo kufundisha shule zaidi ya moja ili kuziba upungufu kwa shule zisizo na walimu hao kabisa; Kufanya mitihani ya kila wiki ili kuwajengea wanafunzi tabia ya kujisomea kila mara; Kutengeneza forum/jukwaa la wasomi na wadau wa elimu (ngazi ya mkoa, wilaya, tarafa na kata) wenye taaluma mbalimbali watakaosaidia kushauri, kuchangia, kuhamasisha na kujitoa ili kuboresha sekta ya elimu; Kutengeneza Maktaba ya Mtandaoni (E-library) itakayosaidia wanafunzi kujisomea, hususani kwa kupata vitabu, nukuu, maswali na majibu kwa masomo mbalimbali; Ujenzi wa mabweni ya wanafunzi kwenye shule zenye uhitaji huo ili wanafunzi wakae shuleni na kupata muda wa kutosha kujisomea. 


3.1. Mfano wa Mpango Mkakati wa Kuinua Ufaulu kwa Shule za   Sekondari za Serikali - Kidato cha Pili na Nne.
Mpango mkakati (kazi) hutegemea njozi/ndoto (vision), dira (mission), malengo (ojectives) na falsafa/kaulimbiyu/utamaduni (motto/philosophy/culture) wa shule husika. Mpango mkakati na utekelezaji wake waweza ukatokana na changamoto zilizobainishwa pamoja na malengo yaliyoandaliwa ili kuzitatua changamoto hizo. Hivyo basi, ufuatao ni mfano wa mpango mkakati unaoonesha namna ya kufanikisha au kuinua ufaulu kwa shule za sekondari za serikali.
 

NA

CHANGAMOTO

LENGO/SHABAHA

MPANGO MKAKATI

SHUGHULI

VIASHIRIA

WAHUSIKA
MUDA WA UTEKELEZAJI

01.
Wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza kutokuwa na uwezo wa kutumia  lugha ya Kiingereza katika kuandika na kuzungumza
Ø  Kusaidia wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza kumudu masomo ya sekondari.
1. Kuwajengea msingi wa awali (baseline) kikamilifu katika lugha ya kiingereza na masomo mengine.
1. Kufundisha Kiingereza kwa wanafunzi wa kidato cha 1 kwa wiki 6 kabla ya kuanza masomo rasmi.

2. Kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiingereza shuleni – kwa kuweka utaratibu wa kudhibiti wanafunzi kutozungumza Kiswahili.

3. Kununua vitabu vya Kiingereza na kamusi za kiingereza

 4. Kudhibiti walim kutozungumza Kiswahili darasani katika ufundishaji

5. Kusisitiza debate, moning talk au story na uandishi wa articles kwa wanafunzi
1. Kumudu masomo ya Sekondari  yanayofundishwa kwa lugha ya Kiingereza na matunmizi ya lugha hiyo kwa kiwango kinachokubalika
DED,DEO, MEK, WAKUU WA SHULE, WALIMU NA WANAFUNZI

Endelevu

02.
Baadhi ya walimu kutowajibika kikamilifu
Ø  Kuongeza uwajibikaji katika ufundishaji wenye matokeo chanya.
1. Kuhimarisha utendaji kazi wa walimu katika ufundishaji kwa kukamilisha mada za masomo mapema.

2. Wasiowajibika kutolewa taarifa kwa mwajiri na ngazi  zingine  za nidhamu ili kuwawajibishwa kulingana na taratibu na sheria
1. Kufanya ufuatiliaji wa karibu  ili kubaini walimu wasiowajibika kikamilifu hivyo kushushwa madaraja au kuachishwa kazi 

2. Kufanya vikao vya mara kwa mara shuleni ili kutathmini utendaji kazi wa walimu.  

3. Kusimamia na kufuatilia kikamilifu hali ya ufundishaji na ukamilishaji wa mada za masomo mapema na kufanya marudio
1. Kuongeza ufanisi kazini 

2. Kuinua kiwango cha ufaulu kutoka 60% hadi 100% ifikapo Novemba 2021
DED, DEO, WAKAGUZI WA SHULE, MEK, WALIMU WAKUU, WATAALUMA, WALIMU, DAO, BODI, SHULE, TSC.

Endelevu

03.
Jamii  kutoshiriki kikamilifu  katika  ufuatiliaji wa maendeleo ya shule
Ø  Jamii kutambua kuwa shule ni mali yao.
1. Wazazi kuhamasishwa  kushiriki katika  shughuli za maendeleo shuleni
1. Kuchangia/kushirIki maendeleo ya shule kwa kutoa fedha na nguvu kazi. 

2. Kuwa na vikao vya wazazi vya kujadili maendeleo ya shule. 

3. Wazazi kufuatilia maendeleo ya wanafunzi shuleni

4.  Kusimamia sheria ya kuwawajibisha wazazi wasiohudhuria vikao vya wazazi.

5. Kutoa Elimu kwa jamii kuitambua shule na umuhimu wake katika mazingira yao.
1. Jamii na wazazi kushiriki vikao na kutoa michango ya kuboresha maendeleo ya shule
DED, DEO, MADIWANI, VIONGOZI WA KATA, KIJIJI, WAZAZI NA  WADAU WENGINE
Juni 2020  hadi Desemba 2020

04.
Kushuka kwa nidhamu ya wanafunzi na Walimu shuleni.
Ø  Kuimarisha nidhamu ya wanafunzi shuleni 

Ø  Kuimarisha nidhamu ya walimu shuleni
1. Kuhakikisha kuwa nidhamu inaimarika kwa wanafunzi ili kuinua kiwango cha taaluma.

 2. Kuhakikisha kuwa nidhamu inaimarika kwa walimu ili kuinua kiwango cha taaluma.
1. Kudhibiti wanafunzi kutojihusisha na mahusiano ya kimapenzi

2. Kufukuza au kusimamisha wanafunzi watakaobainika kuwa na utovu wa nidhamu

3. Kusimamishwa kazi na utumishi kwa mwalimu atakayebainika kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi

4. Wakuu wa shule kuwafuatilia walimu wao  kwa karibu
1. Kuinua kiwango cha taaluma kutoka 60% hadi 100%
WAKUU WA SHULE, BODI YA SHULE, DED, DEO, TSC, DSEO NA WALIMU.

Endelevu

05.
Kutokuwepo kwa   huduma ya Uji na chakula cha mchana shuleni
Ø  Kuwafanya wanafunzi kukaa muda mrefu shuleni   kujifunza na kufundishwa kwa muda wa ziada.  

Ø  Eneo la shule kutumika kwa ajil ya shughuli za uzalishaji mali.

Ø  Kupanua mfuko wa     fedha  wa shule
1. Kuhamasisha jamii kuchangia huduma ya chakula shuleni.
 
2. Kuhamasisha  shule kuanzisha miradi ya uzalishaji mali (EK)
1. Kuita kikao cha wazazi na kujadili kuhusu uchangiaji wa chakula

2. Mkurugenzi mtendaji kuwasiliana na Mkuu wa Wilaya ili aweka amri kwa jamii kuhusu kuchangia chakula shuleni

3. Mkuu wa Wilaya au Mkurugenzi kuwaagiza watendaji wa kata/vijiji na Makatibu Tarafa kufuatilia na kuwahimiza wazazi kuchangia chakula  

4. Kuhamasisha uanzishaji wa  mashamba  na bustani shuleni ili kupata chakula shuleni
1. Kuongezeka ufaulu wa wanafunzi kutoka 60% kufikia 100% ifikapo Juni 2020

2. Kupunguza idadi ya  wanafunzi kuacha shule
DC,DED, DEO, MADIWANI, MEK, WALIMU WAKUU, WALIMU, VIONGOZI WA KIJIJI,TAASISI BINAFSI, WANAFUNZI

Endelevu

06.
Utoro wa wanafunzi unaopelekea ufaulu wa daraja sifuri
Ø  Kuimarisha taaluma ya wanafunzi katika masomo na kuondoa ziro
1. Kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayekuwa mtoro shuleni bila sababu za msingi hasa kwa madarasa ya mtihani (kidato cha pili na nne)

2. Kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi atakayepata daraja sifuri katika mitihani ya kidato cha nne 2016
1. Kuwafuta wanafunzi wanaokuwa watoro zaidi ya siku 90 mfululizo

2. Kutoa adhabu kwa wanafunzi watoro

3. Kuwapeleka wazazi wa wanafunzi wanaokuwa watoro mahakamani
1. Kuinua kiwango cha ufaulu kutoka 60% hadi 100% ifikapo Novemba 2021
WAKUU WA SHULE, WALIMU, BODI YA SHULE, DED, DEO, TSC NA WALIMU.

July 2020 hadi Oktoba 2021

07.
Wanafunzi kutojibidisha katika masomo kikamilifu
Ø  Kuimarisha taaluma
1. Kuwa na wanafunzi wasiopata daraja la sifuri katika mitihani ya kidato cha pili na nne ifikapo Octoba 2021
1. Kuanzisha program maalumu/operation  maalumu ya kuondoa daraja la sifuri

2. Kusaidia wanafunzi wasiojiweza kwa kuweka juhudi kubwa katika masomo mawili hasa katika somo la Kiswahili na urahia ili aweze kupata daraja la D katika masomo hayo

3. Kutoa mazoezi kila wiki au mwezi na kuwasaidia wanafunzi jinsi ya kujibu maswali
1. Kuinua kiwango cha ufaulu kutoka 60% hadi 100% ifikapo Novemba 2021
WAKUU WA SHULE, WALIMU, BODI YA SHULE, DED, DEO, TSD, DSOA NA WALIMU.

April 2021 hadi Oktoba 2021

08.
Usimamizi na ufuatiliaji duni wa shughuli za ufundishaji shuleni
Ø  Kuimarisha taaluma ya wanafunzi katika masomo na kuondoa sifuri
1. Kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za ufundishaji shuleni
1. Kuhimiza wakuu wa shule kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kwa walimu katika shughuli za ufundishaji darasani 

2. Kuzaja fomu maalum ya kuonyesha hali ya ufundishaji na ukamilishaji wa mada kwa kila somo na kuiwasilisha katika ofisi ya DEO kabla ya tarehe 1 ya kila mwezi 

3. Mkuu wa shule  kukagua kikamilifu shughuli za ufundishaji kwa kila mwalimu darasani na uandaaji wa nyaraka mbalimbali za ufundishaji 

4.Kuanzisha program  maalumu (Operation ya tokomeza sifuri) ya kuondoa daraja la sifuri

5.Kusaidia wanafunzi wasiojiweza kuweka juhudi kubwa katika masomo mawili hasa katika somo la Kiswahili na urahia ili aweze kupata daraja la D katika masomo hayo

6. Walimu kushirikiana na kubadilishana katika ufundishaji
1. Kuinua kiwango cha ufaulu kutoka 60% hadi 100% ifikapo Novemba 2021
WAKUU WA SHULE,WALIMU, BODI YA SHULE,DED NA DEO

Endelevu

09.
Upungufu wa miundo mbinu shuleni
Ø  Kuongeza miundo mbinu ili kufikia uwiano wa Kitaifa mfano Madarasa nyumba za walimu matundu ya vyoo, Maabara,Hostel, Maktaba na kumbi za mikutano.
1. Kuhakikisha kuwa miundombinu inajengwa na kukarabatiwa. 

2. Kuweka mtazamo chanya  kuhusu Elimu na kuhamasisha jamii kujitolea katika kujenga miundo mbinu
Kuhamasisha jamii kushirikiana katika ujenzi wa miundombinu na kufuatilia utekelezaji wa ujenzi
1. Kupunguza tatizo la uhaba wa miundombinu kwa 50% ifikapo Juni 2021
MBUNGE,DED, DEO, MADIWANI, WARATIBU ELIMU KATA, WALIMU  VIONGOZI WA KATA/KIJIJI NA WANANCHI

Endelevu

10.
Kutokuwepo mfuko wa Elimu.
Ø  Kuboresha  miundo mbinu
 
Ø  Kutoa motisha chanya kwa walimu na wanafunzi.
1. Kuanzisha na kusimamia  mfuko wa Elimu shulen
1. Kuboresha utendaji kazi wa walimu na kuvutia mazingira ya kazi. 

2. Kuboresha miundombinu katika shule za   sekondari.  

3. Kubaini walimu wanaostahili kupewa motisha chanya.  

4. Kuajiri walimu wa muda wa masomo ya sayansi
1. Walimu kuyakubali na kufurahia mazingira ya kazi.
MBUNGE, DED, DEO, MADIWANI,WE0, VEO, WARATIBU ELIMU KATA, WALIMU NA VIONGOZI WA KIJIJI/KATA NA WADAU WENGINE WA ELIMU.

Endelevu

11.
Ø  Wanafunzi wenye uwezo mdogo na  wasiojua KKK kuchaguliwa na kujiunga na Elimu ya Sekondari
Ø  Kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayeingia darasa la  saba  bila kumudu stadi za  kusoma, kuandika na kuhesabu 

Ø  Kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayeingia kidato  cha kwanza bila kumudu stadi za  KKK
1. Idara ya Elimu Sekondari na Msingi  kushirikiana katika kuimarisha madarasa ya elimu ya  awali 

2. Kuwajengea walimu uwezo  wa kufundisha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK)
1. Kubaini wanafunzi wa kidato cha kwanza  wasiojua KKK na kuwasilisha orodha yao kwa Afisa Elimu Msingi na Mdhibiti Ubora wa Shule ili kudhibiti tatizo la wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika kuingia kidato cha kwanza   

2. Kuandikisha wanafunzi wa madarasa ya awali kwa wakati  

1. Kutokuwa na    wanafunzi wasiojua K3 ifikapo januari 2021
DED,DEO, WAKAGUZI WA SHULE, WARATIBU ELIMU KATA, WALIMU , TRCs, WANAFUNZI,BODI NA KAMATI ZA SHULE

Endelevu

12.
Upungufu wa madawati
Ø  Kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anakaa kwenye dawati ifikapo june 2021
1. Kuhamasisha jamii, watu binafsi na wadau mbalimbali kutoa mchango kwa ajili ya utenganezaji wa madawati yanayopungua kwa kila shule
1. Kuandika barua ya maombi na kupeleka kwa wadau mbalimbali ikiwemo Taasisi za kifedha (banki ya NMB,CRDB) na watu binafsi

2. Kutuma maombi kwa Mh. Mbunge kwa ajili ya kufadhiri na kusaidia kupata wafadhili wengine watakaosaidia ufadhili wa madawati

3. Kuomba kiasi cha fedha kutoka makusanyo ya ndani ya Halmashauri  ili kupunguza tatizo
1. Kuondoa tatizo la ukusefu wa madawati katika shule za sekondari

DED,DEO

Julai 20120 hadi Juni 2021

13.
Upungufu wa nyumba za walimu
Ø  Kila mwalimu kuishi karibu na shule ili kuwawekea walimu mazingira bora ya kuishi na kuwaondolea usumbufu wanaopata kutokana na ukosefu wa nyumba ili kuinua kiwango cha taaluma
1. Kuhakikisha kupatikana kwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu angalau kufikia kwa asilimia 50%
1. Kuomba fedha kutoka serikalini kwa kuweka bajeti ya ujenzi wa nyumba za walimu

2. Kutuma maombi kwa wafadhili mbalimbali ili kuweza kusaidia ili kupunguza tatizo la ukosefu wa nyumba za walimu
1. Kuinua kiwango cha ufaulu

2. Walimu kuishi katika mazingira yatakayowasa idia katika kutimiza wajibu wao
DED,DEO, MBUNGE, JAMII NA WADAU MBALIMBALI

Endelevu

14.
Upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi
Ø  Wanafunzi wengi  kusoma masomo ya sayansi na kuyafaulu masomo hayo
1. Kuongeza walimu wa masomo ya sayansi kutoka walimu wachache waliopo  ili kufikia ulinganifu sahihi wa walimu wanaotakiwa kwa kila shule
1. Kushirikiana na Mh. Mbunge ili kuiomba serikali  kutupangia walimu wengi wa masomo ya sayansi kutokana na upungufu mkubwa tulionao
1. Kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika masomo ya sayansi

2.  Kuongeza idadi ya wanafunzi wa kusoma ya sayansi
DED, DEO, MH. MMBUNGE

Aprili 2021 hadi Juni 2021






Mwl, Frank P. Karoli                                                                                     naxfra@gmail.com
0762 426 746
© 2020

Comments

Popular posts from this blog

MAJINA YA WANAWAKE KATIKA BIBLIA ‘A’ HADI ‘Z’

SOMO: MADHARA YA KUKATAA KUMTII MUNGU

MFANO WA MPANGO KAZI