GONJWA LA LEO LINALOENEA KWA KASI KWA WATU WENGI



Utangulizi
Pamekuwepo na panazidi kuongezeka magonjwa mengi ya ajabubuajabu katika ulimwengu wa sasa tunaouishi katika dhama za mwisho wadunia; hususani ndani ya sayari yetu Dunia. Magonjwa hayo yamekuwa kikwazo na kusababishwa changamoto nyingi sana katika maisha ya mwanadamu. Ukiachana na magonjwa ya kisaikolojia, kiakili, kimwili na mengineyo mengi sana yanayozidi kubainika na kuongezeka siku hadi siku katika kizazi cha ulimwengu wa sasa; lipo gojwa la muda mrefu, ambalolimedumu karine kwa karine.
Gonjwa hilo sugu ni kongwe kuliko magonjwa mengine baadhi yaliyoibuka hivi karibuni. Gonjwa hili limekuwa likienea kwa kasi ya ajabu kulingana kubadirika kwa mitindo ya maisha ya mwanadamu. Gonjwa hili linajibainisha katika na hari na dalili zifuatazo:
*     Kupenda raha na maisha ya bila kutoa jasho,
*     Kupenda kulala kuliko kujibidisha,
*     Kukosa moyo wa kujituma,
*     Kupenda starehe kuliko kujishughulisha,
*     Kutokujitambua kwa sababu ya kukosa tafakuri, njozi dira na malengo,
*     Kutotaka kuteseka ili kuifikia raha ya badae,
*     Kutojali muda au wakati na hupelekea kuahirisha kufanya mambo kwa wakati,  na
*     Kupoteza maarrifa  na ubunifu.
Gonjwa hili hakika linatisha, maana ukilipata; tiba yake inahitaji kujikana nafsi, bila hivyo linaweza kukutesa hadi wakati wa kufa, unakufa nalo na marehemu usiweze kukumbukwa kwa lolote juu ya dunia hii.  Ukiachana na magonjwa mengine unayoyafahamu; gonjwa hili la ajabu na linalotisha kuliko magonjwa baadhi mengi. Gonjwa hili kwa namna ya ajabu huwapata watu wenye afya zao nzuri, wenye nguvu tele za kufanya kazi, wasio na ulemavu mowote katika miili yao. Hakika ni gonjwa la pekee na laajabu sana.
 Gonjwa hilo linaandikwa na kutamkwa kwa herufi nne (irabu ni tatu na konsonati ni mbili). Gonjwa hili linaitwa ‘‘UVIVU’’. Neno UVIVU ni neno ambalo haliwezi kubadirika maana yake hatakama utasoma kinyumenyume, au ukitumia kioo; ndani yakioo litasomeka vilevile bila kupoteza maana yake halisi. Gonjwa liitwalo UVIVU, nitalizungumzi kwa kirefu katika upande wa hasara pekee, hasa linapokuwa limempata mwanadamu aliye na nguvu, afya, na akili timamu.
Uvivu ni hari inayompata mtu na asiweze kujituma katika kufanya kazi au kukosa uwezo au ari ya kufanya kazi kwa bidii. Uvivu ni uzembe, na kinyume cha Uvivu ni kutofanya kazi kwa bidii. Uvivu kwa binadamu mwenye nguvu, afya, na akili timamu unatokana na mtu mwenyewe kujiendekeza katika kutojibidisha, kutokuwa na moyo wa kufanya kazi kwa bidii, kukosa ari ya kufanya kazi kutoka moyoni mwake, kutojitambua kunakoendekeza maisha ya raha bila kujituma katika bidii ya kufanya kazi. Mtu mwenye nguvu, afya, na akili timamu asipopenda kufanya kazi na kujituma katika bidii ya kazi, huyo ni mgonjwa mwenyegonjwa la uvivu.
Taifa lolote likiwa na watu wenye ugonjwa utokanao na uvivu; tutegemee taifa lenye umasikini wa kutupwa maana watu wake hawana ari, bidii, na moyo katika kufanya kazi. Uvivu kwa mtu mmojammoja huzalisha umasikini kwa mtu mmojammoja, hatimae umasikini huo hupanda ngazi katika familia na mwishowe taifa zima kwaujumla. Taifa la wavivu huzaa taifa legelege lenyeombaomba na tegemezi hadi ngazi ya kitaifa.
Tabia au sifa ya uvivu uliokithiri kwa watu, hupelekea wengi kupenda maisha ya mteremko na mepesi, ambapo hutafta mafanikio yao kwa njia zisizohalali kwa kupata pesa zipatikanazo kinyume cha sheria, utaratibu na maadili ya jamii. Ujambazi, biashara za kujiuza mwili, utapeli, ukabaji, wizi, uzulumaji, kamali, kuombaomba ndizo shughuli za wengi waliowavivu katika kuchapa kazi ili wapate pesa kwa uhalali. Mtu aliye mvivu na asiyejishughulisha hufanya mambo mengi katika muda mwingi yale yasiyo na tija ambayohuathiri uwezo, moyo na ari ya uchapa kazi. Mfano; kuzululaji, kukaa vijiweni kupiga ili soga, umbea, utumiaji wa madawa ya kulevya, kuambatana na makundi au marafiki wasiokuwa na mwelekeo wowote, n.k.
Vitabu vingi vya kiulimwengu na vya kiroho/imani vinasisitza kufanya kazi kwa bidii ili kupata mafanikio au kupata mali zilizo za halali zitokanzo na jasho la mtu husika anayechakalika. Huko nyuma, zamani kabisa; kazi zikuwa mbili tu; ya kwanza ilikuwa ni kulima/kilimo pakifuatiwa na ufugaji wa wanyama. Leo hii kuna kazi nyingi sana halali duniani ambazo mwanadamu awezafanya ili kujipatia kipato kitakachomwezesha kuendesha maisha yake ya kila siku bila kutegemea serikali. Kwa mujibu wa Bibulia Takatifu; kazi ya kwanza ya mwanadamu wa kwanza (Adam) ilikuwa ni kulima (kulima na kuitunza bustani ya Edeni) Mwanzo 2:15.
Shamba lako la weza kuwa karamu, ‘computer’, gari, duka, soko, ajira, fani, ujuzi, kipaji n.k kiwezacho kukupatia kipato na kukuletea mafanikio; hivyo basi, kwa aina yoyote ya shamba au kazi; fanya kazi kwa bidii na kwa moyo wako wote. Yesu mwenye kabla ya kuanza kufanya kazi ya injili, alifanya kazi ya uselemala aidha akiwa anamsaidia baba yake (Yusufu) au yeye mwenye (Mariko 6:3); maana pia Mungu hufanya kazi bila kuchoka (Yohana 5:17). Mitume wa Yesu nao walifanya kazi huku wakiipeleka injili. Mtume Paulo anasema katika 2Wathesalonike 3:10, “….ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, na asile chakula”. Ili ile, yakupasa ufanye kazi na ule jasho lako, na sio uwe unakula jasho la wengine walohangaika kutafuta.

Sifa na tabia za mtu mvivu pamoja na changamoto zake
Zifuatazo ni tabia na sifa bainishwa za mtu mvi. Endapo mtu mwenye afya, ananguvu, hana ulemavu wowote wala matatizo ya kiakili; akiwa katika sifa na tabia baadhi zifuatazo, basi mwanadamu huyo gonjwa la uvivu:
1.      Mtu mvivu hupenda kulala na huthamini usingizi kuliko kujituma
Mvivu yeyote hutumia muda mwingi kulala (usiku na mchana) kama ilivyo nafsi yake, jua huchomoza yeye bado yupo kitandani kila siku. Usingizi kwake ni starehe. Mvivu anaependa usingizi, njaa kwake ni kawa maana hutumia muda mwingi kulala kuliko kutafta mkate (chakula) wake wa kila siku. Mithali 19:15 ‘’Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito; Na nafsi yake mvivu itaona njaa’’. Mfalume Sulema anaonya na kututahadharisha katika Mithali 20:13; anasema “Usipende usingizi usije ukawa masikini; Fumbua macho yako nawe utashiba chakula. Mvivu hujigeuzageuza kitandani kama ilivyo kwa bawaba za mlango; ufungwapo na kufunguliwa (Mithali 26:14)
2.      Mtu mvivu hafanikiwi, kwa sababu hana moyo wa kujituma
Yeyote aliyemvivu kufanikiwa kwa jambo lolote kwake ni nadra sana, hiyo ni kutokana na kukosa ari ya kujituma kwa bidii katika kufanya kazi yoyote na nasfi yake imefanyika kutopata na kufanikiwa. Tofauti na mvivu, mwenye bidii hubarikiwa na hufanikiwa katika kujibidisha kwake. Mithali 13:4 “Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa”. Mara zote mtu Yule ajitumae katika kufanya kazi kwa bidii, Mungu humbariki katika kupata mafanikio, maana Mungu ameahidi “…. kubarikia kazi yote ya mkono wako….” (Kumbukumbu la Torati 28:12)
3.      Mtu mvivu ni mzembe wa kutupwa; hata kwa vitu au kazi isiyohitaji nguvu na maarifa yeye humshinda
Mvivu hata ukimsogezea fursa mlangoni kwake umefanya kazi bure. Hata kama fursa zipo kila mahali, mvivu hawezi kuthubutu katika kujisumbua kufanya jambo lolote, maana yeye kila jambo kwake ni kero na usumbufu. Mtu mvivu ni sawa na mtu asiyeweza kufunga goli katika mpira wa miguu, hata kama klinda mlango (goal keeper) akiondoka, yeye hawezi akafunga. Mithali 19:24 “Mtu mvivu hutia mkono wake sahanini; Ila hataki hata kuupeleka hata kinywanipake”. Pia Mithali 26:15, inazungumzia jambo lilelile.
4.      Mtu mvivu hujiona sahihi kwa hali aliyonayo, hata kama akishauliwa hachukui hatua
Mvivu hawezi akashaulika kwa jambo lolote la mafanikio yake, hujiona sahihi jinsi alivyo, hata ufanye vipi hawezi akabadirika, maana kwake uvivu ni gonja linalomshambulia daima. Mithali 26:16 “Mtu mvivu ni mwenye hekima machoni pake, kuliko watu saba wawezao kutoa sababu”.
5.      Mvivu kutumika au kwake kujituma ni kuchungu
Daima mvivu hapendi kutumika na kujituma katika bidii ya kazi.  Mvivu hukeleka, huumia pale aambiwapo kufanya kazi au kutumwa kufanya kazi, na huwa mkali au hulalamika sana apewapo majukumu ya kufanya kazi. Mithali 10:26 “kama siki menoni, na moshi machoni, ndivyo alivyo mtu mvivu kwao wamtumao”.
6.      Mvivu hutawaliwa, hufanywa mtumwa na wale wenyebidii na waliofanikiwa.
Mvivu haheshimiki, hugandamizwa na kunyonywa na wale waliofanya bidii katika maisha yao na kufanikiwa. Kwa kuwa uvivu huleta umasikini, basi mvivu ni mtumwa kwa wale walifanikiwa au kujibidisha katika kazi. Sanjali na kunyonywa, waliofanikiwa hufanya lolote kwa waliowavivu. Mithali 12:24 “Mkono wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipiswa kodi”
7.      Mtu mvivu ni ombaomba; hali na kutumia vya jasho lake mwenyewe
Mvivu hawezi kujibidisha ili apate pesa, vitu, au mali itokanayo na nguvu zake; bali yeye haishi kuomba kila kukicha. Kwa kukosa fikra yakinifu za kujitambua pamoja na kujituma atika kutafuta na kufanya kazi, mtu mwenyegonjwa la uvivu haishi kuombaomba kwa wale wenye kuzitafuta pesa kwa nguvu zao. Mithali 12:27 “Mtu mvivu hapiki mawindo yake; Bali mwenye bidii anamali za thamani”. Neno la Mungu pia linawaonya watu wavivu wanaokula, kutumia na kuishi kwa kutegemea jasho la watu wengine. 2Wathesalonike 3:10, 1210Kwa kuwa hata ule wakati tupokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula 12Basi twawagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivi na kula chakula chao wenyewe”
8.      Maisha ya mtu mvivu huwa ni magumu na ya shida sana
Mtu aliyeathirika na gonjwa la uvivu, kwake siku zote maisha ni magumu na ya shida sana. Mvivu hawezi pata ahueni ya maisha, kwa sababu yeye hana hasumba ya kujishughulisha katika kutafuta ili afanikiwe; bali hutumia muda mwingi kwa mambo yasiyo ya msingi, sitarehe, majungu, anasa, na kulala kwingi. “Njia ya mtu mvivu ni kama boma la miiba……..” (Mithali 15:19)
9.      Mtu mvivu hupenda maisha rahisi, hapendi kujitesa katika bidii ya kutafuta
Mvivu hapendi kujisumbua, kujibidisha katika kazi, wala kuteseka ili hapo baadae afanikiwe na kufaidi matunda yake; bali yeye (mvivu) hupenda maisha rahisi yenye mteremko ili aseleleke hadi mwisho. Maisha ya kupanda mlima kwa mvivu ni machungu mno tena ni zaidi ya pilipili kichaa. Mithali 20:4 “Mtu mvivu kataki kulima wakati wa baridi; Hivyo wakati wa mavuno ataomba, hana kitu”
10. Mikono ya mtu mvivu hufanya kazi kilegevulegevu
Muhubiri 10:18 “Kwa sababu ya uvivu paa hunepa; Na kwa utepetevu wa mikono nyumba huvuja”. Kutokana na kukosa moyo au ari ya kufanya kazi kwa bidii, mtu mvivu hufanya kazi kizembe tena kwa ulegevu na utpetevu wa mikono. Mikono ya mtu asiyependa kazi ni milegevu na haitaki daima kutenda kazi. Mithali 21:25Matakwa yake mtu mvivu humfisha, Kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi”.
11. Mtu mvivu hawezi kuthubutu, kuvumilia wala kuzikabili changamoto ili ayafikie mafanikio.
Binadamu mwenyegonjwa la uvivu ni mwoga, anatawaliwa na mashaka, sio mvumilivu, hawezi kuthubutu wala kujitesa katika kuzikabili changamoto, iwalau mwisho wa siku ayafikie malengo yake. Mvivu ni mvivu hata katika kufikiria, hawezi kufanya kazi, biashara wala jambo lolote bila kubebwa au kusaidiwa. Mvivu huzungukwa na mashaka, wasiwasi, pamoja na uoga uliokithiri, hivyo hawezi kuthubutu kwenye kazi au jambo linalohitaji ushupavu wa moyo, nguvu, akili na uwezo wa maarifa, pamoja na ustahimilivu kubwa. Mithali 22:13 “Mtu mvivu husema, Simba yuko nje; Nitauawa katika njia kuu”. (kwa jinsi hiyohiyo; Mithali 26:13, Sulema alizungumzia) 
12. Mtu mvivu huharibu, hatunzi, hutumia kwa pupa na kwa uharibifu vitu au mali zilizotafutwa na wengine.
Kutokana na kutojua uchungu, mateso, usumbufu, gharama na jasho lililotoka katika kuvipata vitu au mali zilizotafutwa na watu wengine; mtu mvivu azikutapo mali hizo au vitu hivyo yeye hutapanya, hufuja, huharibu, hutumia kwa pupa na fujo vitu au mali hizo (zilizokwishatafutwa na watu wengine tayali). Mithali 18:9 “Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake ni ndugu yake aliye mharabu”. Mharabu ni mtu mharibifu.
13. Mtu mvivu ni mzigo na hunyonya wengine
Tabia ya uvivu, utegemezi, kuombeleza, kudandiadandia vitu na mali za wengine; mtu mvivu huwa mzigo kwa marafiki, jamii hata taifa kwa ujumla. Binadamu mwenye gonjwa la uvivu ni mzigo mkubwa na mnyonyaji kwa wengine wale wanaojibidisha katika kuchapa kazi na kutafuta; wale ambao usingizi, raha wala anasa kwao hazina thamani, maana kila siku, kila saa, kila muda; nafsi zao, damu zao, fikra zao huwaza na kusema “Hapa Kazi Tu”. Neno la Mungu linaonya kuwa, tusiwe mizigo na kunyonya wengine wanaojibidisha. 2Wathesalonoke 3:7-10 “ 7Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu; 8wala hatukula chakula kwa mtu yeyote bure; bali kwa taratibu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote. 9Si kwamba hatuna amri, makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate. 10Kwa kuwa hata ule wakati tupokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula”
14. Mtu mvivu hupenda kufuatilia mambo na mafankio ya wengine.
Mvivu asiyefanya kazi; masikio yake, macho yake, miguu yake na mdomo wake huwa makini na shapu kufuatilia na kusema mambo na mafanikio ya wengine (yasiyomhusu hata kidogo). Kutokana na kukosa kazi, shughuli na mambo ya kufanya, mvivu hufuatilia ya watu wengine na kuyatapakaza mtaani au kuyasambaza kwa watu wengine. Tabia hii ya mtu mvivu, huzaa tabia ya umbea, usengenyaji na  kuchunguza chunguza maisha ya wengine au kutumia muda mwingi kwa kuzulula na kukaa vijiwezo kupiga soga zisizokuwa na maana badala ya kufanya kazi. 2Wathesalonike 3:11 “Maana twasikia  kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli  zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine”
15. Mtu mvivu hawajali wala kuwahudumia na kuwatunza walio wa family yake
Kutoka na kuathiriwa na gonjwa la uvivu, mtu mvivu hukwepa majukumu na hawezi kuwahudumia wala kuwatunza vyema wale waliowafamilia yake kwa kiwango kinachotakiwa. Apate wapi pesa, mali, maarifa mtu mvivu hadi aweze kuhudumi walio wa familia yake? Family inayomtegemea mtu mvivu haina uhakika wa maisha ya kesho wala keshokutwa. Haikosi njaa, haina akiba wala matunzo yanayokidhi. Paulo mtumishi wa Mungu anasema “Lakini mtu yeyote asiyewatunza walio wake, yaani wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini” 1Timotheo 58.
16. Kazi, mali, na vitu vya mtu mvivu havipo katika utaratibu, matunzo na mpangilio maalumu
Kila jambo, kila kazi, na kila kitu cha mtu mvivu kipo ‘shaghalabaghala’; hakuna matunzo, hakuna mpangilio, hakuna utaratibu. Hakuna kipi kianze wala kipi kifuatie baada ya kingine. Muda gani jambo au kitu gani kifanyike na kifuatiwe na kitu gani  kingine. Kazi ipi ifanyike vipi, muda gani na kwa namna gani, ianzeje na imalizikeje, kitu gani kitunzwe na kihifadhiwe kwa namna ipi? Muhubiri 10:18 “Kwa sababu ya uvivu paa hunepa; Na kwa utepetevu wa mikono nyumba huvuja”. Mithali 24:30 30Nalipita karibu na shamba la mvivu, na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili. 31Kumbe! Lote pia limemea miiba; Uso wake ulifunikwa kwa viwavi; Na ukuta wake wa mawe umebomoka”
17. Mvivu hapendi wengine wafanikiwe, anataka wabaki kama alivyo yeye
Kushindwa kwake mvivu, hutamani na wengine wafeli na washindwe kama alivyoshindwa yeye. Kwa maana nyingine; mvivu huwaonea wivu wale wanaofanikiwa na hujenga kinyongo na chuki juu yao. Mathayo 25:18, 24-27 18Lakini Yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake. 24Akaja…..aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; 25basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyoyako….”
18. Kwa tabia ya uvivu, mvivu hawezi akathaminika wala kuheshimika
Mara zote mvivu haheshimiki, kutokana na matendo, mienenodo natabia zake zisizokuwa na uelekeo wala malengo. Tabia yake ya uvivu humpunguzia hadhi ya kuheshimika, kwani kila Nyanja yeye huwa anafeli; kiuchumi, kibidii, kimafanikio, kiubunifu na kimaarifa. Mathayo 25:24, 30 “24Akaja…..aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya;…. 30Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; …….
19. Mvivu ni mvivu wa kujifunza maarifa mapya ili aweze kubadirika
Kutokana na uvivu kumtawala; mtu mvivu ni mvivu kujifunza maarifa mapya ili aweze kufanikiwa na kujikwamua kimaisha. Hata kama atapatiwa elimu, ushauri na maarifa mapya anaweza kushindwa kutokana na kuwa mvivu katika kusimamia, kutekeleza na kujibidisha kwa kile alichojifunza au kushauliwa na wengine. Suleman alitoa ushauli kwa mvivu kuwa apashwa kujifunza hata kwa wadudu aina ya chungu wafanyavyok kazi kwa bidii. Mithali 6:6-11 6Ewe mvivu, mwendee chungu, zitafakari njia zake ukapate hekima. 7Kwa maana yeye hana akida, wala msimamizi, wala mkuu, 8Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno”
20. Mvivu anaugonjwa wa kuahirisha ahirisha kazi na mambo yake
Tatizo la mtu mwenye gonjwa la uvivu ni kuahirisha-ahirisha kutimiza, kutekeleza mambo na shughuli zake kwa wakati. Huu ni ugonjwa au tatizo linaloitwa kwa kingereza “Procrastination”. Tatizo hili huwakabili wavivu na huchukua sehemu kubwa ya maisha yao. Kuwaza na kusema “nitafanya tu” ndiyo kauli mbiu ya mtu mvivu mwenye tabia ya kuahirisha-ahirisha mambo/kazi/majukumu. Mithali 6:9-11.
21. Mvivu hujipataia pesa, vitu na mali kwa njia zisizo halali
Mtu mvivu hudhulumu, hutapeli, hukaba, huiba, hunyang’anya vitu, mali, au pesa; hivyo njia azitumiazo hujipatia mali, vitu, pesa; huwa sio halali. Mvivu aweza dhuru, ua, teka; ili mwisho wa yote apate kitu, mali, pesa kwa njia hatarishi zilizo kinyume na talatibu. Matokeo ya kutumia njia zisizofaa, ni kutokana na kutopenda kufanya kazi kwa bidii, kupenda maisha ya mteremko, hahitaji kuteseka. Kwa tabia hizi, neon la Mungu limeonya katika Waefeso 4:28.

Suluhisho la kuondoa, moyo tabia ya uvivu kwa mtu mvivu
Uvivu hujengeka katika moyo, fikra na mwili, kutokana na mtu mwenyewe alivyokuwa na kulelewa katika jamii au family atokayo. Pia mfumo wa elimu yetu ya sasa (Tanzani) imejikita kuandaa au inaandaa taifa la watu wavivu na tegemezi wasiopenda kufanya kazi ngumu, kujiajili, kwa kupenda kazi nyepesi na rahisi na wanaobagua kazi za kufanya maishani. Wanafunzi wawapo shuleni, kwa ngazi za shule ya msingi sekondari na vyou, hawajengewi misingi ya kuzalisha pamoja na kujitegeme. Sijui kama na magereza yetu yote yanawapatia ujuzi, maarifa na uwezo kujitegemea na kuzalisha punde watokapo gerezani? Huko sijawahi kufika na siwezi kusemea.
Tanzania inaasilimia nyingi sana ya watu wasiozalisha na asilimia ndogo ya watu wanaozalisha; mfano: ukichukua idadi ya wato wenye miaka 1-14, wanafunzi wenye miaka 15-30 na wazee miaka 64+. Wengi wao ni tegemezi na sio wazalishaji ndani ya taifa masikini. Mambo ya kuzingatia, kufanya, kufuata na kujifunza kwa mtu mwenye gonjwa la uvivu  ili kukomesha au kutibu ugonjwa au tabia ya uvivu iliyokithiri:
1.      Mvivu na ajitahidi kuepuka uzembe; ajitahidi kuwa na moyo wa kufanya kazi kwa bidii (Mithali 6:6-10)
2.      Mvivu ajenge mazoea ya kufanya kazi kwa kujituma au kufanya kazi kwa bidii bidii (Mithali 3:27)
3.      Mvivu ajitahidi kutunza na kujali muda. Atambue kuwa muda ni mali na ukipotea haurudi
4.      Mvivu ajitahidi kuweka mambo yake katika mpangilio na ayatekeleze kulingana na mpangilio (Luka 14:25-35)
5.      Afanye kazi halali inayomwingizia mali, vitu au pesa halali
6.      Asitumie njia zisizo sahihi ili kufanikisha kujipatia mali au kipato (Wakolosai 3:25)
7.      Yote afanye kwa kumtumainia na kumtegemea Mungu sambamba na kujibidisha katika kufanya kazi (Wakolosai 3:17)
8.      Atambue faida, hadhi na umuhimu wa kutumia vitu, mali na pesa alizo zitafuta kwa jasho lake; ili kuepuka masimango (Waefeso 4:28)
9.      Aache kupoteza wakati na muda kwa kuzulula na kufanya mambo yasiyokuwa na tija wala faida juu ya maisha yake maana kufanya kazi kunafaida (Mithali 14:23).
10. Ajue kufanya kazi kwa kutumia akili na mikono yake, atabarikiwana Mungu()
11. Mvivu ajitume na ajitahidi kupenda kazi maana katika kutenda kazi kwa ustadi kunaleta furaha (Mithali 8:30,31)
12. Atambue kufanya kazi kunaleta matunda au faida maishani (Mithali 14:23)
13. Afanyaye kazi hupata kitu cha kusaidia wengine walio wahitaji, hivyo atachuma mibaraka na kujiwekea hazina mbinguni (Matendo 20:35), kwani anaposaidia huua tabia ya uchoyo (Mithali 3:27)
14. Mvivu akubali kutaabika ili kuyafikia mafanikio kutokana na kutenda kazi (Muhubiri 4:6)
15. Wakati mwingine mvivu ajifunze kufanya kazi kwa mazoea, kwani kunawakati huja; yampasa afanye kazi zaidi masaa au siku zote alivyozoea (Mathayo 5:41)

Faida azipatazo mtu katika kufanya kazi, tofauti na mtu mvivu
Kumekuwepo na mitazamo na mawazo potofu kwa watu wengi, hususani wale wavivu; wanadai kuwa kufanya kazi kwa bidii hasa kazi zinazohitaji kutumia nguvu nyingi ni kazi za mateso kwao; hivyo kuitaji kazi nyepesi na rahisi. Kazi ni kazi tu haijalishi kuwa unatumia nguvu, akili, miguu, mikono au mwili mzima; bali zote ziaitwa kazi kwa namna yake. Hoja ya msingi ni kufanya kazi kwa bidii na kujituma kwa moyo wote huku ukiipenda hiyo kazi.
Mtu yeyote afanyaye kazi kwa bidii anapata faida zifuatazo katika maisha yake ya kila siku juu ya utendaji wa kazi yoyote:
1.      Kufanya kazi ni moja wapo ya kufanya mazoezi ili kujenga nakuulinda mwili usishambuliwe na magonjwa ya kawaida
2.      Hujenga moyo wa uvumilivu na kujituma katika jambo lolote gumu
3.      Mtu afanyaye kazi kwa bidii; Mungu humbariki (tofautisha mibaraka na mafanikio)
4.      Hujiepusha kushiriki, na kuhusika katika mambo, makundi yasiyofaa
5.      Kuonesha utii kwa Mungu, kama alivyoamulu na kuelekeza tangu kwa Adamu
6.      Kufanya kazi, kunasaidia mwanadamu kujenga akili na uwezo kutafakari
7.      Kufanya kazi kwa bidii huongeza uzalishaji ndani tasisi au taifa
8.      Kufanya kazi kwa moyo na bidii, huleta maendeleo kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla.



Comments

Popular posts from this blog

MAJINA YA WANAWAKE KATIKA BIBLIA ‘A’ HADI ‘Z’

SOMO: MADHARA YA KUKATAA KUMTII MUNGU

MFANO WA MPANGO KAZI